NJIA MPYA ZA KUFANYA MAMBO: DUNIA, BIASHARA, AJIRA VINABADILIKA KWA KASI YA AJABU | JIFUNZE UJASIRIAMALI

NJIA MPYA ZA KUFANYA MAMBO: DUNIA, BIASHARA, AJIRA VINABADILIKA KWA KASI YA AJABU

njia mpya za kufanya mambo
Kila kitu Duniani kinabadilika kwa kasi ya ajabu sana tangu mapinduzi mapya ya viwanda duniani(new industrial revoluton) yalipoanza miongo kadhaa iliyopita. Na mabadiliko hayo yamesababisha biashara nayo kubadilika kwa spidi hiyo hiyo kwani huwezi kutenganisha biashara na teknolojia kwa urahisi. 


Kwa kadri njia mpya au teknolojia mpya za kufanya mambo mbalimbali duniani zinavyoibuka, basi unakuta na biashara nayo inafuata mkumbo huo huo.

Mapinduzi mapya ya kiviwanda yalianza tangia matumizi ya  kompyuta yalipoanza kushika kasi katika miaka ya 50 na 60, tangu hapo dunia imeshuhudia kuporomoka kwa teknolojia nyingi zilizokuwepo kabla sambasamba na kuzaliwa teknolojia nyinginezo mpya kabisa. Na hali hiyo bado inaendelea na itaendelea kushuhudiwa kwa miaka mingi inayokuja. Kila mabadiliko hayo yanapotokea duniani watu huwa na hofu, lakini pia huwa kunakuwa na matumaini na vyote hivi viwili ni lazima vitokee kutokana na sababu kwamba kunatokea uharibifu na ujenzi kwa wakati mmoja.


Kwa mujibu wa ripoti ya taasisi moja kutoka Silicon Valley nchini Marekani iitwayo, Singularity University(SU). Taasisi hii inafadhiliwa na shirika la NASA na Kampuni ya Google na inalenga katika kutabiri maswala ya maendeleo ya sayansi na teknolojia zinazobadilika kwa kasi zaidi duniani katika kusaidia kubainisha ni kipi kifanyike wakati tuliokuwa nao sasa na kipi kitafanyika katika wakati ujao unaokaribia kwa kasi.

Kwenye mlolongo wa makongamano ya taasisi hiyo wanalenga zaidi kuzungumzia teknolojia zinazobadilika haraka kwa kasi na ambazo huziathiri sekta za fedha, madawa, afya, elimu, viwanda, na chakula. Wanasema kwa kiasi kile teknolojia inavyobadilika na kukua kwa kasi, kizazi kijacho cha uongozi katika biashara  kinatakiwa kiwe na uwezo wa kuyasimamia hayo mabadiliko yanayojenga  pamoja na yale mabadiliko hasi yanayobomoa kwa haraka na kwa ufanisi kuliko muda wowote hapo kabla. Kubomoa kunakojenga(creative destruction)  katika uchumi wa soko huria kunaongezeka kwa kiwango cha kipeo cha kumi.

Hivi karibuni,  Udo Gollub kutoka Berlin nchini Ujerumani baada ya kuhudhuria kongamano hilo aliandika  baadhi ya yale yaliyojadiliwa. Lakini  ukumbuke kwamba mambo hayo yaliyozungumzwa  yote  ni utabiri wa mwenendo wa  teknolojia zinazobadilika kwa kasi  uliofanyika na taasisi ya Singularity University, hakuna hata kitu kimoja kilichokuwa kamilifu, kila kitu ni mfululizo wa mabadiliko.

Utafiti huu ni kwa ajili tu ya kutia moyo na kusisimua mawazo na umetumia baadhi ya dondoo muhimu kutoka katika kongamano hilo. Katika ripoti hiyo pia mimi mwenyewe nitaongeza baadhi ya uchunguzi wangu binafsi nilioufanya katika teknolojia mbalimbali na nyingine zilizowahi kuwa hapa Tanzania lakini zikatoweka na kuja zingine.

