BIASHARA YA UREMBO INALIPA, NI YA PILI KUTOKA HARAKA BAADA YA CHAKULA, NI FURSA KUBWA! | JIFUNZE UJASIRIAMALI

BIASHARA YA UREMBO INALIPA, NI YA PILI KUTOKA HARAKA BAADA YA CHAKULA, NI FURSA KUBWA!


BIASHARA Y UREMBO TANZANIA
Biashara ya urembo na biashara ya vipodozi ni ni kitu kimoja kilekile kwani lengo la mtu kutumia vipodozi  ni ili apendeze au kuwa mrembo. Kwahiyo unaposema, biashara ya bidhaa za urembo unamaanisha vipodozi na vile vitu vinavyohusiana na watu kupendeza au kuwa katika hali ya usafi na unadhifu. 


Hata hivyo watu wengine huiweka biashara ya urembo katika kundi lake na biashara ya vipodozi kwenye kundi jingine kulingana na wanavyoona. Wanahusisha urembo na vitu vya kuvaa kama vile hereni, bangili, mikufu, kucha nk. huku wakihusisha vipodozi na bidhaa zote za ngozi, nywele na manukato mfano losheni, cream na pafyumu.


Kitaalamu, vipodozi ni kitu chochote kile kinachoweza kutumiwa katika kufanya muonekano wa mtu uwe wa kuvutia zaidi au kuwa na harufu nzuri. Vitu hivyo ni pamoja na bidhaa mbalimbali za mwili na ngozi kama vile sabuni, lotion, krimu, dawa za mswaki, perfume, make-ups nk.

UREMBO

Sidhani kama kuna binadamu leo hii duniani anaweza akadai hatumii kipodozi cha aina yeyote ile na kama basi atakuwepo binadamu wa namna hiyo basi atakuwa hana tofauti na sokwe mwitu au nyani wanaoishi katika misitu minene kule congo na Brazili


SEKTA YA BIASHARA YA UREMBO NA VIPODOZI NCHINI TANZANIA
Kutokana na ongezeko la kipato kwa watu wa tabaka la watu wa kati nchini Tanzania, matumizi ya bidhaa za urembo na vipodozi yameongezeka tangu mwanzoni mwa miaka ya 90 na kuendelea mpaka hivi sasa. Ukuaji huo unakadiriwa kuwa ni wa kiwango cha asilimia 8% kwa mwaka. Hata hivyo matumizi ya vipodozi na urembo Tanzania kwa kiasi kikubwa watu wamekuwa wakitumia vipodozi bandia ambavyo siyo halisi na hatari kwa afya zao.


Vipodozi hivyo bandia huingia nchini kutoka nchi za China, Jamhiri ya Kidemokrasia ya Congo(DRC), Zambia na Kenya. Lakini pia vipodozi halisi(Original) hupatikana katika maduka machache makubwa, Saluni kubwa kubwa, baadhi ya maduka ya madawa, maduka makubwa ya kisasa kama shopping malls na supermarkets pamoja na kwa watu wanaoagiza vipodozi hivyo moja kwa moja kutoka ng’ambo au Dubai.

Juhudi kubwa za serikali chini ya mamlaka zake mbalimbali kama vile TRA na TFDA kwa kiasi kikubwa zimekuwa zikitoa elimu kwa wananchi dhidi ya vipodozi hivyo haramu na juhudi hizo sasa zimeanza kuonyesha kuzaaa matunda ingawa bado kuna mahitaji makubwa ya vipodozi hivyo yanayochangiwa na urahisi wa bei pamoja na matokeo yake ya muda mfupi. Vipodozi haramu au bandia vina tabia ya kuonyesha matokeo ya haraka hasa vile vya kutakatisha ngozi ambapo kwa mtu asiye na uelewa hudhani ndiyo vizuri kutumia.

KWANINI BINADAMU TUNAPENDA KUTUMIA VIPODOZI AU KUJIREMBA?
Bila shaka yeyote ile leo hii ulivyoamka asubuhi ulipokuwa ukioga au kufua nguo zako ulitumia sabuni kama siyo ya unga ni sabuni ya kipande. Na ikiwa sijakosea pia baada ya kuoga, ulijipaka mafuta hata kama ni baby care au Ashes, au ulijipaka losheni au cream. Hukuishia hapo bado uliendelea kujipaka deodorant kwapani na kujipulizia pafyumu inayonukia kwenye nguo zako nzuri ulizovaa. Na ikiwa wewe ni mwanamke basi mambo yalikuwa ni moto zaidi kwani uliweka na makeup, lipstic na vitu vingine kibao.


