BIASHARA YA SODA MAJI JUISI NA SIGARA: TUMIA SIRI HII KUONGEZA MAUZO × 2 | JIFUNZE UJASIRIAMALI

BIASHARA YA SODA MAJI JUISI NA SIGARA: TUMIA SIRI HII KUONGEZA MAUZO × 2

BIASHARA YA SODA, MAJI, JUISI, SABUNI NA SIGARA
Nimekuwa nikifanya biashara ya kuuza bidhaa rejareja kwa muda mrefu sasa na kuna vitu kadhaa nilivyogundua kutoka kwa wateja wa bidhaa hizo ambavyo pengine hata wazalishaji wa bidhaa zenyewe au wenye viwanda na makampuni ya uzalishaji bado hawajavifahamu. Na isitoshe hata wanapofanya utafiti wa soko la bidhaa zao mitaani hawajisumbui kuwauliza vitu hivyo wauzaji wa maduka ya rejareja au wamiliki wa biashara zinazouza bidhaa zao. Hawajui kama wanafahamu siri nyingi sana za kufanikiwa au kuanguka kwa mauzo ya bidhaa wanazozizalisha.

Muuzaji wa duka au yeyote yule anayefanya biashara ya kuuza bidhaa rejareja, bidhaa kama vile, maji ya chupa, juisi za matunda na zile za kawaida, sigara na hata sabuni, unapofahamu siri hizo na ukazitumia kikamilifu utakuta ukizidisha mauzo yako mara dufu au hata zaidi ya ulivyokuwa ukiuza hapo awali.

SOMA: Hakuna biuashara isiyokuwa na faida.

Sababu ni kwanini wateja huamua kupenda bidhaa ya kampuni fulani dhidi ya kampuni nyingine.
Utakuta bidhaa fulani kwa mfano maji ya kunywa, yanazalishwa na makampuni tofauti A, B na C, lakini jambo la ajabu wateja wanapofika dukani kununua maji hutaka wapewe maji aina A tu  huku B na C yakitoka kwa uchache. Ukiangalia aina zote za maji wala hazitofautiani kiubora na ujazo ni uleule, kama ni chumvi, maji yote, A, B na C hayana nk.

Zipo sababu nyingi kwanini wateja huamua kuchagua kununua bidhaa ama huduma za kampuni fulani dhidi ya nyingine lakini sababu ambayo mimi nitajikita nayo zaidi hapa leo ni Mtazamo wa wateja(customer Perception). Mtazamo ni kitu kikubwa sana kwa mteja kuchagua kununua bidhaa ya kiwanda fulani. Na mtazamo wa mteja juu ya bidhaa  unategemea vigezo vingi kama vile, kifungashio, bei, matangazo nk.

Nitatoa mifano kadhaa, ambayo sitayataja moja wa moja majina ya bidhaa husika au makampuni, bali nitatumia tu herufi A, B na C

1. MAJI.
Wateja wanaweza wakawa wanayapenda maji ya kampuni fulani kwa sababu tu ya mtazamo wao katika chupa yalimowekwa. Sababu inaweza ikawa ni umbile la chupa, rangi ya chupa, au ukubwa/ujazo. Kwa mfano niliwahi kushuhudia kampuni moja(tuiite A) wakati fulani maji yake wateja walikuwa wakiyapenda  na yalikuwa yakiuzwa kwa wingi sana. Lakini ilifika kipindi kampuni ikabadilisha rangi ya chupa zake. Kila mteja aliyefika dukani kununua maji akawa anauliza, “Ni rangi gani hii waliyotuwekea? Maji hayapaswi kuwa na rangi bwana”

SOMA: Hatua 10 za kuanzisha biashara ya rejareja.

Wateja zamani walizoea chupa nyeupe inayoonyesha maji kama yalivyo(clear). Lakini sasa rangi ya chupa waliyoweka ilikuwa inayafanya maji yaonekane kana kwamba yametiwa rangi au dawa fulani vile. Nilishangaa kuona wateja karibu wote wa maji wakihamia kupenda maji ya kampuni nyingine B ambayo chupa zake hazikuwa na rangi, zilikuwa ‘clear’. Sijui kwa maeneo mengine lakini eneo lile zima nilipokuwa na biashara hata na maduka ya jirani walisikika wakilalamika juu ya kampuni ile kubadilisha rangi ya chupa zake za maji.