RIPOTI KAMILI.
Kampuni ya kutengeneza kamera na vifaa vya picha ya Kodak iliyoanzishwa mwaka 1888 na George Eastman mpaka kufikia mwaka 1998 ilikuwa ni kampuni inayoongoza katika sekta hiyo na hakuna mtu ambaye angeliweza kudhania kama miaka michache tu mbele ingeliweza kuja kufilisika kabisa na mahali pake kuchukuliwa na makampuni mengine yaliyokuja na teknolojia za kutoa picha za dijitali. Kile kilichotokea kwa Kodak kitatokea katika sekta nyingine nyingi ndani ya miaka 10 ijayo na watu wengi hawawezi kuliona hilo likija.

Ungeweza kufikiria kwamba miaka 3 tu baada ya 1998 usingeliweza tena kupiga picha katika mikanda ya kamera ya film? Hata hivyo si kama kamera za digitali ziligunduliwa juzijuzi tu hapana, ni tangu mwaka 1975 lakini teknolojia yake haikuwa bado ikiweza kutoa picha zenye ubora wa hali ya juu na hata hivyo watu kama kawaida kinapoanza kitu kipya hawakuichangamkia sana na ilichukua muda mrefu kukubalika sokoni. Mgunduzi wake Steven Sasson  akiwa ni mfanyakazi katika kampuni hiyo ya Kodak, wala viongozi wa Kodak hawakuweza kuona fursa hiyo, wangelijua wakamtumia pengine leo hii wasingelikuwa wamefilisika.

Kilichotokea kwa Kodak pia kitatokea katika sekta za afya, usafirishaji, nishati, elimu, kilimo, ajira, mashine zinazofanya kazi kama binadamu na hata katika ufyatuaji wa maumbo mbalimbali(3D Printing). Zitakuwa ni zama mpya za Mapinduzi mapya ya kiviwanda ya teknolojia inayobadilika kwa kasi.


Unaweza kuona hata hapa Tanzania mabadiliko hayo yanavyotokea, kwa mfano miaka michache nyuma kulikuwa na teknolojia zilizotamba hapa kama vile mikanda ya redio za kassetti, mikanda ya video(VHS) na redio kaseti zenyewe leo hii hata watoto waliozaliwa miaka kumi tu iliyopita hawawezi kujua kama kulikua na vitu vya namna hiyo. Teknolojia zingine zimechukua mahali pake kwa kasi, DVD, DVD players, CD, Memory card, Flash disks, Hard disks, Kompyuta na Simu za mikononi ndiyo zinazotamba sasa.  

Nakumbuka miaka ya 90 kuingia 2000 wakati naandaa jarida(gazeti) letu nililokuwa likitoka kwa mwezi, lilikuwa mfano wa majarida yale ya Sani ya zamani lakini tulikuwa tukiandika stori za kawaida. Tulikuwa tunatumia kompyuta moja, nadhani ilikuwa Pentium, 66 MHZ wakati huo hakukuwa na mitandao ya kijamii, njia pekee za watu kujieleza na hata kutoa maoni yao kupitia vyombo vya habari ilikuwa zaidi ni kwa kupitia magazeti, majarida na kidogo redio. Teknolojia haikuwa imekua kama ilivyokuwa sasa hivi, kuandaa gazeti mpaka ukalifikishe kwa mchapaji ilikuwa ni shughuli pevu kwelikweli kwa mtu ambaye hukuwa na uwezo mkubwa wa pesa.

Tukiwa hatuna kifaa chochote cha kubebea kazi kama flash za siku hizi, kupeleka jarida lile kwa mchapaji ambaye alikuwa ni kampuni ya Business Printers wakati huo ilitubidi tubebe kompyuta nzimanzima mpaka pale Kariakoo gerezani, wafanyakazi wa Business Printers acha watucheke, “nyie vipi si mngetumia CD au email”. Sawa CD zilikuwepo lakini kompyuta yetu haikuwa na CD ROM ya kuweza kuburn cd, na pia email hatukuwa na moderm ya kuunganisha intaneti ambazo wakati huo zilipatikana kwa tabu tena mpaka uwe na line ya simu ya TTCL.

Vifaa pekee wakati huo vilivyopatikana kwa urahisi kwa ajili ya kusevu au kubeba faili za kompyuta zilikuwa ni Floppy disk au  3.5 inch diskette, hizi zilikuwa zinafanya kazi sawa na flash disks au memory card lakini tatizo lilikuwa, havikuwa na uwezo wa kubeba mafaili makubwa kama gazeti, vilikuwa na ukubwa wa 1.44MB pekee.

