BIASHARA YENYE MTAJI MDOGO ISIYOJULIKANA NA WATU WENGI BADO-1 | JIFUNZE UJASIRIAMALI

BIASHARA YENYE MTAJI MDOGO ISIYOJULIKANA NA WATU WENGI BADO-1

BIASHARA ZILIZOSAHAULIKA
Mpenzi msomaji wa blogu ya jifunzeujasiriamali, blogu yako imeanzisha kipengele kidogo kitakachokuwa na mfululizo wa zile aina za biashara ndogondogo ambazo tumezoea kuziona watu wakizifanya mitaani lakini mara nyingi hatuzitilii maanani, tunadhani ni biashara ambazo hazilipi au za watu wasiokuwa na mitaji, kumbe tunasahau ya kwamba ni biashara kama zilivyokuwa biashara zingine zozote zile na huwaingizia faida ya kutosha tu wale wanaoamua kuzifanya kwa malengo.

Unaweza ukakaa mahali huna cha kufanya kutokana na kukosa pengine mtaji ama uao mtaji lakini ni kidogo sana na unahofia ikiwa kama utaamua kuanzisha biashara kubwa kidogo au hata ya kati basi mtaji wote utaishia hapohapo. Nataka nikutie moya kwamba unapojikuta kwa bahati mbaya ukiwa katika hali kama hiyo, usikate tamaa bali angalia ni biashara gani ndogo kabisa unayoweza ukaianzisha kwa mtaji kidogo kabisa uliokuwa nao, haishindikani, na wala hamna kitu kisichouzika ilimradi tu, umeangalia katika mazingira yako ni kitu gani wateja wanachohitaji kweli.


Ondoa aibu kwani yule utakayemuoonea aibu hata ukimfuata kumuomba akupe mia mbili  ununulie kipande cha mhogo wa kukaanga atakuona mtu wa ajabu. Kwa leo biashara ndogo ya mtaji kidogo niliyokuandalia si nyingine bali ni hii hapa chini;

Biashara ya kuuza supu.
Biashara ya supu inaonekana kuwa ni biashara ya kawaida sana miongoni mwa biashara zinazofanyika katika mitaa yetu kila siku hasa hasa mijini lakini biashara hii siri yake kubwa ni kwamba haihitaji uwekezaji wa mtaji mkubwa sana kusudi mtu aweze kuanza, siri nyingine kubwa katika biashara hii ni kwamba supu safi, halali na nzuri hupendwa sana na watu wa kada mbalimbali, haijalishi mtu ni wa dini gani au kabila, karibu kila mtu anapenda supu hasahasa nyakati za asubuhi au jioni.

Ni biashara endelevu kwani mtu anapokunywa supu leo na kukuta ina ladha nzuri ya kupendeza na kesho yake atakuja tena na tena na hivyo kukupa faida endelevu. Siri kubwa ya kuvuta wateja kwenye biashara ya supu ni USAFI katika vyombo, eneo lenyewe la biashara na mhusika anayewahudumia wateja.

Mtaji wa biashara ya kuuza supu.
Unaju ni kwanini nimetangulia kusema biashara ya supu haihitaji mtaji mkubwa? Hapa sasa nitaenda kukufafanulia. Ili biashara nzuri ya supu iweze kukamilika vinahitaika vitu hivi vitatu;

1)  Eneo au mahali pa kuuzia supu
2)  Vifaa kama vile jiko, sufuria, sahani, bakuli, kisu na vijiko.
3)  Nyama na viungo vyake kama pilipili, ndimu, tangawizi, nk.

Ukitazama vitu hivi vikuu vitatu ambavyo ndiyo mahitaji yetu makubwa kwa ajili ya kufungua biashara ya kuuza supu ni mahitaji ambayo bila shaka yeyote ile kama mtu utaamua kikamilifu hayawezi kukushinda. Ni kweli kabisa hata mimi nafahamu kuanzisha biashara yeyote ile hata ikiwa mtaji ni mdogo kiasi gani lakini kama hauna pesa yeyote mfukoni hata ungeambiwa zinahitajika shilingi elfu tano tu, inakuwa
mtihani.


