HATUA 7 RAHISI ZA KUANZISHA BIASHARA YAKO NDOGO UKIWA BADO KAZINI UMEAJIRIWA | JIFUNZE UJASIRIAMALI

HATUA 7 RAHISI ZA KUANZISHA BIASHARA YAKO NDOGO UKIWA BADO KAZINI UMEAJIRIWA

1.  Anza kwa kuwa na mtazamo sahihi akilini wa kijasiriamali.

Kwanza kabisa anza wewe mwenyewe kuiandaa akili yako kisaikolojia kuwa na mtazamo wa kijasiriamali(entrepreneurial mindset) kwani mafanikio yeyote yale ama utajiri huanza na mtazamo sahihi, maneno sahihi na mpango sahihi. ”Miongoni mwa watu zipo tofauti ndogo lakini tofauti  hizo ndogo matokeo yake huzaa tofauti kubwa. Tofauti hizo ndogo ni mitizamo na  tofauti kubwa ni ikiwa mitizamo hiyo ni hasi au chanya.”-maneno hayo yaliwahi kutamkwa na mwandishivitabu na mfanyabiashara mashuhuri  W. Clement Stone.


Ni dhahiri kabisa kwamba kuanzisha biashara, ni lazima ipo siku itakubidi ufanye uamuzi mgumu wa kuamua kuachana kabisa na ajira uliyokwisha izoea na ambayo inakupa ulinzi kifedha, utakuwa sasa unahama rasmi kutoka kuwa mwajiriwa na kuwa mwajiri hivyo inakupasa ujiandae kiakili na changamoto zote zinazoambatana na hatua hiyo ya awali ya kuanza biashara kuanzia mizizini.

Thomas Jefferson, Rais wa tatu wa Taifa la Marekani naye aliwahi kusema hivi; “Hakuna chochote kiwezacho kumzuia mtu mwenye mtazamo sahihi wa mawazo kutimiza malengo yake;  na hakuna chochote kile juu ya Dunia kinachoweza kikamsaidia mtu mwenye mtazamo potofu wa akili”

SOMA: Njia za kujiingizia kipato cha ziada nje ya kazi yako ya msingi.

Kuanzisha biashara ndogo, iwe ni katika muda wako wa ziada, nje ya kazi ama kama shughuli yako ya kudumu  masaa yote inakupasa kuwajibika au kubeba majukumu na ili kuifanikisha kwa mafanikio unatakiwa kujijengea stadi au tabia za kijasiriamali kama vile, uvumilivu, mbinu za uongozi, stadi za mawasiliano, stadi za mauzo, majadiliano nk. Somo zima la stadi na tabia za ujasiriamali limeelezewa kwa kina sana katika kitabu chetu kiitwacho “MICHANGANUO YABIASHARA NA UJASIRIAMALI” kukipata bonyeza maandishi hayo.

2.  Andika Mpango wa Biashara.
Hatua inayofuata katika kuanza biashara muda wako wa ziada ni kuandika mchanganuo wa biashara kutokana na wazo lako la biashara uliyoichagua. Unaweza ukawa tayari unao mpango wako wa biashara kichwani na ni lazima utakuwa nao kwani kitendo tu cha kufikiria kuanza biashara tayari ni hatua moja ya kuanza kupanga. Ninachosisitiza hapa ni kuandika katika karatasi. Mpango wa biashara unaweza ukaandika vyovyote vile hata kama ikiwa hautafuata zile taratibu rasmi za kuandika mpango wa biashara.


Unaweza ukaorodhesha yale mambo ya msingi tu yatakayosaidia katika kufanikisha biashara yako kama vile, una malengo gani na biashara yako, biashara itakuwa mahali gani,  mtaji wako ni shilingi ngapi na utaupata kutoka wapi, ni nani utakayemuachia majukumu ya biashara wakati haupo,  ni kina nani unaotarajia kuwauzia bidhaa/huduma zao, ni akina nani wanaofanya biashara kama unayotaka kufanya, ni mbinu gani utakazotumia kujulisha wateja juu ya uwepo wako, unatarajia bidhaa/huduma zako utauza shilingi ngapi, faida unayotegemea kuipata katika kipindi fulani, chaweza kikawa ni  siku, wiki, mwezi au hata mwaka nk.

Kwa kifupi unapaswa kufanya tathmini nzima na kwa kina jinsi unavyotarajia  kuianzisha na kuiendesha biashara yako ndogo ungali bado na majukumu mengine ya kazi au ajira.

3. Tafuta msaidizi  au mbia mwenye malengo na biashara.
Kabla hujachagua mbia wa biashara au msaidizi, ni lazima uhakikishe kwanza, kuwa huyo utakayekwenda kushirikiana naye katika biashara anayo maono na ndoto sawa na za kwako. Anapaswa kuzifahamu barabara changamoto zinazoweza kutokea kwenye biashara mnayotaraji kuifanya na anatakiwa pia kuwa tayari kutoa mchango wake uliokuwa sawa na wa kwako  kuhakikisha uhai wa biashara.

