Mikopo midogomidogo ya biashara: kabla hujakimbilia kufuga ng’ombe anza angalao na kuku au bata kwanza | JIFUNZE UJASIRIAMALI

Mikopo midogomidogo ya biashara: kabla hujakimbilia kufuga ng’ombe anza angalao na kuku au bata kwanza

Kikundi cha mikopo midogo midogo wakifanya marejesho ya mikopo yao
Kuna semi na dhana nyingi kuhusiana na suala la kuchukua mkopo wa biashara kwa mfano wapo wanaosema kwamba; “hakuna tajiri asiyekopa duniani akafanikiwa kuwa tajiri”, “matajiri ndio wanaokopa tu, masikini huwa hakopi bali yeye huomba tu misaada”. Misemo hii mingine ina ukweli lakini pia mingine ni upotoshaji mtupu.

Duniani watu wamegawanyika katika makundi mawili linapokuja suala la kukopa fedha kwa ajili ya kuendeshea biashara. Kundi la kwanza ni wale wasioamini kabisa kama mikopo ina uwezo wa kumtoa mtu pale mahali alipo na kumfikisha mahali bora zaidi kiuchumi. Lakini kundi la pili ni wale wanaoamini kwamba mkopo wa biashara ndio nyenzo muhimu zaidi kwa mjasiriamali yeyote yule ikiwa atataka kupiga hatua ya kuelekea uhuru wa kifedha.


Binafsi mimi ni mmoja wa kundi lile la pili la wale wanaoutazama mkopo kwa jicho chanya na ndio maana katika kitabu changu cha MAFANIKIO YA BIASHARA YA DUKA LAREJAREJA nimezitaja nyenzo kubwa mbili(leverage) mtu anazoweza akazitumia kukuza biashara yake haraka sana hata kuweza kufikia hatua ya kufungua maduka au biashara nyingine nyingi.

Katika kitabu hicho ipo nyenzo hii ya Mkopo lakini pia ipo na nyenzo ya pili ambayo ni muhimu sana hata kushinda hii ya kwanza. Ni watu wachache sana wanaozijua nyenzo hizi zinavyofanya kazi na hata wale wachache wanaozifahamu vizuri huwa hawapendi kabisa kuzitajataja ovyo kwa hofu ya kuibuka washindani kwenye biashara zao zinazoshamiri.


Tukiachana na hayo, hebu tuendelee kujadili mada yetu ya leo ya mikopo midogomidogo ya biashara kwanini kabla ya kukimbilia kufuga ngombe uanze angalao na kuku au bata kwanza. Ninachokimanisha hapa ni kwamba, usikimbilie kuchukua mkopo mkubwa kwanza kabla haujapata uzoefu na suala la mikopo. Na njia pekee ya wewe kuupata huo uzoefu na mikopo ni kuanza kukopa kutoka katika taasisi ndogondogo kwanza na kisha baadae unaingia mikopo mikubwa kwenye taasisi au benki zinazotoa mikopo mikubwa. Experience unayoipata wakati ukiwa na mkopo mdogo ndiyo ileile unayoipata wakati ukiwa na mkopo mkubwa.

Zipo benki pia zinazotoa mikopo midogomidogo kuanzia hata laki 3 na kuendelea lakini watu wengi bado hudhani kwamba benki hizo zenye majina makubwa haziwezi kutoa mikopo midogomidogo yenye masharti nafuu isiyohitaji dhamana za kutisha. Karibu benki na taasisi kubwa kubwa zote siku hizi wana vitengo vinavyoshughulika na kuwakopesha wajasiriamali wadogowadogo wasiokuwa na dhamana za uhakika za kuweka. Mara nyingi hutoa mikopo kwa vikundi ambavyo ni wanakikundi wenyewe wanaodhaminiana. Mwanakikundi mmoja akishindwa kurejesha marejesho ya mkopo basi wenzake ndio hubeba jukumu la kumlipia au kumfuatilia ikiwezekana kumfilisi kwakuwa wao ndio waliomdhamini.

Sababu kubwa 5 ni kwanini uanze kwanza na mkopo mdogo kabla haujaomba mkopo mkubwa

1. Kwanza kabisa mkopo mdogo utakupa uzoefu utakaokufanya ujijengee nidhamu ya hali ya juu ya fedha. Kitendo cha kujua unawajibika kurejesha fedha za marejesho ya mkopo wako kila wiki au kila mwezi kitaifanya akili yako kisaikolojia ichukue tahadhari kubwa kwenye matumizi ya fedha.


