JINSI YA KUANDIKA MPANGO WA BIASHARA UTAKAOSHAWISHI BENKI NA WAFADHILI KUKUPATIA FEDHA | JIFUNZE UJASIRIAMALI

JINSI YA KUANDIKA MPANGO WA BIASHARA UTAKAOSHAWISHI BENKI NA WAFADHILI KUKUPATIA FEDHA

Kuna aina nyingi za uandishi wa mpango wa biashara kutegemeana na lengo lako la kuandika. Ijapokuwa faida za kuandika mpango wa biashara ni nyingi na muhimu zaidi ikiwa ni kusaidia katika uendeshaji wa biashara yenyewe kwa ufanisi, lakini watu wengi sana na siyo hapa Tanzania tu peke yake wamezoea kuandika mpango wa biashara au kutafuta wataalamu wa kuandika andiko hili pale tu wanapokabiliwa na jukumu la kuomba mkopo benki, kutafuta mwekezaji au wanapotakiwa popote pale kuwasilisha mpango wa biashara kwa madhumuni yeyote mengine.

Leo nimelenga zaidi kuzungumzia namna ya kuandika mpango wa biashara kwa madhumuni ya kuomba mkopo wa benki au taasisi nyingine za kifedha. Wajasiriamali wengi huona ni jambo gumu sana kuandaa mchanganuo wa biashara hasa pale unapokuta mjasiriamali hajawahi kulifanya zoezi hili siku nyingine, huwa wanajiuliza maswali mengi kama vile; naanza anzaje kuandika mpango wa biashara? Nitakokotoa vipi mahesabu ya mpango wangu wa biashara? Nitajuaje ikiwa kila kitu nimeandika kwa usahihi? nk.

Ikiwa na wewe ni miongoni mwa hao walio na mashaka kama hayo  basi nikukumbushe tu kwamba haupo peke yako, hata na mimi kuna wakati nilikuwa kama wewe na isitoshe leo wasiwasi wako wooote utakwenda kuyeyuka kama bonge la barafu…….Na ikiwa mpango huo unauhitaji kwa ajili ya kouombea mkopo mahali basi fuatana nami mpaka mwisho wa makala hii.

Kwa kawaida mpango wa biashara umegawanyika katika vipengele mbalimbali na vilevile unaweza kuvigawanya vipengele hivyo katika sehemu kadhaa. Kwahiyo kabla ya kuanza chochote ili kurahisisha kazi ya kuandika mpango wowote ule wa biashara ni lazima kwanza ugawe vipengele au sehemu hizo na uanze kuandika ukilenga kipengele kimoja baada ya kingine na hatimaye sehemu moja baada ya nyingine.

Hapa chini nitakwenda kukuangazia hatua kwa hatua mchakato mzima jinsi unavyoweza kuanza mpaka unamaliza kuandika mpango wa biashara wenye sifa ya kushawishi benki, wafadhili au wawekezaji katika biashara au kampuni yako.

Ingawa Mpango wa biashara hauna idadi maalumu ya vipengele lakini mara nyingi una vipengele 8 au 9 kulingana na vile utakavyoamua, kwani kuna watu wengine huamua kuunganisha vipengele viwili kuwa kimoja na wengine huhesabu jalada la nje(cover page) kama moja ya kipengele. Mimi nitatumia vipengele vinane (8) ambavyo ni hivi vifuatavyo;-

1.  Muhtasari Tendaji(Executive summary)

2.  Maelezo ya Kampuni(Business Summary)

3.  Maelezo ya Bidhaa/Huduma(Product/Service Description)

4.  Maelezo ya Soko(Market analysis summary)

5.  Mikakati na utekelezaji(Strategy & Implementation Summary)

6.  Maelezo ya Utawala(Management Summary)

7.  Mpango wa Fedha(Financial Plans)

8.  Viambatanisho/Vielelezo(Appendix)

Kama nilivyotangulia kusema, ili kufanya kazi iwe rahisi vipengele hivi 8 nitavigawa katika sehemu ama unaweza ukasema hatua 4. Hatua hizo nne zitawezesha kazi ya kuandika mpango wa biashara kwa ajili ya kushawishi benki, taasisi za fedha au wawekezaji kuwa rahisi kwani nitajua ni kitu gani ninachotakiwa kukifanya kwa wakati gani, kifupi nitaweza kuwa na malengo(focus)