Kampuni hii A, hata kama ikiwa nia yake kubwa ilikuwa ni kujihuisha upya “rebranding” basi pengine ingeliweza kusuluhisha sintofahamu hii kwa wateja wake, kwa kuendelea kuzalisha maji ndani ya chupa zote mbili yaani ile ya zamani isiyokuwa na rangi sambamba na hii mpya yenye rangi, na kisha kutathmini taratibu jinsi mwenendo wa uitikiaji wa wateja wao unavyotokea.

2. SODA
Utawasikia wateja wengi wakikuambia, “Nataka chupa ya zamani” au wengine, “Nipe chupa mpya” na unapowauliza tofauti ya soda iliyokuwepo ndani ya chupa ya zamani na chupa mpya ni ipi, wengine watakuambia, ya “zamani haina sukari sana” au wengine pia hudai, “ina sukari zaidi” na wengine, “ladha zake ni tofauti”. Basi ilimradi hakuna atakayekupa jibu halisi la kitaalamu la ni kwa nini atake ‘soda ya zamani na siyo mpya’.

SOMA: Mbinu 7 za kutumia ikiwa unatembeza bidhaa za jumla maduka ya rejareja.

Kimsingi soda za kiwanda tuseme labda A, hutengenezwa sehemu moja na wala hakuna ya zamani wala mpya isipokuwa tu ni yale matoleo ya chupa ndipo watu huona kama kuna soda ya zamani na soda mpya. Na hii hutokana na chupa hasa hasa zile za kioo kuwa zinarudishwa tena kiwandani, kuoshwa na kujazwa soda upya tena na tena. Kwa hiyo hapa ni swala la mtazamo zaidi “perception” , kuwa ile chupa ya zamani au mpya ndiyo bora zaidi. Pengine kampuni za soda ingelifaa zijue ni kwanini wateja huchagua chupa za zamani kuliko mpya, au vinginevyo basi wanapobadilisha waondoe kabisa zile za zamani au kutoa mpya lakini zilizokuwa na sura ileile kama za zamani, na hilo litaondoa mkanganyiko unaokuwepo.

3. SIGARA
Kuna wakati kampuni A ya sigara iliweka mstari fulani kwenye paketi zake wateja wakaja juu sana hata wengine wakadiriki kususa na kuhamia sigara za kampuni B. Sababu kubwa waliyokuwa wakiitoa wateja ni kuwa, sigara mpya za paketi iliyokuwa na mstari zilikuwa zimeongezewa ukali zaidi. Nilipochunguza nikabaini wala hakukuwa na mabadiliko yeyote ya ladha bali tu kampuni ilitaka kuzitofautisha paketi za sigara zinazouzwa nje ya nchi na zile zinazouzwa hapa nchini.

Ilifikia hatua hata wateja wa sigara aina X wakahamia sigara aina Y ambayo bado paketi zake zilikuwa hazijaanza kuwekewa mistari ijapokuwa ni sigara za kampuni moja hiyohiyo A wakilalamika aina X ni kali kupindukia.  Kiuhalisia sigara haikuwa imeongezewa ukali wala kubadilishwa ladha bali ni kutokana tu na mtazamo wa akili za wateja bada ya kuona ule mstari wakajenga picha kuwa na ladha nayo ilikuwa imebadilishwa.

4. JUISI
Kampuni A inayotengeneza juisi za matunda, zamani chupa zake za juisi zilikuwa na mdomo mwembamba. Wakati fulani walianza kutengeneza chupa za juisi zilizokuwa na midomo mipana zaidi. Hata hivyo kampuni hii iliendelea kuzalishaa juisi zenye chupa za aina zote mbili, midomo mikubwa na midogo.

Nilichogundua ni kwamba, wateja walianza kupenda zaidi zile juisi zilizokuwa na mifuniko mipana na ikawa sasa kila mteja aliyefika dukani ukimpatia juisi ya mfuniko mwembamba, mteja huyo anakuwa radhi kukuambia anakwenda duka jingine. Kumbuka ubora na ladha ya juisi vilikuwa ni vilevile hakukuwa na kitu kilichobadilishwa isipokuwa upana wa mzunguko wa mdomo wa chupa peke yake.

