KUANZISHA KIWANDA RAHISI CHA JUISI YA MATUNDA, TANZANIA YA VIWANDA YAJA JIANDAE | JIFUNZE UJASIRIAMALI

KUANZISHA KIWANDA RAHISI CHA JUISI YA MATUNDA, TANZANIA YA VIWANDA YAJA JIANDAE

Kiwanda kidogo cha juisi ya matunda
KIWANDA NI NINI?

Maana ya kiwanda ni kwamba, bidhaa huzalishwa kwa kutumia mashine, kwa kiasi kikubwa na kwa gharama nafuu katika muda mchache zaidi kuliko kama vile ambavyo mikono ya binadamu ingeliweza kuzalisha. Mapinduzi ya viwanda yalianza huko Ulaya hususani nchini Uingereza katika karne ya 18 na 19 na baadaye kusambaa karibu maeneo mengine yote ya dunia.

Leo hii baada ya karne karibu 2 kupita Tanzania na sisi tunataka kufanya mapinduzi makubwa ya viwanda Tanzania. Hii haimaanishi kwamba Tanzania hatuna viwanda ila unapotaja orodha ya viwanda na idadi ya viwanda vilivyokuwepo au aina za viwanda vyetu, ni chache mno kulinganisha na zile nchi zilizoendelea kama za Ulaya, China na Marekani kiasi kwamba unaweza ukafananisha na tone moja tu la maji katika bahari kubwa.


Ikiwa kama kweli Tanzania tunataka kuufikia uchumi wa viwanda, ni lazima tukubali kwamba hakuna njia ya mkato zaidi ya kuanza kidogokidogo. Hata Uingereza wenyewe na Uchina wakati wakianza hawakuanza na viwanda vikubwa sana bali viwanda vidogovidogo na mwishowe wakajikuta wakihitaji kujenga viwanda vikubwa vikubwa kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya vile viwanda vidogovidogo vilivyotangulia kuanzishwa.

Kwa mfano unapoanzisha kiwanda kidogo cha juisi ya matunda baadaye utahitaji kuwa na kiwanda kikubwa cha chuma kwa ajili ya kutengeneza spea na vinu kwa ajili viwanda hivyo vidogo. Hivyo unaweza kuona kwamba viwanda vidogo huzaa viwanda vikubwa. Viwanda vya nguo halikadhalika na vile viwanda vya kubangulia korosho au pamba.

MAAJABU YA KIWANDA
Kiwanda huweza kufanya kazi ya kushangaza sana, ndiyo maana huko Uingereza na Marekani wakati huo wanamapinduzi hao wa viwanda walipata shida sana na hata wengine kuuwawa au kuteswa kutokana na mapinduzi hayo kuonekana yatapunguza au kuondoa kabisa ajira za watu. Hofu hiyo ilitawala lakini hatimaye ilikuja kuonekana haina maana yeyote sawasawa tu na ile hofu wakati wa Y2K miaka ya 2000 au mapinduzi ya kompyuta miaka ya 70 mpaka 90.


ATHARI ZA VIWANDA
Matokeo ya maajabu hayo ya viwanda matokeo yake hujitokeza kwenye uchumi kwa kuleta pia mapinduzi makubwa ya kiuchumi. Mapinduzi hayo huweza kuifanya nchi au hata mtu mmoja mmoja kubadilika kiuchumi katika muda mchache ajabu kutoka hali duni sana ya kiuchumi kuelekea hali bora zaidi ya kiuchumi au kutoka kuwa masikini na kuwa tajiri. Kwa hiyo tunaweza tukasema kwamba viwanda huleta neema, viwanda huleta utajiri na kiwanda kina uwezo mkubwa wa kumfanya mtu aondokane na umasikini wa kutisha.