Sasas basi, ni kwanini binadamu huwa tunafanya jambo hilihili kila siku? Jibu ni rahisi sana, TUNAPENDA KUONEKANA NA KUJISIKIA VIZURI” Kuonekana na kujisikia vizuri ni hitaji la msingi sana kwa binadamu karibu sawa kabisa na ilivyokuwa kwa chakula au malazi. Sababu hii ndiyo hufanya vipodozi na vifaa vya urembo kuwa ni bidhaa au huduma zinazonunuliwa haraka karibu sawa na bidhaa za chakula zinavyotoka haraka.


Kila mtu hata masikini kabisa anayeishi chini ya dola moja kwa siku anapenda kuonekana na kujisikia vizuri, tunapenda urembo na utanashati. Lakini mbali na kujisikia na kuonekana vizuri pia vipodozi hutusaidia katika suala zima la usafi, kutufanya tujiamini zaidi mbele ya wenzetu na hivyo kwa kiasi kikubwa kuamua ni kwa kiwango gani tunachoweza kuwashawishi watu wengine na jinsi watu wengine nao wanavyotuchukulia. Hivyo biashara ya urembo na vipodozi ni biashara iliyo na fursa kubwa sana duniani kote, Afrika na Tanzania kwa ujumla.

SABABU MBALIMBALI ZA ONGEZEKO LA WATU KUTUMIA VIPODOZI ZINATAJWA KUWA NI HIZI ZIFUATAZO;

1. Vipodozi kuwa ni mahitaji ya msingi ya kila siku, kila mtu siku hizi hutumia vipodozi. Urembo na mitindo huwezi tena ukavitenganisha na maisha ya binadamu ya kila siku.

2. Kuongezeka kwa idadi ya watu pamoja na kipato kwa watu wa daraja la kati na la chini Tanzania.
Kwa mujibu wa Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, idadi ya watu imeongezeka kutoka milioni 34 mwaka 2002 mpaka kufikia watu milioni 44.9 mwaka 2012 sawa na kasi ya ongezeko la asilimia 2.7 kwa mwaka. Inakadiria Tanzania bara kuwa na idadi ya watu wapatao milioni 63.3 mwaka 20125. Aidha umasikini wa kipato umepungua kutoka asilimia 33.6 mwaka 2007 hadi kufikia asilimia 28.2 mwaka 2012.


3. Idadi kubwa ya vijana chini ya miaka 25
Vijana  ndio watumiaji wakubwa wa bidha za urembo kwa mfano Tanzania katika sensa ya watu na makazi  ya mwaka 2012, vijana wa umri chini ya miaka 17 walikuwa ni asilimia 50.1% ya watu wote wanaopatikana nchini sawa na watu milioni 22.5. Duniani idadi ya vijana chini ya umri wa miaka 25 ni bilioni 1.2  na kati ya hao asilimia 90% wapo katika nchi zinazoendelea Tanzania ikiwa miongoni mwazo.

4. Wanawake kuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kipato na wa kununua vitu.
Katika jamii za Kiafrika na hata sehemu nyingi duniani mwanamke anakabiliwa na shinikizo kubwa zaidi ya mwanaume la kuwa na muonekano wa kuvutia(urembo). Hii ndiyo sababu kubwa ya bidhaa za vipodozi za nyele, ngozi, kucha na make-up kuwa ndiyo zinazoongoza duniani kuuzwa kwa kiasi kikubwa zaidi ya aina nyinginezo za vipodozi. Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na mwamko mkubwa wa wanawake kutaka usawa na wanaume katika nyanja mbalimbali zikiwemo ajira na hata katika elimu.


Matokeo yake ni kwamba wanawake wengi sasa wana uwezo mkubwa wa kununua vitu mbalimbali vikiwemo vipodozi. Pia wanawake pamoja na kujinunulia wenyewe vipodozi huwa wananunuliwa pia na wapenzi wao, waume au ndugu na jamaa zao katika familia kama zawadi. Hivyo biashara ya urembo wa wanawake ni kubwa na iliyo na soko la uhakika.