 

1. HATUA / SEHEMU YA KWANZA KABISA: 

              i)      ONYESHA FURSA ILIYOPO (THE OPPORTUNITY)

Hiki ndicho kiini hasa cha mpango wa biashara yako na inatakiwa impe afisa wako wa mkopo uelewa bayana wa mambo yafuatayo;

·       Tatizo hasa biashara yako inalotatua

·       Jinsi bidhaa au huduma zako zinavyoendana na soko lililokuwepo

·       Kile kitu hasa kinachoitofautisha biashara yako na za washindani waliokuzunguka.

Katika Sehemu/Hatua hii kuna vitu muhimu vitatu kama ifuatavyo;

              ii)     Tatizo na Suluhisho lake

Hapa utaelezea tatizo hasa unalotatua kwa ajili ya wateja wako, ni kwa jinsi gani maisha yao yatakuwa bora zaidi baada ya kuwapatia hilo suluhisho (pain point solution). Ni vyema kwanza kabla haujaanza ukawa umefanya utafiti wa soko kwa kuwahoji wale unaotarajia watakuwa wateja wako(target customers) ili uweze kujiridhisha kwa uhakika kwamba ni kweli wanalo hilo tatizo unalotaka kulitatua.

Katika kitabu chetu cha MICHANGANUO YA BIASHARA NA UJASIRIAMALI tumeweka sura nzima inayoelezea jinsi ya kufanya utafiti wa soko (Feasibility study) kabla hujaandaa mpango wako wa biashara.

Hakikisha pia umelielezea tatizo lako kwa ufasaha. Kwa mfano tuseme tatizo lako unalotaka kusuluhisha  ni la watu katika mtaa mmoja kule Sinza kuhangaika sana nyakati za mchana kwa kukosa mahali muafaka pa kupata lunch mpaka wengine kulazimika kufungasha viporo kuja navyo kazini ijapokuwa wana pesa zao na wangeliweza kuzitumia kama wangelipata mahali pazuri na pasafi pa kupata mlo. Suluhisho lako laweza likawa ni kufungua mgahawa safi na wa kisasa katika mtaa huo utakaowahudumia vyakula na vinywaji masaa ya mchana.

             iii)     Soko Lengwa

Kitu cha pili kwenye hii hatua ni Soko unalolilenga, Ni kina nani hasa utakaowauzia? Na pia unaweza kukisia idadi yao wako wangapi?, siyo lazima kupata idadi kamili. Taarifa hizi zina umuhimu mkubwa na zitaamua ikiwa biashara yako itafanikiwa ama itafeli huko mbeleni.

Kamwe usifanye kosa la kudhania tu eti “kila mtu atakuwa mteja wangu bwana” Kwa mfano ni rahisi sana mmiliki wa mgahawa kumlenga kila mpita njia midhali yupo njia panda, lakini ni vizuri zaidi akahakikisha anawalenga kundi la wateja fulani maalumu ili aweze kuufikia uwezo kamili wa mauzo ya biashara yake. Hapa anaweza badala yake akawalenga wafanyakazi wa maofisini na wenye biashara tu ambao mchana ni lazima watafute chakula na wana uhakika wa kula kwani kipato wanacho cha uhakika pia.

            iv)    Ushindani.

Washindani wako wa moja kwa moja ni kina nani? Hawa ni wafanyabiashara kama ya kwako iwe ni watu binafsi au makampuni wanaofanya biashara  yenye suluhisho la kutatua matatizo ya wateja kama lakwako. Kisha elezea sifa zako za kiushindani(competitive advantage). Maana yake unaeleza ni kwanini wateja wako watarajiwa(soko lengwa) wachague kununua kutoka kwako na wala siyo kwa washindani wako?

