UNAPENDA KUWA KAMA BAKHRESA MENGI DEWJI NA ROSTAM? FUATA NJIA HIZI 10 UONE MAFANIKIO YAKE | JIFUNZE UJASIRIAMALI

UNAPENDA KUWA KAMA BAKHRESA MENGI DEWJI NA ROSTAM? FUATA NJIA HIZI 10 UONE MAFANIKIO YAKE









Muda mwingi nimekuwa nifuatilia maisha ya watu wengi maarufu na waliofanikiwa duniani wakiwemo wafanyabiashara matajiri zaidi wa hapa kwetu Tanzania kama vile Mohamed Dewji, Rostam Aziz, Said Salim Bakhresa na Reginald Mengi. Nilikuja kubaini kwamba hakuna kitu cha ajabu au cha kipekee sana mtu kuweza kufanikiwa kiuchumi au kuwa bilionea, siyo elimu kubwa sana wala akili nyingi sana wala kuzaliwa katika ukoo tajiri sana kunakoweza kukakufanya wewe uwe tajiri au milionea.

Kikubwa unachokihitaji zaidi ili utajirike au ufanikiwe kama nilivyokwisha andika miaka kadhaa iliyopita wakati naanza shughuli hii ya kublogu ni, “Roho ya ujasiriamali”, unahitaji pia uwe na ndoto(maono), nia thabiti na mpango unaotekelezeka. Vitu hivi ni vwa kawaida sana na wala hauhitaji kuwa na fedha yeyote ili kuwa navyo. Lakini bado nafahamu utaendelea tu kuniuliza, kuwa na vitu hivyo peke yake kunatosha mtu kuwa tajiri?, mbona watu kibao wanavyo na huishia kufa wangali masikini?.

Jibu langu kwako ni kuwa, hata mimi mwenyewe sijui, hakuna njia moja rasmi mtu anayoweza akaitumia kutajirika, hata hao kina Mengi, Dewji, Rostam na Bakhresa unaowaona leo, hawakufuata njia moja inayofanana, kila mmoja alitajirika kivyake. Katika kitabu cha “Robert Kiyosaki” ‘Rich Dad’s Guide to Investing’, anasisitiza kwamba zipo njia nyingi za watu kutajirika, alifafanua kwamba, mtu unaweza ukawa tajiri kupitia kurithi mali, kupitia njia haramu za wizi au ufisadi, na hata kuna wanaotajirika kwa kuoa mwenza ambaye kwao 'mambo ni safi'. Lakini vyovyote vile mtu anavyoweza kuwa tajiri ukiondoa njia hizo haramu, haijalishi mtu kapitia biashara gani; ni lazima kuna kitu kimoja ambacho mabilionea wote duniani huwa nacho kwa pamoja, nacho siyo kingine bali ni roho ya ujasiriamali(spirit of entrepreneurship).

SOMA: Ni nini hasa unachohitaji ili uweze kufanikiwa kiuchumi?

Kwa hiyo ikiwa utapenda na wewe kufanikiwa kama wao hakuna budi kuwauliza kwa kuwa wameshapita njia hiyo na wanaelewa kuliko mtu mwingine yeyote namna ya kutajirika. Na si rahisi kila mtu kuwafuata uso kwa uso na kwenda kuwauliza, ni kwa njia kama hizi, baadhi ya watu kutafuta historia zao na yale waliyoyafanya na kisha kuwagawia na wengine ambao hawana muda wa kuyafuatilia.

Sasa tutakwenda kuzitazama njia 10 au hatua ambazo watu wengi wanaofanikiwa  huzipitia iwe ni kwa kujua ama hawajui lakini ni lazima kwa namna moja ama nyingine hujikuta wamezipitia katika safari yao ya kutajirika.

1. Huanza na Ndoto au Maono.
Kutajirika huanza na maono. Moja ya kitu cha bure kabisa Mungu alichotujalia sisi wanadamu ni zawadi ya akili(uwezo wa kufikiri) Haimgharimu mtu kitu chochote kuota(kuwa na maono) lakini watu wengi huwa hawajisumbui kufanya hivyo na hata wale wanao kuwa nayo basi huwa na maono mafupi au kwa maana nyingine huota mambo madogomadogo yasiyoweza kuwatajirisha. Na mara zote watu wanaoota mambo madogo huendelea maisha yao yote kuwa masikini.