Toleo lililofuata tukaamua kuchomoa hard disk tukaipeleka, wao kule kiwanda cha kuchapa wakaiunganisha na kompyuta zao ili kuweza kukopi kazi yetu kwa ajili ya mchakato wa kuichapa. Baadae sasa tukaja kuwapata jamaa fulani pale Kariakoo waliokuwa wakitengeneza kompyuta ikawa tunawapelekea hard disk wanatoa kazi na kuiburn kwenye CD ndipo sasa tunakwenda na CD kule kiwandani.




Changamoto nyingine tuliyoipata ilikuwa ni katika picha, ilikuwa ili uweze kuingiza picha katika kompyuta ni lazima kwanza picha hiyo iwe katika mfumo wa dijitali na kwa kipindi hicho kamera pekee zilizotumika kupiga picha ni zile za film, ambazo picha zilitoka kwenye karatasi hivyo ili uweze kuitumia katika kompyuta ni lazima kwanza ukaiscan na scaner, uiweke kwenye diskette ndipo uje uihamishie katika kompyuta yako kwa ajili ya kuitumia katika gazeti au jarida. Picha zilizopigwa na kamera za digital zilikuwa bado hazijasambaa sana ingawa zilishaanza kuwepo na simu za kamera ndio kwanza zilikuwa wala hazipo.

Kwa ujumla program za kudizaini vitu kama majarida, vitabu na magazeti hazikuwa zimeboreshwa sana kama siku hizi, ‘Desk Top Publishing’ ilikuwa ndiyo ipo katika hatua zake za mwanzo kabisa ingawa ilikuwa imekwishaanza kufanya kazi, Software za kutengeneza kurasa kama vile Quark express, Indesign na Adobe Photoshop zilikuwepo lakini zilikuwa ghali, haikuwa rahisi sana kwa kampuni ndogo kuwa nazo. Badala yake tulitegemea zaidi programu moja iliyoitwa Page maker kwa ajili ya shughuli za uandaaji jarida.

Lakini kipindi hicho mambo yalibadilika kwa kasi sana, ndani ya miaka miwili tu au mitatu kila kitu kilibadilika, tukaanza kushuhudia mitandao ya kijamii iliyoanza taratibu kuondoa ule ukiritimba wa vyombo vya habari mama kama magazeti, vijarida na redio, kukaanza kuingia kompyuta zenye nguvu na spidi kubwa zaidi, Pentium 1 mpaka Pentium 4, zikaingia Flash disk, memory card, card reades, simu za mkononi, external hard disks na teknolojia nyinginezo kibao ambazo miaka mitatu nyuma usingeliweza kudhania kabisa kama zingekuja kuwepo.

Kasi ya mabadiliko hasa katika teknolojia ya mawasiliano siyo ya kawaida kama tuliyozoea katika mabadiliko ya vitu vingine duniani, wakati mabadiliko ya kawaida yakifuata utaratibu wa hesabu, 1, 2, 3, 4,…………mpaka 10, mabadiliko ya kasi ya teknolojia, yenyewe huhesabu 2, 4, 8, 16,………mpaka 1024 kwa mfano ukipiga hatua 30 tu za kawaida ni sawa na umbali kwenda mwezini na kurudi wa mabadiliko hayo ya kasi ya teknolojia ya habari na mawasiliano.


Katika kizazi cha kompyuta za mwazo miaka ya 50, wanafunzi waliweza kutumia kompyuta moja kubwa iliyojaza chumba kizima lakini leo hii kompyuta unayotumia kwenye simu yako ya mkononi, ni ndogo zaidi mara elfu na iliyokuwa na nguvu mara elfu moja zaidi na bado miaka mingine 25 ijayo itazidi kupungua ukubwa na gharama. Kipimo cha kasi ya mabadiliko katika teknolojia ya habari na mawasiliano ni kanuni iitwayo “Gordons Moors Law” isemayo, “Namba ya transistors katika saketi ya IC(intergrated circuit) huongezeka mara mbili karibu kila baada ya miaka 2”

