NJIA 7 UNAZOTUMIA KUBANA MATUMIZI LAKINI KUMBE ZINAKUZIDISHIA UMASIKINI | JIFUNZE UJASIRIAMALI

NJIA 7 UNAZOTUMIA KUBANA MATUMIZI LAKINI KUMBE ZINAKUZIDISHIA UMASIKINI


Siyo njia zote tunazotumia kubana matumizi ni sahihi kwetu. Jinsi ya kudhibiti matumizi wakati mwingine tunajikuta tunatumia mbinu ambazo  badala ya kutupeleka katika hali bora zaidi kiuchumi ndio zinazidi kutudidimiza kwenye umasikini. Kuzifahamu mbinu hizo potofu kutakuwezesha kuzikwepa na hata kukufanya uchukue tahadhari katika njia zako unazozitumia kuzisimamia vyema fedha zako au kwa lugha nyingine ni kuacha matumizi mabaya ya pesa na kushika matumizi bora ya pesa.


Kila mtu anayetaka kufanikiwa kimaisha  hasa katika eneo la kiuchumi au kifedha hana budi kujiwekea akiba na hatimaye akiba hiyo kuitumia katika uwekezaji kwenye biashara au vitegauchumi vitakavyomuingizia fedha. Utajiri ni matokeo ya mtu kutumia kidogo kuliko kile anachoingiza(nidhamu ya matumizi ya pesa), kuhakikisha unatumia mbinu sahihi za utunzaji au usimamiaji wa pesa ili hatimaye kiasi cha fedha unachoingiza kiwe kingi kuliko kile unachotoa ni jambo la msingi sana.

MBINU ZENYEWE ZA UTUNZAJI WA FEDHA ZINAZOWEZA KUKUPELEKA KWENYE UMASIKINI BADALA YA KUKUTAJIRISHA NI HIZI ZIFUATAZO;

1.Kununua kwa promosheni(punguzo kubwa la bei!) ukitarajia kupata vitu vingi kwa bei rahisi.
Huu ni mtego kwa watu wengi wanaonunua vitu na hata wale wajanja usioweza kuwadhania kama wanaweza kuingia mkenge kama huo. Baadhi ya wauzaji wengi kwenye maduka na wale wanaotembeza vitu mitaani kuna wakati hujidai wanauza bidhaa zao kwa punguzo kubwa la bei kumbe hawana lolote, kwa mfano wanaweza kukutangazia kwamba ukinunua vitu 10 unapata na vitano juu yake bure! Kumbe hujui bei waliyokuuzia ni ileile ya kawaida. Unajikuta umeuziwa dazani nzima ya bidhaa wakati hukuwa na haja navyo vyote. Kanuni ya pesa inashauri kununua tu kile kitu unachohitaji na wala usihadaiwe na promosheni zisizokuwa na msingi.


Wengine watakuambia kuwa bidhaa fulani zimebakia chache sana kusudi tu upaparike na kutaka kununu kwa wingi kwa hofu kuwa bidhaa hizo zinaweza zikamalizika stoo muda mfupi ujao.

2. Kuzima mara kwa mara taa unapokuwa ukitoka na kuingia chumbani ukidhani unaokoa fedha unazotumia kulipa bili ya umeme  kumbe siyo.
Kuzima na kuwasha mara kwa mara taa hasa hizi  za kisasa(energy server na tube lights), kunazidisha gharama zaidi kuliko kuokoa kwani taa hizi zina tabia ya kula umeme mwingi pindi ziwashwapo hivi halafu ndipo hupunguza kiwango cha ulaji umeme baada ya dakika kadhaa.

Vilevile taa hizi zina tabia nyigine ya kuungua haraka zinapozimwa na kuwashwa kila mara. Inatakiwa baada ya kuzima ukae angalao dakika 15 ndipo ziwashwe tena, hivyo ikiwa utarudi chumbani chini ya muda huo ni bora ukaiacha iendelee kuwaka wakati unapotoka nje, utakuwa umeokoa pesa.

3. Akiba kwako ni mabaki ya kile unachotumia.
Huweki akiba mpaka fedha zinazotumika kwa matumizi yako ya kawaida zibakie. Ina maana  kama hamna mabaki na akiba inakuwa hakuna, akiba unaifanya kitu cha ziada. Usishangae kama unayo tabia hii kuona kwamba hutakaa uweke akiba maisha yako yote. Badala yake unashauriwa kutenga kabisa kiasi ulichojiamulia kuweka akiba kama ni asilimia 10%, 15% au asilimia yeyote utakayopanga kabla hata hujafanya matumizi mengine ya aina yeyote yale.


4. Kubana matumizi kupitiliza.
Unafikiri kwamba namna ya kutumia pesa vizuri ili ufanikiwe haraka basi inakubidi uishi kama ‘Mtauwa’. Ndiyo unaweza ukajinyima karibu kila kitu kisichokuwa muhimu ili uweke akiba lakini mbinu hii siyo endelevu hata kidogo katika matumizi ya fedha, hautachukua muda mrefu kabla haujakata tamaa na kuachilia mbali kuweka akiba. Utakuta labda mtu alizoe kunywa chai asubuhi au kinyaji chake chupa moja au mbili jioni, kisha ghafla tu from no where unamwambia aache kabisa kunywa kwa lengo la kubana matumizi aweke akiba. Itakuwa ni jambo gumu sana kwa mtu kama huyo.

