JINSI MPANGO WA BIASHARA UNAVYOWEZA KUONGEZA MAFANIKIO YA BIASHARA YAKO | JIFUNZE UJASIRIAMALI

JINSI MPANGO WA BIASHARA UNAVYOWEZA KUONGEZA MAFANIKIO YA BIASHARA YAKO


Kumekuwa na mjadala mkubwa kuhusiana na ikiwa mpango wa biashara unaweza kusaidia katika mafanikio ya biashara au la, watu wengi kwa muda mrefu wamekuwa na dhana kwamba mchanganuo au mpango wa biashara ni kwa ajili ya kuombea pesa(mkopo) tu na baada ya hapo basi ni kuuweka kabatini uendelee kuliwa na wadudu.

Zipo sababu nyingi zinazoweza kuwafanya wajasiriamali wengi kutokuandika mpango wa biashara lakini iliyokuwa kubwa zaidi ni hii ya kufikiri kwamba, kuandika mpango wa biashara ni jukumu zito linalohitaji muda mwingi na utaalamu katika tasnia ya biashara na fedha. Lakini kumbe ni kinyume chake kabisa.

SOMA: SABA(5) KWANII UANDIKE MPANGO WA BIASHARA YAKO

Kwanza mpango wa biashara siyo kwa ajili ya kuombea fedha tu peke yake, isitoshe siyo kweli kwamba kuandika mpango wa biashara mtu anatakiwa kuwa amesomea masomo ya biashara ndipo aweze kuandika.

Kama unao uwezo wa kufikiria wazo la biashara, ukatafuta mtaji wa kuanzisha biashara yenyewe pamoja na kuiendesha, basi wewe tayari unao uwezo wa kuandika au kuandaa mpango wa biashara yako kuliko hata mtu mwenye digirii ya biashara. Kila siku, kila mahali duniani na karibu kila binadamu katika wakati fulani wa maisha yake ni lazima aandae mpango/mchanganuo wa biashara, penda asipende. Haiwezekani kabisa mtu ufanye biashara yeyote ile hata kama ni ya kuuza karanga mitaani pasipo kwanza kufanya mchanganuo wa biashara hiyo akilini kwako.

SOMA: Kwanini mpango wa biashara wa kuandikiwa siyo mzuri kwako?

Kitendo tu cha kujua utapata faida kiasi gani kwenye kilo moja ya karanga utakazokaanga, tayari hiyo ni hatua mojawapo ya mchanganuo wa biashara hiyo ya kuuza karanga. Sasa iweje useme huwezi kutengeneza mpango wa biashara? Siku hizi mambo yamerahisishwa mno siyo kama zamani, Mpango wa biashara wa kukuwezesha kuendesha biashara yako kwa ufanisi mkubwa siyo lazima tena uandike kurasa 20 au 50 kama unapeleka benki kuomba pesa. Lakini pia unaweza kuandika haikatazwi na ni faida zaidi ikiwa unaweza kufanya hivyo.

Pointi yangu hapa ni kwamba, ikiwa unaona uvivu kuandika mchanganuo wa biashara wenye kila kitu kama michanganuo iliyokuwepo katika kitabu cha MICHANGANUO YA BIASHARA NA UJASIRIAMALI, basi zipo njia fupi zinazoweza kukufanya ufurahie kufanya mchanganuo wa biashara yako pasipo kutumia muda mwingi wala utaalamu mkubwa sana.

Njia mojawapo mimi binafsi ninayoikubali sana, ni ya kujifunza namna ya kufanya michanganuo ya biashara. Ukishajua mbinu zinazotumika wakati wa kuandaa mpango wa biashara, hiyo ni nusu ya kuandika mpango wenyewe wa biashara kwani sasa unaweza tu kufanya biashara yako kwa kutegemea mpango unaouweka kichwani(akilini) mithili ya matajiri wa zamani ambao hawakuwa wamesoma hata darasa moja lakini ulikuwa huwezi kuwaeleza kitu chochote kwenye usimamizi na uendeshaji wa biashara zao.

Watu hawa ‘walimaster’ mbinu za kuendesha biashara zao kutokana na uzoefu tu walioupata na uwezo wao wa kufanya ufuatiliaji wa kila kitu wanachojipangia au kumpangia mtu kufanya katika kutimiza malengo yao ya biashara.

