KUANZISHA BIASHARA NIKIWA CHUONI NASOMA NIPENI USHAURI NINA WAKATI MGUMU | JIFUNZE UJASIRIAMALI

KUANZISHA BIASHARA NIKIWA CHUONI NASOMA NIPENI USHAURI NINA WAKATI MGUMU


Kitengo chetu cha ushauri hupokea maswali na changamoto mbalimbali kila siku na kuwajibu wahusika na mara nyingi hufanya hivyo kupitia simu ya mkononi au sms, isipokuwa kwa wale wanaotuma kwa email huwa maswali au ushauri wao tunawajibu kwa email au pamoja na kuuweka hapa kwenye Blogu ya jifunzeujasiriamali lakini pasipo kuanika majina yao kabisa, tunatumiaga vifupi vya majina yao au majina yasiyokuwa halisi. Hapa chini ni ushauri alioomba mwanafunzi mmoja wa chuo kutoka Singida;

Habari, naitwa C……  niko singida kwa sasa, ni mwanafunzi wa chuo. Nmesoma makala zako nikawiwa kukufatilia. Niko kwenye wakati mgumu wa kuanzisha biashara, nahitaj msaada wa mawazo ili kuweza kuvuka hatua hii

Pole ndugu C….., na nashukuru sana kwa kupitia makala zangu, lakini napenda kukuambia pia kwamba hauko peke yako, ni watu wengi wanapitia kipindi kigumu pengine hata kushinda wewe, hebu fikiria mtu ambaye hata nafasi ya chuo hajaweza kuipata na pia hana hata uwezo hususan mtaji wa kuanzishia japo kabiashara ka kuuza karanga.

SOMA: Natengeneza sabuni, shampoo, batiki na unga wa lishe lakini mambo bado ni magumu nifanyeje?

Nimefurahi kusikia wewe upo chuoni na bado unalo wazo la kuanzisha biashara. Jambo hili linawezekana kabisa japo inakubidi uwe "Smart" kidogo, nikimaanisha kwamba inakupasa kama utaanzisha biashara  yeyote ile ungali bado chuoni ni lazima uhakikishe unatengeneza mfumo madhubuti utakaokuwezesha kutekeleza mambo hayo mawili kwa wakati mmoja vinginevyo unaweza ukajikuta unafanya vibaya pande zote mbili, kwenye masomo na kwenye biashara pia.

Kutengeneza mfumo huo kuna gharama zake ambazo ni lazima ziwe aidha katika maana ya rasilimali fedha au rasilimali muda. Biashara ili iweze kusonga mbele ni lazima itahitaji uwekeze muda wako au fedha vinginevyo haiwezekani kabisa kuendesha biashara. Ukiwa na rasilimali ya fedha unaweza ukaanzisha biashara fulani na ukamtafuta mtu akawa anaiendesha hata ikiwa wewe binafsi hautakaa pale kila wakati na wewe kazi yako kubwa itakuwa ni kuja na kukagua mahesabu yako kikamilifu tu, poteza hata saa moja au saa moja na nusu kwa siku ili uhakikishe mtaji wako upo salama na faida iliyopatikana siku hiyo.

Kwa upande wa rasilimali ya muda, inakubidi mtu uutumie muda wako karibu wote kwa siku kuendesha na kusimamia biashara yako ndogo uliyoianzisha kwa kuwa hauna rasilimali pesa ya kutosha kuajiri mtu. Shughuli zote pengine kuanzia kufuatilia bidhaa kama ni biashara ya kuuza bidhaa mpaka shughuli ya kumuuzia mteja itakubidi uifanye wewe mwenyewe. Mchakato mzima wa biashara kuanzia asubuhi mpaka jioni unaotumika mpaka biashara inatengeneza faida ndiyo tunaoweza kusema ni mfumo wa biashara yako.

Ninavyofahamu mimi ukishakuwa mwanafunzi au mwanachuo kama wewe, rasilimali ya muda ni lazima itakuwa adimu sana kwa upande wako, sijajua kwa upande wa rasilimali ya fedha upoje mfukoni mwako, na hiyo nadhani itakuwa ni siri yako sipaswi hata kujua.

Lakini hebu "tuassume" tuchukulie labda mfukoni kwako upo vizuri kidogo, nikimaanisha kwamba unao mtaji wa kutosha kuendesha biashara, kazi ya kuweka mfumo wa biashara yeyote ile inayolingana na mtaji huo uliokuwa nao itakuwa rahisi sana ilimradi tu ubuni wazo la biashara iliyokuwa na uwezo wa kutengeneza faida na biashara ya namna hiyo mtu unachunguza katika mazingira yaliyokuzunguka kuna mahitaji gani ya watu yanayotakiwa sana, watu wanashida zipi zinazohitaji kutatuliwa? ukishabaini basi unaweza kutafuta eneo na kuweka biashara itakayotatua zile shida za watu.
Kumbuka mchakato wote huo utahitaji fedha kuukamilisha na kwa kila hatua inabidi utumie fedha hiyo kwa umakini wa hali ya juu sana kwani fedha hiyo ikipotea inaweza kuwa vigumu sana kuipata tena nyingine ndani ya muda mfupi. Wakati huo huo hakikisha ratiba zako za masomo haziingiliwi kabisa.

