SIKU 4 TAREHE 28/12/2022 KUANDIKA MCHANGANUO WA BIASHARA YA UPENDO CAFE HATUA KWA HATUA | JIFUNZE UJASIRIAMALI

SIKU 4 TAREHE 28/12/2022 KUANDIKA MCHANGANUO WA BIASHARA YA UPENDO CAFE HATUA KWA HATUA

Cafe-upendo

MPANGO WA UENDESHAJI, UONGOZI & WAFANYAKAZI

 

6.0 UENDESHAJI

Mara nyingi kipengele hiki hutegemea kama biashara inahusisha shughuli nyingi za kiuendeshaji mfano kiwanda, au hata biashara ya uzalishaji bidhaa kama hii ya chakula. Ni kipengele wakati mwingine kinachojitegemea na ndio maana hata kwenye mchanganuo huu wa Upendo kimepewa sura yake chenyewe ya 6.

Ikiwa uendeshaji kwenye aina ya biashara yako hauna mambo mengi basi unaweza kujumuisha vipengele vyake kwenye Sura ya mikakati na utekelezaji kwani utekelezaji na uendeshaji ni kitu hichohicho kimoja.

Kwenye sura hii ya Uendeshaji  kwa kawaida huwa na maelezo ya jinsi biashara itakavyoendesha mambo mbalimbali kila siku. Hapa chini ni vipengele vidogo mbalimbali unavyoweza kuvitumia katika sura hii; 

 

1. Hatua mradi ulipofikia mpaka sasa hivi

2. Mchakato mzima wa uzalishaji utakavyokuwa

3. Teknolojia/maelezo ya kiufundi

4. Vihatarishi vya mradi

5. Eneo 

6. Vifaa na gharama mbalimbali

7. Malighafi na vyanzo vyake

8. Masuala ya kisheria

9. Sera ya mikopo nk. 

Kama nilivyotangulia kusema, unaangalia tu vile vipengele vinavyofanya kazi kwenye biashara yako, vingine kama unaona haviendani unaachana navyo, kwa mfano kwenye biashara hii ya Upendo waliweka vipengele vifuatavy katika sura yao ya uendeshaji;

Kwanza kwenye Muhtasari wa Sura waliweka maelezo kidogo ya namna mchakato mzima wa uendeshaji wa shughuli za biashara unavyofanyika kila siku kisha chini vikaendelea vipengele vingine vidogo vya;

1)  Eneo au Chumba cha biashara

2)  Mahitaji ya Kisheria

3)  Tathmini ya Vihatarishi vya Mradi

4)  Vifaa na mashine

5)  Mauzo na Gharama mbalimbali

Hapa ndipo unapoweza kuonyesha kwa kina jinsi mauzo na gharama zako zitakavyokuwa na namna ulivyokisia. Kwa mfano katika kukisia Mauzo ya siku na gharama zake, Upendo walichora jedwali na kuweka safu ya Gharama na mauzo ambapo kwa kila aina ya chakula yaliwekwa makisio ya mauzo yake kwa siku na kisha orodha ya gharama za kila aina za vyakula hivyo na jumla yake. Kwa njia hiyo waliweza kupata jumla ya mauzo yote ya siku na gharama za mauzo hayo ambazo pia zimeweza kutabiri mauzo ya mwezi na mwaka.

Hapa pia unaainisha gharama zote za kudumu za uendeshaji wa biashara yako kama Upendo walivyoainisha kwenye jedwali hili hapa chini;

..............................

 

Tumemaliza Sura au Sehemu yetu ya Uendeshaji sasa tuingie Sura nyingine ya Uongozi na Wafanyakazi

 

7.0 UONGOZI & WAFANYAKAZI

Maelezo haya pia unaweza ukayaita maelezo ya Utawala na Nguvukazi. Kama kawaida Sura inaanza na muhtasari mdogo unaoandikwa mwishoni na unaacha kwanza nafasi ya aya moja hivi. Kisha unazingatia vipengele vidogo vinavyounda sura hii ambavyo mara nyingi huwa ni hivi hapa chini; 

7.1 Mfumo/Muundo wa uongozi

 7.2 Timu ya uongozi na wafanyakazi

 7.3 Mpango wa mishahara 

7.1 Muundo wa Utawala

Hapa unaweza ukapaelezea tu kwa maneno ikiwa ni biashara ndogoisiyo na wafanyakazi wengi au kama watu ni wengi basi unaweza ukatumia mchoro/chati ya utawala. 

7.2 Timu ya uongozi na wafanyakazi

Taja kila kiongozi, wadhifa wake kwenye kampuni, historia yake kitaaluma na kikazi pamoja na uzoefu aliokuwa nao kulingana na majukumu atakayokuwa nayo kwenye kampuni. Eleza pia idadi ya wafanyakazi watakaohitajika, eleza pia kama kuna mapungufu au pengo la utawala kama kuna watu wanaohitajika lakini bado nafasi zao hazijapata watu na sababu za upungufu huo.

Kwenye Upendo Cafe baada ya muhtasari wa sura nzima walielezea mfumo wa utawala kwa maneno kwani biashara haina bado watu wengi;

Timu yetu itakuwa na Mkurugenzi mtendaji mmoja na msaidizi wake ambao wote ni waanzilishi wenza, mmoja atashikilia nafasi ya mpishi muu na mwenzake mtu wa manunuzi ya malighafi na vifaa mbalimbali vya biashara. Kutakuwa pia na wafanyakazi wawili, mmoja atashughulika na kazi ya kuhudumia wateja wakati mwingine atamsaidia mpishi mkuu jikoni

Kisha walimuelezea kila kiongozi, majukumu yake na sifa zake.

 

7.3 Mpango wa Mishahara

Katika kipengele hiki kidogo unaanza na maelezo kidogo kisha unachora jedwali linaloonyesha kiasi cha mishahara ya wafanyakazi wote kwenye kampuni kwa kila mwaka kwa miaka yote mitatu. Unaanza kwa kujumlisha mishahara ya mfanyakazi mmoja mmoja kila mwezi kisha kwa mwaka. Namba hizi ndio huja kuunganishwa na gharama nyingine za kudumu  kwenye ripoti ya Faida na Hasara hapo baadae kwenye ripoti za fedha;

...............................................

Mpaka hapo tumemaliza vipengele vyetu kwa siku ya leo tukutane tena kesho kwa sehemu ya mwisho ya Taarifa za fedha.


Masomo haya yanatolewa ndani ya group la MICHANGANUO-ONLINE kila siku na hii ni sehemu ndogo tu ya somo la leo. Ili kupata masomo kamili pamoja na masomo yote mengine ya siku za nyuma jiunge na group hilo kwa kulipia ada kidogo ya mwaka shilingi 10,000/=. Unaweza kutumia moja kati ya namba zetu hizi, 0712202244 au 0765553030 jina Peter Augustino Tarimo.


Wahi leo kabla zawadi yetu ya mwisho mwaka huu ya vitu 22+ haijamalizika rasmi.

Kusoma dondoo za somo la fedha bonyeza maneno haya>> NJIA 9 ZA KUVUTA PESA, BAHATI & MAFANIKIO 2023

0 Response to "SIKU 4 TAREHE 28/12/2022 KUANDIKA MCHANGANUO WA BIASHARA YA UPENDO CAFE HATUA KWA HATUA"

Post a Comment