Unaweza ukachunguza mifano midogo tu mazingira yanayokuzunguka, hebu angalia watu wenye viwanda vidogo vidogo vifuatavyo, mashine ya kukamua juisi ya miwa, mashine ya kuchonga viazi vya chipsi, kiwanda cha chakula cha mifugo, mashine ya kusaga na kukoboa nafaka, mkulima anayemiliki trekta au jembe la maksai, kiwanda cha kukamua mafuta ya alizeti, mashine ya kufyatua tofali za umeme, cherehani ya umeme, mashine ya kukorogea unga wa kuokea keki au mikate, mashine ya zege nk.

Bila shaka shughuli au viwanda vidogo nilivyovitaja hapo juu, huweza kufanyika kwa urahisi sana na bila shaka yeyote ile wale wanaozifanya au kumiliki mashine hizo, hali zao za kiuchumi haziwezi zikafanana na zile za wale wanaofanya shughuli hizo kienyeji kwa mikono bila ya kutumia mashine.

Ingawa dhana ya kiwanda ni pana zaidi ya mashine kwa maana ya kuhusisha michakato mingine mingi kama vile soko, ufungashaji(packaging) na suala la biashara kwa ujumla, lakini kikubwa hapo suala la kutumia nyenzo au mashine huwa na umuhimu mkubwa na wa kipkee zaidi.

KIWANDA KIDOGO CHA KUTENGENEZA JUISI YA MATUNDA KWA KUTUMIA MTAJI MDOGO.
Hakuna ubishi wowote kwamba changamoto iliyo kubwa zaidi baada ya mjasiriamali kupata wazo la biashara yake ni jinsi ya kupata mtaji wa kutosha wa kuanzisha biashara hiyo. Wajasiriamali wengi hupata wazo la kuanzisha viwanda vya juisi ya matunda na hilo hutokana na Mikoa mingi ya Tanzania hasa ile Mikoa ya Kaskazini kama Tanga na Morogoro na baadhi ya Mikoa ya kanda ya Kusini kama vile Iringa na Mbeya kuwa inazalisha matunda mengi sana na ya aina mbalimbali lakini matunda hayo wakati wa msimu hufurika sokoni na mwishowe kuozea mashambani bila faida yeyote ile kwa wakulima.

juisi nzuri ya matunda
Karibu kila tunda hutoa juisi
Karibu kila tunda linaweza kusindikwa na kisha kwenda kuuzwa hata baada ya msimu wake kuisha lakini tatizo mara nyingi huwa ni gharama za kununulia mshine kwa ajili ya usindikaji. Hata hivyo wakati mjasiriamali unasubiri uweze kupata mtaji kwa ajili ya kuanzishia kiwanda cha kutengeneza juice ya matunda, unaweza ukaanza kutengeneza na kuuza juisi hizo kwa kutumia mashine rahisi unazoweza kumudu gharama yake na ukakidhi mahitaji makubwa ya wateja ambao inabidi kwanza uchunguze na kubaini ni kitu gani wanachopendelea zaidi kwenye juisi za matunda. Anza hata na blenda na friji yako ya nyumbani.


Aina za juice za matunda zinazopendwa sana na watu ni kama vile juisi ya ukwaju, juisi ya ubuyu, juisi ya passion, juisi ya miwa, juisi ya karoti, juisi ya parachichi, juisi ya limao, juisi ya papai, juice ya tende, juisi ya ndizi,  juice ya embe, juisi ya chungwa, juisi ya zabibu, juisi ya tikitimaji, juice ya nanasi,  mchanganyiko wa juice ya parachichi na passion, parachichi na embe, mchanganyiko a juisi ya embe na chungwa nk.

SIRI KUBWA YA MAFANIKIO KATIKA KIWANDA KIDOGO CHA KUTENGENEZA JUICE MBALIMBALI ZA MATUNDA.
Kiwanda hata kiwe kidogo kiasi gani, ni lazima uhakikishe ile misingi mikuu ya biashara inazingatiwa ili kupata matokeo yaliyokuwa bora kabisa. Misingi hiyo iliyoainishwa katika kitabu cha MICHANGANUO YA BIASHARA NA UJASIRIAMALI ni kama vile, kufanya utafiti wasoko(upembuzi yakinifu), kutengeneza mpango wa biashara nk. Vitu hivi na vinginevyo kama kutafuta soko, uwekaji wa kumbukumbu nk. ni muhimu sana katika kuhakikisha kiwanda au biashara inafanikiwa.

