WANAOFANIKIWA KATIKA MAISHA HUAMINI VITU HIVI (4) VINNE | JIFUNZE UJASIRIAMALI

WANAOFANIKIWA KATIKA MAISHA HUAMINI VITU HIVI (4) VINNE


Mamilioni ya watu kote dunani tangu kuumbwa kwa ulimwengu huu wamekuwa na ndoto kila mtu na za kwake. Wapo walioweza kuzitimiza ndoto zao na vilevile wengi walikufa na kuzikwa na ndoto zao kabla hawajafanikiwa kuzitimiza. Hii inamaanisha kwamba kama ndoto au malengo yangelikuwa ni vitu vya kushikika mfano wa magunia ya viazi, basi makaburi yangelijaa siku nyingi na duniani pengine pasingelikuwa tena na mahali pa kuzikia.

Mamilioni ya watu wenye ubunifu na vipawa vya aina mbalimbali  wamekuwa wakiishi na ndoto zao wanazotamani kuzitimiza lakini kuna kitu kinachowavuta nyuma na kuwazuia kuzitimiza. Wana ndoto za kuanzisha biashara, kujenga nyumba, kununua kiwanja, kutunga kitabu, kupata mafunzo fulani, kuimba, kujifunza upishi, kwenda ulaya, kumiliki gari, kuoa, kuwa kiongozi wa siasa, kufanya hija maeneo matakatifu nk.


Lakini cha kushangaza ni kwamba wakati asilimia kubwa ya watu hao wakihagaika(wakistruggle) kutaka kutimiza ndoto zao hizo bila mafanikio, wapo baadhi ya watu siyo wengi sana lakini tunaowaita waliofanikiwa sana ambao wao huweza, tena kwa urahisi sana kutimiza malengo yao wanayojiwekea. Kwa kweli kwa macho ya kawaida watu hawa huwa tunaona kama vile wamepata mafanikio kirahisi sana. Hivi ni kweli hupata mafanikio kirahisi namna hiyo? Na kama hivyo ndivyo basi wanatumia mbinu gani?

Katika makala hii ya leo nitakuelezea vitu vine 4  ambavyo watu wenye mafanikio makubwa huwa wanaviamini ili hali watu wa kawaida huwa wanaviona kama havina maana yeyote kwao. Vitu hivyo ndivyo huwapa nguvu ya kutimiza malengo yao haraka na kwa urahisi na zaidi ya hayo nitakueleza pia namna mtu unavyoweza ukazitumia siri hizo 4 kufikia malengo yako ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakikukwepa.

Nadhani umewahi kusikia stori nyingi za watu waliowahi kuhangaika na maisha na kisha wakati fulani wakaja kutoka kabisa kimaisha . Mifano hata hapa nchini  kwetu tunayo, watu kama akina Mzee Reginald Mengi, Eric Shigongo, Diamond platnumz, na wengineo wengi, hawa ni baadhi tu na nimetaja wajasiriamali lakini wewe unaweza ukawa na mifano kutoka sekta nyinginezo kama vile siasa, elimu nk. Kulingana na maelezo ya wajasiriamali hao nyakati mbalimbali katika safari zao za maisha, kabla hawajafanikiwa waliweza kuanguka wakainuka tena, wakaanzisha biashara hii na ile, wakaacha, wakaanzisha nyingine tena mpaka pale walipokuja kugundua vitu hivi na kuviamini ndipo wakaweza kutoka moja kwa moja.


Siyo ajabu hata kidogo unakuta mtu anakuambia, kabla hajafanikiwa alianzisha biashara hata zaidi ya 10 ambazo zote zilikufa au kumletea hasara lakini moja tu au mbili zikaja kumletea mafanikio. Watu wengi wa kawaida wamekuwa wakifikiria kimakosa kwamba mafanikio maishani hutokana na kile mtu anachokijua kwa mfano watu hupima mafanikio ya mtu kwa kutumia kigezo cha elimu lakini ukweli ni kwamba elimu ni njia tu ya kufanikisha mtu aweze kupata mafanikio. Elimu isipotumika vizuri haina uwezo wa kumfanya mtu aliye nayo kufanikiwa hata angelikuwa na digirii ngapi. Wala mafanikio pia hayawezi kutokana na wale watu unaowajua au na kipaji ulichozaliwa nacho ikiwa hujachukua hatua zozote zile za kukigeuza kipaji hicho kuwa pesa.