2. Mkopo mdogo unakujengea kuaminika na taasisi za fedha na kuwa mtu unayekopesheka kwa urahisi zaidi popote pale utakapokwenda kukopa kwani siku hizi taasisi nyingi za kifedha hasa mabenki wana utaratibu na mfumo maalumu unaobeba taarifa za kila mkopaji nchini, hivyo ukikopa benki ‘A’ kisha ukazingua, benki ‘B” watakubaini pindi tu wakicheki jina au kitambulisho chako cha taifa.

3. Unajijengea kidogokidogo rasilimali za kutosha zitakazokusaidia hapo baadae kuwa kama dhamana ya wewe kukopa mkopo mkubwa zaidi.

4. Kwa kukopa fedha kidogo kwanza unajipima uwezo wako wa marejesho upoje. Utajua kama unao uwezo wa kupata shilingi ngapi kwa siku, mwezi na hata mwaka.

5. Mikopo midogomidogo kwanza itakufanya ujenge mazoea na watu wengi wa aina mbalimbali  kama vile wakopaji wenzako wajasiriamali, maafisa mikopo kwenye taasisi za kifedha ambao hata unaweza kuomba kwao ushauri au msaada mwingine wowote ule wa kibiashara kwa urahisi.


Mbali na mikopo midogomidogo ya vikundi kuna taasisi na mabenki wanaotoa mikopo kwa mtu mmojammoja lakini mikopo ya namna hii huwa ina tabia ya kuambatana na masharti magumu kidogo ya dhamana kuliko ile ya vikundi. Mjasiriamali utatakiwa kuhakikisha unaonyesha dhamana za mkopo wako kusudi ikijakutokea umeshindwa kulipa marejesho basi benki au taasisi iweze kuziuza dhamana hizo na kulipia marejesho ya deni la mkopo uliobakia.

Dhamana yaweza kuwa ni mali na samani zako za ndani, nyumba, kiwanja, kadi ya gari, pikipiki au mali yeyote ile isiyohamishika. Mshahara wako wa mwezi pia unaweza ukatumika kukudhamini ukachukua mkopo wa biashara au mtu mwingine yeyote yule anaweza kukudhamini kuchukua mkopo wa biashara endapo tu mtu huyo atathibitisha kumiliki mali zilizotajwa hapo juu. Yote hii ni mikopo midogomidoho kuanzia laki mbili, tano mpaka milioni 5. Kwa mikopo mikubwa pia baadhi ya masharti ni hayohayo ya kuwa na dhamana za uhakika.


Lakini ni vizuri ikiwa huna kabisa historia ya kukopa na ndio unaanzisha biashara yako ndogo basi angalau uanze hata na mkopo mdogo, laki mbili, tatu au hata tano kusudi mambo yakija kuwa magumu njiani basi usipatwe na kiwewe au madhara makubwa kwani ikiwa utakuwa umesharejesha kiasi fulani cha pesa bila shaka kiasi kitakachokuwa kimebakia hakiwezi kuwa kikubwa sana wewe kushindwa kabisa kukilipa hata ikiwa biashara yako ni ndogo kiasi gani.

Siku hizi hata kuna mikopo hii ya kwenye mitandao (kukopa online), mikopo kwa njia ya simu janja yako ya mkononi ama kompyuta ya mezani unaingia tu mtandaoni unajaza fomu ikiwa ni pamoja na kupakia taarifa za utambulisho wako kama kitambulisho cha Taifa au cha kupigia kura na kisha unapata mkopo wako fasta bila dhamana wala vitu kama ada ya mkopo au sijui bima ya mkopo na mengine mengi. Sifa kubwa ya mikopo hii ni midogomidogo sana wakati mwingine kuanzia hata shilingi elfu 5, 10, laki, laki mbili mpaka milioni 1. Kuna mifano ya taasisi nyingi zinazotoa mikopo online na moja ni iliyokuwa ikiitwa TALA Tanzania na makampuni karibu yote ya simu za mkononi.


