SABABU KUBWA KWANINI BIASHARA INAWEZA KUFA HATA KAMA INA FAIDA NZURI TU NA YA UHAKIKA?

Baada ya biashara kuanguka sababu ni wewe mwenyewe?
Bila shaka yeyote ile kama hujawahi mwenyewe kuwa na biashara iliyoanguka chini ilihali ina faida kubwa basi umewahi kusikia watu wengine ambao biashara zao ziliwahi kufa au kuporomoka kabisa na sababu kubwa ikiwa si kukosekana wateja wala faida ya kutosha bali sababu nyingine kabisa tofauti.

Linaweza likawa ni jambo la kusikitisha sana kuona biashara nzuri unayoipenda na yenye faida kubwa tu ikikushinda na kuiacha hivihivi kwa sababu ambayo inaweza kuonekana ni nyepesi lakini ni sababu nyeti pengine kuliko sababu nyingine zozote zile zinazochangia kuyumba au kutokuendelea mbele kwa biashara nyingi za wajasiriamali wadogowadogo.


Ili kuielezea sababu hiyo vizuri zaidi itanibidi kutumia mahesabu kidogo ya mpango wa biashara ingawa sitaingia kwa undani sana. Sababu hii ya biashara kufa hata ikiwa ina uwezo wa kuingiza faida nyingi mara nyingi sana mtu unaweza ukaibaini kabla pale unapokaa chini na kuandika mpango/mchanganuo wa biashara yako kabla haujaianza au hata biashara ikiwa tayari inaendelea lakini ukaamua tu kufanya makisio ya mzunguko wa fedha taslimu(cash flow) katika biashara yako jambo ambalo siyo gumu hata kidogo.

Sababu kubwa kwanini baadhi ya biashara zenye faida hufilisika inatokana na biashara hizo kushindwa kulipa baadhi ya gharama zake kunakotokana na ukata au ukosefu wa mtaji wa kutosha kuendeshea kazi au working capital kwa kimombo, maana yake ni fedha ambazo mfanyabiashara inakubidi uzitenge kabisa mapema kwa ajili ya kuja kulipia gharama mbalimbali wakati biashara ikiendelea. Kukosekana kwa fedha hizi maana yake biashara nayo imekufa kwani hutaweza kulipa wanaokusambazia bidhaa wala madeni mengine yatokanayo na uendeshaji wa biashara yako.


Kumbuka biashara kabla haijatengeneza faida  ni lazima kwanza ununue malighafi kwa fedha taslimu. Hata ikiwa ni biashara ya huduma ni lazima kwanza ulipie vitu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujilipa wewe mwenyewe ili uweze kuiendesha hiyo biashara nk. Sasa ikiwa hauna mtaji wa kulipia hivi vitu kabla ya kulipwa na wateja uliowakopesha utaona kwamba biashara ni lazima itafeli tu.

Ili kuweza kuielezea vizuri dhana hii, nitatumia majedwali ya ripoti za mahesabu ya mfano wa biashara ya mtaji wa laki moja (100,000/=) ambayo mjasiriamali aitwaye Juma ananunua vyombo vya ndani na kwenda kuviuza ili kupata faida. Biashara ya Juma ina faida nzuri tu, akinunua vyombo vya mtaji wa shilingi laki moja akienda kuuza anapata faida ya shilingi elfu hamsini(50,000). Huu ni mfano rahisi wa haraka haraka na ambao unatuonyesha uhusianao uliopo kati ya ripoti zote 3 za biashara, Faida na hasara, Mizania(Rasilimali na madeni) na ile ya Mzunguko wa Fedha taslimu


Sasa kabla Juma hajanunua chochote hebu tuone ripoti za biashara yake za Faida & Hasara na ile ya Mali & madeni(Mizania) zipoje;

1. Kabla Juma hajafanya muamala wowote ule.
Ripoti ya Faida & Hasara
Mauzo
0
Gharama zamauzo
0
Faida
0


Ripoti ya Mali na Madeni;
RASILIMALI

Fedha taslimu
100,000
Wadaiwa
0
Jumla
100,000


MADENI & MTAJI

Madeni
0
Mtaji
100,000
Faida
0
Jumla Madeni na Mtaji
100,000

Hapo juu kwenye Fida na hasara tunaona hamna kitu kwani biashara bado haijafanyika. Katika mizania au Mali na madeni tumeona upande wa Rasilimali jumla yake ni sh. 100,000 na kwenye Mtaji na madeni Jumla yake sh. 100,000 pia. Kumbuka kimahesabu, RASILIMALI = MADENI + MTAJI

