MBINU HIZI 2 ZA UENDESHAJI DUKA LA REJAREJA KWA MAFANIKIO HAZIPO MAHALI PENGINE POPOTE | JIFUNZE UJASIRIAMALI

MBINU HIZI 2 ZA UENDESHAJI DUKA LA REJAREJA KWA MAFANIKIO HAZIPO MAHALI PENGINE POPOTE

Biashara ya duka la rejareja inalipa tofauti na tetesi na imani potofu zilizoenea mitaani kwamba biashara hii hailipi, ni ngumu, inachosha na wala haiwezi kumtoa mtu katika umasikini na kumfanya aishi maisha bora yenye mafanikio. 

Ukimsikia mtu akikupa sababu hizo zisizokuwa na mashiko, mwambie hebu akachunguze vizuri mtu kama Mohammed Dewji CEO wa METL Group na tajiri kijana zaidi Afrika alianza na biashara gani au baba yake Mzee Gulam Dewji kabla mwanaye hajafanya mapinduzi makubwa katika kampuni yake alikuwa akifanya biashara gani?


Baada ya utangulizi huo kidogo naomba sasa nikakupe dondoo muhimu za leo ambazo siyo nyingi ni 2 tu lakini naamini kabisa kuwa ni moja kati ya mbinu ambazo ukizitumia vyema kamwe hautakaa useme eti biashara ya maduka ya vyakula mitaani maarufu kama maduka ya rejareja, hayawezi kumpa mtu mafanikio na utajiri katika maisha yake.

1. MTU SAHIHI WA KUKUUZIA DUKA LAKO(Shopkeeper)
Kama unapanga kufungua duka la rejareja, hakikisha kwanza una uhakika ni nani atakayeuza kwenye duka hilo. Kama ni wewe mwenyewe basi hamna shida kwani tayari kwa kuwa unao uchungu na mtaji uliowekeza pale utahakikisha mambo hayaendi mrama, hata hivyo kuwa ni wewe utakayeuza dukani mwenyewe isijekuwa ndiyo tikiti ya kutapanya mtaji, inakupasa uwe na nidhamu ya pesa ya hali ya juu kabisa kwani wengine huwa wabaya hata kushinda hata vile wangeweka mfanyakazi.

Kama utamuweka msaidizi, ambaye anaweza akawa ni mfanyakazi uliyemwajiri, ndugu wa karibu, mke au mme nk. basi hakikisha kunakuwa na vipimo au tuseme mnahesabiana mali kabisa na kuhakikisha kunakuwa na mfumo thabiti wa uwekaji na ukokotoaji kumbukumbu za mahesabu ambao utatumika kumwajibisha huyo msaidizi endapo mambo yataharibika pasipokuwa na sababu ya msingi. Hapa hasa ndipo penye kizungumkuti katika biashara nyingi za rejareja, ndipo mahali chuma ulete anapoibuka, ndipo unaposikia watu wakilalamika biashara ya duka ni kichaa nk.

Kwa bahati nzuri kwenye kitabu cha “SIRI YA MAFANIKIO: BIASHARA YA DUKA LA REJAREJA” nimeelezea kwa kina sana mifumo yote mikubwa mtu unayoweza kuitumia kwa ufanisi katika kuhakikisha kizungumkuti hiki hakikukuti wakati ukiendesha biashara yako ya duka hata ikiwa unaendesha maduka zaidi ya 6 kwa wkati mmoja.

2. MUDA MUAFAKA WA KUFUNGUA NA KUFUNGA DUKA LAKO.
Katika listi ya vitu vinavyochangia sana kufanikiwa au kufeli katika biashara ya duka la rejareja au dula la vyakula mtaani hii inashika namba mbili 2 baada ya mtu wa kukuuzia. Muda ni kigezo muhimu sana kwenye biashara ya duka. Hakikisha unafungua mapema na kufunga angalao baada  ya masaa 12 kulingana na vigezo vingine kama umbali kutoka unapoishi, usalama wa eneo nk.

