MAPENZI YA PESA: KAWELE MUTIMANWA, “NILIUTUNGA NIMETULIA TANCUT ALMASI ORCHESTRA” | JIFUNZE UJASIRIAMALI

MAPENZI YA PESA: KAWELE MUTIMANWA, “NILIUTUNGA NIMETULIA TANCUT ALMASI ORCHESTRA”

Mwanamuziki mkongwe mwenye asili ya Congo Kawele Mutimanwa  amewaasa wanamuziki wa Tanzania hususan wale wanaopiga muziki wa dansi, kuwa wabunifu na kutokukubali kuajiriwa daima, wawe mabosi wao wenyewe kwa kuanzisha bendi zao.

Kawele Mutimanwa aliyasema hayo alipokuwa akifanya mahojiano katika kipindi cha Zilipendwa kinachorushwa hewani kila wiki siku ya ijumaa na mtangazaji maarufu TBC1, Manju wa muziki, Masoud Masoud. Alikiri kuwa ni kweli hali ya wanamuziki wa hapa Tanzania inasikitisha lakini alisema kuwa yeye binafsi hali hiyo hawezi kuibadilisha ila ataongea nao kufikiria kitu kingine tofauti, wabadilike, siyo kuacha muziki la hasha bali;

Ni lazima wafikirie kufanya muziki kama bendi yenu  na sio bendi ati ya bosi, kama mtakuwa  watano sita watu kumi… maisha ni mazuri, afadhali hata kama hamna vyombo, afadhali muanze  kukodisha vyombo, ni bendi yenu, mkipata shilingi kumikumi ni yenu, lakini ikiwa kwamba, mnasubiri bosi, bosi kwanza ashibe, familia yake ishibe, ndio aje kuangalia nyinyi hiyo ni wrong way” Alisema Kawele Mutimanwa.

Alipoulizwa  ni siri gani iliyomfanya atunge kibao hiki cha mapenzi ya pesa na kikafanikiwa kuwa kizuri kiasi hicho alijibu kwamba ni utulivu wa nafsi aliokuwa nao akimaanisha kwamba wakati huo akiwa Tancut Almas wanamuziki walikuwa wakipewa maslahi mazuri tofauti na bendi nyinginezo alizokuwa amewahi kupiga. “Hufikirii, watoto watakula nini, watavaa nini, utawapeleka shule namna gani” alisema Kawele.


Akijibu kwa nini basi alikuja kuihama Tancut Almasi, na kuhamia MK.Group  alisema aliahidiwa donge nono zaidi na Bendi ya MK Group ‘akaruka’ tena. Alitolea mfano bendi kama ya Ok Jaz, tangu enzi za Franco, wapo wanamuziki kama Simaroo Lutumba, hawaoni sababu ya kuhama kwani wanapata kila kitu.

Kuhusiana na muziki wa Bongo flava kuwaharibia soko alisema hiyo ni kweli, wanamuziki wanakosa ‘creation’ wanapenda kukopi na kupiga miziki kama bendi za Congo mfano wanapenda wapige muziki kama  Wenge, Kofii…

Alisema unapokopi ni lazima original itakuwa juu yako, mtu anapokwenda dukani akikuta rekodi ya bendi ya hapa Dar es salaam imepiga kama Wenge na ya Wenge original, moja kwa moja mtu huyo atanunua ile ya Wenge. Alitolea mfano kuliwahi kuwa na bendi moja iliyoitwa Tatu Nane wakaja na mtindo wao wa ajabu ajabu, lakini ‘waliruka’ mara moja kwa sababu walikuja na kitu kipya tofauti. “Uki create kitu ambacho watu kinakuwa kama kipya kwao unaweza uka penetrate”  Alisema Kawele.

Kawele Mutimanwa akilicharaza gitaa la solo.
Kawele Mutimanwa yupo hapa Dar es salaam kwa shughuli za utafiti katika maswala ya muziki, Alizaliwa mwaka 1957 huko Bukavu, baada ya kutoka DRC miaka hiyo ya 70 na kuja Tanzania kutafuta maisha kimuziki alipita vikundi mbalimbali pamoja na kuzunguka maeneo mengi yakiwamo Kenya, Uganda, Zambia, Rwanda na Burundi. Aliwahi pia kuwapigia gitaa wanamuziki wengi wa Kicongo na hata wa hapa nchini wakiwemo, Kanda Bongoman, Sam Mangwana, Ndala Kasheba, Makassy, Samba Mapangala, Remmy Ongala, King Kikii pamoja na bendi mbalimbali.

Dr.Remmy Mtoro Ongala
Mnamo miaka ya 90 katikati alialikwa kufanya ziara na mwanamuziki Remmy Mtoro Ongala, katika nchi za Ulaya Marekani na Asia, ndipo alipoamua kubaki na kuishi nchini Uingereza ambako baada ya miaka mitano kupita aliomba na kupewa Uraia wa Uingereza. Lakini anasema Tanzania ni nchi yake na anaipenda ndiyo maana karibu kila mwaka huja Dar es salaam kubadilishana mawazo na wanamuziki wa hapa ikiwa ni pamoja na kuwapa wawazo mapya.

0 Response to "MAPENZI YA PESA: KAWELE MUTIMANWA, “NILIUTUNGA NIMETULIA TANCUT ALMASI ORCHESTRA”"

Post a Comment