SETH KATENDE, MWANAUME UTAJIITAJE BIKIRA? | JIFUNZE UJASIRIAMALI

SETH KATENDE, MWANAUME UTAJIITAJE BIKIRA?

SETH KATENDE, MHAMASISHAJI, MJASIRIAMALI, MTANGAZAJI MAARUFU NA KOCHA WA VIJANA
Mazishi ya Seth Katende(Bikira wa Kisukuma) yaliyofanyika leo jumatano tarehe 12 Julai 2017 katika makaburi ya Kinondoni baada ya mwili wake kuagwa rasmi katika viwanja vya Leaders Club, jijini Dar es salaam yametoa taswira halisi ya maisha ya kijana huyo mdogo namna alivyoishi na kila kitu alichofanya katika miaka yake michache aliyoweza kuishi hapa duniani. 

Utata wa jina la Bikira wa Kisukuma.
Seth Katende a.k.a Bikira wa Kisukuma kwa kifupi alikuwa Mtangazaji wa redio, mhamasishaji, mjasiriamali, mwanamitandao ya kijamii(social media marketeer), na hata kocha wa maisha kwa vijana wenzake na makundi mengine mbalimbali katika jamii. Seth kwa kifupi tu alikuwa ni mtu mwenye vipaji lukuki, alikuwa kijana wa kushangaza kwa mujibu wa maelezo ya watu mbalimbali kutoka kada tofauti waliohudhuria kumuaga pale leaders Club na baadaye mazishi yake makaburi ya Kinondoni wakiwemo viongozi wakubwa kutoka vyama na serikalini, wanahabari na wananchi wa kawaida.

SOMA: Siri za mamillionea 10 vijana chini ya miaka 30 na utajiri wao.

Mara ya kwanza kusikia jina la utani la Seth Katende katika redio ya EFM kwa kweli jina hilo hata mimi binfsi lilinipa ukakasi mkubwa na kusababisha nijiulize mwenyewe, “Huyu kijana ni mwanaume, itakuwaje ajiite Bikira wa Kisukuma, haoni haya?”. Hali hiyo ikanisukuma nitake zaidi kujua habari zake, akili yangu moja kwa moja ikiniambia “huyu inawezekana kabisa akawa miongoni mwa wanaume mashoga maarufu kama ‘mtoto si riziki’”. Na kwa kweli nilipo google jina lake nilishangazwa na kukutana na 'comments' nyingi kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii ambazo nazo zilikuwa na dhana ileile niliyokuwa nayo mimi. Wengine hata walienda mbali zaidi na kufikia hatua ya kumtusi.

Lakini nilizidi kuingiwa na tashwishi ya kumfahamu zaidi kwani haikuniingia akilini kabisa watu wa EFM wampe kazi, tena ya utangazaji wa kipindi maarufu cha Ubaoni kijana mwenye tabia na vitendo visivyokubalika na jamii kubwa ya watu hasa Waafrika. Niliingia karibu kila mtandao wake wa kijamii ukiwemo facebook, twitter na Instagram, lakini nilichokutana nacho huko kwa kweli kilinistua. Ukijaribu kusoma mambo aliyokuwa akiandika Seth huwezi kabisa kuamini kama ni yeye yule unayemuona katika picha na wala havilingani kabisa na umri aliokuwa nao. Uthibitisho nimekuja kuupata leo pale Leaders Club.

Nilijikuta namaliza karibu usiku mzima nikisoma posts za mtu ambaye hapo awali nilidhani alikuwa mtu wa hivihivi tu. Tena kilichonishangaza zaidi ni kwamba kijana huyu alikuwa akifanya vitu vinavyofanana sana na vile nifanyavyo mwenyewe kwenye mitandao, kuelimisha na kuhamasisha juu ya elimu ya ujasiriamali na maendeleo ya mtu kwa ujumla.

SOMA: Mfahamu kijana mbunifu mkubwa wa majengo duniani aliyezaliwa Tanzania.

Lakini bado nilizidi kujiuliza, hili jina Bikira wa Kisukuma maana yake ni nnini? Alikuwa akimaanisha kitu gani, chanzo chake ni nini, lakini mpaka leo hii sikuwa nimepata jibu lililokuwa dhahiri. Lakini niliposikia yeye mwenyewe akilitaja redioni bila aibu yeyote, wafanyakazi wenzake akiwemo Gadner G. Habash na Mpoki wakilitaja bila kumungunya maneno na hata mabosi wake kama meneja wake Denis Sebo wakilitaja jina la Bikira wa Kisukuma bila wasiwasi nikashawishika kabisa kwamba jina hilo halikuwa na jambo lolote lile baya na lilipaswa tu kuchukuliwa kawaida kama lilivyo na kila mtu.

Utata wa jina hili la Bikira wa Kisukuma umefanya watu wengi kuwa na tafsiri nyingi hasi na chanya, tukiachana na zile hasi kama ile niliyokuwa nayo mwanzoni kabla sijamfahamu vizuri Seth Katende kama mtaalamu aliyebobea wa masoko katika mitandao ya kijamii na nje ya mitandao hiyo. Miongoni mwazo ni ile ambayo wanadai eti Seth alijiita hivyo akimaanisha kwamba yeye alikuwa na vipaji vingi mno ndani yake ambavyo vilikuwa bado kufanya kazi, maana ya neno bikra au bikira ni kitu ambacho bado hakijaguswa bado, bado kutumika. Hivyo vipaji vyake yeye kama kijana kutoka Usukumani vilikuwa bado kabisa vipya.

