BAJETI: JINSI YA KUSIMAMIA, KUTUNZA NA KUTUMIA VIZURI FEDHA BINAFSI NA ZA BIASHARA YAKO (KANUNI 80/20) | JIFUNZE UJASIRIAMALI

BAJETI: JINSI YA KUSIMAMIA, KUTUNZA NA KUTUMIA VIZURI FEDHA BINAFSI NA ZA BIASHARA YAKO (KANUNI 80/20)

Usimamizi wa fedha

Somo letu hili la leo linahusu USIMAMIZI MZURI WA FEDHA. Bila ya kujali kama ni fedha za mtu binafsi katika mfuko wake mwenyewe au ni fedha za biashara, maana hasa ya dhana hii ya elimu ya usimamizi mzuri wa fedha ni hii hapa chini;

Usimamizi mzuri wa fedha ni kitendo au mchakato wa uendeshaji shughuli binafsi au zile za kibiashara kwa kuzingatia bajeti, uwekaji malengo, uwekaji wa kumbukumbu za mapato na matumizi, uwekaji akiba pamoja na uwekezaji katika miradi inayoleta faida siku za baadae.

Lengo kuu la matumizi bora ya fedha ni kuhakikisha pesa ambayo ni rasilimali muhimu sana duniani inaelekezwa kwanza kufanya mambo yale yaliyokuwa muhimu zaidi katika maisha au biashara zetu badala ya kuzitapanya katika mambo ya hovyo yanayosababisha hatimaye mtu au biashara kuishiwa fedha na kuhangaika huku na kule (kufilisika)

SOMA: Pesa tuonazo ni makaratasi tu, jifunze njia ya kupata pesa za ukweli

Hivyo katika somo hili tutakuwa na sehemu kuu mbili; ya kwanza ni usimamizi mzuri wa fedha binafsi mifukoni mwa mtu mmoja mmoja na ya pili ni usimamizi mzuri wa fedha za biashara. Watu wengi wanajua kwamba kuna muongozo katika usimamizi wa fedha lakini kitu wasichokijua sana ni ikiwa kuna aina mbili za usimamizi na matumizi bora ya fedha.

Ijapokuwa aina hizi mbili za elimu ya matumizi ya fedha zinafanana sana katika vipengele vingi kama tutatakavyoenda kuona lakini ipo tofauti kubwa pia na tutakwenda kuiona huko mbele katika makala hii ya jinsi ya kusimamia vizuri pesa zako na zile za biashara. Mtu huhitaji kuwa mhitimu wa chuo cha usimamizi wa fedha ili uweze kusimamia vizuri fedha zako mwenyewe au za biashara yako. 

Kitu cha msingi kuliko vyote ni kujifunza tu namna ya kutengeneza fedha na njia bora za kuzidhibiti zisitumike vibaya basi, ndio maana utakuta hata wazee wetu zamani ambao hawakusoma hata darasa moja wengine walikuwa matajiri vilevile, wewe unadhani walitumia mbinu zipi kutajirika? Leo tunaenda kuzijua mbinu hizo moja baada ya nyingine, so stay tuned.

SOMA: Biashara saba 7 nzuri za kufanya zitakazokuingizia pesa hata kama umelala

Kabla hatujaanza ni muhimu sana kuifahamu vizuri dhana maarufu kwamba, biashara na mmiliki wake ni nafsi mbili tofauti zinazojitegemea na hivyo pia fedha kutoka kwa nafsi hizo mbili ni vitu viwili tofauti na mahali pekee vitu hivi 2 vinapohusiana au kukutana ni kwenye faida na mtaji ambapo mmiliki ndipo hupata gawio lake kama malipo kwa mchango wake katika hiyo biashara au kutoa mtaji kama uwekezaji kwa biashara husika.

 

SEHEMU YA KWANZA (1) : Jifunze Usimamizi wa fedha binafsi 

Umuhimu wa kujifunza usimamiaji mzuri wa fedha binafsi za mtu mwenyewe mfukoni mwake unatokana na sababu kwamba vipato vya watu mbalimbali havitokani na biashara tu peke yake bali pia hutoka vyanzo vingine mbalimbali mfano, ajira, ruzuku, sadaka, zawadi, mikopo nk. Kwa hiyo ni muhimu pia watu wawe na uwezo wa kusimamia vyema matumizi ya fedha zao binafsi mifukoni kusudi ziweze kuwafanyia mambo makubwa zaidi na ya maana maishani.