Ikiwa kama unadhania huna mshindani, jaribu kufikiria tena mara mbili, wateja wakati mwingine wanaweza kutafuta suluhisho la matatizo yao hata kutoka kwa wale washindani wako wasiokuwa wa moja kwa moja wanaotumia njia tofauti kutatua tatizo lilelile. Kwa mfano watu wa mtaa nilioutaja kule Sinza wanaweza kuamua kwenda kula mihogo ya kukaanga au hata mahindi ya kuchoma kukidhi njaa yao ikiwa mgahawa wako hautakidhi shida inayowasumbua.

Tumemaliza hatua au sehemu ya kwanza ya kuelezea fursa iliyopo kwenye biashara unayoandikia mchanganuo wako. Sasa hapa umegundua nini?

Bila shaka kama wewe ni mdadisi utakuwa umegundua kwamba katika vile vipengele vyetu 8 vya mpango mzima wa biashara, FURSA inajikita zaidi katika vipengele vya, Biashara, Bidhaa na Soko.  

 

2. HATUA / SEHEMU YA PILI

ONYESHA NI JINSI GANI UTAKAVYOTEKELEZA MPANGO WAKO.(EXECUTION)

Hapa ndipo vitendo halisi hutokea! Utaingia kwa undani kuonyesha ni kwa namna gani utaitumia kikamilifu fursa uliyoionyesha katka hatua ya kwanza. Sehemu hii unaionyesha benki au taasisi ya fedha kwamba unao mpango thabiti wa kuyafikia mafanikio. Vitu muhimu vitatu(3) katika sehemu hii ni hivi vifuatavyo;-

              i)      Mikakati ya Masoko na Mauzo

Masoko na mauzo ni somo pana,  na kwenye mpango wa biashara urefu wa kipengele hiki utategemea aina ya biashara na ukubwa wake. Lakini kitu cha muhimu zaidi hapa unatakiwa kuelezea ni jinsi gani umepanga kulifikia soko lako lengwa na jinsi utakavyowageuza watu katika soko hilo kuwa wateja wako. Baadhi ya vitu muhimu vinavyopaswa kuwekwa katika kipengele hiki ni kama ifuatavyo;.

Mkakati wa kujipanga sokoni (Positioning strategy) – hiki ndiyo kitu kinachoifanya biashara yako kuwa ya kipekee na inayowavutia zaidi wateja wako walengwa.

Mtangazo (promotion). Utatangaza biashara yako kwa njia ipi? Mabango, redio, TV, Mitandao ya kijamii au vipeperushi?

Bei: Kile utakachotoza kwa ajili ya bidhaa/huduma zako ni lazima kiakisi mahitaji ya wateja wako. Kuna njia kuu 2 za kupanga bei,       ya 1) Kwa kuzingatia gharama ulizotumia(cost plus pricing) na       ya 2) Kwa kuzingatia thamani ya bidhaa/huduma (Value pricing)   

              ii)     Uendeshaji (Operations)

Katika hatua ya pili ya utekelezaji, uendeshaji ndiyo jambo la msingi kuliko vyote

Ni muhimu hasa hasa katika biashara zile zinazofanyikia  kwenye eneo maalumu (Brick & Mortar Business) zilizo na ofisi, fremu au stoo na maghala ya kuhifadhia malighafi na bidhaa mfano kiwanda nk. Unaweza kuelezea hapa ni kwanini eneo lako ni muhimu kwa hiyo biashara husika au ni eneo lenye ukubwa kiasi gani. Katika kipengele hiki pia unaweza kueleza ikiwa biashara yako itafanyikia nyumbani au ni mahali gani, ukubwa wa eneo la ofisi pamoja na vitu vingine mbalimbali vinavyopatikana katika eneo la biashara kama vile mitambo, vifaa na hata programu za kompyuta zinazotumika.