Lakini ni nini kitatokea baada ya kanuni hiyo kufikia ukomo?, maana itafika mahali hizo transistors zitashindikana kuongeza kama ilivyokuwa miaka hiyo ya 50, vacuum tubes(diodes) zilivyoshindwa kupunguzwa ukubwa ndipo zikagunduliwa transistors. Na wakati huo, SU wanatabiri kuwa ni kuanzia mwaka 2020 lakini habari njema ni kuwa wanasema kitakuja tena kizazi kingine cha kompyuta kilichokuwa na nguvu zaidi(sixth paradigm) au (three-dimensional, self-organizing molecular circuits.) kama ilivyokuwa kutoka vacuum tubes, transistors mpaka Intergrated Circuit(IC)

Software ndizo zitakazokuwa zikitawala katika sekta nyingi kwa miaka 5 – 10 itakayofuata kama tunavyoshuhudia sasa hivi, kampuni mpya ya teksi ya Uber inatumia software tu na wala hawamiliki hata gari moja lakini ndiyo wanaomiliki biashara ya tax dunia nzima kwa sasa. Halikadhalika pia kwa Airbnb katika sekta ya hoteli, ingawa hawana jengo lolote. Kwa hiyo mabadiliko haya ingawa kwa upande mmoja yanabomoa au kuharibu zile fursa zilizokuwepo zamani lakini pia yanatengeneza fursa nyingine nyingi mpya. Hivyo jiandae kwa vyote viwili, fursa lakini pia hatari au maanguko.

Maroboti(Artificial Intelligence)
Singularity University(SU) wanatabiri kuwa ifikapo mwaka 2030 kompyuta itakuwa na akili kumshinda binadamu. Chip mpya ijulikanayo kama “Virtual Processing Unit” (VPU) iliyo na uwezo wa kukokotoa  mpaka mara trilioni 8 kwa sekunde moja  itakuwa na kasi kubwa sana kushinda hata kasi ya mawazo ya binadamu.

Kwa mfano huko Marekani sasa hivi wanasheria wanaomaliza vyuo wameshaanza kupata ugumu wa kupata ajira kutokana na kampuni moja iitwayo IBM Watson inayotumia software kutoa  huduma za kisheria kwa haraka zaidi na katika usahihi mkubwa asilimia 90% kulinganisha na asilimia 70% unapopata ushauri kutoka mwanasheria wa kawaida( binadamu). Hapo baadae ni wanasheria wale waliobobea tu ndiyo watakaopata ajira kiurahisi.


Siyo hivyo tu Kampuni hiyo pia ina “madaktari wa bandia” waliokuwa na uwezo wa kupima na kugundua kansa kwa usahihi mara 4 zaidi kushinda daktari binadamu na wanaweza pia wakatengeneza roboti itakayokuwa mshauri katika maswala ya kifedha.  Face book nao wametengeneza software iliyo na uwezo wa kugundua sura ya mtu vizuri zaidi kushinda binadamu.

Magari yanayojiendesha yenyewe bila dereva
Ifikapo mwaka 2018 magari yasiyokuwa na dereva yataanza kuonekana mitaani na kuanzia 2020 kwenda mbele teknolojia ya zamani ya magari haya ya kawaida tuliyoyazoea itaanza kukumbwa na mparaganyiko. Watu hawatakuwa tena na sababu ya kumiliki magari, utaita gari kwa simu yako ya mkononi, litakuja na kukubeba mpaka unakotaka kwenda, hutakuwa na haja ya parking wewe kazi yako ni kulipa na gari kuondoka zake. Tena isitoshe watu watakuwa na uwezo wa kufanya shughuli zao wakati wakisafiri ndani ya magari hayo.


Ajali zitapungua sana, hakutakuwa na bima tena au zitakuwepo chache, vyuo vya udereva vitakufa, maeneo ya parking yatageuzwa ya shughuli zingine, na hata watu hawatakuwa na sababu tena ya kupanga maeneo karibu na miji kutokana na usafiri kuwa ni wa haraka na salama, mtu anaweza akaishi morogoro kazi akafanyia Dar. Kelele zitapungua kutokana na magari mengi kutumia umeme(Tesla).

