DIAMOND PLATNUMZ, BELLE 9 NA DARASSA WALIVYOMTOA TENA SAIDA KAROLI UPYA | JIFUNZE UJASIRIAMALI

DIAMOND PLATNUMZ, BELLE 9 NA DARASSA WALIVYOMTOA TENA SAIDA KAROLI UPYA

DIAMOND PLATNUMZ, SAIDA KAROLI, DARASSA NA BELLE 9
Malkia wa muziki wa asili nchini Tanzania na Afrika ya Mashariki Bibi Saida Karoli aliyetamba mwanzoni mwa miaka ya 2000 na vibao vyake maarufu kwa lugha ya Kihaya na kiswahili vya Maria Salome(Chambua kama Karanga), Kaisiki, Ndombolo na Mimi nakupenda, anatuthibitishia dhahiri kabisa kwamba kufulia ama kuanguka kimaisha siyo mwisho wa dunia bali inawezekana kabisa mtu akaibuka tena au kwa maneno mengine kujirudishia tena ukuu wako uliopotea.(#makeyourselfgreatagain)

Kama unakumbuka na upo sambamba na blogu hii, mwanzoni mwa mwaka huu wa 2017, tulianzisha kampeni tuliyoipa jina, KUJIRUDISHIA TENA UKUU WAKO ULIOPOTEA au MAKE YOURSELF GREAT AGAIN, kampeni ambayo tulisema itakuwa ni ya mwaka huu mzima kuhakikisha kwamba wale wote ambao wangependa kufanya mabadiliko makubwa maishani mwao na kurudisha hali zao mbalimbali walizokuwa nazo hapo mwanzo lakini kwa sababu mbalimbali wakaja kuzipoteza basi wanafanya hivyo.

Ukuu wako uliopotea waweza kuwa ni hali yako kiuchumi, afya, kiimani, mahusiano, heshima nk. Sasa hivi miezi 6 imekatika na hatuna budi sasa kufanya tathmini ya kampeni yetu hii tulikotoka na tunakoenda miezi mingine tena 6 ijayo. Kumbuka bado safari inaendelea na ndiyo maana ukaona leo hii nimeamua kukuletea mfano huu wa Saida Karoli pamoja na Diamond Platnumz, Belle 9 na Darassa, ushirikiano wao katika kibao maarufu cha muziki, chambua kama karanga au salome wangu ambacho kilitungwa na mwana mama huyu Saida Karoli. enzi za ukuu wake alipokuwa katika kilele cha ubora katika muziki wa asili nchini Tanzania na Afrika wa ujumla.

Kuibuka na kuanguka kwa Saida Karoli miaka ya 2000 Mwanzoni.

Saida mwenyeji wa Mkoa wa Kagera jirani na nchi ya Uganda alianza shughuli zake za muziki rasmi mwaka 2001 kwa kutoa albamu iliyoitwa Maria Salome au maarufu kama Kanichambua kama karanga(Wanchekecha) chini ya meneja Felician Muta, mkurugenzi wa kampuni ya FM Production ltd, Saida alipata umaarufu ndani ya kipindi kifupi na akaweza kupata mialiko sehemu mbalimbali za Afrika Mashariki na kati kama vile Burundi, Rwanda, Uganda katika sherehe za kutumbuiza hafla ya mfalme Kabaka na hata baadhi ya nchi za Ulaya.


Katika mahojiano yake mwenyewe na vyombo mbalimbali vya habari nchini Saida Karoli mwenyewe anakiri kwamba sababu kubwa ya yeye kuja kuanguka kimuziki na maisha yake kuwa duni tena kiasi cha kuamua kuishi maisha ya kujifiha kulitokana na kushindwa kusimamia mapato yake vizuri wakati mambo yalipokuwa mazuri. Anasimulia kwamba alikuwa haelewi ni nini maana ya mikataba wala kudai stahili za malipo yake aliyopaswa kulipwa kutokana na mikataba mbalimbali aliyoingia. Anadai hata kudai stahili za matumizi ya nyumbani kutoka kwa mumewe alikuwa hajui, sembuse malipo kutokana na kazi zake za kisanii.