SOMA: Njia 6 za kuondoa woga na stress za fedha katika maisha yako

Mambo muhimu ya kuzingatia kwenye usimamizi wa fedha za mtu binafsi

Mtu binafsi haijalishi unafanya biashara, umeajiriwa au unapata fedha zako kwa njia gani nyingine, ni lazima na ni muhimu kujifunza elimu ya usimamizi na matumizi mazuri ya fedha unazozipata ili ziweze kukusaidia kutimiza malengo mbalimbali muhimu unayojiwekea katika maisha yako.

Hapa tofauti na biashara, chanzo cha fedha zako chaweza kuwa ni gawio la faida kwenye biashara, ajira, kibarua, ‘pocket money’, mkopo, ruzuku, sadaka, uuzaji wa mali binafsi, au njia nyingine yeyote ile inayokuingizia fedha.

SOMA: Jinsi ya kukwepa mitego inayokuvutia kwenye matumizi mabaya ya fedha zako 

Hata ikiwa labda umepata pesa zako kutokana na kucheza bahati na sibu au michezo mingine ya kubeti nk. ni lazima utafute njia bora kabisa ya kuzitumia fedha hizo vinginevyo zitaisha muda mfupi na kwa haraka sana bila ya kuona manufaa yeyote yale ukabaki na stori tu (simulizi) kuwa uliwahi kushika mabilioni ya pesa zikayeyuka.

1. Weka malengo na mipango ya kifedha

Weka malengo ya muda mfupi na yale ya muda mrefu. Malengo yako kifedha huanzia pale unapofikiria akilini ni kitu gani hasa unachotaka kukifanya, una malengo gani? Je unataka kujenga nyumba, kununua kiwanja? Unataka kusoma chuo? Unataka kununua bajaji/pikipiki? Unataka kununua gari? Unataka kufungua biashara mpya? Unataka kusafiri? Una mpango wa kununua TV, redio na vyombo vya ndani?. Ili uweze kufanikisha jambo lolote lile zuri maishani unapaswa uwe na wazo dhahiri la ni wapi unakotaka kufika na kisha uweke mpango wa kufika hapo

SOMA: Kufanikiwa malengo yako, focus kwenye mfumo(utekelezaji) na siyo kwenye matokeo ya mwisho

2. Tengeneza Bajeti.

Baada ya kuweka malengo, kinachofuata ni kutengeneza mpango au bajeti. Bajeti ni sehemu muhimu sana katika mpango wowote ule wa kifedha na ndiyo itakayokusaidia kuyafikia malengo uliyojiwekea pasipo kuhangaishwa na vidakizi vingine mbalimbali. Bajeti kwa kifupi kabisa maana yake ni kukisia mapato na matumizi yako katika kipindi fulani tuseme labda siku, mwezi au hata mwaka na kisha kufanya ufuatiliaji kulingana na hali halisi itakavyojitokeza.

*(Ikiwa upo katika darasa langu la MICHANGANUO-ONLINE -MASTERMIND-GROUP-2022, nadhani somo la bajeti utalifurahia sana kwani ndiyo sehemu muhimu mno kwenye maandalizi ya michanganuo ya biashara/business plans)*

3. Punguza matumizi na zidisha mapato

Baada ya bajeti ni wakati sasa wa kuhakikisha unachunga vilivyo matumizi yako yasizidi kile unachokipata ikiwa ni pamoja na kutafuta njia zaidi mbadala za kujiingizia kipato mfano kuanzisha biashara ya pembeni, kufanya kazi muda wa ziada au biashara za mtandaoni zisizohitaji muda mwingi. Huu ndio wakati wa kubana matumizi na kuondoa kabisa kila aina ya matumizi yasiyokuwa na umuhimu kwako. Jifunze kila wakati jinsi ya kuwa na pesa nyingi zaidi ya zile ulizokuwa nazo

SOMA: Njia 7 unazotumia kubana matumizi lakini kumbe zinakuzidishia umasikini.

4. Weka Akiba, tumia kanuni ya 80/20

Katika kipato chako unachokipata, weka pembeni kama akiba asilimia 20% ya fedha hizo na utumie asilimia nyingine 80% inayobakia kwa ajili ya matumizi yako ya kawaida. Pesa hizi asilimia 20% ni kwa ajili ya dharura ikiwa lolote litaweza kutokea katika maisha yako ambalo hukulitegemea mfano majanga kama ugonjwa na mengineyo, na hutakiwi kuzigusa kabisa kwa jambo jingine lolote lile. Kanuni ya 80/20 ni muongozo tu na siyo msahafu/sheria kwamba ni lazima iwe asilimia hizo, lakini kiasi hicho cha akiba ya dharura angalau kisiwe kidogo.

