BIASHARA YA KUUZA CHAKULA USIPOKUWA MSAFI UTAIONA CHUNGU | JIFUNZE UJASIRIAMALI

BIASHARA YA KUUZA CHAKULA USIPOKUWA MSAFI UTAIONA CHUNGU

mbwa akiramba sahani ya chakula mgahawani
Kila biashara ina siri yake ya mfanikio ambayo mjasiriamali asipoizingatia basi hawezi kuona mafanikio aliyolenga kuyapata. Kwa upande wa biashara ya chakula, inaweza ikawa ni mgahawa, hoteli, mama na baba lishe au biashara yeyote ile inayohusisha vitu vinavyoliwa na binadamu, siri yake kubwa ya kupata wateja wengi na wa kudumu ni kudumisha usafi wa hali ya juu.

Mpaka naandika makala hii leo ni matokeo ya uchunguzi wangu binafsi baada ya kuwa kila mara napita eneo fulani panapouzwa chakula hususani kifungua kinywa nyakati za asubuhi. Mahali hapo kila nipitapo asubuhi huwa naona pana watu na wameketi wakinywa chai, supu na vitafunwa mbalimbali. Mimi ni mpenzi sana wa supu na kila mara huwa natamani nijiunge pale siku moja ili na mimi nipate japo supu kidogo na chapati. Lakini kwa kuwa mara nyingi nakuwa tayari nimeshapata kifungua kinywa nyumbani basi huwa ‘napotezea’ na kujisemea moyoni, “lakini ipo siku tu nitapata supu pale”


Ikaja siku hii ambapo nilitoka zangu nyumbani sijapata chochote nikasema sasa leo ndiyo siku ya kutimiza ile dhamira yangu, ninywe supu ya moto pale katika ile café pamoja na chapati zangu mbili au tatu. Wakati nasogelea pale kwenye ule mgahawa, kumbuka siyo mgahawa mkubwa ni eneo tu uswahilini la wazi lililozungushiwa ua na viti aina ya mabenchi. Niliweza kuwaona mbwa wawili wakirandaranda eneo karibu kabisa na vyombo vinavyotumika pale mgahawani, nikashtuka na hamu yote ya supu ikaniisha kabisa.

Nilizuga kama vile naulizia bei ya supu wakanijibu ni shilingi elfu moja na mia tano, nikajibu asante na kugeuza kisogo nikaondoka zangu. Nia yangu ya kunywa supu pale siku moja ikawa ndiyo imeishia palepale. Siyo kila mtu huona kinyaa kwa wanyama kama mbwa au paka lakini ni watu wengi huwa hawapendi wanyama hao kuwaona maeneo ya chakula, wana kawaida ya kuramba vyombo kama sahani, masufuria  na hata vijiko ikiwa wataachiwa kiholela.

Ni vizuri kabla hujachagua eneo utakaloweka biashara yako ya chakula basi ukahakikisha eneo hilo wanyama kama hawa hawafunguliwi ovyoovyo, hata ikiwa jirani na hapo wapo basi tafuta njia yeyote ya kuwazuia wasikaribie eneo lako la biashara kwani watakupotezea wateja wengi. Siyo mbwa tu kuna hata paka nao huwa kero sana maeneo ya nayouza vyakula kwa kuwasongasonga wateja na mikia yao wakitaka wapewe mifupa au nyama. Wakati mwingine hata hudondoshea manyoya kwenye vyakula.

Wapo watu wengine huamua kufuga paka ndani ya maduka yao ya vyakula kwa lengo la kukomesha panya, ni lengo zuri lakini kwa mteja anayezijua vyema tabia za mnyama huyu paka, kamwe hataweza kuwa mteja wako mzuri wa vitu vya kupima kama unga, mchele na sukari. Paka wana tabia moja ya ajabu sana, hupenda kujisaidia haja mchangani au katika vitu vinavyofanana na mchanga kama vile unga, sukari na mchele.


Eneo la kuuzia chakula pia halitakiwi liwe na panya kwa mfano mteja anaweza kuwa anakula chakula ghafla anamuona panya akikatiza njia kwenye kona za chumba cha mgahawa, mteja huyo inaweza ikawa ndiyo siku yake ya mwisho kufika katika mgahawa wako kwani akilini mwake atajenga picha kwamba mapanya hurambaramba vyombo vya chakula usiku au hata kula vyakula vilivyohifadhiwa na kwa mfanyabiashara asiyejali hawezi kutupa nyama, mboga au tunda lililoliwa na panya badala yake atakata kidogo eneo lililoliwa na kuuza hivyohivyo.

Inzi nao ni kikwazo kikubwa kinachowafanya wateja kuwa mbali na biashara yako ya chakula, inzi huwa hawapendi usafi na hiyo ndiyo dawa yao pekee ya kuwafanya wasisogee. Biashara kama ya chipsi, mishikaki, biashara ya juisi, biashara ya nyama, biashara ya utumbo nk mara nyingi inzi hupendelea sana biashara hizi lakini mjasiriamali makini unatakiwa ubuni njia zitakazozuia ama kuhakikisha inzi hao hawawezi kuwa kero kwa wateja wako wanaofika kununua.

........................................................................................................

Mpenzi msomaji wa makala hii, ikiwa unapenda kujifunza biashara na ujasiriamali kwa kina kabisa, basi jipatie vitabu vya self help books kupitia email yako kwa bei rahisi kabisa ya punguzo msimu huu wa sabasaba. Ni shilingi elfu 15 tu badala ya elfu 18 kwa vitabu vyote 3 hapo chini na unatumiwa mara moja unapolipia kupitia namba 0712202244  au  0765553030 jina Peter Augustino Tarimo.

     





AU tembelea SMART BOOKS TANZANIA kwa maelezo zaidi.

0 Response to "BIASHARA YA KUUZA CHAKULA USIPOKUWA MSAFI UTAIONA CHUNGU"

Post a Comment