BIASHARA YA VINYWAJI JUMLA, MTAJI MILIONI MOJA (1) NAOMBA USHAURI | JIFUNZE UJASIRIAMALI

BIASHARA YA VINYWAJI JUMLA, MTAJI MILIONI MOJA (1) NAOMBA USHAURI

Swali la msomaji wetu:


Nani kakuambia fursa za biashara Tanzania zipo chache? Zimejaa tele, kila siku nakutana na maswali mengi watu wakitaka kupata taarifa kuhusiana na biashara mbalimbali zenye faida ya haraka. Miongoni mwazo ni biashara ya vinyaji vya jumla, kuuza bia za jumla na soda aina zote, biashara ya kuuza maji ya kunywa pamoja na jinsi ya kupata uwakala wa kuuza vinywaji mbalimbali mfano kuwa wakala wa makampuni kama ya pepsi, cocacola nk.

Leo kwenye safu yetu hii ya uliza ujibiwe nitajibu swali kutoka kwa msomaji wetu mmoja ambaye swali lake ametuma kupitia njia ya whatsap kama ifuatavyo;

Naomba ushauri kaka,

Nataka kufanya biashara ya vinywaji ya kuuza kwa jumla sasa nina mtaji wa million moja, je naweza nikafanikiwa kuanza hata kidogo?

Majibu ya swali hilo ni haya hapa:

Ndugu msomaji,

Ingawa sijafahamu ikiwa biashara yako hiyo ya kuuza vinywaji vya jumla utaifanyia katika eneo au mazingira ya namna gani lakini nitajitahidi kukupa majibu kwa kuzingatia mazingira yote, iwe utafanyia kwenye eneo maalumu kama vile dukani au hata kwa njia ya kuwasambazia wateja wako watarajiwa wa vinywaji mpaka mlangoni kwa kutumia usafiri.

SOMA: Nina mtaji wa milioni moja ya mkopo, nifanye biashara gani inayolipa?

Siku zote mimi huwa nasema ikiwa una mapenzi na biashara fulani na unajua una uwezo nayo nikimaanisha unazijua mbinu zote muhimu za kuifanya na kuingiza faida basi mtaji siyo tatizo hata kidogo. Kwanini nasema hivyo? Inawezekana wewe una wasiwasi mkubwa juu ya kiwango chako cha mtaji ambacho umeshakitaja kuwa ni shilingi milioni moja tu. Mtu mwingine hapa anaweza akakushauri milioni moja ni kiasi kidogo mno kuweza kutosha kuanzisha biashara ya jumla ya kuuza vinywaji iwe ni vinywaji baridi kama soda na maji au hata vinyaji vikali kama bia na aina nyinginezo za pombe.

Yamkini hujui hata kreti ya soda jumla inauzwaje, usijiloge ukaingia kichwakichwa biashara hii kwani utakuwa na wakati mgumu sana wa kujifunza kwanza kabla hujaanza. Hakikisha una uelewa wa kutosha nayo kwa kufanya utafiti wa soko kama ilivyoainishwa vizuri katiaka kitabu cha MICHANGANUO YA BIASHARA NA UJASIRIAMALI.

SOMA: Jinsi mpango wa biashara unavyoweza kuongeza mafanikio ya biashara yako 

Kuanzisha biashara ya aina yeyote ile ikiwemo pia na biashara ya kuuza vinywaji vya jumla ni lazima  mtu uorodheshe katika karatasi mahitaji yako yote muhimu ambayo yatakuwezesha wewe kuianza biashara husika. Huo ndio mpango wako wa kwanza kabisa rahisi wa biashara.

Fikiria akilini mwako ni vitu gani utahitaji kwa makadirio ya chini kabisa ili uweze kuanza japo hata ikiwa ni kwa kiasi kidogo kabisa iwezekanavyo. Ikibidi hata unaweza kuanza na kreti za soda tano, ilimradi tu ufahamu kuwa utapata mteja atakayezinunua.