5. SABUNI.
Kampuni A inayozalisha sabuni za miche ilikuwa vifungashio vya sabuni zake ni maboksi tu peke yake na miche yenyewe ya sabuni ilikuwa ikipangwa ndani ya boksi ikiwa ‘uchi’. Kampuni nyingine ya sabuni B, yenyewe ilianza kuvalisha miche yake karatasi ya nailoni kwanza kabla ya kuipanga ndani ya maboksi.

Nilichogundua ni kuwa wateja walianza kuonyesha mapenzi zaidi kwa sabuni za miche zilizokuwa zikizalishwa na kampuni B ambazo zilikuwa zikivalishwa karatasi nyembamba ya nailoni kuliko sabuni za kampuni A zilizokuwa zikiwekwa ndani ya maboksi yake zikiwa uchi. Lakini hapo pamoja na mtazamo pia kuna kuongeza dhamani  kwa sabuni  za kwenye nailoni za kampuni B kwani ile nailoni husaidia sabuni kutokupoteza unyevu na kubadilika kuwa ngumu.

HITIMISHO
Kwa wauzaji na wamiliki wa biashara za rejareja kama vile, maduka ya vyakula/rejareja, vioski, ‘super markets’, magenge na hata wauzaji bidhaa wanaopanga barabarani, kigezo hiki cha mtazamo wa mteja/wateja juu ya bidhaa au huduma wanazonunua kutoka kwenu ni kitu cha kutilia maanani sana.

Unapofahamu mitazamo ya wateja wako, ni fursa nzuri sana kwako ya kuongeza mauzo zaidi ya bidhaa na huduma zako. Kwa mfano baada ya kujua  wateja wako wengi wanapendelea maji ya kampuni A zaidi, kutokana na muonekano wa chupa, rangi au chochote kile, basi huna budi kuhakikisha maji A hayakosekani dukani kwako au kwenye biashara yako. Halikadhalika ni hivyo hivyo kwa bidhaa na huduma nyinginezo.

SOMA: Chuma ulete anavyowanyanyasa wenye maduka Dar.

Kwa makampuni yanayotengeneza bidhaa za viwandani, kama maji, sigara, juisi, sabuni, vyakula, pombe nk. Wanatakiwa kujua kwa uhakika ni nini mitazamo ya wateja wa bidhaa zao hasa hasa wale wa mwisho(walaji). Wataepuka kutengeneza bidhaa zisizotoka. Wafanye utafiti na kuheshimu matokeo ya majibu ya utafiti  wanaofanya.

…………………………………………………………………………
Ndugu msomaji, endelea kupata elimu ya Ujasiriamali hapa katika Blogu hii bila kukosa kila siku na Utakapohitaji msaada zaidi ili uweze kufahamu kwa kina zaidi maswala mbalimbali yahusuyo Ujasiriamali na biashara katika hatua ya juu kabisa basi usisite kujipatia vitabu vyetu mbalimbali hapa SMARTBOOKSTZ.

Vitabu vya Self Help Books ni tofauti sana na vitabu vingine vya kawaida kwani vinatoa mafunzo ya kina ya jinsi ya kuanzisha na kuendeleza biashara kivitendo zaidi kuliko nadharia, unasoma kitu ambacho moja kwa moja unakwenda kukitumia katika biashara yako, Kitabu kwa mfano cha “Michanganuo ya Biashara na Ujasiriamali” chenye kurasa 410, kina kila kitu ambacho mjasiriamali anahitaji kuweza kuanzisha na kufanikiwa katika biashara yeyote ile.

Uzuri sasa vitabu vyote kutoka SELF HELP BOOKS unaweza ukavinunua kupitia mtandaoni na malipo ukafanya kwa Mpesa, Tigopesa au mitandao mingine. Tunakutumia kitabupepe(softcopy) kupitia E-MAIL au TELEGRAM @petertarimo. Unatutumia e-mail yako au namba ya simu unayotumia kwa telegram katika namba za simu, 0712 202244  au email: jifunzeujasiriamali@gmail.com

0 Response to "BIASHARA YA SODA MAJI JUISI NA SIGARA: TUMIA SIRI HII KUONGEZA MAUZO × 2"

Post a Comment