             iii)     Utekelezaji vitendo na Vipimo

Wakopeshaji na Wawekezaji hutaka kujiridhisha kwamba unafahamu jinsi ya kutekeleza mpango wako kupata mafanikio kibiashara. Haya ni malengo yanayowekwa ambayo hukusaidia biashara yako kupiga hatua. Kwa mfano tuseme unafungua kiwanda chako, moja kati ya malengo yanaweza yakawa ni, ukamilishaji wa bidhaa za mfano, ufunguzi rasmi, kufikisha bidhaa sokoni nk. Vipimo huonyesha namna utakavyopima mafanikio ya biashara yako, je ungependa kuzalisha kiasi fulani cha bidhaa? au kuhakikisha gharama hazizidi kiwango fulani? Fikiria ni kipimo kipi muhimu zaidi ya vingine kisha ueleze jinsi utakavyopima kwa ajili ya ukuaji wa biashara yako.

Katika hatua hii ya pili ya Utekelezaji (execution) utagundua kwamba inahusisha vipengele vya, Mikakati na Utekelezaji pamoja na kile cha Utawala.  

 

3. HATUA YA TATU

MPANGO WA FEDHA KWA UNDANI (FINANCIAL PLAN DETAILS)

Hii ndiyo sehemu muhimu zaidi ya mpango wa biashara kwa ajili ya kuombea mkopo benki au wawekezaji na ndiyo sehemu watu wengi huona ni ngumu zaidi kuandaa, Wakopeshaji wengi na wawekezaji ndiyo sehemu wanayoitazama kwa umakini zaidi ili kutambua uwezekano wa biashara yako kufanikiwa au kuanguka.

Lakini sehemu hii haipaswi kuwa ngumu ikiwa mtu utaigawa katika sehemu ndogondogo na zifuatazo ni sehemu ndogondogo 3 ambazo ni lazima mpango wako uwe nazo;

              i)      Mahitaji na vyanzo vya fedha

Unaonyesha ni kwa namna gani utatumia fedha zitakazowekezwa kwenye biashara iwe ni fedha za mmiliki, mkopo au fedha kutoka chanzo chochote kile kingine. Matumizi yanaweza yakawa ni ya kununulia vifaa, kununulia malihafi/bidhaa au kulipia gharama mbalimbali za biashara.

              ii)     Makisio(Forecast)

Haya ni makadirio ya fedha kwenye biashara yako. Yanakupa wewe na benki wazo la ni faida kiasi gani biashara inaweza kutengeneza baada ya kipindi fulani kupita. Hapa kuna vitu vitatu vinavyotakiwa kuwepo;

Mapato. Unaorodhesha bidhaa zote au huduma biashara yako inazotarajia kuuza ili kuingiza pesa.

Gharama za moja kwa moja (Direct costs) Kwa maneno mengine ni zile gharama za kutengeneza kile unachouza

Expenses; Hizi ni gharama za kudumu za uendeshaji kama vile mishahara, pango, umeme na maji, gharama za masoko nk.

             iii)     Taarifa za kifedha

Watu wa Benki hapa ndipo hutupia jicho zaidi na ni vitu vifuatavyo utahitaji kuweka;

Taarifa Faida na Hasara (Profit and Loss) – Taarifa hii huchukua namba kutoka kwenye makisio yako ya mauzo na maeneo mengine madogomadogo kama gharama za mauzo kuonyesha kama unapata faida au hasara.

Makisio ya Mali na Madeni (Projected Balance Sheet) Ni kitu cha kwanza kabsa afisa wa mkopo atakiangalia. Inaonyesha madeni ya biashara, mtaji na rasilimali za biashara(assets) inaangazia uimara wa biashara yako kifedha.

Makisio ya Mtiririko wa Fedha taslimu. Ni taarifa inayopima kiasi cha fedha taslimu biashara ilizokuwa nazo mkononi au benki katika muda fulani. Maafisa mikopo wanapendelea waone mtiririko halisi wa fedha katika miezi yote 12 ya mwaka wa kwanza wa biashara.