2. Hujijengea akilini mtazamo wa watu waliofanikiwa.
Ili kutajirika ni lazima akili yako ifikirie kama wale watu waliotajirika. Hata kama bado haujaanza kutajirika lakini inabidi ujijengee uwezo katika akili yako wa kutenda mambo kama wanavyotenda watu waliofanikiwa. Vitendo hivyo ni kama vile, kuchukua hatari inayotokana na pesa zako mwenyewe au hata za kukopa, kuwa tayari kupata faida lakini wakati huo huo kutokuogopa kupata hasara kama ikitokea, kujitoa kikamilifu katika kukamilisha majukumu ya biashara pamoja na kuwa na uwezo wa kuziona fursa zilizojificha katikati ya matatizo ambazo watu wengine wa kawaida inawawia vigumu kuziona. 

Unapokuwa na uwezo wa kukabiliana na matatizo mbalimbali basi ujue wewe unao pia uwezo wa kuzitambua fursa mbalimbali. Mjasiriamali mzuri ni yule mwenye tabia kama za mwandishi wa habari, mwandishi wa habari anao uwezo wa kunusa habari popote pale ilipo, na mjasiriamali anapokuwa ameifundisha akili yake mbinu stahiki huwa na uwezo wa kunusa fursa popote pale wengine wanapoona mikasa na majanga. Wakati Mzee Mengi anaanzisha kiwanda cha maji ya Kilimanjaro watu wengi waliamini hawezi kufanikiwa kwa sababu kwanza waliamini maji ya kunywa huwa hayauzwi bali hupewa tu bure. Sasa hivi hebu tazama, maji yanauzwa kila kona.

3. Huongeza ufahamu wao juu ya biashara wanazozifanya.
Kitakachokufanya utajirike siyo pesa bali ni maarifa sahihi juu ya pesa” - Kitabu chaSiri za mafanikio: Biashara ya Rejareja.
Kujiongezea maarifa ya biashara kwa mjasiriamali yeyote yule ni jambo muhimu sana. Matajiri siyo tu hutegemea elimu walizopata vyuoni ama shuleni bali pia hujifunza kupitia uzoefu wa kila siku wanaokutana nao katika shughuli zao.Kiyosaki  anakuambia; Uwezo wa kuuza ni ujuzi namba moja katika biashara, ikiwa huwezi kuuza, usijisumbue kufikiria kuwa mmiliki wa biashara”.-Robert Kiyosaki

4. Hutafuta wazo la biashara lenye uwezo wa kulipa haraka.
Kama uonavyo siku hizi magari ya mwendo kasi na yale yanayokwenda taratibu, mawazo ya biashara pia kuna ambayo yana uwezo wa kukutajirisha haraka na yale yatakayo kwenda taratibu kama mwendo wa kinyonga. Hapa sasa ndipo kazi ya ujasiriamali huanza. Kutimiza ndoto zako ulizojiwekea utahitaji wazo la biashara unayojua kabisa litakuvusha haraka likifuatiwa pia na mpango wa haraka unaotekelezeka.

Ninamaanisha kitu gani ninaposema “wazo la biashara lililokuwa na uwezo wa kulipa haraka?. Ndiyo maana pale mwanzoni nikatangulia kusema kwamba mjasiriamali anayetaka kutajirika ni lazima ahakikishe anaongeza maarifa na ufahamu wake juu ya biashara. Hii ina maana kwamba, dunia imejaa mawazo tele ya biashara, na kwa kweli karibu kila wazo linao uwezo wa kumletea mtu utajiri lakini kila wazo kuwa na uwezo wa kumtajirisha mtu hiyo tu haitoshi. Unahitaji wazo lenye uwezo wa kukutajirisha harakaaa. Wazo la namna hiyo ni lile ambalo kwa wakati huo linashika chati ya juu zaidi, ikiwa ni bidhaa au huduma basi zina uhitaji mkubwa sana na wateja. Lina uwezo wa kutatua tatizo kubwa kwa watu na wakati mwingine wazo la namna hiyo, linakuwa ni tegemeo la kwanza la watu katika mahitaji yao.

SOMA: Siri matajiri wasiyopenda kuitoa.