Kama ilivyokuwa kwa sekta za teknolojia ya habari na mawasiliano katika maswala ya vingamuzi, (analojia kwenda dijitali), hapa Tanzania sekta ya usafirishaji na miundo mbinu kwa ujumla inabadilika kwa kasi kubwa, tumeshuhudia mabadiliko mengi ngani ya kipindi kifupi sana. Miaka mitatu tu nyuma hakuna mtu ambaye angeweza kuamini  kama leo hii kusingekuwa tena na daladala au hice(vipanya) vinavyokwenda kariakoo kutoka Ubungo na Mbezi.

Ujio wa Mabasi ya Mwendo kasi umeharibu ajira za madereva wengi wa daladala, makondakta na wapiga debe lakini wakati huo huo umeibua ajira mpya kwa watu wengi kupitia ujenzi wa vituo vya mabasi hayo(UDART), madereva wa Mabasi ya mwendokasi, wahudumu katika vituo, wakatishaji tiketi, walinzi pamoja na wanaofanya usafi katika vituo na ofisi zao.

Bado tutegemee mabadiliko mengine ya kasi na ya haraka katika kipindi kifupi sana kijacho. Yanakuja mabadiliko makubwa katika usafiri wa barabara, barabara za juu(flyovers), treni za umeme, na mabasi yaendayo kasi kuzunguka jiji zima la Dares salaam. Magari yaendayo kwa nguvu za umeme nayo yanategemewa kuingia muda siyo mrefu.

Sekta ya Maji.
Kutokana na umeme wa jua kuzidi kuwa rahisi maji safi nayo yatapatikana kwa urahisi zaidi kwani maji ya chumvi yataweza kuondolewa chumvi(desalination) kwa urahisi zaidi. Kuondoa chumvi kwa mita moja ya ujazo ya maji zinahitajika Kilowatt 2 tu za umeme huo, Kumbuka Dunia haina uhaba wa maji bali maji mengi ni ya chumvi yasiyofaa kwa matumizi ya kawaida ya binadamu.

Afya.
Kampuni moja iitwayo, Qualcomm inadhamini mashindano ya dola milini 10 kuleta huduma za afya kiganjani na tayari kuna makampuni 312 katika nchi 38 yanayoshindana kuunda kifaa cha matibabu kinachoitwa TRICORDER ambacho kitafanya kazi na simu za mkononi kugundua aina yeyote ile ya ugonjwa uliokuwa ndani ya mwili wa binadamu baada ya mtu huyo kukipumulia, kuweka sampuli ya damu pamojana kuscan macho.

Ufyatuaji wa maumbo ya vitu(3D Printing)
Kama vile unavyotoa fotokopi ya maandishi ya kitu, zipo printa maalumu ambazo unaweza kukitoa kitu chochote kile kama kilivyo. Kwa mfano unataka kiatu cha namna fulani, unakipiga picha(scan) kile kitu na kisha unakiprint(kukiunda) kama kilivyo. Halikadhalika unaweza kutoa spea za aina mbalimbali za mashine kama magari, ndege, pikipiki nk. Huko nchini china wameanza hata ku3D majengo ya ofisi na inakisiwa ifikapo mwaka 2027 karibu asilimia 10% ya vitu vyote vinavyozalishwa viwandani vitakuwa vinaweza kufyatuliwa.

Fursa za biashara.
Ikiwa unafikiria kuingia katika biashara fulani, hebu jiulize kwanza kama biashara hiyo itakuwepo miaka kadhaa ijayo au haitakuwepo, na kama jibu ni itakuwepo basi jiulize tena ni kwa namna gani utakavyoweza kuitekeleza biashara hiyo haraka iwezekanavyo. Na kama biashara hiyo haiwezi kufanyika kupitia simu yako, sahau kabisa kuhusiana na wazo la biashara hiyo. Biashara yeyote ile iliyokuwa ikionekana ni yenye faida katika karne ya 20 itakuwa haina faida tena katika karne ya 21.


Tayari kuna application iitwayo, “moodies” inayoweza kukueleza kama upo katika mudi gani. Ifikapo 2020 kutakuwa na app itakayokuwa na uwezo wa kutafsiri hali ya uso wa mtu ikiwa kama anachozungumza ni ukweli au uwongo. Hebu fikiria itakuwaje wakati wanasiasa watakapokuwa wakinadi sera zao majukwaani wakati wa kampeni huku ukiwa na simu yako yenye uwezo wa kutambua ikiwa anatoa sera za uwongo au za kweli.