2. Muamala wa kwanza wa Juma.
Ni pale Juma atakapokwenda kununua vyombo na kuviuza kwa mara ya kwanza.

Faida & Hasara
Mauzo
150,000
Gharama zamauzo
100,000
Faida
50,000

Mizania (Mali na Madeni);
RASILIMALI

Fedha taslimu
150,000
Wadaiwa
0
Jumla
150,000


MADENI & MTAJI

Madeni
0
Mtaji
100,000
Faida
50,000
Jumla Madeni na Mtaji
150,000

Hapo juu inamaana kwamba Juma alitumia mtaji wa shilingi laki moja (100,000/=) kununulia vyombo vya ndani na alipoviuza alipata faida ya shilingi elfu hamsini (50,000/=) sawa na kusema, MAUZO – GHARAMA ZA MAUZO = FAIDA. Kwa upande wa Mizania ataishia kuwa na fedha taslimu sh. 150,000/= wakati Madeni na mtaji ikiwa pia ni jumla sh. 150,000 na pande hizo mbili zinalingana.


Juma anarudi tena mara ya pili kwenda kununua mzigo (vyombo) kwa mtaji uleule wa shilingi laki moja na kwenda kuviuza tena kama alivyofanya mwanzoni. Anarudia zoezi hilo mpaka anafikisha mara tatu na ripoti zake sasa zitasomeka kama ifuatavyo baada ya miamala hiyo mitatu;

Faida & Hasara
Mauzo
450,000
Gharama zamauzo
300,000
Faida
150,000

Mizania (Rasilimaliali na Madeni);
RASILIMALI

Fedha taslimu
250,000
Wadaiwa
0
Jumla
250,000


MADENI & MTAJI

Madeni
0
Mtaji
100,000
Faida
150,000
Jumla Madeni na Mtaji
250,000

Hapo juu ni ripoti za Faida na Hasara na Mizania ya biashara ya Juma baada ya kuuza vyombo mara 3 kwa mtaji wa laki moja aliokuwa nao. Lakini ukiangalia katika uhalisia wa biashara ulivyo, biashara haiwezi kuwa namna hii, kwa mfano mauzo mengine unaweza kufanya kwa mkopo wateja wakaja kukulipa baada hata ya siku 30 au zaidi ya hapo.

Kwa hiyo kwa mfano ikiwa kama Juma atakuwa aliuza kwa mkopo vyombo vyake hatuwezi tukasema kwenye mizania yetu hapo juu Juma atakuwa na fedha taslimu zote mfukoni au benki shilingi laki mbili na nusu, 250,000/=. Atakuwa akidai na hivyo ni lazima katika mizania yetu tufanye marekebisho kama ifuatavyo ingawa faida itabakia kuwa vilevile,

3. Mauzo ya Juma kwa mkopo;
RASILIMALI

Fedha taslimu
0
Wadaiwa
150,000
Jumla
150,000


MADENI & MTAJI

Madeni
0
Mtaji
100,000
Faida
50,000
Jumla Madeni na Mtaji
150,000

Juu: Mauzo na faida vipo vilevile lakini mfukoni Juma hana kitu, amekopesha vyote. Sasa hapo ndipo shida inapoanzia, Juma atakwenda kununua mzigo mwingine kwa pesa ipi wakati hajalipwa na wateja wake? Ili kusuluhisha tatizo hili kwa muda Juma anaamua kununua baadhi ya vyombo kwa mkopo pamoja na kuomba mkopo benki wa sh. 200,000 na majedwali yataonekana kama ifuatavyo;

Faida & Hasara
Mauzo
150,000
Gharama zamauzo
100,000
Faida
50,000

Juma anakopa mali na fedha;
RASILIMALI

Fedha taslimu
0
Mali za stoo(alizokopa)
100,000
Wadaiwa
150,000
Jumla
250,000


MADENI & MTAJI

Madeni(wadai)
100,000
Mtaji
100,000
Faida
50,000
Jumla Madeni na Mtaji
250,000

Hapo biashara angalao sasa inaoneka ni nzuri baada ya Juma kukopa vyombo vya shilingi 100,000(Wadai) vyombo hivi vitamwezesha kuendelea na biashara hata kama bado wadaiwa wake hawajamlipa deni la sh. 150,000. Sasa anavyo vvyombo vya shilingi laki moja stoo huku akisubiri kulipwa sh. 150,000 zake.

