AINA ZA BIDHAA ZA DUKA ZENYE FAIDA NDOGO LAKINI HUTOKA HARAKA HARAKA | JIFUNZE UJASIRIAMALI

AINA ZA BIDHAA ZA DUKA ZENYE FAIDA NDOGO LAKINI HUTOKA HARAKA HARAKA

Duka la rejareja au duka la vyakula, mara nyingi aina ya maduka haya huwa tunayaona huko mitaani, huwezi ukatembea hatua 20 mpaka 30 pasipo kukutana nalo hata moja. Bidhaa utakazokutana nazo huko mara nyingi ni zile ambazo zinahitajika katika matumizi ya binadamu ya kila siku kuanzia vyakula mpaka dawa za maumivu kama panado na asprin.(mahitaji ya msingi kabisa ya binadamu)


Zipo bidhaa ambazo mteja yeyote anapokwenda katika duka la rejareja hutegemea kwa asilimia kubwa kuzikuta na anapofika dukani na kukuta vitu hivyo havipo basi hukata tamaa hata ya kurudi tena katika duka hilo siku nyingine. Na kwa bahati mbaya bidhaa nyingi za namna hiyo utakuta faida yake siyo kubwa sana katika kila bidhaa moja unayouza. “low gross profit goods”.  

Kwa upande mwingine wa shilingi, uzuri wa bidhaa za namna hiyo ni kwamba hutoka haraka haraka sana(high turn over ). Faida ghafi tunayoizungumzia hapa ni ile baada ya kuchukua bei ya bidhaa uliyonunulia na kutoa bei ya kuuzia. Kwa mfano umenunua sukari kilo moja shilingi 2,000/= na kwenda kuiuza shilingi 2,400/= kwa kilo, faida ghafi yake hapo ni shilingi 400 katika kilo moja ya sukari.

Kama mmiliki wa duka au muuza duka la rejareja unatakiwa uzifahamu bidhaa  hizo na hata ikiwezekana uhakikishe hazikosekani dukani kwako hata siku moja, Zipo bidhaa ambazo kutokana na eneo na mazingia ya eneo husika bidhaa za namna fulani hutoka harakaharaka lakini pia kuna bidhaa zingine, zenyewe bila kujali eneo wala mazingira mahitaji yale popote pale ni muhimu mno kwa binadamu kiasi kwamba zinauzika chap chap ijapokuwa faida yake siyo kubwa sana.

Kwanini bidhaa zinazotoka haraka haraka lakini zilizokuwa na faida kidogo ni nzuri kwenye duka lako?

Kuna ule usemi usemao, “kidogo dogo hujaza kibaba” na “bandu bandu hatimaye humaliza gogo” misemo hii naihusisha na dhana hii kwa mantiki kwamba, ile faida unayo iona kidogo kidogo lakini unaipata kila baada ya muda mfupi inao uwezo mkubwa wa kujilimbikiza na kuwa kubwa kwa haraka kiasi cha kushangaza.


Duka lako unahitaji wateja wanaojirudia tena na tena kusudi uweze kufanya biashara endelevu, hivyo unapokuwa na bidhaa hata zile zilizokuwa na faida kidogo lakini wateja wanazotaka, unawafanya wateja wasikauke katika duka lako hata siku moja na wanapokuwa wanaridhika zaidi na huduma zako ndipo huwavuta na wateja wengine wenye mahitaji kama ya kwao nao kuja dukani kwako kukuunga mkono.

Aina za bidhaa zenye faida kidogo dukani kwako lakini zinazotoka upesi upesi na hivyo kukuingizia faida ‘fasta fasta’(haraka haraka)

Bidhaa zenyewe zilizokuwa na uwezo wa kuuzika haraka haraka ijapokuwa faida ghafi yake siyo kubwa sana ni hizi hapa;

v Vocha za simu za mkononi
v Sukari
v Chumvi,
v Unga wa sembe
v Maharage
v Majani ya chai,
v Unga wa ngano
v Kiberiti
v Dona
v Mafuta ya kula
v Majani ya chai
v Dawa za mswaki
v Sabuni ya mche
v Sabuni za vipande
v Sabuni za kuogea
v Sabuni ya kufulia
v Sabuni ya unga
v Vitu vya kutafuna watoto kama vile, pipi, karanga, biskuti, chama, bazoka, big ghee, peremende, ubuyu, bublish, nk.
v Mafutaya taa na
v Soda.