Mbali na sababu mahsusi utakayobaini mwenyewe katika utafiti wako wa soko utakaoufanya kwa mujibu wa kitabi hicho, lakini kuna hii sababu ambayo ipo kotekote(ni universal) kwa mtu yeyote yule anayefanya biashara ya kutengeneza na kuuza juisi ya matunda, awe ni mtengenezaji mdogo mdogo anayetembeza na jagi barabarani au mwenye kiwanda kikubwa kama Bakhresa na Dewji. Ni muhimu sana kuifahamu siri hii, kwamba wanywaji wote wa juisi za matunda duniani kote wanapenda kunywa juisi SAFI, SALAMA NA INAYOBURUDISHA.

Nayasema hayo kwa sababu katika utafiti wangu mitaani nimewahi kuona jinsi wauzaji wengi wa juisi hizi za kutembeza na majagi, madeli au ndoo wanavyokosa wateja bila ya wao wenyewe kujua sababu hasa ni nini. Na mjasiriamali akishaona leo amemwaga juisi, kesho tena hivyo hivyo, hukata tamaa na kuona biashara ya kuuza juisi ni biashara kichaa isiyokuwa na faida, huiacha na kwenda kujaribu biashara nyingine.

Katika kuhakikisha USAFI NA USALAMA wa juisi, vigezo ambavyo ndiyo siri kubwa ya mafanikio katika biashara au kiwanda cha juice mbalimbali za matunda, mjasiriamali ni lazima uzingatie sana suala la KIFUNGASHIO cha juisi yako. Juisi hata iwe tamu kiasi gani lakini usafi na usalama wake unapokuwa wa mashaka mteja huwezi kumshawishi anunue kwako kamwe.

SOMA: Wateja wanahitaji sababu ya kununua kutoka kwako.

Hebu jiulize ni mara ngapi wewe mwenyewe umekutana na juisi za kupima huko mitaani, ukapuuzia kununua kwa sababu tu, wanapima kwa kikombe ambacho husuuzwa kwa maji ya kawaida pindi mteja mmoja anapomaliza kukitumia na kuwekewa mteja mwingine?. Wakati mwingine unaweza ukaona juisi nzuri sana inayovutia machoni lakini unashindwa kununua kwa sababu tu juisi hiyo imetiwa katika chupa au kopo la maji ambalo muuzaji aliliokota baada ya mtumiaji kumaliza kunywa maji na kulitupa, je usalama wake ni wa kuridhisha? Je, unafikiri ikiwa muuzaji wa juisi hiyo kama anashindwa kuwa na kifungashio cha uhakika basi na uandaaji wake utakuwa makini?

Kama mjasiriamali mwenye malengo na maono ya kuja kumiliki kiwanda chako cha kusindika juisi za matunda mbalimbali ndani ya Tanzania ijayo ya viwanda, basi huna budi kuhakikisha wateja unaowauzia juisi yako unawaondolea mashaka yote yaliyoainishwa hapo juu. Ikiwa utashindwa kuwaondolea mashaka wakati huu ukiwa na kiwanda kidogo basi ujue hata utakapomiliki hicho kiwanda kikubwa hautaweza pia.

VIFUNGASHIO BORA VYA JUISI KWENYE KIWANDA CHAKO KIDOGO CHA JUICE ZA MATUNDA.
Ikiwa juisi yako unauzia dukani, mgahawani au kwenye kioski, hakikisha vyombo unavyohifadhia juisi na kuwapimia wateja ni visafi muda wote na kila siku unaviosha kwa maji ya moto na sabuni. Jitahidi uwawekee wateja juisi katika vikombe au glasi zile za kutumia na kutupa(takeaway) kwa usalama zaidi. Kama unatumia mashine ya kuchanganyia na kupoozea juisi(juice dispeser), usafi wa mashine uwe ni wa hali ya juu sana kila siku.