SOMA: Je, huna muda wa kutosha wa kuandika mpango wa biashara yako?

Njia nyingine maarufu sana siku hizi ni kutengeneza kitu kinachoitwa Mpango wa biashara Ukurasa mmoja. Hii ni aina ya mpango wa biashara ambao haihitaji muda mwingi kuandaa lakini vipengele vyote muhimu vya biashara hujumuishwa ndani. Mfano na Template ya namna ya kuandika mpango huo upo kwenye BLOGU YA MASOMO YA SEMINA YA MICHANGANUO ambayo kuingia humo mtu anatakiwa kulipia kiingilio au ada ya Sh. elfu 10.

Sasa basi ni kwa jinsi gani unavyoweza ukatumia mchanganuo au mpango wako wa biashara kuiendesha biashara yako ikakuletea mafanikio?

Hakuna mtu asiyefahamu kuwa kwenye biashara yale tunayoyapanga hayawezi kuja kuwa sawasawa na matokeo yenyewe halisi wakati wa kufanya biashara yenyewe halisi. Mambo mara nyingi huja kwenda tofauti. Lakini hauwezi ukasema kuwa mpango wa biashara hauna maana kwa sababu hata ikiwa hujafanya mpango rasmi wa biashara kama nilivyotangulia kusema hapo juu ni lazima tu ulipanga kichwani, hilo halina ubishi, ukisema hukupanga basi wewe siyo binadamu ni roboti.

Ingawa tunapanga lakini vilevile tunahitaji kujiandaa na mabadiliko yatakayojitokeza kwa kasi katika hali halisi mbele ya safari. Na hivyo ndivyo binadamu tunavyofanya kila mara tunapopanga kufanya jambo lolote lile katika maisha yetu ya kila siku. Sasa kwa faida zaidi ya kupanga ndipo utakuta watu wakipanga “simple” na katika kutafuta urahisi huo ndiyo maana mimi huwa nashauri kila  wakati mtu ujue …ABCD…. kuhusiana na mipango ya biashara na kisha kwenye kuandika uandike mpango simple utakaokusaidia katika kusimamia biashara yako kwa uhakika na kisasa, pasipo hata kuandika mamia ya kurasa.

Kuna vitu kwa mfano kama;
·       Malengo ya biashara
·       Mikakati
·       Vitendo halisi
·       Vipimo katika utekelezaji
·       Hesabu na namba za msingi kama vile mauzo, bajeti ya gharama mbalimbali na mzunguko wa fedha taslimu.

Ukishaandika vitu hivyo kwa ufupi sasa unatakiwa wakati wa utekelezaji wa biashara ufanye mapitio mara kwa mara, unaweza ukaamua kujipangia ratiba ufanye mapitio ya mpango wako vs hali halisi katika kipindi fulani, kwa mfano unaweza kufanya kila siku, kwa wiki au kwa mwezi. Unaangalia tofauti iliyokuwepo kati ya mpango na matokeo halisi. Hapa huhitaji kuwa mtaalamu wa biashara bali unatumia akili ya kawaida tu ya kuifahamu vizuri biashara yako na kufuatilia kujua ni kitu gani kilichotokea ukilinganisha na kile ulichopanga.

SOMA: Utambulisho rasmi wa semina ya michanganuo ya biashara awamu ya kwanza 1

Katika ulinganisho huo ni lazima utagundua kwamba, mpango wa biashara mara nyingi hauwezi kwenda sawasawa kwa asilimia 100% kama ulivyopanga. Lakini kuna umuhimu mkubwa na faida kiutendaji kwani kunakuwezesha kufahamu ni kwa nini hali haikwenda sawa na ulivyopanga. Kumbuka hali halisi siyo mara zote huwa tofauti kwa mana ya mambo kwenda mrama hapana, kuna wakati mwingine hata pengine katika mpango ulikisia mauzo kuwa Sh. 1,000,000/= lakini katika hali halisi unashangaa mauzo yanakuja kuwa 1,300,000/=. Kwa hiyo zoezi hili litakusaidia kuamua ufanye mabadiliko gani, na utegemee matokeo gani kwa wakati ujao.