Kama nilivyotangulia kusema, kulingana na mazingira ya eneo lilipo duka lako la rejareja, bidhaa zinazotoka haraka lakini faida yake kidogo zinaweza kuwa tofauti na hizi au zaidi ya hizi lakini hapa nimejaribu kutaja tu zile ambazo ndiyo mara nyingi hukuta karibu kila eneo iwe ni kijijini ama mjini basi utakuta ndizo zinazoongoza kwa kuwa na mahitaji makubwa sana na ya kila wakati hivyo faida yake kufanywa kuwa kidogo sana kwa kila kipimo cha bidhaa moja inayouzwa.


Kama hujui unaweza ukazidharau bidhaa za namna hiyo na kujisemea, “niweke za nini, zinanimalizia nafasi ya bure tu, bidhaa zenyewe kwanza faida yake ni kidogo kama nini” Kumbe hujui nguvu yake ni nini katika kasi ya kutoka. Ili mradi kitu kinahitajika na wateja wewe wawekee hata kama faida yake siyo kubwa sana, kuna faida nyingi utakazozipata kama nilivyokwisha kueleza katika aya zilizopita.

Kwa leo naona niishie hapa, ila nakuahidi kukuletea makala za mara kwa mara kuhusiana na jinsi ya kuboresha biashara yako ya duka hususani kama ni la rejareja pamoja na biashara nyingine zozote zile za rejareja, kwani biashara za rejareja kanuni yake ni ile ile, uwe unauza nyanya, vifaa vya ujenzi, chakula au supermarket.

Usisahau siri kubwa katika biashara hii ni mahusiano yako mazuri na wateja ambayo huhusisha vipengele vingi, Hivi unafahamu hata kitendo cha kumwambia mteja, sina chenchi katafute, ni kosa kubwa?


Asante, ila kama unahitaji mbinu hizi kwa ukamilifu zaidi ujifunze umetulia, basi nakushauri ununue kitabu cha, MAFANIKIO YA BIASHARA: DUKA LA REJAREJA, bei yake ni Tsh. 10,000/= kitabu halisi cha karatasi na Shilingi 5,000/= softcopy kwa email. Tupo MBEZI KWA MSUGURI stendi ya daladala, au tuwasiliane kwa simu: 0712 202244  au 0765 553030

BUSINESS PLANS / MICHANGANUO YA BIASHARA

Karibu, tunatoa huduma ya kuandika mpango wa biashara yeyote ile unayotaka kwa ajili ya mahitaji mbalimbali kama vile kuombea mkopo, kuwasilisha kwa wabia, wawekezaji au kwa ajili tu ya uendeshaji wa biashara yako. Bei zetu ni nafuu sana, unachagua mwenyewe lugha ya kuandikia kati ya kiswahili na kiingereza.

Vilevile tunatoa mafunzo(course) nzima ya jinsi ya kuandika mpango wa biashara yeyote ile. Package nzima ya mafunzo hayo ni pamoja na vitabu 2 cha kiingereza na cha kiswahili, templates au vielezo, Samples au Michanganuo kamili katika lugha ya kiingereza na kiswahili pamoja na semina mbalimbali kuhusu uandishi wa michanganuo ya biashara.

Kupata moja kati ya huduma hizi wasiliana na sisi kwa namba;
whatsapp/simu:  0765553030
SMS/Simu:          0712202244

2 Responses to "AINA ZA BIDHAA ZA DUKA ZENYE FAIDA NDOGO LAKINI HUTOKA HARAKA HARAKA"