JE, MTANZANIA UNAKOPESHEKA NA TAASISI ZA FEDHA AU BENKI? | JIFUNZE UJASIRIAMALI

JE, MTANZANIA UNAKOPESHEKA NA TAASISI ZA FEDHA AU BENKI?


Kutokuwa na  uwezo wa kukopa mkopo wa biashara benki au taasisi za fedha hasa hasa kwa vijana na wale wasiomiliki rasilimali za uhakika imekuwa ni kikwazo kikubwa sana kwa wajasiriamali wengi nchini. Ili mtu aweze kukopa kiasi cha fedha kitakachomuwezesha kukidhi mahitaji yote ya mtaji wa biashara yake anapaswa  kwanza kutimiza masharti yaliyowekwa na Benki kuu chini ya taasisi mbalimbali za kifedha pamoja na Mabenki.

SOMA PIA NA: Njia 7 za kupata mtaji wa biashara unayoipenda.

Ufafanuzi huu ulitolewa na mtaalamu wa biashara na maswala ya uchumi, Mabuye S. Mabuye katika kipindi cha redio cha Kijana na uchumi kinachorushwa hewani na Wapo radio fm siku ya Jumatano. Miongoni mwa wataalamu wengine waliokuwemo ni Askofu Rwezaura na  Mchungaji Juma lema.  

Kipindi hicho huendeshwa na Mtangazaji, Father Philemon Rupia. Mada kuu iliyokuwa ikizungumziwa katika kipindi hicho ilikuwa; NI KWA NINI WATANZANIA HAKOPESHEKI, MADHARA YA HUYU MTANZANIA KUTOKUKOPESHEKA,  FAIDA ZINAZOPATIKANA IWAPO WATANZANIA WENGI ZAIDI WATAKOPESHEKA PAMOJA NA TAABU INAYOWAPATA WALE WACHACHE WANAOKOPESHEKA.

Mtaalamu huyo bwana Mabuye kutoka taasisi ya ushauri wa biashara alianza kwa kutoa sababu ni kwa nini Watanzania tuliokuwa wengi hatukopesheki, alisema kwamba  ili mtu aweze kupewa mkopo kuna masharti ambayo ni lazima ayakidhi, nayo alibainisha kuwa ni; biashara kuwa imesajiliwa na kupata hati mbalimbali kama, TIN namba, leseni, mkataba wa pango la sehemu ya biashara kusudi wajue watakupata wapi endapo hutarejesha.

Sharti jingine alitaja ni kuwa na dhamana, ili taasisi iweze kukuamini na kukupa mkopo inabidi uwe na dhamana kwa maana ya hati, inaweza kuwa nyumba, kiwanja, au hata gari. Lakini wengi hawana dhamana na hasa wengi wao ni vijana wa kiume. Kwa upamde wa vijana wa kike na wanawake wao hudhaminiana kwenye vikundi na kupewa  mikopo kuanzia laki tano na kuendelea.

Sasa kutokana na kukosa sifa hizo za kukopa mabenki hujikuta wanapata wateja wachache sana, na kwa sababu mabenki na taasisi za fedha wanatakiwa kutimiza sheria za nchi chini ya benki kuu inayowataka  wajiendeshe kwa faida katika mazingira ya wakopaji wachache  hivyo hawana budi kuwawekea hao wateja wachache riba ya juu ili kukidhi sharti la kutokupata hasara. Wachache wanabeba mzigo wote.

Suluhisho la changamoto hizo ni kwa Watanzania kumilikishwa ardhi, kupewa hati miliki kusudi sasa waweze wakawa na dhamana za kuombea mikopo, mitaa na vijiji vipimwe kusudi watu wapewe hati miliki na huo alisema ni mpango maalumu wa serikali ambao tayari upo. Wakishamilikishwa ardhi ni ukombozi.  Swala jingine alisema kuwa ni mitizamomindset”, mtizamo wa watu wengi unakuwa hauko sahihi,” mtu akishafikiri tu biashara kitu cha kwanza anaanza kufikiria mkopo, lakini hajafikiria ile biashara itajiendeshaje, atazalishaje, soko likoje, ushindani ukoje, soko la ile biashara likoje, uhitaji wa ile biashara ukoje. 