Sasa basi ni vitu gani hivyo wanaofanikiwa huamini na kuwatofautisha na watu wa kawaida? Kama nilivyotangulia kusema na kuwataja baadhi ya wajasiriamali waliofanikiwa hapa nchini Tanzania, hebu wewe mwenyewe wachunguze. Bila shaka utagundua kuwa, karibu kila mmoja wao alianza taratibi,  kidogokidogo mpaka akafanikiwa, hakuna hata mmoja wao aliyelala tu usiku na kesho yake asubui kuamka akiwa tajiri, tena basi cha kushangaza ni kwamba hakuna hata mmoja aliyekata tamaa njiani licha ya vikwazo vingi walivyokutana navyo. Ni kitu gani kilichowapa nguvu wasikate tamaa na kuachana na biashara zao?


Unapowafuatilia kwa undani utagundua kwamba, kile kilichowapa nguvu ni kile WALICHOKUWA WAKIKIAMINI, basi. Na kukosekana kwa kichocheo hiki ndiko kunakosababisha makaburi au dunia kujaa mno ndoto na malengo yasiyotimizwa. Kile mtu anachoamini au kwa maneno mengine MTAZAMO WA AKILI(Mindset) ndiyo “petrol” au nishati inayochochea mafanikio kutokea, Wajasiriamali niliowataja na watu wote duniani walio na mafanikio makubwa, mafanikio yao hayo yalitokana na kile walichokiamini akilini mwao.

Kwa mfano Eric Shigongo katika historia ya maisha yake aliwahi kusema kwamba, alianza kufanikiwa baada ya kufuta akilini mwake mawazo aliyokuwa amepandikiziwa angali mdogo kwamba yeye ni duni na hawezi kufanikisha jambo lolote lile la maana. Alibaini pia kwamba hata majina mabaya aliyoitwa utotoni yalikuwa na mchango hasi katika maisha yake na hivyo alipaswa kuyapuuzilia mbali ili kuwa na mtazamo chanya mpya uliomwezesha hatimaye kuja kupata mafanikio ya maana kiuchumi na kimaisha kwa ujumla.


Ukiwa uliaminishwa tokea utotoni kwamba umetokana na familia duni na hivyo huwezi kufanikiwa, na kweli ikiwa hautachukua hatua za makusudi za kufuta imani hiyo akilini mwako, itakuwia vigumu sana kufanikiwa. Basi bila kuzidi kuchelewa hebu twende sasa nikakupe vitu hivyo vinne 4 wanavyoamini wale wanaofanikiwa katika maisha.

1. Hakuna mafanikio ya ghafla,
Ni lazima uanze kidogokidogo ndipo baadae uweze kumalizia na kikubwa. Ingawa kweli wapo watu wanaochukua muda mfupi kuliko wengine kupata mafanikio, lakini kwa ujumla mafanikio yeyote yale makubwa ni matokeo ya mchakato wa muda mrefu. Hatari ya kuamini katika mafanikio ya haraka ni kwamba utakata tamaa mara tu utakapokutana na kikwazo hata ikiwa ni kidogo, hii tena ni sababu nyingine ya dunia kujaa ndoto nyingi zisizotimia kwani watu wengi hujaribu mara moja, na wanapoanguka, huacha mara moja wakiamini wazo lao halikuwa sahihi.

2. Ukikosea mara ya kwanza hujashindwa bado kwani siyo jaribio lako la mwisho.
Kuna mfano mmoja maarufu wa mgunduzi wa taa hizi za umeme tunazotumia mpaka leo hii (balbu) kufeli karibu mara 9999 na mara ya elfu 10 ndipo akaja kufaulu. Angeachilia pale pale mara ya kwanza tu alipofeli, leo hii pengine dunia ingelikuwa bado inatumia vibatari na taa za mafuta ya wanyama kama zama hizo. Mbaya zaidi katika imani hii namba 2 ni pale mtu unapokosea na kisha watu wengine kukubeza; “Hee! Ulishindwa kiangazi masika utaweza?”, “Umeshindwa na taa ya Mungu mchana, utaweza  na taa ya Mzungu usiku?” nk. hayo ni baadhi tu ya maneno watu hutumia kuzidi kuwavuja moyo wenzao wanaoshindwa jambo. Na wewe ukiwa na mtazamo potofu(negative mindset) utakata tamaa kweli na kujiona hufai, huwezi na wala hutokaa uweze tena kitu maisha yako yote.


