HATUA ZIPI NIFUATE KUANZISHA KAMPUNI NA NI JINSI GANI YA KUIENDESHA? | JIFUNZE UJASIRIAMALI

HATUA ZIPI NIFUATE KUANZISHA KAMPUNI NA NI JINSI GANI YA KUIENDESHA?


ONGEA NA MSHAURI KUSAJILI KAMPUNI
Katika Ongea na Mshauri leo hii tumepokea swali kutoka kwa msomaji mmoja wa blogu hii, hajajitambulisha anatokea wapi ila swali lake ametuma kwa njia ya email kama ifuatavyo na mimi hapa chini siongezi wala kupunguza neno kwenye email hiyo;


“Naomba kusaidiwa nawezaje kuendesha biashara yangu kwa mfumo wa kampuni? Hatua zipi nifuate?

NAWEZAJE KUENDESHA BIASHARA YANGU KWA MTINDO WA KAMPUNI?
Jibu ni ndiyo, biashara yeyote ile iwe kubwa au ndogo, ya jumla au biashara ya rejareja, utoaji wa huduma na hata biashara ya kuzalisha bidhaa kama kiwanda, unaweza ukaiendesha kwa mfumo wa kampuni. Kisheria mifumo ya biashara ipo zaidi ya minne lakini ile iliyozoeleka zaidi na inayotumika mara kwa mara na watu wengi ni hii mitatu ifuatayo;

1.  MTU BINAFSI(sole proprietorship
2.  UBIA(Partnership)
3.  KMPUNI YENYE DHIMA YA UKOMO(Limited company)


Kampuni kama ulivyouliza tofauti yake na mifumo hiyo mingine miwili ni kwamba, wamiliki mnaweza kuwa ni watu 2 mpaka watu 50 na faida yake kubwa ni kuwa mali binafsi za wanahisa hazihusiani kabisa na zile za kampuni na haziwezi kuwajibika kulipia mdeni yaliyosababishwa na kampuni ikitokea labda kampuni inataka kufilisika au inadaiwa. Ni kampuni yenyewe kama kampuni itawajibika kulipa deni siyo wamiliki wake waingie mifukoni mwao au wakauze mali zao binafsi. Kampuni huchukuliwa kama nafsi ya mtu binafsi kisheria.

Tukirudi katika swali lako ni kwamba, hakuna taratibu maalumu au za kipekee za uendeshaji wa biashara katika mtindo wa kampuni isipokuwa tu maswala hayo ya kisheria yaliyotajwa. Hata hivyo kampuni mtu unakuwa na wigo au uhuru mpana zaidi wa kuendesha biashara yako kutokana na kuaminika zaidi na watu wakiwemo wateja wale unaofanya nao biashara, makampuni mengine na hata wakati mwingine  serikali. Kwahiyo unaweza kuona ya kwamba kampuni inao uwezo wa kutanua  biashara zake zaidi kuliko mifumo ya Mtu mmoja na Ubia.


·       Gharama za kwanza ni zile za usajili. Gharama hizi ukilinganisha na za mifumo mingine 2, zipo juu zaidi na huhusisha shughuli nyingi za makaratasi.

·       Ghrama kwenye uendeshaji kutokana na sababu kwamba kampuni licha ya kuwa na wamiliki/wakurugenzi mbao ndio wenye hisa, kampuni pia inatakiwa kuwa na meneja pamoja na timu yote ya uongozi na wafanyakazi kama vile mhasibu nk.

·       Ukaguzi wa mahesabu kila mwaka na hesabu hizo kuwasilishwa kwa msajili wa makampuni. Shughuli zote hizo zina gharama ya fedha na muda tofauti na kutumi mifumo mingine miwili ya biashara kisheria.

HATUA ZA KUFUATA WAKATI WA KUANZISHA KAMPUNI TANZANIA.
1)  Kwanza kabisa unapeleka majina yako matatu pale BRELA ambayo ungependa mojawapo ndilo litumike ukianza na lile unalopenda zaidi liwe ndio jina la kampuni yako. Sababu ya kupeleka majina matatu ni ili kama itaonekana jina la mwanzo lilishatumika na mtu mwingine basi waangalie uwezekano wa hayo mengine 2.


2)  BRELA ndiyo taasisi inayohusika na usajili wa makampuni na pia majina ya biashara kwa biashara ya mtu mmoja na ubia. Makao yake makuu yapo jijini Dar es salaam katika jengo la Ushirika pale Mnazimmoja. Unaweza pia kutembelea mtandao wao kwenye intaneti ambapo unaweza kudownload fomu za kusajili kampuni na mjina ya biashara.

3)  Jina likishakubalika na Brela, nenda katika ofisi yeyote ile ya mwanasheria wakuandalie katiba ya kampuni yako(Memorandum and Articles of Associations) pamoja na kukujazia makabrasha mengine ya kisheria  na kugonga mihuri. Ikiwa wewe mwenyewe unao uwezo wa kuandaa makabrasha hayo, kwa mwanasheria ni lazima uende kwa ajili ya kugongewa mihuri au kusaidiwa kupitia kama kuna makosa yeyote kisheria.


4)  Ukishamaliza hapo peleka makabrasha hayo Brela, watakupa fomu za kujaza, ikiwa ni pamoja na kulipia ada kulingana na ukubwa wa mtaji uliopendekeza wa kampuni yako. Baada ya hapo Brela watakupa cheti chako cha usajili wa kampuni ndani ya siku 5 mpaka 7.

HITIMISHO.
Unapoanzisha ,biashara yeyote ile, cha kwanza kabisa angalia kwanza uwezo wako uliokuwa nao hasa katika mtaji, kisha ndipo uamue kama ni mfumo upi utakaoanza nao. Kama mtaji ni kidogo unaweza ukaanza na mfumo wa mtu mmoja au ubia kwani unaweza kuja kubadilisha hapo baadae, lakini kama hali kifedha inaruhusu ni vizuri zaidi ukaanza moja kwa moja na mfumo wa kampuni.

...............................................................

Kwa vitabu vyako bora kabisa vy ujasiriamali, wasiliana nasi kwa namba 0712202244  au  0765553030 wasap 0765553030 au tembelea SMART BOOKS TANZANIA


2 Responses to "HATUA ZIPI NIFUATE KUANZISHA KAMPUNI NA NI JINSI GANI YA KUIENDESHA? "

  1. Mkataba kati ya kampuni ya mifugo na mawakala unakuwaje

    ReplyDelete
  2. Habari,,, Je nilazima kampuni iwe na mwanasheria ama akimaliza kaz ya kuandaa memorandum/kugonga mhur tunaachana🙏🙏

    ReplyDelete