KAMA UNA BIASHARA NDOGO YA MTAJI MDOGO, HIZI HAPA NJIA 11 ZA KUIBUSTI | JIFUNZE UJASIRIAMALI

KAMA UNA BIASHARA NDOGO YA MTAJI MDOGO, HIZI HAPA NJIA 11 ZA KUIBUSTI


MAFANIKIO YA BIASHARA NDOGO
Siku zilizopita niliwahi kuandika makala moja nikasema hivi, Huna mtaji wa kutosha, hukopesheki?Jaribu njia hii ya kufunga mkanda(Bootstrapping). Katika makala hiyo nilieleza jinsi mjasiriamali mdogo asiye na mtaji mkubwa anavyoweza kutumia rasilimali kidogo alizokuwa nazo kuendesha biashara yake pasipo kutafuta msaada kutoka nje.

Sasa leo tena nimekuja na mikakati mingine 11 tofauti ambayo yeyote yule mwenye biashara inayoanza au iliyozorota anaweza akaitumia katika kukabiliana na changamoto kubwa ya mtaji. Mbinu hzi za kujikwamua au kufunga mkanda zimetumiwa na watu wengi zikiwemo hata na taasisi na nchi mbalimbali kama nilivyoeleza kwenye makala hiyo iliyopita. Mbinu za leo 11 ni hizi zifuatazo;


1.Kasi na viwango.
Unapokuwa ukiendesha biashara yako tambua kuwa gharama muda wote zipo palepale uwe umeuza ama haujauza kabisa. Lakini kwa upande wa mapato yanajiamulia yenyewe ni mda gani yaingie kwa mfano mapato yataingia tu pale utakapouza, usipouza hamna kitu! Kwahiyo piga ua kama mjasiriamali, kila kitu kinakutegemea wewe na unapaswa kuhakikisha unajitosheleza muda wote ili mambo yasiende mrama.

Kitu utakachotakiwa kukifanya ili kulitimiza hilo kwa kuwa mfukoni hauna pesa cash za kutosha ni KUONGEZA KASI YAKO YA MAUZO pamoja na kuwa mtu wa VIWANGO. Unapaswa kuwa ni mtu wa kufanya majaribio(utafiti) haraka sana kujifunza haraka na pia kuingiza pesa haraka! Vinginevyo utajikuta umeishiwa kabisa fedha kidogo ulizokuwa nazo na kusababisha biashara kufa au kuanguka vibaya.


2.Anza kidogo.
Kidogokidogo hujaza kibaba na kuna dhana moja inayotumiwa sana katika mabenki na taasisi za fedha, “Compound Interest” ambayo maana yake ni hii, kitu kidogo kinapojiongeza chenyewe halafu kile kilichoongezeka nacho kikawa kinajiongeza sambamba na kile cha mwanzo mfano, riba katika mikopo inapoongezeka huku riba nayo ikizaa riba pia, matokeo yake ni ya kushangaza sana!

Kitu hicho hatimaye huongezeka haraka na kufikia ukubwa wa kushangaza. Na biashara nayo unapoanza kidogo tu lakini huku ukiirudisha faida ile inayopatikana katika mtaji wa awali faida itaongezeka haraka sana na biashara kuwa kubwa ndani ya muda mfupi.

3.Tekeleza kwanza ndipo upange.
Hapa inaweza kuonekana nakinzana na dhana nzima ya mpango wa biashara(business planning) lakini hapana nitafafanua. Moja ya tatizo kubwa la wajasiriamali wanaoanza kushindwa kutoka  pale walipo na kupiga hatua zaidi ni kupanga kupita kiasi. Mipango haiepukiki lakini kuna kiwango anachotakiwa mfanyabiashara mdogo anayeanza kupanga tofauti na wafanyabiashara wakubwa au makampuni.

SOMA: Huna muda wa kutosha kuandika mpango wa biashara? tumia njia hizi 3 rahisi.