Zoezi hili la kufanya marekebisho ya mpango pamoja na kulinganisha mpango na matokeo halisi ni jambo muhimu sana na katika hali ya kawaida kabisa ni zoezi linalofanyika katika maeneo mengi ya kazi na biashara. Kwa mfano unapoingia katika nyumba nyingi za habari(News room) iwe ni katika magazeti, redio au Televisheni, utakuta kila siku wana mikutano, wengine huiita “postmortem” Mhariri mkuu hukaa na wafanyakazi wote na kuanza kufuatilia kile walichofanya jana yake ikiwa walifikia malengo waliyojiwekea jana yake kwa kiwangio gani. Kisha siku hiyo mhariri huandaa mpango mwingine kwa ajili ya siku hiyo, nani aende wapi, akafanye nini, na kwa gharama gani nk.

Ingawa utakuta kuna vitu havikuenda sawa kama mpango ulivyosema, lakini hapa kumbuka mhariri hamtafuti mchawi wala kumlaumu mtu, bali yeye anachotafuta ni kwa nini mambo hayakwenda sawa au kwanini yalikwenda vizuri zaidi kushinda ilivyokisiwa, kusudi mbinu hizo ziweze kutumiwa zaidi wakati ujao.

Kwa hiyo matokeo ya mchakato wa kupanga au mpango mzuri wa biashara siyo maandishi bali ni utekelezaji wake(management), jinsi unavyopanga vipaumbele vya biashara yako na kufuatilia utekelezaji wake kujua ni kipi kimeenda sawa au ni kipi kimeenda mrama kwa ajili ya kufanya marekebisho kwa ajili ya wakati ujao.

Kusimamia biashara ni sawa na mtu unavyoendesha gari, unatakiwa uelewe ni uelekeo upi unaokwenda na uwe na maono ya kule uendako, picha ya hatma ya safari yako. Ukichanganya vitu hivyo na marekebisho ya hapa na pale njiani kama vile kuruka matuta, kukwepa vitu barabarani nk. hata kama ikiwa ni barabara kubwa kama morogoro road, hakukosekani matuta na vizuizi vya hapa na pale. Lakini muda wote unatakiwa kushikilia usukani wako pasipo kutetereka kwa kuwa tayari unao mpango na maono kichwani ni wapi unaaakokwenda.

………………………………………………………………….

Ndugu msomaji, kama wewe unapenda kujifunza namna ya kuandaa mpango wa biashara au unahitaji kupata ‘material’ zote zinazohusiana na michanganuo ya biashara na vitabu kwa kiswhahili na kwa kiingereza, kwenye blogu hii ndiyo mahali pake.

Tuna kitabu kinachoitwa, “MICHANGANUO YA BIASHARA NA UJASIRIAMLI” katika lugha ya kiswahili, bei yake ni Sh. 20,000/= hardcopy na Sh. 10,000/= softcopy.(kwa email)
Business plan book(kiswahili)

Tuna BLOGU YA MASOMO YA SEMINA YA MICHANGANUO ambayo kiingilio chake au ada ni Sh, 10,000/=. Ukishajiunga mara moja unaendelea kupata masomo ya kila awamu ukianza na awamu ya 1 na ya 2 ambazo tayari zimeshawekwa katika blogu hiyo pamoja na awamu zingine zote zitakazofuata.

Semina ya Michanganuo ya biashara

Unapolipa ada yako kupitia namba 0712202244  au 0765553030 na kutuma anuani yako ya email, tunakuunganisha na masomo ya semina hiyo pamoja na kukupa bure softcopy ya kitabu cha MICHANGANUO YA BIASHARA.

Ofisi yetu inapatikana MBEZI KWA MSUGURI jirani na stendi ya daladala.

Simu: 0712 202244  au 0765 553030

Kwa sasa hivi hatupo tena katika ofisi yetu iliyokuwa BUGURUNI karibu na AKIBA BANK.


1 Response to "JINSI MPANGO WA BIASHARA UNAVYOWEZA KUONGEZA MAFANIKIO YA BIASHARA YAKO"

  1. Habari! Nahitaji kuandika andiko la ukarabati wa vyumba viwili vya madarasa na ujenzi wa madarasa matatu ya wanafunzi wenye mahitaji Maalum. Naweza kusaidiwa juu ya hilo?

    ReplyDelete