MTAJI WA BIASHARA YA DUKA LA REJAREJA: NIANZE NA SHILINGI NGAPI ILI NIFANIKIWE? | JIFUNZE UJASIRIAMALI

MTAJI WA BIASHARA YA DUKA LA REJAREJA: NIANZE NA SHILINGI NGAPI ILI NIFANIKIWE?


Duka la rejareja, biashara rahisi kuanzisha
Katika safu yetu leo ya Ongea na Mshauri ama Uliza ujibiwe tutamjibu msomaji wa blogu hii aitwae Edson, swali lake nitaliweka kama alivyouliza kwenye “screenshot” hapo chini lakini pia kama kichwa cha post kinavyosema. Alimaanisha hivi; MTAJI WA BIASHARA YA DUKA LA REJAREJA ANAWEZA AKAANZA NA MTAJI WA SHILINGI NGAPI?


MTAJI WA DUKA LA REJAREJA NI SHILINGI NGAPI?

Majibu:
Ingawa sijajua aina ya duka la rejareja unalotaka kuanzisha kwani kuna biashara za maduka ya rejareja ya aina nyingi. Kwa mfano unaweza ukawa unataka kuanzisha duka la rejareja la vyakula mchanganyiko maarufu kama maduka ya mtaani/maduka ya kina Mangi nk. au hata duka la rejareja la nguo, duka la dawa muhimu, duka la vifaa vya umeme, duka la vipodozi na urembo, biashara ya duka la vinywaji au laweza kuwa ni duka la rejareja la aina yeyote ile zikiwemo biashara za supermarkets.

Zoote hizo ni aina za biashara za maduka ya rejreja kwa mujibu wa kitabu cha MAFANIKIO YA BIASHARA YA DUKA LA REJREJAREJA, kitabu mashuhuri Tanzania chenye uchambuzi wa kina kuhusiana na biashara zote za rejareja duniani ikiwemo biashara ya duka la rejareja iliyojizolea umaarufu mkubwa sana katika mitaa mingi ya miji na vijiji vya Tanzania.

Ukijaribu kuuliza watu mbalimbali ni kiasi gani cha mtaji (fedha) mtu unachohitaji kuwa nacho ili uweze kufungua duka la rejareja la kawaida mtaani, utapewa majibu mengi na miongoni mwa majibu hayo hauwezi ukasema lipi ni sahihi zaidi ya jingine. Ukweli ni kwamba hauwezi ukasema duka linatakiwa lianze na kiasi fulani cha fedha kwani kila mtu anayeanzisha duka uwezo wake ni tofauti na mwingine, hivyo watu hufungua maduka yenye ukubwa na hadhi tofauti. Kioski(kiduka kidogo) na supermarket zote ni aina za biashara za maduka ya rejareja lakini mitaji yao inatofautiana kwa kiasi kikubwa sana

Ndiyo maana tunasema kwamba kabla haujaanzisha duka lako, tengeneza kwanza Mchanganuo mfupi wabiashara ya duka lako(Mpango wa biashara au kwa kimombo Business plan) kujua kiasi cha fedha zitakazohitajika kama gharama za awali pamoja na gharama za uendeshaji.


Gharama za awali za kuanzia zinajumuisha, pango la mwezi mmoja au miezi 6 ya chumba utakachotumia, gharama za kumlipa dalali kama utamtumia, gharama za ukarabati wa eneo la biashara yako ama matayarisho ya fremu yako ya duka, vitu kama mzani, makasha(shelfu za duka), meza, viti n.k. ambapo gharama za kuendeshea zinajumuisha fedha za kununulia bidhaa kwa ajili ya kuuza, mshahara kwa msaidizi /wasaidizi pamoja na kulipia bili mbalimbali zikiwemo umeme, ushuru, wa taka na maji.

Kwa mfano una shilingi zako laki tatu(300,000) tu na unataka kuanzisha duka dogo, je itawezekana?  jibu ni ndiyo, kwani itakubidi kuhakikisha katika mchanganuo wako gharama za vitu mbalimbali zilizotajwa hapo juu unaziweka chini kwa kadiri inavyowezekana ikiwa ni pamoja na kutumia mbinu za aina mbalimbali ikiwemo, kuweka aina za bidhaa za duka zenye faida ndogo lakini hutoka haraka haraka, kutafuta mbia, kukopa kwa karadha (karadha maana yake ni kwamba unaazima vifaa mfano mafriji kwa mtu na kisha unamlipa riba ya kuvitumia kwa muda mtakaokubaliana huku vifaa vikiendelea kubakia kuwa mali  yake).


Maduka mengine watu huanzia nyumbani kwa kupanga baadhi ya bidhaa barazani, wanapopata mtaji wa kutosha hufungua kioski au genge na mwishowe duka la ukweli lenye kila kitu ndani yake. Kwa mantiki hiyo hauwezi ukasema eti kuna kiasi maalumu cha mtaji unachopaswa uwe nacho kwanza ndipo uweze kufungua duka lako la rejareja.