Kwa hiyo pamoja na kusema kwamba ni biashara isiyohitaji mtaji mkubwa bado kulingana na mazingira ya mtu mwingine anaweza kuona bado mtaji kwake ni changamoto kubwa. Kwa hiyo nasema ni biashara isiyohitaji mtaji mkubwa ukilinganisha ba biashara nyingine nyingi ndogondogo.

Eneo.
Eneo kwa ajili ya kuuzia supu, halina usumbufu mkubwa sana kupatikana kutokana na biashara yenyewe kuwa ni ya muda mchache maalumu. Supu inaweza ikauzwa kwa wastani wa masaa mawili mpaka matatu tangu kuiva hivyo eneo litakalotumika linaweza likawa siyo la kudumu kama vile barazani, stendi ya magari, mbele ya duka kabla wenyewe hawajafungua au baada ya kufunga nk. Hivyo unaweza kuona ni kwa namna gani biashara hii inaweza ikawa na urahisi katika sula zima la eneo la kuuzia.

Vifaa mbalimbali.
Sufuria kubwa la kuchemshia supu, jiko la mkaa au kuni, kisu, bakuli kadhaa na sahani zake, vijiko, meza pamoja na viti au benchi ndiyo vifaa muhimu zaidi vitakavyohitajika. Hapa kidogo panaweza pakawa na gharama lakini itategemea, wakati mwingine mtu unaweza hata kuazima vyombo vyako mwenyewe kutoka nyumbani ukavitumia mpaka pale mambo yatakapokuwa “super” basi ukanunua vya biashara.

Nyama na viungo vyake.
Nyama yaweza kuwa ni ya ng’ombe, kuku, mbuzi, au hata samaki, ngisi na pweza. Vilevile supu inaweza ikawa ni ya nyama ya kawaida, supu ya kongoro au makongoro ambayo hujumuisha miguu ya mbuzi au ng’ombe na baadhi ya sehemu za kichwani. Inaweza pia ikawa ni supu ya utumbo na nyama zinazopatikana ndani ya mnyama kama vile, mapafu, figo na firigisi hasa kwa supu ya kuku wa kienyeji na wale wa kisasa.


Viungo mbalimbali vinavyoambatana na supu itategemea na mtayarishaji mwenyewe ataamua kuweka viungo gani. Wengine huweka tangawizi na vitunguu, wengine karoti, pilipili hoho, kuna wengine pia hawaweki chochote zaidi ya chumvi na mteja hujiwekea mwenyewe kwenye bakuli viungo vingine kama vile ndimu na pilipili.

Mtaji wa kununulia vitu hivi siyo mkubwa sana ukilinganisha na ununuzi wa bidhaa au malighafi katika biashara nyingine, na uzuri wake ni kwamba biashara ya supu ni biashara inayofanyika na kuisha siku moja hiyohiyo, unafahamu umepata fedha kiasi gani, unatenga kabisa pesa kwa ajili ya kwenda kununulia malighafi kwa ajili ya siku inayofuata na faida pembeni. Hata kama unakopa mtaji wa mtu kwa maana ya fedha taslimu au vifaa, inakuwa rahisi sana jioni kumrudishia fedha zake zote ukabaki na faida yako mkononi.

Kwa kawaida supu huendana na vitafunwa hasa chapati, lakini pia vitafunio vingine huweza kutumika kama vile mandazi, mikate, skonzi, mihogo, viazi, mkate wa kumimina, kababu, kachori nk. Vitafunwa hivi kama huwezi kuviandaa mwenyewe unaweza ukamtafuta mtu atakayehakikisha kila siku vinapatikana na katika ubora wa hali ya juu.

Utamu wa supu ya kuku wa kienyeji!
Hakuna mtu yeyote yule labda awe “vegetarian” asiyeujua utamu wa supu ya kuku wa kienyeji, ukipata eneo zuri la biashara hasa hasa stendi ya mabasi au daladala ukaanza biashara  polepole na watu wakakuzoea, unaweza ukapata faida nzuri, kubwa na ya uhakika ndani ya kipindi kifupi sana.