Lakini wewe badala ya kuvunjika moyo, hebu jaribu kutofautisha utendaji wako na uwezo mkubwa uliojificha ndani yako ambao kama utaamua kuutumia kila mtu anaweza akashangaa. Jiulize tena, ni nani aliyezaliwa akiwa anajua kusema, kuandika au kuhesabu? Vyote tulikuja kujifunza siyo? Aliye na mtazamo sahihi wa akili huamini kuwa, duniani hakuna aliyezaliwa akiwa anafahamu kitu, kila taaluma duniani inaweza kufundishika na mtu yeyote yule ana uwezo wa kujifunza taratibu mpaka akawa bingwa kabisa katika fani yeyote ile. Uwezo wa akili ya binadamu yeyote yule ni wa ajabu sana kiasi kwamba hakuna asiloweza kujifunza akaelewa.


3. Ili ufanikiwe fanya kile unachokipenda.
Huwezi kufanikiwa katika shughuli usiyoipenda na usiweke malengo yako kwenye pesa kwanza bali fanya kwa uaminifu kile kitu unachokipenda zaidi kiasi kwamba watu macho yao yote yakutazame wewe. Watu wa kawaida hudhani kimakosa kwamba wanaofanikiwa hufanya kwa kujilazimisha vitu au kazi wasizozipenda mpaka wanafanikiwa, kumbe ukweli siyo hivyo kabisa. Huwezi kufanikiwa kwa kufanya kitu usichokipenda.

4. Mafanikio siyo kupaa tu, kuna kuanguka pia.
Kwa mfano kwenye Ujasiriamali tunajifunza kwamba, tunapochukua hatari katika biashara kuna mambo mawili, kupata faida au kupata hasara, na vyote viwili  kila kimoja kina nafasi sawa ya kutokea. Hii inamaana kwamba unapopanga kufanikiwa vilevile panga na kuanguka. Mara nyingi watu wanaoanguka na kuinuka wakaendelea na safari ndio ambao huja kuibuka washindi mwishoni.

………………………………………………

Mpenzi msomaji wa blogu hii, tulikuwa kimya kidogo kwa siku chache lakini sasa tumerudi tena na kampeni yetu ya kuhakikisha MZUNGUKO CHANYA WA FEDHA KWENYE BIASHARAZETU UNADUMISHWA inaendelea kama kawaida hapa bloguni, ndani ya GROUP LA WHATSAPP LA MICHANGANUO ONLINE, katika blogu ya private ya MICHANGANUO na katika EMAIL LIST yetu.

Usajili katika group unaendelea na kuna offa mpya zimeongezwa sambamba na maboresho au updates kadhaa katika offa za zamani bila kusahau kile kifurushi maarufu cha michanganuo 3 ya kuku. Vile vile nichukue fursa hii kutangaza kwamba kitabu chetu cha MAFANIKIO YA BIASHARA YA DUKA LA REJAREJA kimefanyiwa maboresho makubwa kwa kuongezewa sura yenye mfumo mpya wa usimamizi wa duka la rejareja usioruhusu kabisa msaidizi kumuibia tajiri(2 IN 1 SYSTEM).

Aidha mfumo huo utatolewa peke yake (bila kitabu)  free katika GROUP LA WHATSAPP LA MICHANGANUO ONLINE. Pia ikiwa uliwahi kununua kitabu hiki na ungependa tukutumie softcopy ya mfumo huo bure, tuma anuani yako ya email kwenye namba 0712202244.

Ndani ya GROUP LA MICHANGANUO ONLINE tunaendelea na ratiba yetu kama kawaida, makala za kila siku za Michanganuo pamoja na Mzunguko chanya wa fedha.
   

0 Response to "WANAOFANIKIWA KATIKA MAISHA HUAMINI VITU HIVI (4) VINNE "

Post a Comment