 


4. HATUA YA NNE

MUHTASARI TENDAJI (EXECUTIVE SUMMARY)

Ingawa hii ndiyo sehemu inayoonekana ya kwanza katika mpango wowote ule wa biashara lakini kimlolongo ndiyo huandikwa mwishoni kabisa baada ya kumaliza sehemu nyingine zote. Kimsingi hii ndiyo huitambulisha biashara yako ukifupisha pointi zile muhimu kutoka katika kila sura zinazounda mpango wako mzima. Mara nyingi huwa na urefu wa ukurasa mmoja au miwili tu, jaribu kuandika kwa kifupi na kwa uwazi kadiri iwezekanavyo ukizingatia kwamba hii ndiyo sehemu ya kwanza kabisa itakayomfanya mkopeshaji wako au mwekezaji kuhamasishwa na biashara yako hivyo kukubali kutoa pesa.

 

HITIMISHO

Huhitaji kuwa na elimu kubwa sana ili uweze kuandika mpango wa biashara yako mwenyewe. Ikiwa unao uwezo wa kufanya biashara na ukapata faida basi na ujue pia unaweza kuandika mpango wa biashara hiyo. Kinachotakiwa tu ni kufahamu namna ya kupangilia mawazo yako kwani ukishakuwa na wazo la biashara kichwani au kuanza kuifanya basi tayari na mpango unao kichwani mwako.

 

MAOMBI YA MKOPO (FUNDING REQUEST)

Kipengele hiki katika makala hii sijakiweka popote kwa makusudi kwani mara nyingi huandikwa tu pale mtu unapoandika mpango wa biashara kwa ajili ya kuombea mkopo.

Maelezo yake kwa kina nimeyatoa katika darasa letu watsap, ni kakipengele muhimu sana na mara nyingi watu hawafahamu umuhimu wake. Kina uwezo mkubwa wa kuamua upate mkopo au ukose.

Nitakufundisha kwa kina ni wapi kiwekwe, kiandikwe nini na mambo mengine mengi kukihusu yatakayosaidia kumshawishi mkopeshaji wako au mwekezaji  hata akakupatia fedha unazohitaji – Tukutane darasani!

 

UNAHITAJI MPANGO WA BIASHARA?

Kuna njia mbili unaweza kupata mpango wa biashara yako

1.  Kutafuta mtaalamu kama sisi akuandikie: Njia hii utatakiwa kulipia kiasi fulani cha fedha na utashiriki kuandika kwa kujibu maswali machache utakayoulizwa na mtaalamu huyo kama vile jina la biashara, malengo, makisio ya mauzo,soko lako nk.

2.  Kuandika mwenyewe: Hii ndiyo njia yenye faida zaidi kwako kwani inakufanya ufikirie kila hatua utakayopitia kwenye biashara yako, ni kama vile unafanya mazoezi kwa ajili ya mechi utakayoicheza baadae ili muda ukifika uweze kupata ushindi kwa wepesi zaidi. Unaweza kujua kuandika mchanganuo kwa kujifunza kupitia chuoni, katika vitabu mbalimbali au kupitia kozi mbalimbali mitandaoni.


Sisi tunatoa huduma zote mbili hapo juu kwa anayehitaji, kufundisha lakini kumuandikia mtu anayehitaji huduma hiyo.

Sasa hivi tunalo darasa mtandaoni katika Group letu la Whatsapp liitwalo MICHANGANUO-ONLINE. Ambalo tunafundisha kwa kina jinsi ya kuandaa mipango ya biashara mbalimbali hasa zile zilizokuwa na ubunifu wa kipekee.