AINA MBALIMBALI ZA VIPODOZI, UREMBO NA BIDHAA ZA USAFI.
Sekta hii ya vipodozi au urembo tunaweza tukazigawanya katika makundi mbalimbali yafuatayo kulingana na aina na matumizi yake mbalimbali.
1. Bidhaa za urembo za nywele.
Kundi hili lina  bidhaa kama vile, nywele za bandia, shampoo, conditioners, rangi mbalimbali na dyes, relaxer na bidhaa mbalimbali za mitindo ya nywele. Wadau wakubwa katika kundi hili ni saluni za kike na za kiume na wanawake majumbani wanaozitumia bidhaa hizo wakiwa wenyewe au na mashog zao. Wanaume nao pia hawako nyuma katika sekta hii ya nywele kwani utakuta wakiweka dreads, wave na hata Afro katika masaluni mbalimbali ya kiume.
2.Bidhaa za Ngozi.
Kundi hili la vipodozi vya ngozi ndilo kubwa na lililo na aina nyingi zaidi ya bidhaa kushinda makundi mengine. Karibu asilimia 30% ya vipodozi vyote vinavyouzwa sokoni hutokana na kundi hili mfano ni “skin moisturizers”, “cleansers”, “toners”, “ant-acne” bidhaa za urembo wa ngozi ya miguu na bidha nyingine za usoni(facial).  Watu wana ngozi tofauti tofauti, wengine ngozi zao ni kavu, wengine ngozi zenye mafuta na wengine ngozi zao zina mzio kwa baadhi ya bidhaa zinazotumiwa.
3. Make up
Make up zinajumuisha bidhaa zote zinazotumika kurembesha na kutia rangi usoni au urembo wa ngozi ya uso, kwenye macho, midomo na kucha. Kundi hili nalo limegawanyika katika bidhaa za aina mbalimbali mfano kuna lipstick, foundation, mascara, eyeliners, bidhaa za urembo wa kucha kama vile rangi za kucha pamoja na make up removers.
4. Bidhaa za usafi na chooni.
Katika kundi hili la vipodozi tunakutana na bidhaa zote zinazotumika katika usafi wa mwili na kujiweka vizuri na siyo lazima ziwe ni za urembo. Bidhaa zinazopatikana katika kundi hili pia ni zile zinazotoka haraka sana na kuwa na mahitaji makubwa mfano sabuni za kuogea na kufulia za maji na za miche, cream za kunyolea, hair removal(depilatories), deodorants, karatasi za chooni(toilet paper), taulo za kike(ped) na nyiginezo nyingi zinazotumika katika usafi wa mwili.
5. Manukato.
Kundi la Manukato ni miongoni mwa bidhaa za urembo zinazouzika kwa kiasi kidogo zaidi lakini cha kushangaza ndiyo kundi lenye faida kubwa zaidi pengine kushinda makundi mengine. Manukato yanajumuisha mchangayiko wa mafuta na vitu vyote vinavyonukia ambavyo huupa mwili wa binadamu harufu ya kupendeza. Kuna pafyumu, Eau de Toilette, airfreshner, aftershave nk.    

JINSI UNAVYOWEZA KUNUFAIKA NA FURSA KUBWA ILIYOKUWEPO KATIKA SEKTA HII YA UREMBO NA VIPODOZI NCHINI TANZANIA.

Pasipo kujali unao mtaji kiasi gani au ni uelewa kiasi gani uliokuwa nao kuhusiana na biashara hii ya urembo(jinsi ya kuanzisha biashara ya urembo), unaweza ukaanzisha na kunufaika na fursa kubwa iliyopo katika biashara hii kwa kuifanyia nyumbani kwako, kutembeza mitaani au kufungua eneo lako.

 

Zipo njia kuu mbili ambazo unaweza ukaanzisha biashara yako mwenyewe ya urembo au vipodozi nazo ni hizi hapa chini;

 

1. Kutengeneza bidhaa zako mwenyewe za vipodozi na urembo.

Ingawa soko limesheheni bidhaa za aina nyingi za urembo na vipodozi kutoka sehemu mbalimbali duniani, hata hivyo bado kuna mahitaji makubwa ya vipodozi hasa vinavyotokana na mimea ya kiasili ya kiafrika.


 

Kuna watu wengi siku hizi ambao hawapendi  kabisa vipodozi vinavyotokana na kemikali za kizungu bali wanapenda urembo wa asili, aidha  vipodozi vingi kutoka ng’ambo vimetengenezwa kwa ajili ya kukidhi mazingira na mahitaji ya ngozi za watu wa mabara zinakotengenezwa, Waafrika tuna mahitaji yetu maalumu ambayo hayawezi kufikiwa na bidhaa hizo hivyo ukiweza kutengeneza vipodozi vinavyokidhi mahitaji ya ngozi nyeusi unakua umetengeneza fursa kubwa ya kuingiza fedha.

 

Afrika tuna miti na mimea mingi ambayo inaweza ikatumika katika kutengeneza bidhaa za urembo, kuna miti na matunda kama vile ubuyu, ukwaju, limao, alovera, na mengine chungu nzima. Haijalishi bidhaa yako itakuwa mpya sana au utaamua tu kuongeza ubunifu kidogo kwenye bidhaa zilizopo sokoni tayari lakini kikubwa hapa ni wewe kuwa mbunifu katika kuitafutia soko bidha yako(marketing) kuanzia jinsi ya kufanya biashara ya urembo, jinsi utakavyoifungasha, maandishi  utakayoweka juu ya nembo yako na hata matangazo utakayotoa katika vyombo mbalimbali vya habari ukiwemo mtandao wa intaneti.