Asilimia hii 20% wataalamu hupendekeza angalao mtu uhakikishe inafikia kiwango cha matumizi yako ya miezi 3 mpaka 6. Hii inamaanisha kwamba mtu unapaswa uwe na akiba ya fedha zitakazokutosha kutumia kwa muda wa miezi 3 – 6 ukiwa huingizi kipato chochote. Tuchukulie kwa mfano labda umefukuzwa kazi au umeumwa na kipato chako kukoma, basi akiba yako hiyo itoshe kukuhudumia kwa miezi 3 – 6 badala ya kwenda kuingia madeni hatari ya riba yatakayozidi kukudidimiza kwenye bahari ya umasikini  

5. Jifunze jinsi ya kusave pesa, Fungua akaunti benki.

Ile asilimia 20% ya mapato yako iweke katika akaunti ya dharura ambayo ni tofauti na akaunti zako nyingine za kawaida za akiba ambapo ukishaiweka, umeweka na hutaweza kuitoa kiurahisi tena labda tu itokee dharura.

SOMA: Sababu kubwa 9 duniani kwanini watu hukopa pesa, nne kati yake ni za kuogopa kama ukoma

Ikiwa una malengo mengine ya muda mfupi kwa mfano malengo ya kununua vitu kama samani za ndani, kiwanja, gari nk., unatakiwa katika mapato yako kutenga asilimia nyingine ya fedha kwa ajili ya malengo hayo mbali na ile asilimia 20%. Kiasi hicho kulingana na malengo yako kinaweza kuwa kiasi chochote kile cha fedha mfano asilimia 5%, 10%, 20% nk. na unaweza kufungua akaunti nyingine ya akiba kwa ajili yake mpaka umehakikisha zimetosha kutimiza kile ulichokusudia kukifanya.

6. Wekeza fedha zako kwa malengo ya muda mrefu.

Wakati uwekaji akiba katika akaunti maalumu ya dharura na ile ya kawaida ya akiba ni kwa ajili ya malengo yako ya muda mfupi, kwa upande wa malengo yako ya muda mrefu itakubidi sasa uanze kufanya uwekezaji wa fedha zako kwa njia mbalimbali kama nitakavyoeleza hivi punde.

Hivi unafikiria kama umeweka akiba yako ya dharura fedha za kutosha miezi 3 – 6 na muda ukapita lakini hakuna majanga yeyote yaliyokutokea unadhani fedha hizi utazifanyia kitu gani zaidi? Bila shaka utaamua kutafuta njia nyingine mbadala zaidi ya kuziweka fedha zako hizo huku zikiendelea kuzaa faida kubwa badala ya kukaa tu kama akiba benki.

Halikadhalika kutokana na mikakati yako mizuri  ya bajeti uliyojiwekea ikiwemo ubanaji wa matumizi na njia mbadala mbalimbali za kuongeza mapato yako, mzunguko wa fedha zako utakuwa chanya kiasi cha kusababisha ongezeko kubwa la fedha za ziada ambazo ni lazima sasa uziwekeze katika miradi mbalimbali ya muda mrefu kutegemeana na ni shughuli gani za kukuingizia kipato unazozifanya kwa ajili ya kuja kukutiririshia fedha nyingi zaidi wakati kipato chako cha kawaida kitakapokoma na kukufanya uishi maisha yasiyo na stress.

SOMA: Stress za pesa zinavyoweza kuzima kabisa ndoto za mtu na hatua za kuchukua haraka.

Kwa mfano ikiwa wewe ni mwajiriwa katika sekta binafsi au mfanyakazi serikalini unaweza kuwekeza fedha zako kwenye mifuko ya uwekezaji ya pamoja(UTT), masoko ya hisa, Ununuzi wa dhamana za serikali(hati fungani), Kufungua akaunti ya akiba benki, Kuanzisha biashara yeyote, uwekezaji kwenye ardhi na majengo nk.

Ikiwa wewe unaingiza kipato chako kupitia shughuli za biashara unaweza pia kutumia kipato chako hicho cha ziada kuwekeza zaidi kwenye biashara unazozifanya au kuwekeza katika miradi mbalimbali kama tulivyoona kwa waajiriwa hapo juu. Ni kwa njia ya uwekezaji pekee ndio utakaokuwezesha wewe kupata uhuru kamili wa kifedha katika maisha yako na si vinginevyo.