Kutokana na hali hiyo alifika mahali akajuikuta anaanguka vibaya kiuchumi kiasi ambacho aliogopa hata kuonana tena na waandishi wa habari amabao mwanzoni ndio waliochangia kwa kiasi kikubwa kumtangaza kwa jamii. Waandishi wa habari hata hivyo hawakukata tamaa, wakaamua kumfuata hadi kijijini huko ndanindani lakini bila mafanikio yeyote jambo lililosababisha hata wengine kuvumisha kwamba Saida Karoli amefariki Dunia kumbe haikuwa kweli.

Kuzaliwa tena upya kimuziki kwa Saida Karoli mwaka 2017

Ndipo mwishoni mwa mwaka 2016 September zikaanzaa kuibuka tetesi kwamba mwanamuziki nguli nchini Tanzania wa Bongo Fleva Naseeb Abdul au Diamond Platnumz na Reyvanny  wameiba mashairi ya wimbo wa Saida Karoli, Salome(Chambua kama karanga) bila kumlipa chochote. Tetesi hizo hata hivyo hazikuwa na ukweli wowote kwani baadae ilibainika kulikuwa na makubaliano fulani. Siyo Diamond tu aliyetumia vionjo na mashairi ya Saida Karoli, Belle 9 na Darassa pia nao wamewahi kufanya hivyo.


Lakini kumbe kitendo cha wasanii hao kutumia vionjo na mashairi ya Saida Karoli kulikuwa na maana kubwa sana kwani ndiko kulikomhamasisha tena upya na kumfanya Saida kuibuka tena upya. Saida Karoli amewashukuru sana wasanii hao na kujifananisha kama vile amezaliwa tena upya kimuziki. Baada ya kuamua kurudi tena upya Saida naye kama kurudisha fadhila kwa wasanii hao naye ameamua kuimba katika albamu yake mpya na wimbo wa Orugambo vionjo kutoka katika vibao mbalimbali vya wanamuziki hao, Belle 9, Diamond na Darassa.

Katika wimbo wa Saida Karoli Orugambo, anasikika akitaja maneno acha maneno, weka mziki ambayo ni kionjo kilichopo ndani ya kibao, Maisha na muziki cha mwanamuziki wa bongo fleva Darassa. Mchanganyiko huo wa muziki wa asili wa zamani kidogo na muziki wa kizazi kipya au bongo fleva umetengeneza ladha nzuri ya kuvutia.

Kitu kikubwa tunachoweza tukajifunza kutoka kwa wanamuziki wote hawa, Saida Karoli, Diamond, Darassa na Belle 9 ni umuhimu wa kushirikiana katika kuhakikisha mambo yanakwenda mbele. Saida Karoli angeendekeza ubinafsi bila shaka angeonyesha upinzani mkubwa kwa kazi zake za muziki kukopiwa na wasanii wa kizazi kipya, lakini uvumilivu wake na kutambua mapema fursa iliyokuwepo kwa wasanii wenye majina kukopi nyimbo zake imemsaidia na yeye kurahisisha kazi yake ya kujirudishia tena ukuu wake uliokuwa umepotea ukiachilia mbali malipo yeyote yale ambayo labda wamempatia.  

Kwa maana hiyo hapa hakuna aliyepoteza, kila mtu amepata na ni jambo la kupendeza sana.


Ndugu msomaji wa makala hii, kampeni yetu ya kujirudishia tena ukuu wako uliopotea, bado inaendelea na katika nusu nyingine ya pili ya mwaka huu iliyobakia tumeamua kuihuisha tena upya. Fuatana nasi mpaka mwisho ili Desemba Mungu akipenda tupate shuhuda za watu wengi waliofanikiwa kurudisha tena ukuu wao kama dada yetu Saida Karoli anavyofanya sasa.


Kampeni hii ni kupitia mitandao ya kijamii ikiwemo blogu hii ya jifunzeujasiriamali, facebook, twitter, you tube, vitabu mbalimbali vya Self Help Books kama hivi hapa pamoja na mitandao mingine yote ya kijamii. 

0 Response to "DIAMOND PLATNUMZ, BELLE 9 NA DARASSA WALIVYOMTOA TENA SAIDA KAROLI UPYA"

Post a Comment