DR. FENELLA MUKANGARA: CLUB RAHA LEO SHOW IJUMUISHE MASOMO YA UJASIRIAMALI WA SANAA | JIFUNZE UJASIRIAMALI

DR. FENELLA MUKANGARA: CLUB RAHA LEO SHOW IJUMUISHE MASOMO YA UJASIRIAMALI WA SANAA


Wakati akifunga mashindano ya kuimba na kucheza muziki yanayoendeshwa na Redio ya Taifa TBC jana tarehe 11 April 2015, Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo  Dr. Fenella Mukangara alisema kwamba  inafaa shindano hilo linaloendeshwa kwa muda wa kipindi cha miezi mitatu, likahusisha pia na mafunzo ya Ujasiriamali wa masuala ya sanaa kwa washiriki kusudi wanapotoka pale,  washindi waweze kupata ajira katika mahoteli mbalimbali pamoja na kuanzisha vikundi  vitakavyokuwa rahisi kupata misaada mbalimbali kwa wale ambao hawatakuwa wakipata ushindi.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo  Dr. Fenella Mukangara

Aidha  Waziri Mukangara aliaasa vijana tunapoelekea kipindi cha uchaguzi mkuu,  kutaibuka  migomo na migogoro ya kila aina, hivyo wajiepushe kabisa nayo kwani maendeleo hayawezi kuja pakiwa na migogoro na migomo isiyokuwa ya lazima. Aliwaasa pia kujiandikisha muda utakapowadia ili kupiga kura kwa wagombea wanaowataka na pia kuhakikisha wanaichagua katiba iliyopendekezwa kwani ni halisi.
Shindano hilo linalosimamiwa na Manju wa muziki, mtangazaji maarufu Masoud Masoud, lilimalizika huku washindi wa kwanza katika vipengele vya Uimbaji na uchezaji wakijipatia vitita vya shilingi milioni tano kila mmoja na washindi wa pili shilingi milioni mojamoja. Kwenye kipengele cha uimbaji washindi walikuwa  ni; Hassana Chibwana kwa upande wa Taarabu, Mshana Mohamed-Dansi, na Mohamed Kupela katika upande wa Bongo fleva, hawa kwa kuwa fani zao zilikuwa tofauti walishea zawadi kwa kupata shilingi milioni mbilimbili kila mmoja.
 
Manju wa muziki, mtangazaji maarufu Masoud Masoud
Katika upande wa uchezaji, Elizabeth Matapa mshiriki pekee wa kike aliyeonyesha maajabu, alijinyakulia kitita hicho cha sh. Millioni 5, baada ya kutangazwa mshindi wa miondoko ya Salsa, iliyokuwa maarufu sana huko visiwa vya Carrebean, (Cuba na Colombia). Twist alijinyakulia Mzee Joseph Chengula huku Pop ikimuangukia kijana Exavery Anton aliyengara jukwaani utafikiri ni Michael Jackson alikuwa amerudi. Kwa upande wa Rhumba aliyeonyesha umahiri na hatimaye kujinyakulia zawadi ya kwanza ni kijana machachari, Ayubu Hans.

Baada ya jaji mkuu ( Chief Justice)  wa mashindano hayo mwimbaji mkongwe wa Reggae nchini Innocent Nganyagwa kumaliza kazi ya kuwatangaza washindi, ndipo, Mc wa shughuli Masoud Masoud alipowakaribisha tena jukwaani Bendi  ya Le Grand Utalii kutumbuza na ukawa ndiyo mwisho wa Shindano hilo lililokuwa na msisimko wa aina yake.


0 Response to "DR. FENELLA MUKANGARA: CLUB RAHA LEO SHOW IJUMUISHE MASOMO YA UJASIRIAMALI WA SANAA"

Post a Comment