MHOGO WA KUKAANGA UNAVYOLIPA DAR, NI BIASHARA WENGI HAWAIFAHAMU VIZURI

mihogo ya kukaanga na kachumbari(chipsi dume)
Muhogo ni zao linalochukuliwa kirahisirahisi na watu wengi duniani siyo tu hapa Tanzania lakini ndiyo zao ambalo kuanzia mizizi yake, shina mpaka majani, hakuna kinachotupwa, vyote huweza kutumika na kumletea binadamu faida kubwa kiuchumi, katika maswala ya lishe na hata katika suala zima la tiba mbadala, watu wengi hasa hapa bongo wamejenga imani kubwa kuwa kutafuna mihogo mibichi ni tiba ya kurudisha nguvu za kiume ingawa bado utafiti wa kutosha unahitajika kuthibitisha madai hayo.

Hakuna asiyezijua faida za muhogo angalao hata zile kuu na mengi sana yameshaandikwa juu kilimo bora cha zao la muhogo, matumizi mbalimbali ya zao la mihogo na jinsi muhogo ulivyokuwa na uvumilivu wa hali ya juu katika hali ya ukame na udongo usiokuwa na rutuba ya kutosha, mihogo inao uwezo mkubwa wa kuota na kustawi hata maeneo yaliyokuwa nusu jangwa huku yakitoa mazao bora kama kawaida. Mihogo haishambuliwi na magonjwa mengi sana kama mazao mengine zaidi ya ugonjwa wa batobato na ugonjwa wa michirizi ya kahawia au matekenya ambayo yote husababishwa na virusi.

Katika mfululizo wetu wa makala za biasharazilizosahaulika lakini zenye kulipa, bado kama nilivyokwisha wahi kusema siku nyingine, ni kwamba biashara hizi ninazosema zimesahaulika ama biashara ambazo bado watu wengi hawajazishitukia, siyo ngeni sana bali ni biashara za kawaida tu lakini ambazo kwa jicho la kawaida lisilokuwa la kijasiriamali mtu anaweza asiweze kugundua fursa kubwa zilizomo ndani ya baadhi ya biashara hizo, “so I am not trying to reinvet the wheel” bali lengo langu kubwa  ni kumfanya mjasiriamali mdogo aweze kuziona na kuzitambua fursa za ajabu zilizojificha kwenye baadhi ya hizo biashara ndogondogo nitakazokuwa nikiziweka hapa.

Tukirudi kwenye mada yetu ya leo, hebu sasa tutazame ni jinsi gani mhogo wa kukaanga na zao la mihogo kwa ujumla wake lilivyokuwa na fursa tamu na nzuri hasa katika jiji la Dar es salaam na hata katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani. Mihogo hustawi vizuri sana Tanzania karibu ukanda wote wa pwani na Kusini mwa Tanzania kuanzia Mikoa ya Ruvuma, Pwani, Morogoro, Dar es salaam, Zanzibar(Unguja na Pemba), Lindi na Mtwara. Zao la mhogo pia limekuwa likisitawi vyema katika ukanda wa Maziwa makuu kama vile Mwanza Shinyanga, Rukwa na Kigoma.


Mihogo ya kukaanga na mafuta au wengine huita chipsi dume Dar es salaam ni biashara kubwa sana kwa sasa hasahasa kwa wafanyabiashara na wajasiriamali wadogowadogo walioamua kujiajiri wenyewe kwa biashara za mitaji midogo. Wanaofanya biashara hii wengi hasa ni akina mama na hata wapo wanaume pia wanaoifanya. Uzuri wa biashara hii ya kukaanga na kuuza mihogo mtaji wake ni kidogo na ina wateja wengi, soko la mhogo ni la uhakika ukiweza kuongeza thamani, hununuliwa haraka na ina faida nzuri. Kwa mfano mihogo mibichi ya shilingi elfu moja unaweza kukata vipande vya shilingi mia mia hata 30 ambavyo utapata shilingi elfu tatu


Ukiondoa hapo gharama zingine kama za kachumbari au chachandu, mafuta, pilipili, mkaa na chumvi, huwezi ukakosa faida halisi shilingi elfu moja mpaka elfu moja na mia tano. Sasa hapo ni mahesabu ya fungu moja tu la mihogo, ukiweza kuuza kiroba kizima cha mihogo utapata faida shilingi ngapi?

Soko la mihogo ya kukaanga ni kubwa kwani watu wengi hupendelea kuitumia kama kitafunio cha chai asubuhi na hata wengine huitumia kama mlo rahisi wa mchana kwa wale wasiokuwa na kipato kikubwa au kwa wale wanaoamua kubana matumizi ya kula chakula cha gharama kubwa. Ukitaka kujua mihogo ni biashara kubwa nenda masoko ya Buguruni, Mbezi na Urafiki uone jinsi watu wanavyoweka foleni kununua mihogo mibichi ya kwenda kukaanga.

Wengine hununua mihogo kwa ajili ya kwenda kutembeza mitaani kwa watu wanaopenda kutafuna ikiwa mibichi. Mhogo wa nazi na samaki wa kukaanga kama ulishawahi kuula huwezi kusahau, watu wengi hupendelea kula muhogo ulioungwa kwa nazi hasa hasa kwenye futari wakati wa mfungo mtukufu wa Ramadhani. Mihogo ya nazi ni chakula kinachopendwa sana hasa maeneo ya mwambao wa Tanzania.
 