Supu ya pweza na ngisi.
Jijini Dar es salaam katika mitaa mbalimbali hasa nyakati za jioni supu hizi ni maarufu sana, pweza na ngisi hupatikana feri na waauzaji wa supu hii huhitaji mtaji kwa ajili ya kununulia pweza wenyewe na ngisi tu, huweka kijimeza kidogo na bakuli kadhaa, kisha wateja humiminika kuja kula ngisi na pweza, wachache hupenda kunywa na supu yake ambayo huwekewa katika vibakuli vidogo. 

utamu wa supu ya pweza na ngisi
Pembeni utakuta wanaweka pilipili iliyoungwa vizuri na wakati mwingine kachori au kababu Ukitaka upate wateja wengi na wa uhakika kila siku kuwa mbunifu katika suala la usafi kwani watu wengi supu hii wanaipenda sana lakini huogopa mazingira ya uchafu na kushea vyombo.


Usimamizi mzuri wa biashara ya supu.
Kama nilivyotangulia kusema hapo awali kwamba biashara ya kuuza supu iwe ni ya kuku, ngombe, mbuzi, bata, samaki, ngisi, pweza au hata sungura, mara nyingi sana hufanyika masaa machache  aidha ya asubuhi au ya jioni. Ikiwa utaamua kumuachia majukumu msaidizi katika biashara hii au utaamua kufungua maeneo zaidi kwa ajili ya kuuza supu tuseme labda mtaji umekua ukaamua uwe na ‘goli’ Tabata, Mbezi, Kariakoo, Mwenge na lingine labda Manzese, basi huna budi kuajiri wasaidizi.

Uzuri uliopo katika biashara hii ni kwamba bidhaa yake inaweza kupimika na ukafahamu ndani ya siku hiyo moja yamepatikana mauzo kiasi gani. Unaweza kumuachia msaidizi idadi ya kilo za nyama unayojua ikimalizika hutoa kiasi gani cha fedha au hata mkahesabiana idadi ya vipande vya nyama ni vingapi ili muda wa kufunga hesabu kusijekuwa na sintofahamu.

Halikadhalika na vitafunwa navyo idadi yake hujulikana kirahisi hivyo kuifanya biashara hii ya kuuza supu kuwa ni biashara nzuri sana katika upande wa usimamiaji. Mapato yako hayawezi yakapotea kiurahisi.

Hitimisho.
Ndugu msomaji wa makala hii, tutaendelea kukuletea biashara hizi zilizosahaulika au zinazochukuliwa ‘poa’ na watu wengi wakati zina uwezo mkubwa wa kumtoa kimaisha mtu yeyote yule anayeamua kuzifanya kwa nia. Wakati ukisema ni biashara kichaa, wapo “wanaopiga hela si mchezo”.

Kama utapenda kujifunza zaidi biashara na ujasiriamali kwa kina kabisa, usisite kupata moja ya  vitabu vyetu hivi hapa chini,

Vitabu vyote 3 kwa pamoja ni shilingi 18,000/=


Kwa vitabu zaidi katika lugha ya kiswahili tembelea, SMARTBOOKS TANZANIA


Business Planning
Tunaandika Mpango wowote ule wa Biashara(Business plan) kwa mahitaji yeyote, benki, wabia, wawekezaji au hata kuendeshea tu biashara yako kwa ufanisi mkubwa zaidi. 

Ikiwa pia unapenda kuandika mwenyewe tunaweza kukupatia course nzima, templates na samples za michanganuo ya kiswahili na kiingereza vitakavyokusaidia kuandika kwa wepesi

Wasiliana na sisi kwa namba zifuatazo;

Whatsapp/call: 0765553030
SMS/Call:      0712202244 

11 Responses to "BIASHARA YENYE MTAJI MDOGO ISIYOJULIKANA NA WATU WENGI BADO-1"