WANASAYANSI WAGUNDUA MNYAMA WA AJABU | JIFUNZE UJASIRIAMALI

WANASAYANSI WAGUNDUA MNYAMA WA AJABU

Wanasayansi wa Marekani wamegundua aina mpya ya mamalia anayeishi misitu minene huko Colombia, na Equado anayeitwa Olinguito na ni  kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 35 iliyopita ugunduzi kama huo kufanyika katika eneo la  Marekani ya kusini. Yupo katika kundi la mamalia wanaokula nyama (Carnivore) na jina lake kisayansi anaitwa Bassaricyon neblina.

Mnyama Olinguito aliyegunduliwa.

Ugunduzi huo uliochukua zaidi ya muongo mmoja umehusisha taasisi ya  Smithsonia  ambapo mtaalamu  Kristofer Helgen  alipokuwa akipanga vitu kwenye jumba la makumbusho la Chicago aligundua ngozi na mifupa iliyokuwa imehifahiwa. “Ilinibidi nisimame kwanza” aliieleza BBC. “Ngozi ilikuwa na rangi nyekundu iliyokolea na nilipotazama fuvu lake, sikuweza kubaini kama ni la mnyama wa aina gani. Lilikuwa tofauti kabisa  na wanyama jamii yake. Mara nikafikiri angeweza kuwa spishi(aina) mpya katika sayansi”


Oliguito ni jamii ya Carnivora(mamalia wanaokula nyama) kundi moja na Paka, Mbwa na Dubu.

Naye Chris Norris, kutoka Makumbusho ya Yale Peabody Museum of Natural History Connecticut na raisi wa taasisi ya (Preservation of Natural History Collections) anasema kwamba mnyama huyu katika miaka ya 70 alidhaniwa kimakosa kwamba yupo katika kundi moja na wanyama wale wanaofanana naye kumbe siyo. “Wataalamu walishangaa ni kwa nini alipochanganywa nao hawakuweza kuzaana na walijaribu kumchanganya katika zoo mbalimbali lakini alikufa kabla hawajamgundua. Pengine ilikuwa ni kutokana na kutokuwepo wakati huo utaalamu wa kisasa kama wa kuchuja DNA.

Mpaka sasa hivi Wanasayansi Duniani kote wameweza kugundua na kuhifadhi sehemu ndogo sana ya viumbehai wa Sayari hii. Spishi mpya za wadudu, minyoo, bacteria na virusi bado wanagunduliwa lakini kwa mamalia imekuwa ni kwa nadra sana.

Mgunduzi Dr. Helgen akiwa na spishi ya mamalia aliyogundua.

“Hii inatukumbusha kwamba Dunia bado kabisa haijatafitiwa vya kutosha na zama za ugunduzi bado kabisa zingali zipo katika hatua za mwanzo” Anasema Dr.Helgen.  MnyamaOliguito anatufanya tufikiri ni vitu gani zaidi ambavyo bado havijagunduliwa.  

0 Response to "WANASAYANSI WAGUNDUA MNYAMA WA AJABU"

Post a Comment