Wafanyabiashara wakubwa na waliofanikiwa  sana kama akina Bill Gates, Steve Jobs, Mark Zuckerberg na wengineo wengi  katika nyakati tofauti wamewahi kukiri kwamba mafanikio yao makubwa kwa kiasi kikubwa yametokana na kutengeneza ubia mzuri tangu hatua za awali kabisa za kuanza kwa miradi yao.

Jambo lingine la kuzingatia unapomchagua mtu wa kusaidiana naye kwenye biashara kama mbia ni nguvu alizokuwa nazo huyo mwenzako; ni lazima uchague mtu mwenye uwezo ambao wewe hauna;  kwa mfano kwa kuwa wewe bado utakuwa kwenye ajira au shughuli nyingine itakuwa ni jambo la busara kumpata mtu ambaye yeye muda wake wote atautumia katika biashara yenu kusudi aweze kujaza pengo lile litakalotokana na kukosekana kwako pale muda wa kazi.

Ikiwa biashara yako utaamua kuifanya na mbia, basi hakikisheni mnaweka ua wa kisheria ili kuepukana na matatizo yanayoweza kuja kujitokeza hapo baadaye. Labda uwe umeamua kufanya mwenyewe ukamuweka mfanyakazi lakini ikiwa ni mbia mkataba wa kisheria ni kitu cha lazima na mara nyingi sana kwa watu wanaoanzisha biashara ndogo “part time” wakiwa wangali bado kazini au katika majukumu mengine tofauti, huwa wanawatafuta wabia na siyo kuendesha peke yao au kuajiri mfanyakazi. Na uzoefu kote duniani unaonyesha kuwa biashara ndogo ukiwa kazini hushamiri na kupata mafanikio makubwa unapoifanya kwa ubia na mtu mwingine.

4. Sasa Anza Biashara yako bila kuchelewa.
Wahenga hawakukosea waliponena, “Asiyeanza, kamwe hatamaliza”  Kuanza biashara ni kama vile mtu unapotengeneza mashua  na kuanza safari baharini huku ukiwa  mkononi  una ramani, mpango, pamoja na timu ya wasaidizi pembeni. Unatakiwa kusafiri pamoja na kutokuwa na uhakika asilimia mia moja wa usalama dhidi ya dhoruba wala hali ya hewa isiyotabirika. Endapo  mashua yako itazama baharini, kuna mawili, ukatishe kabisa  safari  na kuachana nayo, ama uamue kurudi ufukweni, ukatengeneze mashua nyingine na kuanza safari tena upya.


Kwa nini nasema uanze biashara yako bila kuchelewa?, nasema hivyo kwa sababu waajiriwa wengi wamekuwa wakiota kuanzisha biashara zao ndogo wangali bado wakiendelea na ajira zao lakini kitu kikubwa ambacho mara zote kimekuwa kikiwavuta shati kwa nyuma wasianze kimekuwa ni “WOGA”. Huendelea tu kufanya mipango siku hadi siku wakisubiri kila kitu kitengemae, kumbe haitafika siku hata moja kila kitu kikatimia ndipo uanzishe jambo.

Katika kitabu cha Gwiji, Robert Kiyosaki, “Before you Quit your Job, 10 Real Life Lessons…..” anabainisha kwamba, vipo vipengele vitatu unapoanzisha biashara, cha kwanza ni mpango sahihi, cha pili ni timu sahihi na cha tatu ni mtaji(pesa). Katika hili Kiyosaki anaelezea kwamba, hutokea mara chache sana vipengele hivi vitatu vikapatikana vyote kwa pamoja  wakati mtu anapoanzisha biashara. Anaendelea kutanabahisha kwamba;

“Ni jukumu lako mjasiriamali kuchukua kipengele kimojawapo na kuanza kufanya biashara, vingine viwili vinavyobakia utakutana navyo mbele ya safari. Kuvipata vipengele viwili vilivyosalia inaweza ikakuchukua mwaka au hata zaidi ya miaka 10; swala ni kwamba, anza na kile ulichokuwa nacho” – Robert Kiyosaki.