7. Ukikopa tumia busara.

Uwezo wako wa kuaminika na kukopesheka utategemea sana historia yako ya ukopaji na ulipaji madeni siku za nyuma. Huathiri pia moja kwa moja fursa yako ya kuja kupata mkopo kwa ajili ya biashara zako siku za baadae. Hivyo unapokopa mahali popote pale hata iwe ni kwa mtu binafsi licha ya benki au taasisi nyingine za fedha, hakikisha unalipa kwa wakati na kwa uaminifu mkubwa.

8. Weka mapema lengo la kumiliki ardhi na makazi.

Moja ya ndoto muhimu zaidi ya binadamu yeyote katika maisha yake ni kuwa na kwake kwa maana ya kumiliki kiwanja na hatimaye kujenga nyumba yake mwenyewe ya kuishi na familia yake. Rasilimali hii ni muhimu mno siyo tu kwa ajili ya kuishi bali pia itaweza kuwa kama dhamana pale utakapohitaji kukopa mkopo kwa ajili ya kuongezea mtaji wa biashara zako au mkopo kwa ajli ya malengo mengine yeyote yale ya kimaisha.

9. Usijinyime kupita kiasi, jipongeze kidogo!

Kosa moja kubwa watu wengi wanalofanya pindi wanapotekeleza bajeti walizojiwekea ni kujinyima kupindukia, kumbuka binadamu sisi utashi wetu una ukomo, tunaweza tu kuhimili kiasi fulani cha majaribu kabla hatujakata tamaa.

SOMA: Saikolojia ya umasikini: Sababu 9 kwanini hupati pesa za kutosha

Tafiti zimethibitisha kwamba ikiwa mtu atajinyima mfululizo kitu akipendacho mwishowe atashindwa kabisa kuhimili na kujikuta anafanya kosa la kurudi nyuma kulekule alikotokea mwanzoni. Dawa ya tatizo hili ni kujipa zawadi au kujipongeza kidogo pale unapofanikiwa kupiga hatua fulani katika malengo yako mfano hata kujipongeza kwa kinywaji murua, safari/picnic au mlo mzuri baada ya kufikia lengo fulani dogo miongoni mwa malengo yako makubwa.

10. Katu usiache kujifunza elimu ya fedha kila siku

Ulimwengu wa pesa ni tata na hubadilika kila siku lakini kitu cha kustaajabisha ni kuwa pesa ina umuhimu mkubwa katika maisha ya kila binadamu na kama nilivyotangulia kusema pale mwanzoni ya kwamba, mtu hauhitaji kuwa na shahada, stashahada au astashahada kutoka katika chuo cha elimu ya usimamizi wa fedha ndipo uweze kujua jinsi ya kutengeneza pesa, kuzitunza na kuzisimamia ziwe nyingi mpaka kukufikisha kwenye uhuru kamili wa kifedha. Lakini unahitaji kujifunza angalao elimu ya msingi ya fedha kupitia majukwaa mbalimbali mitandaoni na nje ya mtandao. Mfano mzuri kabisa ni jukwaa letu la MICHANGANUO-ONLINE SUPER-MASTERMIND GROUP-2022

 

……………………………………….

 

Mpaka kufikia hapo, mpenzi msomaji wa somo hili la JINSI YA KUSIMAMIA, KUTUNZA NA KUTUMIA VIZURI PESA ZAKO BINAFSI & ZILE ZA BIASHARA YAKO ndio tumemaliza sehemu ya kwanza iliyohusu Usimamizi mzuri wa fedha binafsi. Kesho tutaendelea na sehemu ya pili na tutaangazia zaidi juu ya utunzaji na usimamizi mzuri wa fedha za biashara. Usikose kujua kuna tofauti gani kati ya usimamizi wa fedha kwenye ‘nafsi’ hizi mbili yaani, BIASHARA NA MMILIKI WAKE.

 ..............................

Masomo haya pia yanaendelea katika MASTERMIND GROUP  MICHANGANUO-ONLINE-2022. mahali pekee panapopatikana masomo ya fedha yasiyopatikana mahali kwingine kokote.


……………………..

Pia Vitabu vyetu vyote hapo chini vinapatikana na ukiwa popote pale nchini Tanzania au nje tunakufikishia ulipo kwa uaminifu mkubwa. 

Mawasiliano yetu: 0765553030 au 0712202244






Bonyeza hapa chini kusoma sehemu ya pili ya somo hili; 










0 Response to "BAJETI: JINSI YA KUSIMAMIA, KUTUNZA NA KUTUMIA VIZURI FEDHA BINAFSI NA ZA BIASHARA YAKO (KANUNI 80/20)"

Post a Comment