5. Huwa na watu wao wa mfano(Mentors)
Mtu yeyote anayefanikiwa ni lazima utakuta, alivutiwa na mtu mwingine ambaye alishawahi kufanikiwa. Kwa hiyo unapotafuta mtu wa kukupa hamasa au kuwa kama mtu wako wa mfano, angalia yule aliyefanikiwa tayari katika tasnia uliyokuwepo. Kama wewe unafanya biashara ya usafirishaji, mwangalie mtu aliyefanikiwa katika sekta ya usafirishaji, mambo yake anafanya fanyaje na hata kama itawezekana jenga naye ukaribu muwe hata marafiki atakufunulia siri nyingi za wewe kuweza kutajirika haraka kama yeye. Lakini angalia sana usije ukaanza kumuomba akupe fedha utaharibu kila kitu. Je, wewe mtu wako wa mfano ni nani?

6. Huanza biashara.
Dunia ya leo hakuna njia nyingine rahisi ya kutajirika zaidi ya kumiliki na kuendesha biashara yako mwenyewe. Waangalie Mabilionea wote duniani, kina Larry Ellison, Bill Gates, Warren Buffet, Aliko Dangote, Jerry Yang wa Yahoo, Mark Zuckerberg wa Facebook na wengineo kibao, walianza biashara zao chini kabisa, sijawahi kusikia yupo mmoja wao aliyeanza na mamilioni ya dola, lakini matokeo yake ni makampuni makubwa kabisa tunayoyaona leo na ambayo yamewafanya kuwa watu matajiri wakubwa Duniani. Utajiri uwe tu ni matokeo ya biashara utakayoanzisha na wala isije kuwa eti utajiri ndiyo lengo lako kuu, utafeli.

SOMA: Siori 10 alizotuymia Aliko Dangote kutajirika.

Kwahiyo ikiwa watu waliofanikiwa zaidi duniani walifika pale walipo kupitia kumiliki biashara tu, basi ni ushahidi tosha kabisa kwamba ni kweli mtu yeyote anaweza akatajirika kupitia ujasiriamali. Ikiwa tayari unayo biashara, tengeneza mpango utakaokuvusha haraka, weka malengo katika kuikuza biashara yako na usichoke kujifunza vitu vipya. Mwishowe utatajirika hata kama itachukua muda mwingi kidogo zaidi ya vile ulivyokuwa umepanga.

7. Huunda timu imara ya biashara zao.
Kujenga biashara nzuri ambayo hatima yake itakutajirisha unahitaji kujenga timu nzuri ya watu ambao watakusaidia katika kutimiaza ndoto zako hizo. Watu hawa siyo lazima wawe ni wale wafanyakazi tu hapana, kuna watu wengine kama vile, washauri, makundi ya kubadilishana mawazo “mastermind groups”,  wadau mbalimbali kama, wateja, wanaokusambazia bidhaa nk.

Kwa mfano unapokuwa na timu nzuri ya wafanyakazi, unavutia hata wawekezaji au wabia na hata unaaminika zaidi na wale wanaokukopesha. Mtu kama Mzee Bakhresa utakuta katika timu yake ya usimamizi ameweka watu makini sana, na hata wakati mwingine hulazimika kuajiri watu kutoka nje ya nchi ikiwa utaalamu unaohitajika hawezi kupata watu kutoka hapa. Hakuna mtu yeyote duniani aliyewahi kutajirika mwenyewe. Wote utakuta walikuwa na timu za washaurin na wafanyakazi ambao wakati mwingine wana ujuzi hata kuwashinda wao wenyewe.

8. Hutafuta mtaji wa kuendeshea biashara zao.
Hapo juu tulishaona anayefanikiwa kuwa tajiri baada ya kupata wazo la biashara yenye uwezo wa kulipa haraka, na hatimaye kuanzisha biashara yenyewe kwa mtaji kidogo aliokuwa nao sasa tutaona hatua nyingine wanayopitia ambayo ni hatua ya kupata mtaji wa kulitekeleza lile wazo kikamilifu. Unaweza ukapata mtaji kutoka kwa wabia, au wawekezaji binafsi wanaoweza wakawekeza pesa zao katika wazo lako hilo kwa makubaliano ya kuja kugawana faida itakayopatikana. Njia nyingine pia ni mikopo ya benki au taasisi za fedha.

SOMA: Njia 7 za kupata mtaji wa biashara uipendayo.