Lakini pia mimi mwenyewe binafsi nimefikiria dhana nyingine moja katika mtazamo wa kibiashara zaidi au kimasoko na ambayo inawezekana kabisa kuwa ndiyo iliyomfanya Seth kutumia jina hilo, “Branding” au kwa lugha nyingine kujijengea jina. Katika ulimwengu wa masoko, na hasahasa katika mitandao ya kisasa ya kijamii, branding ni kitu muhimu sana. Branding au kutengeneza jina maana yake ni kwamba, mhusika atajiita jina, kutengeneza mazingira, logo, au alama nyingine yeyote ile ambayo itamtofautisha na watu wengine wanaofanya kitu kinachofanana na cha kwake.

Unaweza kufanya hivyo pia kwa bidhaa au huduma unayoitoa. Mazingira hayo ya kipekee utakayowajengea wateja au wafuasi wako akilini mwao yanapaswa kuwa zaidi ya alama au jina, hali hiyo inatakiwa kuishi na kudumu akilini mwao na katika mioyo yao daima NA HICHO HASA NDIYO BIKIRA WA KISUKUMA ALICHOTAKA KIFANYIKE, NA LEO HII KUTHIBITIKA RASMI PALE LEADERS CLUB baada ya watu wengi kushuhudia jinsi walivyomfahamu Seth Katende.

SOMA: Kutafuta soko la bidhaa zako kunahitaji ubunifu mkubwa.

Kumbuka kuwa Seth alikuwa ni kijana na bila shaka alitaka kufikisha ujumbe wake kwa asilimia kubwa ya vijana. Hivyo hakuwa na budi kutumia lugha ambazo zingewavutia zaidi vijana na lugha ya picha kwa mfano kama hili jina "Bikira wa Kisukuma" ambalo ni tata lisilokuwa na maana ya moja kwa moja hasa ndiyo vijana wengi hupendelea. Si hivyo tu Seth niligundua pia alikuwa ana Domain name, jina la tovuti alilokuwa amesajili kwa ajili bila shaka kwa ajili ya website yake liitwalo "vituflaniflani.com" sasa hapo unaweza ukaona ni jinsi gani Seth alivyokuwa mtundu na mbunifu wa kutumia lugha inayotumika zaidi na vijana ili kufikisha ujumbe wake kwao.


Seth kama Mwanamasoko(Maketeer) mahiri, hakujali watu watamchukuliaje kujiita bikira ili hali yeye ni mtoto wa kiume, wala hakuogopa ikiwa baadhi ya watu wangemchukulia na kumhusisha isivyosahihi na watu wa mapenzi ya jinsia moja. Alichozingatia yeye ni kampeni zake za kimasoko mitandaoni jambo ambalo alifaulu kwa asilimia zaidi ya mia moja. Hata mimi binafsi nakiri kabisa kwamba ukakasi wa jina “BIKIRA WA KISUKUMA” ndio ulionisukuma kumfahamu kwa undani Seth Katende. 

Unapotaka kujenga jina imara la biashara yako au lako mwenyewe hupaswi kuyumbayumba, na inatakiwa kwanza wewe mwenyewe na wale wanaokuzunguka kuliamini na kulikubali jina lako vinginevyo wateja wa mbali hawataweza kufanya hivyo. Na kumbuka siyo jina kama jina ndiyo litakalojenga mahusiano mazuri na wateja bali ni zile faida kwa mteja, sifa njema au chochote kile kinachomridhisha mteja kinachoambatana na hilo jina ndicho kinachojenga huo mshikamano. Seth hata angejiita "Mfalme"  lakini alichokuwa akikifanya kikawa hakiwanufaishi chochote watu, hakuna mtu yeyote angeguswa na jina hilo. Lakini vyovyote vile angejiita yeye na jina hilo likiambatana na sifa njema au faida kwa wafuasi wake bado angekumbukwa tu.

Hivyo tunajifunza kwamba, tusiyumbishwe ovyo na maoni ya watu, bali tuangalie ni kitu gani sahihi tunachokifanya kwa manufaa ya wateja wetu au jamii tuliyoamua kuihudumia. Leo hii watu wengi hawahangaiki kutaka kujua sababu za kifo cha seth katende, wala hawataki kujua chanzo cha kifo cha Bikira wa Kisukuma, bali wanataka kujua Bikira wa Kisukuma, Seth Katende ni kitu gani hasa cha tofauti alichokifanya mpaka watu wamuenzi kiasi hicho. Kilichomuua Bikira wa Kisukuma hakiwezi kuwa na uzito kama kile alichokifanya wakati wa uhai wake hapa duniani.

MUNGU AILAZE ROHO YA MAREHEMU MAHALI PEMA PEPONI AMEN.

0 Response to "SETH KATENDE, MWANAUME UTAJIITAJE BIKIRA?"

Post a Comment