Haya, baada ya kukidhi vigezo, anasajiliwa, ana dhamana, anakopa, mwisho wa siku anashindwa kurejesha mkopo na huo unakuwa ni mgogoro kati ya benki na mteja, ndio maana kati ya watu 10 wanaokopa kwa mara ya kwanza utakuta ni wawili tu wanaorudi tena mara ya pili kukopa, nane wote wameshaingia mgogoro na taasisi ya fedha. Kwanini?  kwasababu  riba ni kubwa na hakutathmini biashara yake vizuri.

Riba inakuwa kubwa kutokana na wakopaji kuwa ni wachache, na benki haiwezi ikajiendesha kwa hasara  na mtu pekee anayebebeshwa gharama hizo anakuwa ni yule mteja aliyekuwepo. Hii pia husababisha wafanyabiashara na wazalishaji bidhaa kwa kutozwa  riba kubwa na wao hupandisha bei za bidhaa zao na hivyo kufanya bidhaa kutoka nchi za nje ambako wao hawana riba kubwa katika mabenki yao kuzizidi kiushindani zile za hapa nchini. Changamoto hizi husababisha mfumo mzima wa biashara kuingia katika mgogoro.

Suluhisho lake ni kama tulivyoona serikali kuchukua hatua za kurasimisha ardhi, ufumbuzi wa kuwafanya hao wasiokopa kuweza kukopa. Siku hizi dhamana siyo kigezo kikubwa tena kama zamani, kuna mfumo ambao kila mtu sasa anayehitaji mkopo anapaswa aingie, hamna tena haja ya dhamana ya majumba, mashamba na hati za magari. Watu hujiunga katika umoja mfano kikundi cha watu watano, mfano ni hao akina mama waliozungumziwa kuwa hupata mikopo kiurahisi siku hizi kutoka taasisi mbalimbali. Ile watu kufahamiana inamfanya mtu athamini kile kitu anachokifanya. Dhamana zile wanaandika tu katika karatasi na wala hazichukuliwi kupelekwa taasisi ya pesa.

Mfumo huu wa kudhaminiana wenyewe kwa wenyewe uliothibitika kuwa unafanya kazi tofauti na ule wa zamani enzi za ushirika uliosimamiwa na serikali, watu huanzisha wenyewe na wala siyo kusukumwa, wanafahamiana na kujaliana hata mmoja akiondoka wenzake ni lazima watamtafuta mpaka wampate. Zamani mashirika ya serikali mtu alikuwa akiajiriwa na watu waliokuwa wakiajiriwa hawawi sehemu ya ule mradi kwa hiyo wao walichokuwa wakisubiri ni mshahara tu pasipokuwajibika wala kuwa na mpango wowote ule wa biashara.
Benki kuu ya Tanzania.
Cha msingi ni taasisi za fedha, na wadau wengine wote wanaohusika ikiwemo serikali kuangalia ni kwa namna gani kunakuwa na ongezeko la wakopaji, kwani namba yao ikipanda basi na ribaya mikopo nayo itapungua. Kiuchumi ni kwamba tutapunguza migogoro ya wateja wa benki na benki na pia mtizamo wa Watanzania wengi  kuhusiana na benki utabadilika kutoka kuwa mgogoro hasi kuwa chanya zaidi. 

Hili ni suala mtambuka kuwahamasisha watu kujijengea mazingira ya kukopesheka ni jibu la changamoto nyingi sana kwenye jamii ya Kitanzania, riba zitashuka, wakopaji watakuwa wengi, na watu watakuwa katika hali ya utulivu”

JE ULIWAHI KUSOMA NA HII HAPA?: Kuendesha biashara na mtaji kidogo ni sawa na kulima shamba kwa jembe lisilokuwa na mpini.


Suluhisho jingine wataalamu hao walisema ni kila mtu kuhakikisha tunashikamana kuhakikisha tunatengeneza maadili hata kwenye familia. Taasisi za fedha huweka masharti magumu wakati mwingine kutokana na kuhofia hatari ya watu wengi kutokuwa na maadili wanapopewa pesa hawaendi kuzitumia kwa uangalifu.