Lakini kwa maoni yangu binafsi mimi kama Peter Tarimo, kwa mfano ukitaka kufungua duka dogo la kawaida lenye vitu muhimu karibu vyote kwa mahitaji ya kila siku ya watu ukiwa na shilingi za kitanzania kuanzia Milioni moja mpaka milioni 6, au tuchukulie wastani milioni tatu  (3,000,000/= ) unaweza ukafungua pasipo kupata usumbufu mkubwa duka lako la wastani kwani mtaji wa kutosha ni kigezo muhimu sana ingawa siyo lazima sana uwe na mtaji mkubwa ndipo uweze kuanzisha duka la rejareja;


Mathalani tukichukua hiyo milioni tatu(3) niliyopendekeza hapo juu tunaweza kufanya uchanganuzi wetu kama ifuatavyo(huu ni mfano tu lakini kulingana na mawazo yangu mwenyewe, wewe yaweza kuwa tofauti)

MAHITAJI YA DUKA LA REJAREJA:
* Friji/freezer
=
400,000/=
* Pango miezi  sita (6)
=
600,000/=
*Mzani mmoja (1)
=
150,000/=
*Makasha ya kupanga bidhaa (fremu)
=
150,000/=
*Vifaa mbalimbali
=
200,000/=
*Bidhaa za kuanzia
=
1,500,000/=
JUMLA.
­    =
3,000,000/=









Faida ya biashara ya duka la rejareja
Kwa mchanganuo huo mfupi wa gharama za kuanzishia duka lako la rejareja unaweza kuona kwamba, gharama za manunuzi ya mali(bidhaa) zitakazouzwa ili kutengeneza faida dukani thamani yake ni shilingi milioni moja na laki tano(1,500,000)

Ni kawaida kwenye duka la rejareja karibu kila bidhaa utakayouza faida yake ni kati ya asilimia 25% mpaka asilimia 30% ya mauzo yake. Hii ni kusema kwamba ukinunua mzigo huo wa shilingi milioni 1.5 ukafanikiwa kuuza wote pengine ukapata shilingi milioni mbili (2) basi ujue hapo ni lazima faida yako itakuwa kati ya shilingi laki 5 mpaka laki 6 yaani asilimia 25% – 30% ya hiyo milioni 2


Kwa hiyo ndugu yangu Edson nikutie tu moyo kwamba mtaji wowote ule uliokuwa nao unaweza ukaanza, ningependa kukupatia mbinu nyingine moja kuhusu mtaji wa duka la rejareja ambayo haijalishi hata kama una mtaji kidogo kiasi gani lakini unaweza ukaanza biashara ya duka. Biashara yeyote ile ukisema usubiri mpaka upate mtaji kiasi fulani ndipo uanze unaweza usiianze maisha yako yote.

Unaweza kuanza vyovyote vile ndio maana kuna mahali katika majibu yangu nimekuambia kwamba wapo watu hata huanzisha maduka yao kwenye vyumba vya kuishi walivyopanga. Siyo lazima uanzie kwenye fremu ya duka na mfano halisi naweza kukupatia ushuhuda wa kwangu mimi mwenyewe nilivyoanzisha duka langu katika mtaa wa Msimbazi Kariakoo nikiwa sina hata senti tano mfukoni.


Nimeeleza mkasa huo mzima katika kitabu changu cha Mafanikio ya biashara ya duka la rejareja kwa shuhuda za picha za rangi, zipo zaidi ya picha 8 katika ukurasa wa 10 wa kitabu hicho toka wiki ya kwanza kabisa naanza mpaka duka linaonekana duka. Na zaidi ya hapo nimeeleza kinagaubaga jinsi ya kuendesha biashara ya duka la rejareja.

Kuna jamaa yangu mwingine mmoja pia alinipa ushuhuda wake wa jinsi alivyopata mtaji wa duka nilipokuwa naandika kitabu hicho, yeye alikuwa akiishi Manzese. Staili aliyoitumia kupata mtaji wa kuanzisha duka lake kwa kweli hata mimi iliniacha hoi, jamaa hakuwa na hata mia mfukoni tena akiishi kwa kaka yake pale Tandale Kwa Mtogole.

Alianza kwenda mjini kama utani akatengeneza ukaribu na matajiri kadhaa wa maduka ya jumla na rejareja wakawa wanamwamini(bila mtaji wa pesa) kiasi kidogo cha mali alizozisambaza katika maduka ya rejareja maeneo ya Manzese na Magomeni. Bei alizowauzia ni zilezile wanazouziwa wanapokwenda maduka ya jumla kufungasha mali hivyo yeye ubunifu wake hapo ulikuwa ni kuwapunguzia gharama za kufuata mzigo.

Kwa kuwa maduka yale ya jumla walimwachia asilimia fulani ya faida kwenye kila bidhaa za duka la rejareja alizochukua, haukupita muda mrefu sana akaanza kumiliki mtaji wake mwenyewe wa duka la rejareja alilomwachia mkewe asimamie pale Kwa Mtogole huku yeye akiendelea kuwasambazia mzigo watu wa maduka ya rejareja kwa pikipiki. Hatimaye yule jamaa ninavyoongea sasa hivi anamiliki maduka kadhaa ya jumla na rejareja maeneo ya Manzese na Magomeni na ni Tajiri wa kutupa! 

.....................................................

Kujipatia vitabu vyetu mbalimbali wasiliana nasi kwa namba 0765553030

Masomo katika group letu la whatsapp & Telegramu pia yanaendelea kila siku na leo hii 28/5/2020 tutakuwa na somo lenye kichwa cha habari kifuatacho; 






5 Responses to "MTAJI WA BIASHARA YA DUKA LA REJAREJA: NIANZE NA SHILINGI NGAPI ILI NIFANIKIWE?"

  1. Elimu nzuri Sana hii hasa kwetu sisi vijana! Let's think beyond we can grow Rich! Thanks for brain's diet

    ReplyDelete
  2. Elimu nzuri ya kufaliji ,naamini hata mm nitaweza tusikate tamaa na tumutangulize Mungu katika yote.

    ReplyDelete
  3. Kwanini hakuna mtu aliefafanua upatikanaji wa eneo?

    ReplyDelete
  4. Vp kuhusu biashara ya nguo

    ReplyDelete