Lakini njia zote  hizi zina hasara zake ambazo wakati mwingine watu huzikwepa mpaka pale wanapokuja kufikia hatua wameshatengemaa kabisa ndipo huzitumia kama kichocheo. Kwa mfano makampuni makubwa karibu yote ya mitandaoni kama facebook, yahoo, google, Apple na hata Amazon, wote hawakukurupuka kwenda kukopa pesa za watu, walikomaa kwanza na mitaji yao mpaka pale kilipoanza kueleweka. Na unapofikia hatua kama hiyo, utachagua mwenyewe ukakope wapi kwani wakopeshaji hukufuata wenyewe wakikuomba wakukopeshe. Ushauri wangu kwako: na wewe jaribu kwanza njia hii kabla hujakwenda kukopa au  kutafuta mbia ndipo baadae ukatafute mtaji kutoka mahali pengine.

9. Hufanya biashara zao katika mfumo wa makampuni.
Mabilionea karibu wote duniani, sidhani kama yupo anayeendesha biashara ya mtu mmoja, “sole proprietorship”, huunda makampuni ambayo hata yakifilisika mali zao zingine haziwezi kisheria kukamatwa ili kufidia madeni yao. Vile vile kupitia mfumo huo wanakuwa na wigo mpana zaidi wa uendeshaji biashara zao kwani huajiri wasaidizi mbalimbali wa kuendesha biashara. Hata mtaji inakuwa rahisi kupata hasa inapofikia hatua kampuni ikawa na uwezo w kuingia katika soko la hisa.

10. Huwekeza katika biashara zingine.
Hii sasa ndiyo ile hatua rahisi kabisa ya mchakato wa mtu yeyote yule anayetaka mafanikio ya utajiri. Uwe tayari umesha kuwa bilionea au bado upo katika ngazi ya umilionea, kuendelea kubakia kileleni au kupiga hatua zaidi ni lazima ukubali kutumia mkakati na mbinu ya kuwekeza kwenye vitegauchumi vingine vingi zaidi ya kile unachomiliki. Na hapa sasa ndipo utakapoona umuhimu wa kufanya kazi na timu ya watu kama tulivyozungumza hivi punde.

Mwisho, kupata mafanikio kipesa au kuwa tajiri ni kitu ambacho kila mtu anao uwezo wa kukifikia, lakini watu wengi tunashindwa kufanya hivyo kwa sababu moja tu, “Tunaogopa mno kulipa gharama ya kufikia hatua hiyo na kuamua tu kubakia kuwa katika maisha ya kawaida tuliyoyazowea”. Ikiwa unayo ndoto ya siku moja kuja kuwa bilionea tajiri kama walivyo kina Reginald Mengi, Said Salim Bakhresa, Mohamed Dewji, Rostam Aziz na wengineo, basi huna budi kufuata hatua zilizotajwa hapo juu. Na zaidi ya yote unatakiwa kuwa mvumilivu. Hakuna kinachoshinda uvumilivu.

....................................................................................................
Ndugu msomaji wa blogu hii, kama ulikuwa hujasoma kitabu cha "Kanuni ya kujifunza elimu ya pesa na mafanikio", tunachokitoa bure baada ya mtu kujiunga na blogu hii, tafadhali KIDOWNLOAD HAPA mapema ili uweze kukisoma au kukihifadhi kwa ajili ya kuja kukisoma hapo baadae. Mwisho wa ofa hii ni hivi karibuni, kitabu hiki kitaanza kuuzwa kama vitabu vingine na bei yake itakuwa ni Tsh. 5,000/= Asante.

Vitabu vyetu vingine vinapatikana kwa njia za E-mail au Telegram mtandaoni na pia ukihitaji vitabu vya karatasi navyo vipo, ila bei hutofautiana. Mtandaoni bei ni nusu ya vitabu vya karatasi. Kwa maelezo zaidi Fungua ukurasa huu wa SMARTBOOSTZ.

Kwa mawasiliano ni;
0712 202244,  0765 553030  na  0689 303098
Telegram:       @petertarimo
e-mail:             jifunzeujasiriamali@gmail.com

1 Response to "UNAPENDA KUWA KAMA BAKHRESA MENGI DEWJI NA ROSTAM? FUATA NJIA HIZI 10 UONE MAFANIKIO YAKE"

  1. Nimefurahia sana masomo ya ujasiliamali, naomba kufahamu kama mna tawi la ofisi Arusha au Kilimanjaro?

    ReplyDelete