SEMINA SIKU YA NNE: JINSI YA KUUANDIKA MUHTASARI TENDAJI (EXECUTIVE SUMMARY) -JANE RESTAURANT | JIFUNZE UJASIRIAMALI

SEMINA SIKU YA NNE: JINSI YA KUUANDIKA MUHTASARI TENDAJI (EXECUTIVE SUMMARY) -JANE RESTAURANT

mlo wa usiku jane restaurant

Kunufaika zaidi na semina hii unahitaji kuwa na michanganuo ya Jane Fast Food na Jane Restaurant katika lugha ya kiswahili na kiingereza.


Katika kila mpango wa biashara Muhtasari ni lazima uwepo pale mwanzoni kabisa na huandikwa baada ya kuandika sehemu nyingine zote. Kazi zake kubwa ni;

·       kutoa picha kwa ufupi ya andiko lako zima kwa kuangazia maeneo yote muhimu.

·       Kumpa msomaji wa mpango wako uelewa wa jumla wa kile unachotaka kumueleza kabla hata hajasoma andiko lenyewe zima

·       Kumpa yule msomaji asiyekuwa na muda mwingi wa kusoma mchanganuo wako wote ufupisho utakaomsaidia kupata zile pointi muhimu.

Urefu wa Muhtasari tendaji haupaswi kuzidi ukurasa mmoja au miwili na aya zinapaswa kuakisi sura za andiko lako.

 

Katika Muhtasari wako unatakiwa kuweka yafuatayo;

 

Utambulisho/utangulizi

Hapa unamdokezea msomaji wako kile unachotaka kuandika katika aya moja. Kwa mfano kwemye Jane Restaurant tumeanza na Dhamira ambayo ni “kuwapa wateja wake mlo mzuri wenye afya katika mazingira mazuri na rafiki kwa bei watakayoimudu” mstari huo unatosha kabisa kumjulisha msomaji juu ya ni nini biashara yako inahusika nacho.

 

Biashara na Fursa iliyopo

Elezea kwa kifupi kuhusiana na biashara au kampuni yako ukijumuisha jina la biashara, kile unachouza, unawauzia kina nani na wako wapi. Yapo mengi kuhusiana na bidhaa au huduma unayouza lakini weka maelezo kwa kifupi sana. 

 

Tathmini ya soko na Sekta

Taja muelekeo au vitu muhimu kwenye sekta na biashara uliyopo, nguvu zako za kiushindani dhidi ya washindani na eleza kwa ufupi kuhusu wateja wako watarajiwa ubainishe ni kwanini wanunue kutoka kwako na wala siyo kwa wapinzani wako.


Mikakati na Utekelezaji

Eleza kwa kifupi mkakati wako wa masoko jinsi utakavyotangaza bidhaa/huduma zako na njia utakazotumia kuwafikia wateja. Onyesha pia ratiba ya matukio muhimu kwenye biashara yako, mhusika atakayesimamia pamoja na bajeti.

 

Usimamizi na Uendeshaji

Eleza kwa kifupi yale mambo muhimu kuhusiana na timu yako ya utawala mfano wasifu wa waanzilishi wa biashara au watendaji wakuu. Pia eleza kwa kifupi jinsi shughuli za kila siku zinavyoendeshwa katika biashara yako mfano ikiwa utatumia njia fulani ya kipekee au mfumo wa usimamizi unazitaja hapa.

 

Mpango wa Fedha

Hesabu kwenye mpango wako zipo nyingi na huwezi kila moja ukaiweka katika muhtasari, fikiria mpango wako ni kwa ajili ya nini, je ni wa kuombea fedha benki? kuvutia wabia? hivyo weka kiasi cha fedha unachohitaji na kile ulichokuwa nacho tayari. Na ikiwa lengo la mchanganuo wako ni kuonyesha tu jinsi utakavyoendesha biashara yako kwa mafanikio basi weka katika muhtasari wako sehemu ya hesabu inayoonyesha ukuaji wa biashara yako.

 

Hitimisho

Unaweza pia kuweka hitimisho kwa kuandika sentensi chache fupi na zenye kushawishi zinazoelezea andiko lako zima na kumwacha msomaji na hamu ya kutaka kuusoma mchanganuo wako mzima. Hitimisho lisizidi aya moja.



Simu/watsap: 0765553030


Je, Ungependa tukuandikie Mchanganuo wa Biashara yako? Tujulishe gharama zetu ni rafiki. 

0 Response to "SEMINA SIKU YA NNE: JINSI YA KUUANDIKA MUHTASARI TENDAJI (EXECUTIVE SUMMARY) -JANE RESTAURANT"

Post a Comment