BIASHARA YA KUTEMBEZA BIDHAA ZA JUMLA MADUKANI, MBINU 7 | JIFUNZE UJASIRIAMALI

BIASHARA YA KUTEMBEZA BIDHAA ZA JUMLA MADUKANI, MBINU 7

Biashara ya kuwasambazia wenye maduka bidhaa hususani  yale maduka yanayouza rejareja, ni biashara ambayo imekuwa ikifanywa na watu wengi jijini Dar es salaam na hata katika mikoa mingine nchini. Mtu anakwenda katika maduka makubwa, au viwandani, ananunua bidhaa kwa bei ya chini, kisha anakwenda kuziuza kwa wenye maduka ya rejareja mitaani kwa bei ambayo yeye hupata faida. 

SIRI YA KUFANYA ILI KUKUPA FAIDA NZURI.
Biashara yeyote ile ili iweze kuwa endelevu na inayolipa inahitaji kuwa na wateja wa uhakika na wakudumu. Katika biashara hii ya kusambaza bidhaa za jumla kwenye maduka ya rejareja, wengi wa wale wanaoifanya kuna kitu kimoja tu wanachoshindwa kukizingatia ambacho ndicho huchangia kuiona biashara hii kuwa ni ngumu na isiyokuwa na faida ya kutosha.

Katika biashara yeyote ile ni lazima umlenge yule mteja wako, na kubaini ni kitu gani hasa anachokitaka. Kushindwa kubaini kile mteja anachokitaka  hasa husababisha biashara kuwa ngumu.

Kumbuka ya kwamba mwenye duka unayekwenda kumuuzia bidhaa ana njia nyinginezo za kupata bidhaa hizo, na mara nyingi huwa ni kutoka katika maduka ya jumla au hata katika zile sehemu ambazo na wewe huwa unakwenda kununua ili kuja kuwauzia.

Hivyo hapa siri kuu ipo katika bei. Kitu cha kwanza mwenye duka anachokifikiria anapomuona mtu amemletea bidhaa hadi mlangoni, ni je, bei yake ukilinganisha na za kule kwingine anakokwenda kununua bidhaa kama hizo zikoje?, ni kubwa zaidi, zinalingana  au zipo chini zaidi?

Ili kupata faida hapa inakubidi uuze kwa wingi, lakini pia kuhakikisha kuwa kule unakonunua na wewe unapata kwa bei nzuri yenye faida. Kwa hiyo hapa kazi ipo kwako kuzunguka na kuhakikisha unapata bidhaa zako kutoka  yale maeneo wanakouza kwa bei nafuu kabisa, lakini pia zingatia na ubora wake usije ukanunua “mchina”(feki) wateja wakakukimbia.

Ili wateja wako wanunue bidhaa zako pasipo kusitasita pindi unapobisha hodi madukani mwao, wanachokitaka wao ni uwauzie bidhaa hizo aidha kwa bei ileile wanayonunulia kwingineko, au bei chini ya hiyo. Hii huwapa kitu cha ziada kwani hawaoni ni kwa nini wapoteze muda wao wa dhamani na nauli ya kwenda kufuatilia bidhaa ambazo wanaweza wakaletewa hadi mlangoni kwa bei ileile au chini ya hapo.

CHANGAMOTO.
Chngamoto kubwa iliyopo katika biashara hii ni jinsi gani mtu utafanya ili uweze kukabiliana na kikwazo hicho cha kuhakikisha wateja wako wanapata bidha kwa bei ileile wanayoweza wakapata kwingineko katika maduka makubwa ya jumla au hata kutoka viwandani moja kwa moja. Mbinu moja wapo 7 ambazo unaweza ukazizingatia ni hizi hapa chini ;
1.Kubali kupata faida kidogo, kwa ajili ya kujenga soko lako  kwani biashara ni wateja kwanza na siyo faida, faida itakuja tu baadaye utakapokuwa umekwishazoeleka vyakutosha.

2. Hakikisha unajitahidi kufa na kupona kupata punguzo kutoka kule unakokwenda kununua kwa jumla, kwani punguzo hilo hilo laweza likawa ndiyo faida yako, ikiwa utataka kuuza chapchap na kujenga mtandao mpana wa soko lako.

3. Omba kupelekewa bidha mpaka unapohifadhi ikiwa umenunua mzigo mkubwa, wauzaji wengine, au wenye viwanda huwa na  huduma ya kumpelekea mteja bidhaa mpaka anakofika kutegemeana na mazingira fulani fulani kama vile wingi wa bidhaa, mteja wa kila mara nk. Utaona kwamba zile gharama ambazo ungelipia usafiri zinageuka kuwa faida kwako.

Omba kufikishiwa bidhaa unapozihifadhi. 

4. Jitahidi kuwa na bidhaa za aina tofauti tofauti, usijihusishe na aina moja tu ya bidhaa  huku ukilenga zile bidhaa zinazotoka harakaharaka hata kama ikiwa faida yake ni kidogo.Utakapouza kwa wingi ile faida kidogo kidogo unayoidharau hatimaye huwa kubwa baada ya muda fulani.

5. Ikiwa unasambaza bidhaa zako kwa kutembea kwa miguu, jaribu kuwa na angalao usafiri wa baiskeli, pikipiki au hata gari kama unao uwezo huo  ili kuongeza tija zaidi kwa kuokoa muda pamoja na kuwa na uwezo wa kubeba bidhaa nyingi zaidi.

6. Kuwa tofauti, jitahidi kutafuta kitu kitakachokufanya uwe tofauti na watu wengine wanaofanya biashara ya kuwasambazia watu bidhaa kama wewe, jambo au kitu hicho chaweza kuwa  hata unadhifu wako, namna unavyozipanga bidhaa zako au kuzifungasha, muda unaowafikishia wateja bidhaa nk.
kuwa na angalao usafiri wa baiskeli, pikipiki au hata gari 
7.Zingatia kanuni zote za uuzaji, kama vile kauli nzuri unapowasiliana na wateja wako, jenga mahusiano mema ukizingatia kwamba mteja ni mfalme na kamwe hakosei.

----------------------------------------------------------------------------------
*Ndugu msomaji wa makala hii, ukitaka kusoma makala zaidi zinazohusiana na masomo muhimu ya Ujasiriamali tu peke yake, basi nenda moja kwa moja pembeni mwa blogu kwenye ‘TAGS’ au pale chini kabisa  mahali palipoandikwa  ‘LABELS’ na ubonyeze kwenye LABEL/TAG yenye jina,  “MASOMO MUHIMU”.

Hali kadhalika  kama wewe ni mpenzi wa makala zinazohusiana na Jinsi ya kuandaa Mpango/mchanganuo  wa biashara basi  bonyeza TAG/LABEL  yenye jina la “KUANDIKA MPANGO WA BIASHARA” utapata mfululizo wa makala zote zinazohusiana na jinsi ya kuandika mpango wa biashara.



0 Response to "BIASHARA YA KUTEMBEZA BIDHAA ZA JUMLA MADUKANI, MBINU 7"

Post a Comment