Kwanini nakuambia hivyo? Biashara ya duka la rejareja faida ya bidhaa zake ni ndogondogo, na hivyo ili kuona faida kubwa inakupasa uuze vitu vidogovidogo vingi ambavyo faida nayo itajikusanya na kuwa kubwa. Sasa ili kuuza vitu vingi inabidi pia duka liwe wazi muda mwingi wa kutosha. Kwa mfano kuna watu maduka yao hufunguliwa saa 12 asubuhi na kufungwa saa 5 usiku. Mtu kama huyo huwezi kumlinganisha na yule anayefungua saa 3 asubuhi na kufunga saa 12 jioni, huyo wa kwanza atapata mafanikio makubwa zaidi na kwa muda mfupi.



Nakumbuka wakati fulani enzi za akina Makamba na Kandoro, nikiwa na kioski pale Msimbazi, kioski hakikuwa na mlango na nilikiendesha hivyohivyo bila mlango kwa takribani zaidi ya mwaka mmoja. Tulikuwa tukiita ‘kukomaa’ maana yake ni kwamba mtu unaanza asubuhi mpaka kesho yake tena asubuhi, lakini ilikuwa huwezi kufanya vile peke yako kwa muda mrefu ni lazima uwe na msaidizi ambaye mnapokezana. Nakumbuka nilikuja kuona umuhimu wa kuweka mlango kwenye kile kioski kipindi cha maandamano ya kesi ya Hamisi Rajab Dibagula iliyohusu mivutano ya kidini baada ya askari waliokuwa wakivurumisha mabomu ya machozi kunilazimisha nifunge kioski na mimi nikawa nababaika nifunge kwa kutumia nini.

Ukweli ni kwamba faida niliyokuwa nikiipata pale sidhani kama hata baadhi ya wenye maduka makubwa waliokuwa wakifunga saa 12 kama walikuwa wanaipata. Sishauri watu ‘kukomaa’ dizaini niliyokuwa nikifanya mimi kipindi hicho cha Yusuph Makamba hapana, kwanza ni kinyume cha sheria siku hizi ukikutwa unaweza ukafungiwa leseni yako au ukatupwa mahakama ya city, ila nataka tu kusisitiza umuhimu wa kufungua maduka muda wa kutosha.

…………………………………………………………………..

Usikose kuwa na mimi kila wakati hapa, nitaendelea kukuletea dondoo mbalimbali kwa kadri muda unavyokwenda kuhusiana na vile unavyoweza kutoka kupitia biashara ya duka. Lakini pia ikiwa utapenda kufahamu kwa kina ni kwa namna gani unavyoweza kuifanya biashara yako ya duka kwa mafanikio makubwa zaidi, basi jipatie kitabu nilichokuandalia cha SIRI YAMAFANIKIO: BIASHARA YA DUKA LA REJAREJA kwa bei ya shilingi elfu 10 tu. 

Ukiwa Dar es salaam utaletewa mpaka pale ulipo na Ukiwa Mkoani tunakutumia kwa basi au mwagize mtu anayekuja Dar akuchukulie. Pia unaweza ukakinunua kama softcopy PDF kupitia email yako kwa bei ya shilingi 5,000/= namba za simu ni 0712 202244  au  0765 553030  Jina ni Peter Augustino. Tarimo

Kuna semina pia inayohusu uandaaji wa mpango wa biashara yako na inafanyika kwa njia ya email sambamba na kwenye blogu maalumu ya uanachama, kwa maelezo zaidi ya semina hiyo fungua, SEMINA YA MICHANGANUO YABIASHARA NDANI YA TANZANIA ONLINE SCHOOL OF BUSINESS PLANNING.



1 Response to "MBINU HIZI 2 ZA UENDESHAJI DUKA LA REJAREJA KWA MAFANIKIO HAZIPO MAHALI PENGINE POPOTE"