Ajira.
Miaka 20 ijayo asilimia 70 – 80% ya kazi zitatoweka na kutakuwa na kazi mpya nyingine ila haijulikani ikiwa kutakuwa na kazi mpya za kutosha katika kipindi kifupi namna hiyo. Wahitimu wa vyuo watatakiwa kufundishwa kwamba baada ya mahafali huwezi tena kwenda kutafuta ajira na badala yake unakwenda kutengeneza ajira.

Kilimo.
Siku zijazo kutakuwa na maroboti ya bei rahisi mpaka kufikia dola $100. Wakulima katika nchi za Dunia ya 3 sasa watageuka kuwa mameneja katika mashamba yao wenyewe badala ya kufanya kazi siku nzima katika mashamba hayo. Uoteshaji wa mazao bila kutumia udongo (Aeroponic) unahitaji maji kidogo zaidi. Nyama iliyotengenezwa maabara sasa ipo na itakuwa bei rahisi kushinda nyama ya kawaida ya ng’ombe ifikapo mwaka 2018.


Kuna makampuni mengi mapya yatakayoleta protini ya wadudu sokoni hivi karibuni, ina protini nyingi kushinda ile iliyokuwepo katika nyama na itaandikwa “Chanzo mbadakla cha protini   (kwasababu watu wengi bado hawakubaliani na wazo la kula wadudu)

Mfumo mpya wa fedha (Fiat Currency)
Badala ya kutumia sarafu na noti za kawaida, utatumika mfumo mpya wa sarafu za kielektroniki(BITCOIN) ambao hautakuwa na mipaka ya nchi kama ilivyokuwa sasa hivi kila nchi na sarafu yake.

Umri wa kuishi binadamu.
Wastani wa umri wa binadamu kuishi umeongezeka miezi mitatu 3 kwa mwaka. Miaka 4 iliyopita wastani ulikuwa ni miaka 79 na sasa hivi umepanda mpaka wastani wa miaka 80. Inakisiwa ifikapo mwaka 2036 watu wengi zaidi watakuwa na uwezo wa kuishi miaka zaidi ya 100

Elimu.
Simu ya kisasa “Smartphone” ya bei rahisi kabisa tayari inauzwa katika masoko ya Afrika na Asia kwa bei ya Dolla za Kimarekani , $10, ifikapo 2020 asilimia 70% ya binadamu wote duniani watakuwa wanamiliki simu za kisasa za  mkononi ‘smartphones’ Hiyo inamaanisha kwamba kila mtu atakuwa na uwezekano sawa wa kupata elimu bora inayopatikana nchi nyingine zilizoendelea. Kila mwanafunzi katika nchi zinazoendelea ataweza kutumia masomo yote yanayotolewa katika mtandao kwa wanafunzi katika nchi zilizoendelea hivyo ndani tu ya mwaka mmoja mwanafunzi katika nchi masikini atakuwa na uwezi wa kuongea kiingereza fasaha.


Ni dunia inayokwenda kwa kasi na inazidi kukimbia, kutakuwa na fursa pamoja na majanga njiani. Viongozi wajao kwenye biashara wanatakiwa wawe na uwezo mkubwa wa kusimamia haya mabadiliko chanya pamoja na mabadiliko hasi haraka na kwa ufanisi zaidi kushinda wakati wowote nyakati zilizopita.

Je, ndugu msomaji, upo katika nafasi ipi katika kujiandaa na mabadiliko haya makubwa ya dunia yanayozigusa sehemu muhimu zaidi za maisha yetu?. Usisubiri kusombwa na mafuriko yatakayosababishwa na dhoruba la mabadiliko haya fanya maamuzi sasa kuona ni jinsi gani utakavyoweza kukabiliana nayo pindi yanapojitokeza.