Ndio maana kwa mfano katika darasa letu la wasap la michanganuo-online tumeweka machaguo(options) mbalimbali kama vile, tuna kitu kinachoitwa “Ukurasa mmoja wa mchanganuo” hiki ni kielezo(template) inayompa mjasiriamali mdogo anayefunga mkanda fursa ya kutengeneza mchanganuo wake mfupi kwa muda mchache sana huku akiendelea na mambo yake mengine ya biashara haraka.

Kuna Advanced Business Plan Template ya kawaida sasa ambayo hutumika kutengeneza mpango kamili wa biashara, na huu sasa kama unataka kuanzisha biashara kubwa au ya kati, pengine unataka kuanzisha kiwanda chako cha kutengeneza juisi, sabuni, mikate huku ukiwa na mtaji wako wa milioni kadhaa, huwezi kukwepa kutengeneza mpango kamili wa biashara.

SOMA: Jinsi mpango wa biashara unavyoweza kuongeza mafanikio ya biashara yako.

Pointi yangu hapa ni kwamba unapokuwa katika ngazi hii ya ufungaji mkanda mipango iwepo lakini utekelezaji uwe mkubwa na wa haraka zaidi, hii itakusaidia kuepukana na kuja kutekeleza mawazo ambayo tayari yameshapitwa na wakati. Ukiendelea kupanga tu pasipo utekelezaji wa haraka utaishia kubakia na ndoto kichwani zisizotekelezeka. Na hii hutokana hasa na sababu kwamba biashara ndogo zina rasilimali chache mno zisizoruhusu muda upotee.

4.Wewe ndio kila kitu kwenye biashara.
Kwa kimombo wanasema hivi,

CEO = Chief Everything Officer.

Usipoiamini kanuni hiyo hapo juu basi na wala usifikirie hata kidogo wazo la kuanzisha biashara yako mwenyewe, na sahau kabisa habari ya kufunga mkanda. Wewe ndiye utakayefanya kila kitu katika biashara yako kuanzia kufanya usafi kama ni ofisi, kuingia mikataba na wateja, kuuza, kutunza mahesabu, kutafuta soko mpaka kurekebisha holder ya taa na kuinstall program mpya kwenye laptop yako.

SOMA: Jinsi ya kusimamia biashara yako ndogo unayomwachia mfanyakazi.

5.Kuuza kwa kubadilishana bidhaa au huduma na mteja(Barter Trade)
Unaweza usiamini kama inawezekana kupata kitu fulani au huduma bila ya kulipa fedha taslimu kwa kubadilishana na mtu mwingine huduma au bidhaa unazouza wewe yeye akakupatia pia huduma au bidhaa anazouza tena kwa gharama nafuu kuliko ungezilipia taslimu. Njia hii licha ya kupunguza gharama pia huweza kukujengea mahusiano imara na wajasiriamali au wafanyabiashara wengine kama wewe. Chunguza wateja wako mbalimbali wanaokuletea bidhaa au huduma kama na wao wanaweza kuhitaji kile unachouza kisha mnabadilishana.

Mtindo huu wa kubadilishana bidhaa/huduma unaweza usiwe sawasawa na ule uliokuwa ukitumika zama zile za kale za mawe lakini unachopaswa tu kufanya ni kuhakikisha unapata punguzo tofauti na vile ambavyo ungelinunua kwa fedha taslimu. Inaweza kuwa vigumu kubadilishana kitu na wafanyabishara waliopiga hatua, tafuta wale mlio katika ngazi(levo) moja.

 6.Fanya majadiliano ya bei ili kupata bei nzuri zaidi.
Hakikisha bei unayouza ina maslahi kwako, unaweza ukaanza kutaja kiasi cha juu kidogo mwishowe mkafikia muafaka kwenye bei itakayokuwa nzuri kwako.

7.Wekeza kwenye teknolojia.
Teknolojia ikitumika vizuri inaweza ikaokoa fedha nyingi sana na kuongeza ufanisi katika biashara. Tumia muda kutafiti teknolojia zinazoweza kukupunguzia gharama na kuboresha mawasiliano. Teknolojia haitakiwi kuwa ni ya gharama ya juu sana, kwa mfano badala ya kununua programu za kompyuta kwa hela nyingi unaweza ukatumia zile zinazopatikana bure mtandaoni ilimradi zikidhi shida unayotaka kuitatua.