MHOGO WA NAZI
 Mihogo iliyoungwa kwa nazi.
Ikiwa ni mjasiriamali unayefikiria biashara ndogondogo ya kuanza Tanzania hasa maeneo ya miji kama Dar basi unaweza pia katika orodha ya mawazo yako ya biashara utakazofanyia uchunguzi ukaiweka na hii biashara ya zao la mihogo, inaweza ikawa ni kukaanga chipsi dume, kuuza kisamvu kilichokwisha kuandaliwa, kuuza miti ya mbegu au mashina ya mihogo, kuuza unga wa mhogo, kutembeza mihogo mibichi ya kutafuna mitaani, kutengeneza vitu mbalimbali kama chapatti za mhogo, crips nk. Sababu kubwa kwanini uamue kudili na mihogo narudia tena kuwa ni gharama zake ndogo za kuanza, kumbuka wajasiriamali wengi wana tatizo la ukosefu wa mitaji ya kutosha kuanzisha biashara zinazohitaji mitaji mikubwa au ya kati, vilevile ni soko lake la uhakika.


Mihogo kama zilivyokuwa biashara zingine zozote zile za vyakula, unapoanzisha katika kiwango chochote kile iwe hata unatembeza barabarani na sinia, siri yake kubwa ya mafanikio ni usafi wa vyombo, eneo unalouzia, mihogo yenyewe na hata wewe mwenyewe unayeuza. Angalao hata hakikisha unaisafisha kwa maji safi siyo ya mto, kuwa na kisu kisafi na hata ikiwezekana unapowamenyea wateja tumia karatasi safi au tishu. Kwa wale wanaokaanga, hakikisha chachandu yako au kama ni kachumbari basi inakuwa salama, safi na inayovutia, halikadhalika ikiwa unauza mhogo wa kuchoma, wawekee wateja pilipili nzuri katika chombo kisafi.

Tukiachana na mizizi, hebu tutazame shina la mhogo kama nilivyotangulia kusema kwamba muhogo una faida kuanzia mizizi yake ambayo ndiyo mihogo yenyewe, shina mpaka majani yake kama kisamvu cha mboga kwa ajili ya kitoweo. Faida kubwa ya shina la mhogo ni kwamba, inatumika kama mbegu kwa ajili ya kuzalishia mihogo mingine. Ukifungua mahali ukaamua wewe kazi yako ni kuuza mbegu ya mhogo tu peke yake unaweza ukatajirika.

Hasahasa nyakati za mvua kama masika mshina ya mihogo huwa dili sana na watu wengi husafiri kwenda maeneo mbalimbali inakovunwa mihogo kwa wingi kama maeneo ya mkoa wa Pwani, Mkuranga, Rufiji na Morogoro kuchukua miti ya mbegu ya mihogo kwa ajili ya kuja kuuza kandokando ya barabara ya Morogoro wanakopita watu wengi wakielekea maeneo yenye mashamba ya mihogo.

Majani ya mihogo ni mboga tamu sana inayojulikana kama kisamvu. Siku hizi kisamvu ni maarufu mno na kimekuwa kikiuzwa mpaka kwenye supermarkets, kutangazwa kwenye mitandao na wapo watu wanaoishi kwa biashara ya kuuza kisamvu tu.

SOMA: Biashara ndogondogo Dar za kufanya na mtaji kidogo.

Hizo ni fursa chache sana kuhusiana na zao la mhogo, hatujagusa kabisa zile faida kuu za mihogo kama moja wapo ya  chanzo kikubwa cha wanga duniani kwa binadamu, unga wa muhogo hutengeneza vitu vingi ukiwemo uji wa muhogo, biskuti za mhogo, mikate, na nk. malighafi za kutengeneza bidhaa mbalimbali viwandani ikiwemo na nishati ya kuendeshea magari na mitambo, chakula kwa ajili ya mifugo na hata matumizi kwa ajili ya tiba au dawa. Kuna crips za mihogo au kaukau za mhogo nazo hupendwa sana katika maduka na supermarkets
…………………………………………………………………..

Chochote kile ufanyacho, ni biashara, hivyo unahitaji kwa namna moja au nyingine maarifa katika nyanja hiyo na napendekeza vitabu 3 vifuatavyo kama utachagua kujifunza kupitia njia ya vitabu;

Njia nyepesi zaidi na ya haraka ya kupata moja ya vitabu hivi au vyote kwa pamoja ni kupitia E-mail kama faili za PDF au softcopy. Lakini pia vitabu vya kawaida vya karatasi tunavyo.

Ukihitaji wasiliana nasi kwa namba hizi hapa;
0712202244  au  0765553030
Tupo Mbezi Kwa Msuguri karibu na stendi ya mabasi

ASANTE SANA

Peter Augustino Tarimo

Self Help Books Tanzania.

0 Response to "MHOGO WA KUKAANGA UNAVYOLIPA DAR, NI BIASHARA WENGI HAWAIFAHAMU VIZURI"

Post a Comment