KUFUNGUA KIWANDA KIDOGO CHA KUSINDIKA & KUFUNGASHA NAFAKA, NAOMBA USHAURI | JIFUNZE UJASIRIAMALI

KUFUNGUA KIWANDA KIDOGO CHA KUSINDIKA & KUFUNGASHA NAFAKA, NAOMBA USHAURI

mashine za kusaga na kukoboa nafaka
Ni makala nyingine tena leo inayohusiana na kipengele cha Ushauri. Huwa tunajibu maswali na changamoto mbali mbali ambazo baadhi ya wasomaji wa blogu hii hukumbana nazo katika maisha yao ya kila siku ya biashara na ujasiriamali. Katika swali la msomaji mmoja ambaye nampa jina lisilokuwa halisi ‘Alex’(hatutaji majina halisi ya wanaouliza maswali bila idhini yao) aliuliza kupitia ujumbe wa simu yake ya mkononi kama ifuatavyo;

Habari Kiongozi, mimi naitwa ‘Alex’, ninao mpango wa kuanza kufanya mchakato wa kuanzisha biashara ya mazao ya nafaka yaani kununua mahindi na mpunga kisha nikoboe, kusaga, na kuuza unga wa sembe dona na mchele ukiwa kwenye vifungashio vyake. Je unaweza kunisaidia vitabu au miongozo ya kufanya biashara hii, kama kiwanda changu kidogo?

Bila shaka Alex kulingana na maelezo ya swali lake atakuwa alikuwa amesoma makala nyingine katika blogu hii iliyosema; Jinsi kiwanda kidogo kinavyoweza kukutoa kimaisha na kuwa tajiri wa kutupa. Jibu zuri(the best aswer) nililoweza kumpatia msomaji wetu huyu anayetaka kuwekeza kwenye biashara ya kuuza nafaka nimeliweka hapa chini kusudi na wasomaji wengine nao waweze kunufaika nalo.

Ndugu ‘Alex’ asante sana kwa swali lako ulilotaka kujua ikiwa unaweza kupata vitabu vya muongozo katika kuanzisha na kuendesha biashara ya mazao ya nafaka. Kwa kweli kiujumla biashara ya nafaka Tanzania inalipa na miongoni mwa biashara ndogondogo za mtaji mdogo ingawa pia unapokuwa na mtaji mkubwa au wa kati biashara hii ya nafaka ndiyo inaweza kukutajirisha haraka.

Kwa upande wa vitabu au miongozo ya jinsi ya kuanzisha biasharaya kukoboa, kusaga, kupaki(kufungasha) au usindikaji wa bidhaa zitokanazo na nafaka kwa ujumla, kwa kweli vitabu tulivyokuwa navyo sisi Self Help Books Tanzanai kwa sasa hivi ni vitabu vile tu vinavyohusiana na kutoa elimu ya biashara na ujasiriamali kwa ujumla wake na siyo kwa biashara moja moja ingawa baadaye tuna mpango wa kutoa vitabu vya namna hiyo.

Biashara moja moja huwa tunazizungumzia zaidi katika makala zetu tunazopost katika blogu hii, blogu nyinginezo na katika mitandao ya kijamii. Hata hivyo katika kitabu chetu cha MICHANGANUO YA BIASHARANA UJASIRIAMALI kuna michanganuo ya baadhi ya biashara moja moja, ambayo waweza kuifananisha na miongozo lakini siyo miongozo ni mipango ya biashara.  

Hata hivyo ndugu yangu ‘Alex’ usikate tamaa, kwani siyo jambo gumu hata kidogo kuanzisha biashara hii ya nafaka ikiwa utaamua kufanya utafiti wa soko lako wa kutosha na kuifahamu biashara yenyewe nje ndani. Na kwa bahati njema utafiti wenyewe ndiyo kama huu hapa ambao tayari wewe mwenyewe umekwishaanza kuufanya pengine pasipo hata kujua. Kitendo chako cha kuingia kwenye mtandao wa intaneti na kuanza kutafuta jinsi ya kufanya biashara ya kusaga unga au nafaka ilikuwa ndiyo hatua yako ya awali kabisa ya utafiti, ona sasa umefikia hatua ya kukutana na mshauri wa maswala ya biashara na ujasiriamali kwenye blogu ya jifunzeujasiriamali, nami bila ya hiyana yeyote ile, naendelea kukupa mbinu zaidi ni vipi utaweza kufanikisha biashara hiyo.