Ni muhimu kwa ajili ya mafanikio yako kiuchumi kwamba unaweka mipango madhubuti kabla ya kuhakikisha unafanya matumizi pale tu panapohitajika kufanya na kujiwekea akiba kiasi unachoweza kuweka. Hata ikiwa utaweka akiba kidogo sana na ikiwa kweli umedhamiria kuweka kila mara ukazoea itaongezeka haraka kuliko ulivyotegemea. 


Ni bora kuweka akiba kila siku shilingi elfu moja na ukadumu ukifanya hivyo kuliko kujilazimisha kuweka akiba shilingi elfu 10 kila siku na kisha kuishia kukata tamaa na kuacha siku chache. Unashauriwa kujiwekea lengo linalotekelezeka utakalodumu nalo(kiasi). Kujaribu kubana kila kitu unachokipata hakuna tofauti na kutokubana matumizi kabisa kwani utafanya hivyo kwa muda mfupi tu na kisha kurudia maisha yako  ya zamani ya kuponda mali.

5. Kuachana na shughuli zote za kijamii kama harusi na misiba ili ubane matumizi vizuri.
Unaweza ukafikiria labda kwa kufanya hivyo itasaidia lakini kumbe ndiyo umejipalia mkaa. Ingawa kweli shughuli nyingi za kijamii zina gharama, lakini kuziacha kabisa ili eti ubane matumizi utakuja kulipa gharama kubwa zaidi ya hizo unazokwepa. Mbinu hii itakufanya ujisikie mpweke na uliyetengwa na jamii inayokuzunguka kiasi kwamba hutaweza kamwe kufurahia mazingira ya ushirikiano unaouhitaji ili kutimiza malengo yako ya kujiwekea akiba.


Badala yake tafuta njia zisizokuwa za gharama kubwa za kushirikiana na jamii kwa mfano badala ya kuwaalika ndugu, jamaa na marafiki mkutanoni katika hoteli au kumbi za gharama kubwa, waalike vikao vyenu nyumbani na uwaandalie vyakula na vinywaji mwenyewe. Wajulishe ndugu, jamaa na marafiki zako malengo yako na watakuwa tayari hata kukuusapoti  badala ya kuwakwepa.

5. Kutokutembea kabisa na pesa taslimu mfukoni.
Unajidanganya kuwa usipobeba hela mfukoni ndio hautapata vishawishi vya kutumia lakini kumbe hujui kwa kufanya hivyo unazidisha kujijengea tabia ya kutokuwa makini ni wapi fedha zako zinakokwenda, ni sawa na mbuni kuficha kichwa chake mchangani huku kiwiliwili kikiwa nje. Fedha mfukoni ni rafiki yako mkubwa hasa ukiwa unataka kujenga tabia ya umakini katika matumizi ya fedha. Kutembea bila pesa mfukoni pia hakutaweza kukufundisha jinsi ya kuepuka madeni kwani hiyo ndiyo njia nzuri zaidi ya kukufanya uingie madeni yasiyokuwa na msingi.

Unachopaswa kufanya ni kuhakikisha unatenga kabisa kiasi cha fedha kinachohitajika kufanya manunuzi ya siku hiyo kabla hujatoka nyumbani na kuhakikisha hutakwenda kinyume na bajeti hiyo kabisa hata ushawishike vipi. Hii itakujengea nidhamu nzuri zaidi kuliko kujidanganya unatoka mifukoni huna kitu.


6. Kukwepa kupanga bajeti kabisa.
Watu wengine hudhani kwa kutokuweka bajeti kabisa kutasaidia katika kuwapa utulivu wa nafsi na akili hivyo sula la kuweka akiba kufanyika vizuri zaidi lakini kumbuka kuweka akiba kamwe hakuwezi kufanyika pasipo juhudi za makusudi na zinazoonekana.

7. Kufungua akaunti nyingi mno za benki na katika benki tofauti.
Kufikiria kwamba ukiweka fedha zako kwenye akaunti na benki tofauti kutasaidia katika utunzaji mzuri wa fedha zako siyo sahihi. Watafiti wamegundua kwamba watu huweka zaidi akiba fedha zao na kutumia kidogo pale wanapokuwa na akaunti moja tu ya benki. Unapokuwa na akaunti nyingi  hasa kwenye benki tofauti ni rahisi zaidi kupoteza malengo na kushindwa kusimamia ni wapi fedha zako zinakokwenda.  

………………………………………………
Masomo kama haya na mengine mazuri zaidi tumewahi kuyafudisha katika group la whatsap la MICHANGANUO ONLINE, ni masomo mengi sana sasa yamefika kitabu kizima. Unaweza kuyapata masomo hayo(PDF) kwa njia ya email yako pamoja na offa ya vitu vingine mbalimbali kwa sh. Elfu 10 tu. Unapata pia fursa ya kujiunga na group hilo kwa ajili ya masomo mengine zaidi yajayo na semina.

SIMU:     0712202244
WASAP: 0765553030

0 Response to "NJIA 7 UNAZOTUMIA KUBANA MATUMIZI LAKINI KUMBE ZINAKUZIDISHIA UMASIKINI"

Post a Comment