 

Hapa Tanzania na Afrika kwa ujumla kuna makampuni na watu binafsi ambao wamenufaika sana na fursa hii, wanatengeneza pesa nyingi na bidhaa zao za asili zinapendwa mno. Mtu yeyote pi anaweza akaanzisha biashara ya vitu vya urembo au bidhaa yake(kipodozi cha asili) na akauza kwani fursa bado ni kubwa.

 

2.  Kuuza bidhaa za watengenezaji wengine mbalimbali.

Hii sasa ndiyo njia ambayo watu wengi tumeizoea hapa kwetu, kufungua biashara ya kuuza urembo na vipodozi mbalimbali kutoka nje ya nchi na hata vile vinavyotengenezwa hapa hapa nchini kwa kuwa msambazaji au muuzaji wa rejareja wa vipodozi.

Unaweza ukaanza kama muuzaji wa rejareja au ukaamua kuagiza kutoka nje yanchi na kuja kuuza jumla kwa wauzaji wengine. Wauzaji wa vipodozi vya jumla huvitoa au kuagiza nje ya nchi kama vile Dubai, China, Ulaya, Amerika ya kaskazini, Mashariki ya kati na hata kutoka nchi za Kenya, DRC, Zambia na Afrika ya Kusini.
Kwa wale wauzaji wa rejareja kuna walio na maduka maalumu ya vipodozi, saloon za kike na za kiume, maduka ya dawa, masoko mbalimbali ya wazi na maeneo watu wanayopenda kwenda kununua vitu kwa urahisi kama stendi au pembezoni mwa barabara. 
Kutegemeana na eneo utakalochagua kuweka biashara yako ya vipodozi, mikakati yako ya soko, na kiwango cha ushindani uliopo, biashara hii ya vipodozi au urembo inaweza kuwa ni biashara iliyo na faida kubwa kwako na ambayo inaweza kukufanya utajirike ndani ya kipindi kifupi.
............................................................................
Mpenzi msomaji wa blogu hii ya jifunzeujasiriamali, napenda kukujulisha kuwa masomo na semina zetu za kila siku ndani ya GROUP LA WHATSAPP LA MICHANGANUO-ONLINE bado zinaendelea kila siku usiku saa 3-saa 4 tukijadili masomo mbalimbali yahusuyo michanganuo ya biashara zinazolipa pamoja na mzunguko wa fedha katika biashara zetu. Group linakaribia watu 100 sasa na kumbuka kuna ukomo wa idadi ya watu hivyo ni muda wa kuwahi mapema kabla nafasi hazijajaa.

Ada ya kujiunga na Group ni shilingi elfu 10, na namba zetu sa SIMU ni 0712202244, WHATSAPP ni 0765553030

Vitu mbalimbali unavyopewa mara unaojiunga tu ni hivi vifuatavyo;
1.  Kitabu cha MICHANGANUO YA BIASHARA NA UJASIRIAMALI kwa lugha ya Kiswahili.

2.  Masomo 11 ya jinsi ya kuandika mpango wa biashara.

3.  Kifurushi maarufu cha michanganuo 3 ya ufugaji wa kuku(MKOMBOZI CHICKS PLAN 3PACKS)

4.  Kitabu mashuhuri zaidi duniani, HOW TO WRITTE A BUSINESS PLAN kwa lugha ya kiingereza, ndio kinachotumika vyuo vikuu vingi duniani.

5.  Mfululizo wa Tafsiri ya kitabu mashuhuri zaidi cha pesa, FIKIRI UTAJIRIKE
6.  Kuunganishwa na blogu ya kulipia ya michanganuo bure.

7.  Vielezo(Templates) za michanganuo ya biashara inayokuwezesha kuandika michanganuo kwa muda mfupi.

8.  Masomo yote yaliyopita katika group kuhusu MICHANGANUO NA MZUNGUKO WA FEDHA.

9.  Mfumo mpya wa usimamizi wa duka la rejareja(2 IN ONE STORE MANAGEMENTA SYSTEM) unaomwezesha mmiliki wa duka dogo la rejareja au la kati kuthibiti mapato yake pasipo msaidizi kudokoa hata senti 5

10.      Somo muhimu sana la mzunguko wa fedha.

11.      Ukurasa mmoja wa mchanganuo.

2 Responses to "BIASHARA YA UREMBO INALIPA, NI YA PILI KUTOKA HARAKA BAADA YA CHAKULA, NI FURSA KUBWA! "