Hata kama hauna mtaji wa kutosha, anza tu na kile ulichokuwa nacho kwani makampuni unayoyasikia  yakitamba duniani leo hii kama vile, ‘Yahoo’, ‘Google’, ‘facebook’ na hata ‘Dell ‘yote hayakuwa na fedha za kukodi vyumba kwa ajili ya ofisi, badala yake walianzia katika mabweni ya shule na vyuo. Siyo hao tu, kina ‘Amazon’, ‘Ford motors’ na ‘Apple’ wao ofisi zao zilianzia katika magereji ya kutengenezea magari

5. Pangilia ratiba zako na gawa majukumu kwa mbia wako.
Hatua ya tano ni wewe kupangilia ratiba zako kwa kufahamu muda utakaokuwa ukijihusisha na biashara yako. Je, utakuwa ukijihusisha usiku, muda baada ya masaa ya kazi, ama mwishoni mwa juma wakati wa ‘weekend’? Ili biashara yako iweze kusimama ni lazima uipe muda wa kuishughulikia, na uuheshimu muda huo kwani kitu kikubwa kuliko vyote utakachopaswa kuwekeza katika biashara yako ikue ni muda. Ili kupata muda, panga ratiba, jua malengo yako ni yapi, panga na kuutumia muda kikamilifu, ainisha vikwazo na fursa kisha tengeneza mikakati.

Ikiwa unaye mbia hapa sasa ndipo mahali anapotakiwa kuonyesha uwajibikaji wake. Mbia atakusaidia kutimiza baadhi ya majukumu huku wewe ukielekeza nguvu zaidi kwa yale majukumu ya msingi zaidi yanayoifanya biashara iweze kukua. Hakikisha mnagawana sawa majukumu na kila mmoja kuwajibika kwa  kila jukumu atakalopangiwa kulifanya.

6. Panga muda au lengo utakapoacha kazi yako.
Baada sasa umekwisha anza biashara yako ndogo, hatua inayofuata itakuwa ni kuweka lengo la muda utakapoachana na kazi yako au ajira uliyokuwa nayo. Bila shaka yeyote  ipo siku moja utakwenda kuacha kazi na kuamua muda wako wote uutumie katika kuijenga biashara yako. Jambo hili  la kupanga tarehe ya kuondoka unaweza ukalifanya kwa kutumia vigezo tofauti, kwa mfano unaweza ukatumia kigezo cha kiwango fulani cha ukuaji wa biashara au kigezo kingine chochote kile kilichofikiwa. Hata hivyo bila ya kuzingatia kigezo chochote ulichochagua, ni lazima ujiwekee muda utakapoachana na kazi yako na kuamua sasa kuelekeza nguvu zako zote na muda kwenye biashara yako.

7. Endelea kuwekeza kwenye biashara yako mpaka utakapofikia malengo yako ya ujasiriamali.
Kumbuka ya kwamba kuwa na biashara endelevu siyo kazi unayoweza ukaifanya kwa siku mbili ama tatu, ni mchakato endelevu. Ili iendelee kuwepo inabidi uendelee kuifanyia ubunifu mpaka pale ambapo itakuwa imekua kubwa kiasi ambacho siyo lazima tena uwepo wewe ndipo iweze kuishi.

Kitu kingine muhimu sana na usichopaswa kamwe kukisahau ni kwamba, kama mjasiriamali, ni lazima ujifunze kuishi bila ya kutumia mapato yatokanayo na biashara yako ili kuhakikisha mzunguko chanya wa pesa unakuwepo mpaka pale biashara itakapokuwa kubwa vya kutosha.

…..……………………………………………………….

Kwa msaada zaidi wa jinsi mtu unavyoweza ukafanikiwa katika mchakato mzima wa kuanzisha  biashara ukiwa bado unaendelea na kazi au majukumu yako mengine ya msingi, ninapendekeza kitabu chetu kiitwacho “MIFEREJI 7 YA PESA NA SIRIMATAJIRI WASIYOPENDA KUITOA”  Toleo jipya lililoboreshwa na kuongezewa vitu, 2016,  nina uhakika kitazidisha uwezekano wako wa kufanikiwa. Kukipata kitabu hicho, bonyeza maandishi makubwa ya jina la kitabu hapo juu. Kinapatikana kwenye mifumo yote,  kama kitabu cha kawaida cha karatasi(hard copy) na pia katika mfumo wa kitabu-pepe(soft copy)PDF file

Pia kupata vitabu vingine vya self help books ltd kupitia email kwa njia ya simu yako ya mkononi, tablet au hata kompyuta ya kawaida, tembelea ukurasa huu maalumu uitwao SMART BOOKS TANZANIA.

Mwandishi na mhamasishaji wako;

Peter A. Tarimo




2 Responses to "HATUA 7 RAHISI ZA KUANZISHA BIASHARA YAKO NDOGO UKIWA BADO KAZINI UMEAJIRIWA"

  1. Asante sana Mentor, umekuwa msaada sana kwangu soon nataraji kujiunga niweze kusoma vitabu vyako..
    Waandishi wengi huishia ku inspire watu tuu lakini hawatoi practical oriented financial educational kama Robert Kiyosaki.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Nashukuru na karibu sana ndugu Mulaki, unachosema ni kweli watu wanahitaji kuwa inspired lakini pia wajengewe uwezo wa kuyatia katika matendo yale wanayojifunza

      Delete