Wasikilizaji wakiuliza maswali baada ya mada hiyo wengi walilalamika kodi za pango la fremu za biashara kutozwa kwa  mwaka au miezi 6 na kudai kwamba wenye nyumba wengi huwa hawana huruma kwani hawazingatii hata mtu kama umekopa pesa au la.

Lakini akijibu swali hilo mtaalamu alisema kuwa kimsingi unapokopa pesa kwa ajili ya biashara ukitaka upate faida na uweze kuzirudisha  unatakiwa uzielekeze zote kwenye mzunguko wa biashara(uendeshaji), moja kwa moja na wala siyo kwenye uwekezaji. Ni lazima uhakikishe vitu vyote vya msingi unakuwa umeshavitafuta mwenyewe,(umejipanga vizuri).

Msikilizaji mwingine aliwaacha watu hoi kwa kicheko alipokuwa akilalamika kuhusiana na Watanzania kuwa na ‘kijicho’, pale wanapoona mtu umeenda kukopa na kuanzisha biashara yako, basi na wao hukutangulia mbele matokeo yake biashara haitoki, biashara haionekani kabisa tena mchana lakini kama umeweka gizani! unanunua wewe mwenyewe na mkeo.

Akijibu mtaalamu alisema, “Watanzania wanahitaji ushauri wa kutosha wa biashara, tatizo linaloonekana hapa ni mazingira, mtu unaenda kupanga fremu mahali fulani, kabla hujapanga hata biashara yako itakuwaje, hujaichambua na kuifanyia upembuzi yakinifu kuhakikisha kwamba kwanza pale ni sokoni, lakini pia hujajua yenyewe itakuingizia kiasi gani kwa siku, hujajua hayo mambo yote na hayo mambo yote ni ya kitaalamu watu huwa wanafikiria kwamba hela ndiyo inayoleta hela, inaleta hela kama umeielekeza mahali penye mkondo.....

Sisi kama wachumi nadhani elimu yetu ndiyo mahali pake, kwamba tunaweza tukatoa usaidizi wa kiushauri kama mtu ana wazo la biashara tunalichambua…. yaani akubali kulichambua.. unajua kuna watu wengi sana; yeye anataka umuelekeze mkopo uko wapi, sasa mimi kama mtu mwenye akili siwezi kufanya hivyo, ni lazima nikuulize maswali magumu na uwe tayari kuyajibu,  ili utakapotumbukiza hela isipotee.

Sasa usipotaka kutaabika hapa mwanzoni na kusumbuliwa na maswali magumu, na unaweza ukaja na mradi mmoja wa kwanza tukakuambia huu mradi haufai, utapata hasara, kabuni mwingine au tukakushauri ni mradi gani unafaa kwa wazo lako.”

Vile vile suluhisho la fremu za biashara wataalamu hao walipendekeza serikali kuanzisha maeneo maalumu kwenye kata yatakayohusika na biashara kusudi wananchi waweze kujipatia maeneo hayo kwa gharama nafuu.

Mwisho kabisa mshauri wa biashara bwana Mabuye alitoa namba zake za simu ambazo ni 0682 600275 kwa ajili ya ushauri zaidi juu ya kusajili biashara, kuiendeleza biashara, kwanini uchukue mkopo, jinsi ya kupata mkopo wa biashara, njia rahisi za kupata mkopo, namna ya kuomba mkopo nk. Alimalizia kwa kusema kwamba “Watu wasilenge mkopo tu bali ni jinsi gani watakavyoendesha biashara zao.”

Hapa chini ni sehemu, tu ya mazungumzo ya kipindi hicho (siyo mazungumzo yote mwanzo mpaka mwisho), katika sauti. CHANZO CHA MAKALA HII NI WAPO RADIO FM. KIPINDI CHA KIJANA NA UCHUMI CHA TAREHE, 16/3/2016. 

0 Response to "JE, MTANZANIA UNAKOPESHEKA NA TAASISI ZA FEDHA AU BENKI?"

Post a Comment