Narudia tena ndugu msomaji kwamba, ripoti hii lengo lake kubwa ni kuhamasisha na kusisimua mawazo. Yote yaliyoandikwa hapa yalikuwa ni makisio tu ya muelekeo wa mabadiliko ya kasi ya teknolojia yaliyofanywa na taasisi ya Singularity University ya jijini California Marekani pamoja na makisio au mtazamo wangu mwenyewe binafsi juu ya teknolojia mbalimbali zilizowahi kutumika hapa nyumbani Tanzania. Makisio hayo hayawezi kuwakilisha uhalisia wa mambo utakavyokuwa kwa asilimia 100% miaka kadhaa ijayo.

*Shukrani kwa tovuti ya EQUITAS 

………………………………………………………………………


FURSA MPYA YA BIASHARA!

Self Help Books Publishers
Inatangaza fursa ya kipekee kwa yule mwenye mapenzi na biashara ya uandishi wa vitabu. Ikiwa una wazo la kuandika kitabu chochote kile au tayari unao mswada wa kitabu uliokwisha andikwa, njoo kwetu tukuonyeshe njia rahisi ya kuugeuza mswada huo kuwa kitabu kamili ndani ya muda mfupi.

·       Ikiwa tayari mswada umekwisha andikwa katika kompyuta, kitabu kitachukua siku tatu tu kukamilika na kuingia sokoni.

·       Utawezeshwa kuchapisha vitabu vya kawaida vya karatasi(Hardcopy) sambamba na vile vya kwenye mtandao(Softcopy)

·       Utatengenezewa blogu nzuri yenye kila kitu muhimu kwa ajili ya kupromoti kitabu chako ikiwemo e-mail listing, mitandao ya kijamii pamoja na kufundishwa namna ya kuihudumia blogu yako hiyo kama hujui ikiweo uandishi wa makala za kuvutia wateja wa kitabu chako.

·         Utafundishwa pia njia za kukitangaza na kukisambaza kitabu chako nje ya mtandao(offline marketing)

·        Gharama ya mafunzo na huduma zote ni shilingi elfu 50 kwa kitabu cha kurasa zisizozidi 100. Kuanzia kurasa 100 na kuendelea ni shilingi laki moja.

·         Gharama za kuchapa vitabu itategemea ni idadi gani ya vitabu unayotaka. Unaweza ukatoa idadi yeyote ile ya vitabu uitakayo ilimradi isipungue vitabu 10. Pia gharama hizo za kutoa vitabu hazihusiani na gharama(ada) ya mafunzo.

·       Ukiamua kwa mfano kuanza na vitabu10  - 15 vya kurasa chini ya 100, gharama zote, mafunzo pamoja na kuchapa vitabu hivyo hazitazidi wastani wa shilingi laki moja. Hivyo unakuwa umemiliki kampuni yako ndogo kwa mtaji wa shilingi 100,000/= tu kuanzia hatua za wazo mpaka mauzo, online na offline

·       Mafunzo ni kwa vitendo kwenye kompyuta pamoja na kwenda field maeneo mbalimbali jijini wakati wa maandalizi ya kitabu na mshiriki anafundishwa peke yake mmojammoja na mtaalamu mwenye uzoefu wa muda mrefu katika fani ya uandishi na uchapishaji.

·        Kitu cha pekee katika mpango huu ni kwamba mtu anawezeshwa kuchapisha kitabu chake kwa gharama ndogo kabisa iwezekanavyo, kitu ambacho kisingewezekana kabisa katika uchapishaji wa kawaida uliozoeleka. Pia haichukui muda mrefu, ni siku 3 tu au nne kama mswada umeshakamilika mtu unaingia sokoni.

·         Tunapatikana MBEZI KWA MSUGURI karibu na stendi au unaweza kuwasiliana nasi kwa namba zifuatazo,

 0712 202244  au  0765 553030


KARINBU SANA UJE TUKUONYESHE NJIA MPYA NA RAHISI ZA KUFANYA MAMBO!


Kwa vitabu mbalimbali, kutoka Self Help Books tembelea, 


Kujiunga na BLOGU YA MASOMO YA SEMINA, lipa kiingilio shilingi elfu 10 kisha ubonyeze hayo maandishi.     

0 Response to "NJIA MPYA ZA KUFANYA MAMBO: DUNIA, BIASHARA, AJIRA VINABADILIKA KWA KASI YA AJABU"

Post a Comment