SOMA: Mawazo ya biashara zitakazovuma miaka ijayo 2018 na kuendelea mpaka 2020

8.Mapato ya ziada ya biashara.
Kuna mazingira mengine biashara inaweza ikatengeneza fedha kwa njia isiyokuwa ya moja kwa moja kama vile;

·       Kukodisha sehemu ya eneo/chumba chako cha biashara au kualika watu wengine kuja kushea na wewe ofisi na kisha mnashirikiana pia kulipa pango kwa mwezi.

·       Kuuza vifaa ambavyo huvitumii tena ofisini kwa mfano kompyuta ya zamani nk.

9.Kuhakikisha hesabu za biashara yako zipo sawasawa.
Unapotaja hesabu za biashara mtu moja kwa moja anaweza akaanza kufikiria kumuajiri mhasibu au mtu aliyesomea utunzaji wa fedha lakini hilo si muhimu kwa mjasiriamali anayefunga mkanda. Kujifunza wewe mwenyewe ABC za mahesabu ya biashara siyo lazima uingie darasani. Vitabu na semina vinaweza vikatosha kukidhi haja hiyo.

Kwa mfano kitabu kama kile cha MICHANGANUO YA BIASHARA NA UJASIRIAMALI tumejitahidi sana kuweka ABC zote za hesabu za biashara kwa mtu wa kawaida kabisa ambaye hata kama hajawahi kusoma masomo ya book keeping anaweza kushika na kuelewa. Vitu kama vile Mapato, gharama, matumizi, Faida na hasara, Mizania ya biashara, mzunguko wa fedha na uwiano wa sehemu za biashara ni vitu vya msingi kufahamu ikiwa kweli utapenda uwe na uwezo kamili wa kuidhibiti biashara yako.

10.Uza bila gharama za matangazo.
Kuna njia nyingi mtu unaweza ukazitumia kutangaza na kuuza biashara yako pasipo kutumia gharama kubwa kwenye matangazo ya biashara. Kila biashara inaweza kutumia njia tofauti lakini njia zilizozoeleka zaidi ni hizi hapa chini,

·       Mitandao ya kijamii
·       Kutengeneza mtandao wa watu mnaojuana.
·       Matangazo ya mdomo kwa mdomo
·       Mahusiano mazuri kwa umma
Njia hizi zina gharama kidogo sana na wakati mwingine hazina kabisa, pia zina uwezo mkubwa wa kukuletea wateja watiifu wakudumu.

11. Zingatia kipaji unapoajiri kisha pima utendaji.
Utakapoamua sasa unataka kuajiri mtu akusaidie shughuli zako, usiangalie cheti wala ana digirii ngapi ingawa navyo pia ni muhimu, cha msingi zaidi pamoja na elimu yake lakini ni lazima afikie vigezo hivyo 2, kipaji na uwezo wa kufanya kazi unayotaka aifanye. Tafuta muda wa kuwaendeleza wafanyakazi wako na kuwajenga waendane na malengo ya biashara yako kisha pima utendaji wao wa kazi na kutoa mrejesho. Ikiwa utaajiri watu/mtu asiyekuwa sahihi hataruhusu biashara yako ikue na mwishowe ataua kabisa dhana nzima ya kufunga mkanda.
………………………………………
Ni matumaini yangu kuwa njia nilizozitaja hapo juu, muendelezo wa mbinu za kufunga mkanda ili mtaji uweze kukua pasipo kuingia madeni zinaweza zikasaidia kuikwamua biashara ndogo inayoanza au iliyozorota. Kwa makala zaidi karibu katika group letu la watsap la MICHANGANUO-ONLINE pia unaweza ukajipatia vitabu vyetu mbalimbali, bonyeza hapa kwenye duka la vitabu mtandaoni kuviona.

1 Response to "KAMA UNA BIASHARA NDOGO YA MTAJI MDOGO, HIZI HAPA NJIA 11 ZA KUIBUSTI"