Biashara inapozidi kushamiri baada ya kukopa bidhaa, Juma anaamua kukopa tena pesa nyingine benki sh. 200,000 kusudi aweze kununua vyombo zaidi na ripoti zitakuwa hivi;
Mauzo
450,000
Gharama zamauzo
300,000
Faida
150,000

Juma anakopa fedha;
RASILIMALI

Fedha taslimu
0
Wadaiwa
450,000
Bidhaa stoo
100,000
Jumla
550,000


MADENI & MTAJI

Madeni(wadai)
100,000
Deni benki
200,000
Mtaji
100,000
Faida
150,000
Jumla Madeni na Mtaji
550,000


Lakini hata hivyo bado katika biashara hii ya Juma hakuna uhalisia sana kwani bado kuna vitu kama vile gharama za uendeshaji wa biashara hiyo mfano pesa za kujilipa mshahara wakati akifanya biashara kwani ni lazima ale apande daladala nk. gharama za mawasiliano kama bando la simu na hata fedha za dharura ikiwa lolote linaweza kutokea, Vile vile wakopeshaji wake (Wadai) ni vipi watakubali kumkopesha Juma ikiwa hana rasilimali zozote zile zinazoonekana kama dhamana? Au hata ni benki gani itakubali kumkopesha mtu asiyekuwa hata na mali au akiba kidogo?


Jibu la maswali hayo yote ni MTAJI WA KUENDESHEA KAZI(Working Capital). Hiki ndio kitu kilichokosekana kwenye biashara hii ya Juma tangu anaianza. Mtaji wa kuendesha biashara ndiyo kitu kinachosababisha mzunguko wa fedha wa biashara yako uweze kuwa mzuri na ni lazima uhakikishe tangu mwanzo unao, vinginevyo hautaweza kudumu kwenye biashara hata kama biashara yenyewe ina faida nusu kwa nusu kama ilivyokuwa kwa biashara ya Bwana Juma hapo juu.

Mtaji wa kazi(Working capital) katika miamala yote 3
Faida & Hasara
Mauzo
450,000
Gharama zamauzo
300,000
Faida
150,000

Mizania ya Biashara;
RASILIMALI

Fedha taslimu benki(working capital)
300,000
Wadaiwa
450,000
Mali za stoo
100,000
Jumla
850,000


MADENI & MTAJI

Madeni(wadai)
100,000
Deni la benki
200,000
Mtaji
400,000
Faida
150,000
Jumla Madeni na Mtaji
850,000

Kama uonavyo jedwali letu hapo juu, Biashara ya Juma ilihitaji kuanzishwa na mtaji wa shilingi laki nne (400,000/=) badala ya mtaji wa shilingi laki moja, 100,000/= za pale awali. Kwa hali hii sasa biashara ya Juma inaweza kuwa na uhalisia kwani mtaji wa kuendeshea biashara(Working capital) ni shilingi,
850,000 - 300,000  =  550,000/= badala ya shilingi 250,00 za awali. Kumbuka Mtaji wa kuendeshea kazi = (Jumla ya mali za muda mfupi – Jumla ya madeni ya muda mfupi).


HITIMISHO
Majedwali hayo yote tuliyoyaona hapo juu yanatuonyesha uhusiano ulokuwepo baina ya ripoti zote tatu za fedha kwenye mpango wa biashara.

Ili kufahamu zaidi kuhusiana na Michanganuo ya Biashara na jinsi ya kuandaa mpango wa biashara yeyote ile kwa njia rahisi kabisa, jipatie kitabu chetu cha MICHANGANUO YA BIASHARA NA UJASIRIAMALI. Ni Kitabu pekee Afrika Mashariki cha Michanganuo kilichoandikwa kwa lugha adhimu ya Kiswahili.

BEI NA JINSI YA KUKIPATA:
22,000/= Kitabu cha karatasi(Hardcopy) tunakuletea popote ulipo jijini Dar es salaa. Kwa mikoani tunatuma kifurushi ila gharama ya basi huongezeka kutegemeana na umbali na aina ya basi.
10,000/= Kitabu kwa njia ya mtandao(Email) (SOFTCOPY) Tunatuma kitabu ukiwa mahali popote pale Duniani kwa njia ya email

MAWASILIANO:
Watsao/simu: 0765553030
Simu/sms:      0712202244

Pia masomo ya kila siku kwenye Group letu la Whatsapp la Mchanganuo-online bado yanaendelea na leo hii tarehe 18 June 2020 tutakuwa na somo lisemalo;

 IKIWA ADUI MKUBWA WA FEDHA ZAKO NI WEWE MWENYEWE UFANYEJE ILI ZIWE SALAMA?”

Kujiunga na group hilo lipa kiingilio chako sh. 10,000/= kupitia namba zetu; 0765553030 au 0712202244 kisha tuma ujumbe usemao; “NIUNGANISHE NA GROUP LA MICHANGANUO NA OFFA MPYA YA MASOMO NA VITABU” Baada ya kujiunga tunakutumia Michanganuo, Vitabu na Masomo yote yaliyopita siku za nyuma.

0 Response to "SABABU KUBWA KWANINI BIASHARA INAWEZA KUFA HATA KAMA INA FAIDA NZURI TU NA YA UHAKIKA?"

Post a Comment