Ni bora mtu ukaanza kuchukua mkopo kama hii ya Tala ya shilingi elfu kumi, laki moja, laki tatu na kuendelea ukapata uzoefu wa mikopo kuliko kuomba moja kwa moja mkopo wa milioni kumi hata ikiwa una dhaminika huku ukiwa huna historia yeyote ile ya kukopa mahali pengine na wala hujui mikopo inafanyaje kazi.

Lakini mikopo hii ya kwenye mitandao kwa njia ya simu ina hatari kubwa moja na ni lazima kwanza mtu ujiridhishe na uhalali wa kampuni au taasisi inayotaka kukukopesha maanake pia kuna matapeli wengi wanaotumia fursa hiyo hiyo kujipatia pesa kijanja mtandaoni.

Utakutana na matangazo ya kuvutia mfano; pata mkopo kwa simu chapchap leo, mikopo ya haraka bila dhamana nk. na ukijiingiza kichakichwa tu unaambiwa utoe kwanza ada ya mkopo huo au chochote kingine kinachohusiana na mkopo kama kiingilio na hapohapo ukikubali kutoa unakuwa umeshalizwa.

Mbali na zile taasisi kubwa zenye majina na mabenki vilevile kuna taasisi nyingine ndogondogo zinazofanya biashara ya kukopesha pesa kwa riba kisheria kama vile Viccoba, Saccos na kampuni za mikopo midogo za watu binafsi(Microfinance), taasisi hizi hazijumuishi vikundi vingine vinavyokopesha mitaani kienyeji kama vile Michezo na upatu kwani huwa hazina usajili wowote ule serikalini.


Kila aina ya taasisi ina taratibu na masharti yake kwa mujibu wa sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa mfano kiwango cha mkopo wanachotakiwa kutoa, ruksa ya kukusanya amana za wakopaji nk. Hata riba za mikopo taasisi hizi kuna kiwango maalumu wanachotakiwa wasizidishe ili kutokuwaumiza wakopaji. Taratibu na sheria hizi husimamiwa na Serikali chini ya Benki Kuu ya Tanzania(BOT) na mamlaka nyingine zilizowekwa kisheria.

Kwa upande mwingine wa shilingi wakopeshaji nao hulindwa na sheria dhidi ya wakopaji pale wanapokaidi au kushindwa kurejesha pesa walizokopa. Sheria huwabana hata kufikia hatua ya mali zao kufilisiwa ili taasisi au kampuni isiingie hasara.


HITIMISHO

Ili kujijengea mazoea na tabia ya kurejesha mkopo bila usumbufu ikiwa ndio unaanza kukopa mkopo wa biashara, anzia mkopo mdogo wa chini kabisa na kisha upande juu taratibu, usione kama unapoteza muda kwani hii itakusaidia sana kujenga msingi wa uaminifu kwa taasisi unayokopa lakini pia kujijenga taratibu kimtaji huku ukikuza rasilimali chache ulizokuwa nazo ambazo ndizo zitakazokuja kuwa dhamana ya kukopa fedha nyingi zaidi hapo baadae. Usikimbilie kufuga ng’ombe kabla hujajaribu angalao kufuga kuku au bata kwani uzoefu unaoupata kwenye mkopo mdogo ndio uleule unaoupata unapochukua mkopo mkubwa wa biashara.



……………………………………………

Je, unahitaji mpango wa biashara kwa ajili ya uendeshaji wa biashara yako, kuombea fedha(mkopo) mahali kama benki na taasisi yeyote nyingine au kwa ajili ya kumtafuta mbia?

Basi usisumbuke, tunaweza kukuandikia au tukakupatia course nzima, vitabu, templates na sample za michanganuo ukaandika mwenyewe kwa njia rahisi.

Gharama zetu ni nafuu sana na kazi yako inamalizika ndani ya muda mfupi. Wasiliana na sisi kwa namba/watsapp: 0765553030

Kununua vitabu vyetu na Michanganuo ya biashara mbalimbali tembelea duka letu, SMART BOOKS TZ

Ukitaka kitabu cha Biashara ya Rejareja toleo jipya la 2020 lenye maboresho na vitu vipya bonyeza jina la kitabu, Mafanikio ya Biashara ya Duka la rejareja


3 Responses to "Mikopo midogomidogo ya biashara: kabla hujakimbilia kufuga ng’ombe anza angalao na kuku au bata kwanza"