KUENDESHA BIASHARA BILA MTAJI NI SAWA NA KULIMA KWA JEMBE LISILOKUWA NA MPINI | JIFUNZE UJASIRIAMALI

KUENDESHA BIASHARA BILA MTAJI NI SAWA NA KULIMA KWA JEMBE LISILOKUWA NA MPINI

Hebu jaribu kufikiri, una shamba hekari 5 na unataka kulima ili upande mazao. Kabla kazi haijaanza unatazama zana ulizokuwa nazo kwa ajili ya kazi hiyo ya kulima na unabaini kuwa kifaa muhimu ambacho ni jembei halina mpini.

Jembe lisilokuwa na mpini.
Kutokana na kukosa maarifa ya kutosha kukuwezesha kuliweka mpini au hata uwezo wa kununua jembe jingine lililokuwa na mpini, unaamua kulitumia hivyo hivyo kulimia kwa kulishika kwa mikono sehemu ile ya kuchomeka mpini kisha kuanza kazi ya kulima huku ukiwa umeinama kwa matumaini kuwa utamaliza tu hata ikiwa utapita muda gani, “Bandu bandu hatimaye humaliza gogo bwana” unajisemea mwenyewe moyoni kujipa nguvu na ari.

Kabla haujatuambia ni nini kilichotokea baada ya kuanza kazi yako hiyo ya kulima hekari 5 kwa jembe lisilokuwa na mpini, hebu kwanza tuoanishe kulima shamba kwa jembe lisilokuwa na mpini na kufanya biashara bila kuwa na mtaji au kuwa na mtaji lakini usiotosheleza mahitaji ya biashara husika.

Watu wengi utawasikia wakisema, siyo lazima kuwa na mtaji ndipo uanzishe biashara, hili ni kweli kabisa asilimia mia moja na wala silipingi. Ndio maana kichwa cha makala hii nimeanza “Kuendesha biashara....” na wala siyo “Kuanzisha biashara......” Kuendesha na kuanzisha ni vitu viwili tofauti. Unaweza ukaanzisha biashara ukiwa na wazo peke yake lakini mtaji wa kuiendesha ukatoka mahali pengine hata kama hauna hata senti tano. Makala nyingine inayozungumzia vyanzo 7 vya mtaji ni hii hapa unaweza ukaisoma.

Zipo stori nyingi za watu walioanza bila mtaji, na unapozisikia unaweza ukadhani kwamba biashara bila mtaji inawezekana tu kirahisirahisi lakini ukweli ni kwamba siyo jambo rahisi vile. Utakuta baada ya kuanzisha bila mtaji itafika mahali ni lazima itahitaji mtaji wa ziada ili iweze kukua vinginevyo basi itabakia vile vile kwa muda mrefu au hata kufa. Hapa ndipo utakuta mtu akienda benki au taasisi za fedha kukopa, kukopa bidhaa toka kwa wanaokusambazia, kutafuta mbia, kuomba ndugu au jamaa akukopeshe, kuomba msaada nk.

Biashara kama haina mtaji wa kutosha ni mtihani mkubwa! Hebu fikiria, pengine una duka, anakuja mteja anataka kitu fulani, unamwambia hakuna, anakuja mwingine ameshika noti ya shilingi elfu kumi, anakwambia nipe soda, “oo..sina chenji” unamjibu, kweli hauna chenji na wala siyo kwamba unamkatalia bure, na hata ukifikiri ukaombe chenji kwa jirani bado unahisi ni kama vile unajisumbua bure kwani ni muda si mrefu ulienda kuomba ya shilingi elfu mbili na bado ukakosa. Kuna changamoto nyingi unapoendesha biashara na mtaji usiotosheleza, hizo ni chache tu.

Biashara hiyo hiyo pengine ndiyo kila kitu unategemea hapohapo nikiwa namaana kwamba inabidi ujilipe kiasi kikubwa cha mshahara ili kukidhi mahitaji yako ya kila siku binafsi na hata ya familia. Biashara hiyo hiyo inatakiwa ilipe pango la chumba unachofanyia biashara, ilipe umeme, ushuru wa takataka, kodi ya mapato pamoja na leseni kila mwaka. 

Kuendelea na biashara kwa mtindo kama huo bila ya kuwa na mtaji wa kutosha ni hatari sana itakupotezea muda wako mwingi huku ukimtafuta mchawi anayekuloga bila ya mafanikio. Tafuta mtaji kwa kutumia njia yeyote ile halali uweze kupaa mithili ya ndege badala ya kuendelea kusota chini kama kinyonga au kobe.

Hauna tofauti na yule anayelima ekari 5 kwa jembe lisilokuwa na mpini. Atasota hapo chini wee! Mpaka msimu wa kulima unamalizika, msimu wa kupanda nao utakuja utapita hajakamilisha hata robo heka, na hata msimu mwingine wa kulima utamkutia tena hapo hajasogea hata heka moja. Atahitaji chakula, gharama mbalimbali pamoja na madawa akiumwa huku familia nayo ikimsubiri pasipokuona hata mhindi mmoja wa kuchoma.

Jembe lenye mpini.
Mwishowe hakuna kitakachokuwa kimefanyika. Tuseme labda angelikuwa na jembe lenye mpini, kazi ingekwenda harakaharaka, na labda hata jembe hilo lingekuwa ni lile la kukokotwa na ngombe au trekta basi kazi ingelikuwa na tija kubwa zaidi.


Suala la mtaji pia hutegemea sana aina ya biashara, kwa mfano, biashara ya kutoa huduma ni tofauti na ile ya kuuuza au kuzalisha bidhaa. Kutoa huduma mtu atahitaji mtaji kidogo zaidi na hata zipo biashara zingine hutahitaji mtaji kabisa kwa maana ya fedha. Uzalishaji wa bidhaa utahitaji mtaji mkubwa hasa wa fedha kununulia malighafi kabla bidhaa zenyewe hazijauzwa. 

Halikadhalika na uuzaji wa bidhaa ni hivyohivyo, utahitaji kuwa na fedha taslimu za kununua bidhaa husika kabla haujaziuza. Ikiwa hauna uhakika wa kupata mtaji wa kutosha kuendeshea biashara kabla ya kuanza fikiria uwezekano wa kufanya biashara ya utoaji huduma.

Una maoni gani ngugu msomaji? au una jambo lolote ungependa kuuliza, basi yaweke hapo chini katika maoni. Asante.





2 Responses to "KUENDESHA BIASHARA BILA MTAJI NI SAWA NA KULIMA KWA JEMBE LISILOKUWA NA MPINI"

  1. Mnaweza kunikopesha mtaji kidogo? ninataka kuanzisha biashara ya kuuza nafaka.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Sisi tunashughulika na utoaji elimu kwa wajasiriamali wadogo kupitia njia mbalimbali kama vitabu, mitangao ya kijamii, blogs nk. Hatuhusiki na utoaji mikopo, ila tunakushauri kama unahitaji mkopo basi wasiliana na taasisi mbalimbali za mikopo kama vile benki, saccos, vyama vya kuweka na kukopa au vicoba. Usiogope kwenda kuwaona na kuwaulizia masharti ya kukopa, linganisha sehemu tofauti kuona ni wapi masharti yao utaweza kuyamudu zaidi.

      Delete