Hebu tuchukulie sasa wewe ni mwanachuo, tayari rasilimali-muda inajulikana 'automatic' kuwa ni adimu kwako halafu pia ukute na rasilimali-fedha nayo huna ya kutosha kuanzisha biashara, nikimaanisha hata ikiwa utaanzisha biashara basi ni kwa kuungaunga tu. Hii ni hatari lakini pia zipo mbinu mtu unazoweza ukazitumia japo kwa kweli nachelea sana kukushauri kwa dhati kabisa kuzitumia lakini 'anyway' nitajaribu kuzielezea ili mwenyewe upime.

Najaribu kukumbuka mifano hai niliyowahi kuiona mwenyewe kwa macho yangu vipindi mbalimbali nilipokuwa nasoma, kwa mfano tulipokuwa shule ya sekondari, O level mimi binafsi nilianzisha biashara ndogondogo nyingi lakini kwa kweli mafanikio yake hayakuwa ya kuridhisha sana kutokana na ugumu wa kubalance muda wa masomo na muda wa biashara. Nilijaribu kuuza vitu vidogovidogo kama majalada ya madaftari na vitabu, siku zingine nilipeleka maembe, na hata kuna wakati nililima bustani za mbogamboga na nyanya niliporudi nyumbani jioni kwa kuwa nilikuwa Day.

Shughuli zote hizo tatizo kubwa nililokutana nalo lilikuwa ni mtaji kidogo. Nakumbuka hata nilianzisha kutengeneza maandazi alfajiri nikamtafuta kijana aliyekuwa akienda kuniuzia sokono mchana lakini napo sikupata mafaniio ya kuridhisa kutokana na faida iliyokuwa ikipatikana kutokutoshelea kumlipa mfanyakazi na mimi mwenyewe.

Kuna mfano wa kijana mwingine aliyekuwa amenitangulia kidato yeye alikuwa na biashara ya kupiga picha akitumia kamera yake ndogo ya YASHICA, kupiga picha wakati huo ilikuwa ni dili kubwa hasa nyakati za sherehe na siku za miisho ya wiki. Kwa kuwa kupiga picha kulikuwa hakuhitaji muda mwingi kijana yule aliweza kupata faida nzuri iliyomuwezesha hata kujilipia ada ya shule mwenyewe.


Wakati nikiwa A level nilishuhudia wanafunzi mbalimbali waliokuwa na biashara, wachache waliweza kufanikiwa kubalansi masomo na biashara na kuna mmoja aliyekuwa na biashara ya usafirishaji(daladala) alipomaliza form six akajiunga na chuo kikuu bado biashara yake iliendelea kushamiria akaja kununua mpaka malori ya kusafirisha mizigo kwenda mikoani. Kwa sasa hivi ni mwanasheria mzuri tu huku biashara zake zikiendelea kama kawaida.

Nimekuonyesha mazingira yote hayo ili uweze kuona changamoto unazoweza kukutana nazo pindi utakapoamua kuanzisha biashara ungali ukiwa bado upo chuoni unasoma. Hata hivyo kuna unafuu kidogo chuoni siyo sawa sawa na shule za sekondari au msingi, chuoni unaweza kuwa “flexible” zaidi, kwa maana nyingine unakuwa na uhuru zaidi kwa maana ya muda na hata masomo siyo mengi na magumu kama ilivyokuwa mashuleni.

Vyovyote vile iwavyo kwa ushauri wangu mimi, wewe anzisha biashara, ila hakikisha unachagua biashara “simple” ambayo utafanya kama majaribio kwanza kuona kama unaweza ukatengeneza mfumo wako wa kujiingizia pesa pasipo kuathiri muda wako wa masomo. Tuchukulie hata labda umeanzisha duka lako dogo na kumuweka mtu wa kukuuzia, ambalo unakuwa na uwezo wa kufika pale kila siku jioni na kukagua mahesabu yako, huo ni mfano tu, inaweza kuwa ni biashara nyingine yeyote ile.

Narudia tena ikiwa utaanzisha biashara utakayomuweka msaidizi, kama kwa kweli hautakuwa na mfumo unaoleweka wazi wa kujua kwa uhakika hesabu zako za siku zimeendaje, basi nakuomba acha kabisa usianzishe biashara bali endelea na chuo chako.

Na vilevile ikiwa hauna uwezo wa fedha za kuanzisha biashara utakayomuweka mtu wa kukusaidia unaweza ukaanzisha biashara rahisi isiyokula muda wako wa masomo, nina mfano mwingine wa rafiki yangu mmoja yeye akiwa chuoni aliweza kubuni biashara ya stationary kwenye bweni lake akawa anawatolea photocopy na printing wenzake na wakati mwingine kuwaunganisha na intaneti, biashara ile ilimgharimu fedha kidogo tu kwa ajili ya kununulia kompyuta, printa na baadhi ya software, lakini aliweza kujiingizia kipato kikubwa pasipo kuingilia kabisa muda wake wa masomo chuoni.

