HUNA MTAJI WA KUTOSHA, HUKOPESHEKI? JARIBU NJIA HII YA KUFUNGA MKANDA(BOOTSTRAPPING) | JIFUNZE UJASIRIAMALI

HUNA MTAJI WA KUTOSHA, HUKOPESHEKI? JARIBU NJIA HII YA KUFUNGA MKANDA(BOOTSTRAPPING)


KUJITEGEMEA KIUCHUMI SERA YA MWALIMU NYERERE
Kufunga mkanda au kwa kimombo Bootsrapping ni njia inayotumiwa na wajasiriamali wengi wadogo wanaoanza lakini pia ni njia ambayo kila biashara inaweza kuitumia iwe ni biashara kubwa au biashara ndogo. Kufunga mkanda kwenye biashara maana yake ni kitendo cha kuanzisha na kuendesha biashara kwa kujitegemea kimtaji pasipo msaada wowote kutoka nje. Unatumia mtaji na rasilimali za ndani peke yake huku ukijitahidi kushusha chini gharama za biashara kwa kadiri inavyowezekana.

Dhana hii ya kufunga mkanda tumeweza kuona ikitumiwa hata na serikali za nchi mbalimbali kwa mfano hapa kwetu sera hiyo ilitumika sana kipindi kile cha awamu ya kwanza na aliyekuwa Rais na Baba wa Taifa la Tanzania Mwalimu J.K Nyerere na sasa hivi tena tunaweza kuona ikitumiwa na Rais J.P. Magufuli kwa kuhimiza kuanzisha na kuendesha miradi mingi ya kiuchumi kwa kutumia fedha za ndani zaidi kuliko kutegemea misaada au mikopo kutoka Mataifa mengine.


Kufunga mkanda kunasaidia sana uchumi wa taasisi iwe ni mtu binafsi, kampuni au nchi kuwa imara zaidi na unaojitegemea. Hujenga nidhamu ya pesa na kuleta matokeo bora. Kwenye kufunga mkanda mjasiriamali anatakiwa kuchunga sana upande wa matumizi ya biashara yasijekuwa juu sana hasa kipengele cha gharama, lakini pia haishauriwi kupunguza kupindukia kila matumizi ya biashara bali kufanya matumizi katika yale maeneo tu yanayohusika moja kwa moja na uzalishaji wa faida.

Kwa maneno mengine tunaweza kusema, tumia fedha zaidi kwenye kuwekeza kuliko katika matumizi ya kawaida yasiyorudisha fedha zilizotumika. Unatumia fedha ukiwa na uhakika kuwa itarudi. Matumizi katika vitu au mambo yaliyokuwa na uhusiano wa moja kwa moja na mapato ya biashara yanaweza yakawa ni ununuzi wa malighafi ya kutengenezea bidhaa, kulipia teknolojia nzuri itakayoongeza wateja, kununua vifaa au zana za kufanyia kazi nk. Lakini pia chunga sana mzunguko wako wa fedha usije ukanunua vitu ambavyo itachukua muda mrefu sana kurudisha pesa.


Kwa biashara ndogo inabidi utumie zaidi pesa katika kuwekeza katika vitu vitakavyorudisha pesa katika kipindi kifupikifupi ili kuimarisha mzunguko wa pesa wa biashara. Matumizi katika kitu chochote kile ambacho hakitaleta mabadiliko yeyote kwenye mapato ya biashara usikipe uzito wowote, matumizi kwa mfano kununua usafiri binafsi, kula na kulala katika hoteli za gharama kubwa ukiwa safarini kibiashara, kupanga katika eneo la biashara la gharama kubwa isiyolingana na biashara, kutumia usafiri wa tax au bodaboda unapofuata bidhaa zako za biashara wakati ungekuwa na uwezo wa kupanda mwendokasi au daladala ya kawaida nk. Hizo zote ni gharama zinazoua biashara na wala siyo uwekezaji unaoweza kuiletea biashara mapato.

Kufunga mkanda siyo jambo rahisi linaloweza kumvutia kila mjasiriamali lakini ni jambo lililokuwa na manufaa mengi kwa biashara yeyote iwe ndogo au kubwa iwapo tu mmiliki wake atataka kuongeza mapato yake zaidi bila ya msaada kutoka sehemu nyingine yeyote ile. Na hasahasa kwa biashara ndogo hii ndiyo silaha kubwa kuliko zote mjasiriamali anaweza kuitumia kuhakikisha anakuwa na udhibiti mkubwa wa biashara yake.

...................................................................

Kwa vitabu vya ujasiriamali katika lugha ya kiswahili fungua self help books tz

Kwa masomo ya kila siku, vitabu bila malipo, michanganuo ya kuku, matikiti maji na semina za kila mwezi jiunge na kundi letu la whatsap la MICHANGANUO-ONLINE namba 0765553030 

0 Response to "HUNA MTAJI WA KUTOSHA, HUKOPESHEKI? JARIBU NJIA HII YA KUFUNGA MKANDA(BOOTSTRAPPING)"

Post a Comment