Unapojiunga na group hili unapata kwanza kozi kamili ya kuandika mpango wa biashara halafu michanganuo mbalimbali bunifu ya biashara zinazolipa inafuata. Unapata vitabu papo hapo na sample za michanganuo zaidi ya 10 kwa kiingereza na kiswahili. Tunatoa pia offa ya Tafsiri kwa kswahili ya kitabu cha THINK AND GROW RICH kwa watu wachache wanaowahi offa hii. Offa inamalizika tarehe 30 August 2021 baada ya hapo haitakuwepo tena.

Kujiunga na group upate offa zote na masomo mengine yote yaliyowahi kutolewa katika group siku za nyuma lipia kiingilio chako sh. Elfu 10  kwa namba, 0765553030 au 0712202244 kisha nitakutumia coupon ya kununulia kitabu cha Think and Grow Rich-swahili kwa sh. Elfu moja katika mtandao huu wa GETVALUE(Bonyeza kukiona). Hivyo offa nzima utakuwa umelipa shilingi elfu 11 tu. Na utakuwa kwenye group ukijifunza kwa miezi 12 (mwaka mzima toka tarehe uliyojiunga)

Mafunzo ya jinsi ya kuandaa michanganuo ya biashara katika group yanatolewa na Wataalamu walio na uzoefu wa kutosha katika fani hiyo. Tumeshaandika michanganuo halisi mingi kwa ajili ya biashara mbalimbali za watu na makampuni kwa ajili ya kuombea fedha bank na taasisi mbalimbali za kifedha. Baadhi ya michanganuo ya biashara na makampuni hayo tumeiweka hapa kama mfano lakini hatujaweka wazi utambulisho wao. BAADHI YA KAZI ZETU NI HIZI (Bonyeza kuzisoma)


Tunafundisha kile tunachokifanya!


Nakukaribisha sana kwenye group letu, na hata ikiwa hupendi kuwa katika magroup ya mitandaoni, basi jipatie tu hii offa kwa ajili ya kupata vitabu na michanganuo ujifunze mwenyewe taratibu. Fungua kiungo kifuatacho kusoma idadi ya vitu vilivyoko kwenye OFFA kubwa ya vitabu na michanganuo ya biashara kikiwemo kitabu Thing & Grow Rich-swahili edition-2021 kwa sh. Elfu 11 tu

Mafunzo ya kuandika mpango wa biashara ikiwa wewe ni mjasiriamali tu wa kawaida, yatakuwezesha wewe kufahamu biashara vizuri zaidi na kwa kina kwani mpango wa biashara unagusa kila hatua inayopigwa katika safari nzima ya kibiashara.

Na ikiwa pengine wewe ni mwanataaluma mwenye nia siku moja uje uwe mtaalamu (business plan expert) kama sisi kwa ajili ya kuwaandikia watu wengine michanganuo ya biashara zao wakulipe pesa, basi mafunzo haya hupaswi kabisa kuyakosa.

Siku ya Leo tarehe 25/08/2021 kwenye group tulikuwa na somo la Matayarisho na kesho tarehe 26 semina yetu ya Jinsi ya kuandika mpango wa Biashara inaanza rasmi.


FUATILA ZAIDI HAPA

SEMINA SIKU YA 1

SEMINA SIKU YA 2

SEMINA SIKU YA 3

SEMINA SIKU YA 4

Prepared by;

Peter Tarimo

Entrepreneur & Business Plan Expert


SOMA PIA;

1. Jinsi Mpango wa Biashara unavyoweza kuongeza mafanikio ya biashara yako.

2. Sababu kuu (5) kwanini uandike mpango wa biashara yako kwanza kabla hujaanzisha biashara yenyewe.

3. Je, huna muda wa kutosha kuandika mpango wa biashara? Tumia njia hizi 3 rahisi

4. Sababu nne kwanini kipengele cha fedha ni moyo wa mpango wa biashara (The heart of a business plan)

5. Ni lini biashara yako itarudisha gharama zote ulizotumia?(Break Even Point) 

0 Response to "JINSI YA KUANDIKA MPANGO WA BIASHARA UTAKAOSHAWISHI BENKI NA WAFADHILI KUKUPATIA FEDHA"

Post a Comment