Unaweza usiweze kupata miongozo au vitabu vya namna ya kuanzisha duka la nafaka lakini kupitia vyanzo vingine mbalimbali vya taarifa kama vile intaneti, kuzungumza na watu wanaofanya biashara ya nafaka, watu wanaouza na kununua nafaka za aina mbalimbali mwishowe utajikuta umeshapata maarifa sahihi na utagundua kumbe biashara hiyo unaweza ukaifanya bila wasiwasi wowote ule.
biashara mazao ya nafaka, kusaga, kukoboa, kufungasha na kuuza
Mjasiriamali akisaga na kukoboa nafaka kwa kutumia mashine.
Ikiwa unataka kufanya biashara ya nafaka kwa kiwango cha juu zaidi, kwa mfano unataka uanzishe kiwanda cha kusaga na kukoboa nafaka za aina mbalimbalikwa jumla kama vile mahindi, mpunga na nyinginezo, utatakiwa pia kujua bei za mashine ya kusaga nafaka, kama vile mashine za kusaga mahindi, vinu vya kukoboa mchele au mashine ya kukoboa mpunga. Bei za vifaa kama hivi unaweza ukazipata kwa urahisi sana katika tovuti ya Alibaba ambao unaweza hata ukaagiza mashine hizo mtandaoni, lakini chukua tahadhari ya kutosha kabla hujaamua kununua vitu mtandaoni kuepuka kutapeliwa.

Vifungashio vya bidhaa au packing ya bidhaa zako zitokanazo na nafaka ni suala nyeti sana hasa ukizingatia siku hizi biashara yeyote ile ni matangazo na matangazo huanzia na lebo nzuri kwenye vifungashio pamoja na umbo zuri pia la kifungashio chako. Vifungashio vya mchele madhalani unaweza ukatumia vifungashio vya plastic au nailoni ngumu, kama unafanya packing ya kilo mojamoja, mbili mpaka tano. 

Kwa upande wa mahindi, vifungashio vya unga uwe ni wa dona au sembe unaweza ukatumia mifuko maarufu kama ‘mifuko ya sulphate’ ambayo huruhusu hewa kidogo kutoka. Halikadhalika vifungashio vya unga wa lishe unaweza ukatumia mifuko ya khaki, nailoni au mikebe ya aluminium. Kwa ujumla kuna aina nyingi sana za vifungashio kutegemeana na mahitaji yako ambavyo ukitaka kupata elimu yake kwa undani zaidi basi unaweza kuwaona watu wa SIDO wakakupa msaada.

Kikubwa zaidi ni kuwa kifungashio chako kiwe na nembo nzuri pamoja na taarifa muhimu kuihusu biashara yako au kampuni kama vile mawasiliano yako, nembo za uthibitisho wa ubora, viungo vinavyounda bidhaa yako pamoja na tarehe ya mwisho ya kuharibika bidhaa “expire date”


Ndugu ‘Alex’ natumaini kabisa kwamba majibu niliyokupatia kuhusiana na jinsi unavyoweza ukapata taarifa za kuanzisha biashara ya nafaka yatakupa mwanga bora katika mradi wako huu mpya unaopanga kuuanzisha, mwisho baada ya kufanya huo utafiti unaweza pia kuandika mchanganuo wa biashara na hiyo haipaswi kuwa kazi ngumu sana kwako, unaweza tu kwa kuorodhesha katika karatasi yale majukumu na mambo muhimu unayopanga kuyatekeleza katika mradi(biashara) yako na ukawa ndiyo mpango wako wa biashara. 

Kumbuka mpango mzuri wa ibiashara ni utekelezaji wake, unaweza ukapanga mambo machache tu ukayatekeleza vizuri na yakakupa matokeo mazuri sana ya kushangaza kuliko kama vile umepanga mambo lukuki bila ya kuyatekeleza vizuri, huwezi kupata matokeo yeyote yale ya maana.

Nakutakia kila la kheri katika mradi wako huo.
Mshauri na mwandishi wako
Peter Augustino Tarimo
Self Help Books Tanzania ltd
0712202244    au  0765553030

………………………………………………………………………..

Kwa vitabu mubashara vya elimu kuhusu maswala yote ya Ujasiriamali, Biashara na Maendeleo binafsi usiache kutembelea ukurasa wako huu wa; SMARTBOOKS TANZANIA

3 Responses to "KUFUNGUA KIWANDA KIDOGO CHA KUSINDIKA & KUFUNGASHA NAFAKA, NAOMBA USHAURI"

  1. Nahitaji kufungua kiwanda kidogo cha kukamua mafuta ya ufuta.Nianze na hatua gani ili nipate mafanikio makubwa.

    ReplyDelete