UREMBO BALAA: WAREMBO WANAOJIREMBA KWA KUJIPAKA VITU VYA KUTISHA USONI. | JIFUNZE UJASIRIAMALI

UREMBO BALAA: WAREMBO WANAOJIREMBA KWA KUJIPAKA VITU VYA KUTISHA USONI.

Katika ulimwengu huu wa Urembo na warembo, kwa miaka mingi Duniani kumekuwepo na njia lukuki za warembo kujiremba. 



Njia hizo tofauti tofauti, nyingine zinaonekana ni za kawaida kabisa lakini pia zipo nyingine kwa hakika ni za ajabu, zinatisha na hata wakati mwingine zinaonekana kuwa ni za hatari kubwa kwa warembo wenyewe.

Tukianza  na hapa kwetu Tanzania, miaka ya nyuma kidogo kuliwahi kuibuka wimbi la kinadada warembo kuusaka urembo kwa kutumia njia za ajabu ajabu, mfano mzuri tu ni pale walipotumia mkorogo, uliochanganywa vitu mbalimbali zikiwemo kemikali mfano Jiki, maji ya betri, sabuni zilizowekwa kemikali hatari ya mercury nk. Orodha ya vitu hivyo ni ndefu, tuachie tu hapo kwanza kwa upande wa hapa kwetu Tanzania.

Mada hasa inahusu njia wanazotumia wenzetu huko ughaibuni katika harakati za kuusaka urembo, wakati kina dada zetu huku wakisaka weupe kwa udi na uvumba  wenzetu huko wao zaidi wanapigana ili ngozi zao zibakie ujana yaani wasizeeke na kuwa na mikunjo mikunjo. Sasa hebu tazama hapo chini njia wanazotumia ili kutimiza ,malengo hayo kwa kweli utawaonea huruma na kusema ni aheri hata hawa kina dada zetu huku wana afadhali.

Kwa kutumia konokono (Snail facial)
Njia hii ya urembo imeanzia huko nchini Japan katika Saluni moja ya kike ambapo inaaminika kwamba protini iliyokuwepo ndani ya utelezi (mucus) wa konokono ambaye amelishwa vyema mbogamboga na matunda yaliyolimwa pasipokuwekewa mbolea za kisasa basi inao uwezo wa kuzuia ngozi ya mwili isizeeke.

Matibabu hayo huhusisha kuwaacha konokono watambae juu ya uso wa mrembo, huku wakati huo mhudumu wa saluni anakuwa akiangalia kwa makini konokono wasije wakazama mdomono, puani ama machoni kwa mrembo.

Njia ya kunyofolewa na samaki(Fish pedicure)
Miguu ya mrembo hutumbukizwa ndani ya chombo chenye samaki wengi wadogo wadogo ambapo samaki hao wenye njaa huachwa wadonoe, wanyofoe-nyofoe ngozi ya zamani kwenye vidole vya miguu ya mrembo, hata hivyo njia hii imepigwa marufuku baadhi ya nchi kutokana na hatari ya kuleta maambukizi katika ngozi za warembo hao.

Massage kwa kutumia nyoka.
Huko nchini Israeli Kundi la nyoka walioondolewa sumu huwekwa mgongoni kwa mrembo na maeneo mengine ya mwili huku wakizunguka zunguka na inasadikiwa hutoa tiba fulani katika ngozi.


Kama nilivyotangulia kusema kuna njia nyingi sana za ajabu na za kutisha, zilizotajwa hapa ni chache sana, wengine hata hapa kwetu utakuta wakijikandika usoni na vitu vya kustaajabisha kama vile kwa kutumia tope la majivu, maziwa ya mgando, parachichi, matango, shayiri, karoti, mkojo, wine, mavi ya ndege, asali, moto, dhahabu, chokleti na mimea chungu nzima warembo wanayoamini itazifanya ngozi na miili yao kuwa nyororo au hata kutokuzeeka.

Angalia picha mbalimbali hapa chini jinsi urembo unavyotafutwa kwa njia mbalimnali;











0 Response to "UREMBO BALAA: WAREMBO WANAOJIREMBA KWA KUJIPAKA VITU VYA KUTISHA USONI."

Post a Comment