Mtu mwingine anaweza akadhani biashara ya mtaji wa laki tano au milioni moja basi ni lazima tu iwe ni biashara ndogo mfano wa mama lishe au baba lishe lakini niamini, hiyohiyo milioni yako moja unaweza ukaanzisha biashara ya jumla ya vinywaji kwa kiwango kidogo kabisa huku ukiwa na maono ya mbali zaidi (Start small but think Big)

SOMA: Huna mtaji wa kutosha, hukopesheki? jaribu njia hii ya kufunga mkanda(Bootstrapping)

Ni sawa kiasi hicho cha fedha hakitoshi kuchukua fremu ya duka la kuuzia vinyaji, unaweza kuwatembelea wenye maduka ya rejareja ukawauliza kama wanahitaji vinywaji, wakijibu uwaletee, unakwenda maduka makubwa kununua mzigo na kuwapelekea. Cha msingi ujue tu unapata hapo faida kidogo.

Kidogokidogo utajikuta unapata mtaji mkubwa au unapata ‘mchongo’ wa kupata mtaji mkubwa zaidi hata wa kufungua duka kubwa la vinywaji jumla kupitia njia nyinginezo tofauti kwakuwa sasa utaweza kuaminika kutokana na watu kuona kwa macho utendaji wa biashara zako.

Kiukweli changamoto kubwa kwenye biashara hii ya jumla ya vinywaji ni mtaji, ili upate faida kubwa na ya haraka zaidi inakubidi uwe na kiasi kikubwa cha mtaji lakini kwa kuanza si lazima uanze na kiasi hicho kikubwa cha mtaji. Unachopaswa kufanya kwanza ni kutengeneza msingi wa wateja, wateja ndio kila kitu mengine huja taratibu. Unaweza hata kuanza biashara yako ya vinywaji kama dalali usiyekuwa hata na senti tano mfukoni.

SOMA: Kama una biashara ndogo ya mtaji mdogo, hizi hapa njia 11 za kuibusti

Kuna jamaa yeye kazi yake ilikuwa ni kuzunguka maduka ya rejareja, mabaa na grocery akiwa na sample za vinywaji kama vile, red bull, malta na aina nyinginezo za vinyaji vinavyobebeka kwa urahisi, akipata oda hata ya pc 6 anakimbia kwa wenye maduka ya jumla ya vinywaji anawaomba wamuamini mzigo, akishaenda kuuza anarudi kuwalipa chao na yeye anabakia na faida yake.

Kidogokidogo hivyo akajikuta anapata mtaji kiurahisi kabisa baada ya muda kupita. Sasa hivi ninavyoandika hapa anamiliki duka la kuuuza bia za jumla pale Mbezi mwisho na duka jingine kubwa la kuuuza maji ya jumla  pale Kiluvya madukani. Ndugu msomaji wangu nikutie tu moyo kuwa million yako hiyo moja unaweza ukatimiza azma yako ya kumiliki biashara ya jumla ya vinywaji ikiwa utaamua kuwa mbunifu na kuhakikisha unaishi chini ya kipato chako hadi pale utakapohakikisha mtaji umetengemaa vya kutosha.

………………mwisho……………..

 

Una swali lolote lile kuhusiana na Biashara na Ujasiriamali? Tutumie maswali yako kupitia Watsap au Sms ya kawaida, 0765553030 au 0712202244 na tutakujibu kupitia safu hii.

Masomo ya fedha(Basic & Advanced Financial Education) yanapatikana ndani ya MASTERMIND GROUP la MICHANGANUO-ONLINE kila siku saa3 usiku. Kujiunga kiingilio cha mwaka(miezi 12) ni sh. Elfu 10 tu. Uwe na account watsap na Telegramu lakini ikiwa huna basi E-mail inatosha, tutakutumia kila kitu kupitia email yako-nijulishe mapema kupata utaratibu.

VITABU vyetu vyote pia vinapatikana;

1. THINK & GROW RICH-SWAHILI EDITION

2. MICHANGANUO YA BIASHARA & UJASIRIAMALI

3. MAFANIKIO YA BIASHARA YA DUKA LA REJAREJA

4. MIFEREJI 7 YA PESA NA SIRI MATAJIRI WASIYOPENDA KUITOA

0 Response to "BIASHARA YA VINYWAJI JUMLA, MTAJI MILIONI MOJA (1) NAOMBA USHAURI"

Post a Comment