JUISI TAKEAWAY
Juisi ndani ya kifungashio safi  na salama.
Ikiwa unatembeza juisi yako barabarani, jaribu kuwa mbunifu kidogo, ni ukweli kwamba wapo wateja wasiojali kuhusiana na swala la usalama au usafi na hivyo kutumia juisi hata kama kifungashio chake ni makopo ya kuokota barabarani, lakini ukumbuke pia kwamba kuna idadi kubwa tu ya wateja wale wanaojali zaidi afya zao.

SOMA: Kufungua  kiwanda kidogo cha kusindika & kufungasha nafaka,  naomba ushauri. 

Hivyo unaweza ukawa na vifungashio vya aina mbili, aina ya kwanza hayo makopo ya bei ‘chee’ ya kuokota na aina ya pili ukawa na makopo yako au vyupa spesho vya kununua kutoka SIDO au kokote kule vinakopatikana na kuwaeleza wateja kwamba unazo chupa safi maalumu kwa ajili ya juisi. Au unaweza pia kutumia mikebe au vikombe vya kutumia na kutupa(takeaway) pamoja na mirija.

Vifungashio hivyo maalumu na visafi vinaweza kugharimu kiasi fulani cha fedha na hivyo kufanya bei ya juisi yako kuwa juu kidogo, lakini hiyo haiwezi kumzuia kununua juisi mtu anayejali afya yake. Hiyo ni mbinu au njia sahihi kabisa itakayokuhakikishia wateja wa uhakika na wa kudumu wa biashara yako ya juisi mpaka pale utakapopata mtaji wa kutosha kuagiza mashine zako kutoka China kwa ajili ya kufungua kiwanda kidogo cha kutengeneza au kusindika juisi za matunda mbalimbali ndani ya Tanzania mpya ya uchumi wa viwanda.

........................................................................................... 

Kitabu  chako hiki cha MICHANGANUO YA BIASHARA NA UJASIRIAMALI, kitakuwezesha kuyafahamu mambo yafuatayo kwa ufasaha katika kuifanya biashara yako kuwa yenye tija na ya kisasa zaidi; 
·       Maana halisi ya ujasiriamali,
·       Jinsi ya kuanzisha biashara,
·       Mbinu bora za kufanya utafiti wa masoko na biashara,
·       Namna ya kusajili biashara yako Brela, TRA, Manispaa nk.
·       Hatua kwa hatua jinsi ya kuandaa na kuandika -mchanganuo/mpango wa biashara yako,
·       Michanganuo halisi na kamili ya biashara zinazolipa,
·       Jinsi ya kuweka kumbukumbu na hesabu za biashara,
·       Namna ya kutoa huduma bora kwa mteja.
·       Kufanya mauzo kitaalamu na
·       Njia kuu wanazotumia matajiri kutajirika.

SOFTCOPY ya kitabu hiki kwa njia ya email ni sh. 10,000/=
uunatuma pesa na anuani yako ya email kupitia moja kati ya namba hizi; 0712202244  au  0765553030  jina: Peter Augustino Tarimo.

HARDCOPY ni sh. 20,000/=, njoo stendi Mbezi kwa Msuguri au uletewe kwa shilingi, 22,000/= ukiwa jijini Dar es salaam. Mkoani tunatuma kwa mabasi kwa shilingi,30,000/= au unaweza kuagiza mtu anayekuja Dar akuchukulie.

VITABU VINGINE KUTOKA SELF HELP BOOKS TANZANIA NI HIVI HAPA chinni. 

SOFTCOPY   5,000/=
HARDCOPY 10,000/=



SOFTCOPY   3,000/=
HARDCOPY 5,000/=


Au tembelea, SMART BOOKS TANZANIA kupata maeelezo na vitabu zaidi.


2 Responses to "KUANZISHA KIWANDA RAHISI CHA JUISI YA MATUNDA, TANZANIA YA VIWANDA YAJA JIANDAE"