Unajua fursa ya kusoma mara nyingi huja mara moja tu na huja kuwa vigumu sana kuweza kurudia mwaka au darasa tofauti na biashara ambayo hata kama utaanguka mwaka huu lakini unaweza ukajaribu tena na tena miaka mingine mpaka umefanikiwa. Unaweza ukasema “Mbona kuna mabilionea kibao tu “walio drop out” kama kina Steve Jobs, Mark Zuckerberg, Bill gates, Larry Ellison na hata Ted Turner na mambo yao bado yakawa supa, lakini hao ni kama tone moja la maji katika bahari kubwa, ni mmoja katika watu 1000, siyo kila mtu anaweza kuwa na bahati waliyokuwa nayo hao.

SOMA: Ungependa kuwa kama Bakhresa, Mengi, Dewji na Rostam? fuata njia hizi 10

Najua tatizo kubwa mwanachuo au mwanafunzi yeyote analoweza kukutana nalo ni ufinyu wa rasilimali za kuanzia hasa pesa na muda wa kutosha kuhudumia biashara, lakini mbinu pekee unayoweza kuitumia kutatua matatizo hayo ni kwa njia ya kutumia rasilimali kidogo ulizokuwa nazo kwa nidhamu ya hali ya juu, nikiwa na maana rasilimali ya fedha na muda. Jibane, acha matumizi yasiyokuwa na ulazima kwako, kujibana huko ni kuanzia matumizi ya fedha mpaka muda. Achana na starehe kama kula vyakula vya gharama kubwa, vileo, kutazama tv, kuperuzi mitandao ya kijamii kupita kiasi nk.

Mwisho kabisa rafiki yangu C………, napenda nikuambie kuwa biashara ukiwa bado chuoni ni kitu kinachowezekana kabisa na tena unajiandaa kwa ajili ya mazingira halisi ya ufinyu wa ajira lakini zingatia sana mazingira niliyokueleza hasa kutokubinya kwa namna yeyote ile muda wako wa masomo au hata kuamua kuachana na chuo uendelee na biashara. Jitahidi kwa kadiri uwezavyo kuifanya biashara yako kuwa inajiendesha yenyewe aidha kwa kuweka msaidizi makini au kwa kuanzisha aina ya biashara itakayokugharimu muda kidogo sana lakini yenye faida ya kutosha pia.

………………………………………………………………

Tumekuwa kwa muda mrefu sasa tukitoa ushauri kwa watu mbalimbali kupitia simu na ujumbe wa simu za mkononi na hata kupitia e-mail. Ni mara chache ushauri tunaowapa watu tunauweka hapa katika blogu ya JIFUNZEUJASIRIAMALI kama tulivyouweka huu hapa na nyingine chache.

Kwa kuwa wengi wa wale wanaotaka ushauri huwa wanarudi kwa mara nyingine tena kuomba ushauri(unaweza kuwa tofauti na ule wa mwanzo au wakati mwingime unakuwa unahusiana na ule wa mwanzo) tumeonelea yakwamba ili kuboresha kitengo hiki basi tuweke huduma ya kuchangia ushauri huo ili kuweza kuutoa kwa kina na kwa muda mrefu zaidi kwa yule anayehitaji.

Hatutaondoa ushauri wa bure wa kawaida wa mara moja kama huu au tuliyokwishatoa kwa wasomaji wengine hapana, ila kutakuwa na chaji, shilingi elfu 5 tu kwa yule atakayehitaji ushauri wa kina kabisa pamoja na huduma ya COACHING katika kipindi kisichopungua miezi 6. Unapotoa shilingi elfu 5, unapata fursa ya kuzungumza na mshauri au kocha kwa muda usiopungua dakika 15 siku hiyo, halafu utaendelea kuwa na mawasiliano ya karibu kabisa na mshauri kupitia jumbe za simu, e-mail  na hata simu kila utakapokuwa na swali au kuhitaji kushauriwa tena ndani ya miezi 6.


Ili kuwa mwanachama wa huduma hii, nitumie ujumbe unaoelezea ni ushauri gani unaohitaji halafu utanipa muda kama saa moja au zaidi ya hapo kulingana na nafasi yako wa kuandaa majibu. Karibu na muda tutakapoanza mazungumzo ndipo utatuma pesa shilingi 5,000/= kwenye namba  0712 202244 au 0765 553030, na kisha tutaanza mazungumzo yetu ukiwa sehemu tulivu isiyokuwa na kelele nyingi.

0 Response to "KUANZISHA BIASHARA NIKIWA CHUONI NASOMA NIPENI USHAURI NINA WAKATI MGUMU"

Post a Comment