NJIA YA MAFANIKIO NI NYEUPE KWA MJASIRIAMALI MDOGO ANAYEWEZA KUVIKWEPA VIDAKIZI HIVI. | JIFUNZE UJASIRIAMALI

NJIA YA MAFANIKIO NI NYEUPE KWA MJASIRIAMALI MDOGO ANAYEWEZA KUVIKWEPA VIDAKIZI HIVI.


Biashara ndogo inayostawi inamhitaji mmiliki wake kuwa na malengo na umakini wa hali ya juu katika usimamizi. Hiyo ndiyo kazi ya mjasiriamali ya kwanza kabisa ikiwa atapenda biashara yake kukua haraka na kufikia kuwa biashara kubwa au ya kati. Umakini huo pia unahitajika katika matumizi mazuri ya muda na utekelezaji sahihi wa majukumu katika kuongeza kasi ya mafanikio ya biashara.

Ni bahati mbaya kwa wajasiriamali wengi wakati wangependa kutekeleza majukumu ya biashara zao kwa ubunifu mkubwa huibuka vidakizi ambavyo vinarudisha nyuma kasi ya utendaji wa shughuli muhimu za biashara na hata wakati mwingine kuwa ndiyo chanzo cha vifo vya biashara nyingi zinazoanza kabla hata hazijatimiza umri wa mwaka mmoja.


Kabla hatujaenda kuona jinsi ya kukabiliana na tatizo hili la vidakizi hebu kwanza tuone vidakizi ni kitu gani, Vidakizi ni kitu chochote kile kinachoingilia kati wakati mtu akitekeleza kazi au jukumu la msingi la biashara. Hivyo tunapomzungumzia mjasiriamali mdogo na biashara yake ni vile vitu vinavyomfanya kuachana na mambo ya msingi anayopaswa kuyafanya na kuelekeza usikivu wake na akili kwavyo. Mara nyingi vidakizi huwa havina faida yeyote ile zaidi ya kula tu muda wa mjasiriamali na kusababisha ufanisi wake kuwa mdogo.

Kwa mfano mtu anakuwa anachapa kazi za ofisini mara meseji, sms ya mapenzi inaingia kwenye simu yake ya mkononi, meseji hii ni kidakizi kwani imeingilia kati kazi ya msingi ya biashara. Vidakizi pia vyaweza kuwa ni moja kati ya vitu hivi vifuatavyo;

·       Kupigiwa simu
·       Kusoma gazeti au kitu kingine chochote kile ambacho hakihusiani na kazi
·       Email
·       Mitandao ya kijamii
·       Kusikiliza redio,muziki au kutazama TV.
·       Kutazama video na picha mbalimbali.
·       Mazungumzo na watu wengine muda wa kazi
·       Kuchati na marafiki
·       Na hata maombi na sala ikiwa siyo muda wake inaweza kuwa ni kidakizi pia.

Chanzo cha mafanikio yeyote yale yawe ni katika biashara, mafanikio kieleimu na hata mafanikio katika kazi mbalimbali ni umakini(focus). Na ili mtu kuweza kuwa makini hapaswi kabisa kuviendekeza vidakizi wakati anapokuwa akitekeleza majukumu yake ya msingi ya biashara au kazi. Kwakuwa vidakizi hatuwezi kuvikwepa kabisa kwa asilimia 100%, lakini zipo njia mjasiriamali anaweza akazitumia na hatimaye kuvipunguza kabisa na kuwa mjasiramali aliyefanikiwa. Njia hizo ni hizi hapa chini;


1.Kuzingatia ratia
Kamwe usikubali kuondoka kwenye jukumu ambalo tayari ulishalipangia muda wa kulifanya. Zingatia unakamilisha kwanza jukumu hilo hata kama vidakizi vitaibuka kwa njia gani. Wajulishe marafiki na wale wanaokutumia ujumbe muda wa kazi kuwa huna nafasi muda huo na ikiwezekana zima kabisa vifaa vinavyohusika katika kukuletea vidakizi mfano simu, redio, kompyuta nk.

2.Gawa majukumu.
Siyo kila wakati utafanya kila kitu wewe mwenyewe, mjasiriamali makini anayefahamu vyema ni nini maana ya ujasiriamali ni lazima wakati mwingine akubali kuwa ili mambo yaweze kwenda mbele basi anatakiwa kusaidiwa majukumu na watu wengine . Kugawa majukumu kwa watu wengine kwanza kunaonyesha unawajali wengine na pia kunazidisha hali ya kuaminiana katika biashara au kampuni. Hupunguza vidakizi kwa kiasi kikubwa.


3.Simamia kikamilifu malipo ya bili mbalimbali.
Hili ni eneo nyeti sana katika biashara yeyote ile ndogo kwani linahusika moja kwa moja na mtiririko wa pesa kwenye biashara yako. Mafanikio na afya ya biashara ndogo hutegemea sana mtiririko mzuri(chanya) wa fedha kwani ndiyo kitu kinachoweza kuamua ikiwa biashara ife au iendelee kuwa hai, Kwahiyo hakikisha kwamba kama kuna mazingira yatakayokulazimisha ukopeshe , vilevile basi kuwe na utaratibu mzuri na unaoeleweka wa kudai madeni kwa wakati.

SOMA: Ikiwa huwezi kusimamia mahesabu ya biashara yako ni bora ukaachana nayo vinginevyo utavuna mabua.

Hali kadhalika ikiwa wewe (biashara yako) italazimika kukopa mahali, hakikisha pia unasimamia kikamilifu deni lilipwe kwa wakati muafaka. Kwa malipo ya zile bili zinazojirudia kama  vile umeme na maji ili kuokoa muda unaweza ukaweka mfumo utakaokata madeni hayo moja kwa moja(automatically) katika akaunti yako ya benki muda wa malipo unapofika.

Hizo ni njia chache za kupambana na vidakizi katika biashara ndogo. Kila biashara na kila mjasiriamali ni tofauti na hivyo kila mmoja anaweza akawa na vidakizi tofauti vinavyoweza kuiba muda wake wa thamani katika biashara. Fikiria ni kitu gani kwa upande wako kinachoweza kuwa kinadakia majukumu yako zaidi  na kukupunguzia ufanisi wa kazi.

Kufanya marekebisho madogo lakini muhimu katika mfumo na mtindo wako wa uendeshaji biashara kunaweza kukasababisha tofauti kubwa itakayokuletea matokeo bora kabisa katika mafanikio ya biashara yako.

...........................................................................

Ukitaka vitabu vya ujasiriamali kwa lugha ya kiswahili tembelea hapa; SMART BOOKS TANZANIA

Kujiunga na group letu la whatsap la masomo ya kila siku na semina za kila mwezi za michanganuo ya biashara lipia kiingilio kupitia namba zetu, 0712202244  au 0765553030 whatsap 0765553030

Kuandikiwa mchanganuo wa biashara yako bonyeza hapa, HUDUMA ZETU

Leo tarehe 22 August katika group la wasap tutakuwa na somo lihusulo, "JINSI YA KUSIMAMIA HESABU KWENYE BIASHARA NDOGO UNAYOMWACHIA MFANYAKAZI" Ni saa 3 mpaka saa 4 usiku, usikose.



0 Response to "NJIA YA MAFANIKIO NI NYEUPE KWA MJASIRIAMALI MDOGO ANAYEWEZA KUVIKWEPA VIDAKIZI HIVI."

Post a Comment