Kwanza kabisa hebu tujikumbushe maana ya Mpango wa biashara ni nini. Kwa mujibu wa kitabu chetu cha MICHANGANUO YA BIASHARA NA UJASIRIAMALI ambacho naamini kila mtu hapa katika group letu anacho, Mchanganuo wa Biashara una maana hii hapa;
Mchanganuo wa biashara au mpango wa biashara kwa
kimombo (Business plan) ni maandishi yanayoelezea kila jambo kuhusu biashara
unayoiendesha, mambo hayo ni, malengo, mikakati, bidhaa/hudumu utakayouza, soko
(wateja), shughuli mbalimbali za masoko na uongozi, gharama, mahitaji, na
masuala yote yanayohusiana na fedha.
Au maana nyingine unaweza
ukasema hivi;
Mchanganuo wa biashara ni dira au ramani ya biashara
yako kuonyesha unakotoka na unakokwenda
Sasa tunaanza anzaje kuandika
mchanganuo wetu?
Ili uweze kuaandika
mchanganuo wa biashara yeyote ile kitu cha kwanza kabisa cha kufanya ni UTAFITI
WA HIYO BIASHARA, wengine husema UTAFITI WA SOKO
Kwa kifupi kabisa Utafiti wa
biashara unayotaka kuiandikia mchanganuo mfano hii yakwetu ya Mgahawa, unapaswa
kuchunguza mambo mbalimbali yanayoihusu biashara hiyo kuanzia Wateja(soko),
Washindani, Bidhaa, Eneo la biashara, Mahitaji ya pes(mtaji) na kila kitu
kinachohusiana na biashara ya Mgahawa. Mchakato wa utafiti au upembuzi yakinifu
umeelezewa kwa kina kwenye Kitabu hicho, hapa tutagusa zile pointi muhimu tu.
Njia nyepesi ya kufanya
utafiti ni kwa kuwauliza maswali wateja watarajiwa kwa mfano unaweza kuwauliza
wanapendelea zaidi aina gani za vyakula (menu),
ni nini kinachowaudhi wanaponunua kutoka kwenye migahawa iliyokuwepo na pia
unaweza kuchunguza katika eneo unalotarajia kuweka mgahawa wako kuna idadi ya
wateja wangapi kwa makisio nk.
Nenda mjini maduka yanayouza
vifaa vya migahawa uliza bei zake, nenda sokoni uliza bei za vyakula na viungo
mbalimbali uwe nazo zote.
Njia nyingine ya kutafiti
soko/biashara yako ni kwa kusoma machapisho mbalimbali kuihusu pamoja na
kufuatilia vyombo vya habari vinasemaje juu ya biashara hiyo ama sekta nzima
inayohusiana na hoteli na migahawa. Majibu utakayoyapata kutokana na utafiti
wako au uelewa wa kina wa biashara hii vitakusaidia uweze kupata kitu cha
kuandika katika mchanganuo wako vinginevyo utakuwa ukisimulia hadithi ambayo
haina uhalisia.
Sasa tuchukulie (tuassume) kwamba tumekwishafanya utafiti
wetu na tayari tumekwishafahamu ‘nje
ndani’ kuhusiana na biashara hii ya mgahawa, soko tunalolenga (wateja), mahitaji yote yanayotakiwa ili
uweze kuanza, bidhaa ikiwemo jinsi ya kupata malighafi mbalimbali na bei zake
zote pamoja na washindani wanaokuzunguka udhaifu na nguvu zao. Baada ya hatua
hii saa tupo tayari kuanza kuandika MCHANGANUO WETU.
Ili tuweze kuwa na lengo (focus)
tutaweka katika karatasi vipengele vyote vinavyounda mpango mzima wa biashara
ili tuandike kipengele baada ya kipengele, hii itatusaidia kuweka nguvu (concetration) kwenye kipengele kimoja
mpaka kiishe ndipo tuhamie kingine. Kwahiyo tutaongozwa na vipengele hivyo kwenye
kila hatua tutakayopita.
1.0 MUHTASARI
2.0 MAELEZO YA KAMPUNI
3.0 MAELEZO YA BIDHAA/HUDUMA
4.0 TATHMINI YA SOKO
5.0 MIKAKATI NA UTEKELEZAJI
6.0 UTAWALA NA NGUVUKAZI
7.0 MPANGO WA FEDHA
8.0 VIELELEZO
Ingawa kipengle cha kwanza kinaonekana
ni MUHTASARI, lakini hatutaanza nacho huwa kinakuwa cha mwisho kabisa, Kwa hiyo
tutaanza moja kwa moja na cha pili, MAELEZO YA KAMPUNI ambacho nacho kinakuwa
na vipengele vyake vidogo chini yake. Tungeliweza kuanza na kipengele kingine
chochote kile hata cha soko na si lazima kiwe hiki.
2.0 MAELEZO YA KAMPUNI / BIASHARA
Maelezo kuhusu Biashara /
kampuni kwa kiasi kikubwa yanahusu taarifa za ndani ya biashara zaidi kuliko
kutoka nje ya biashara. Hapa chini naorodhesha vipengele vidogo
nitakavyozingatia wakati nikiandika kipengele hiki kikubwa, kwa ujumla tutatoa
maelezo kulingana na vipengele hivi vidogo. Siyo lazima kuandika juu ya kila
kipengele kwani itategemea biashara inahitaji kitu gani, kama kitu hakina
umuhimu hukiweki
2.1 Dhamira
kuu (mission)
2.2 Vision (Maono)
2.3 Malengo (Objectives)
2.4 Siri za
mafanikio
2.5 Umiliki
2.6 Jina
2.7 Usajili
2.8 Kianzio
2.9 Eneo na
vifaa vilivyopo.
Aya ya kwanza inayoanza na
namba “2.0 Maelezo ya biashara/kampuni”
huandiki chochote kwanza panabaki wazi
kwani ni muhtasari mdogo wa vipengele hivyo vingine vidogo vidogo chini
yake.
“2.1 Dhamira kuu”
Dhamira
kuu ni ile biashara unayoifanya. Kwa mfano sisi hapa tutasema hivi;, “Kutoa huduma bora ya
chakula na vinyaji vyenye afya kwa wateja
katika mazingira rafiki na ya kuvutia
2.2
Maono
Maono ni
picha ya biashara yako unayotaka uione baada ya kipindi fulani kupita, mfano
tungeweza tukasema hivi “Kuja kuwa na mgahawa mkubwa zaidi jijini Da es salaa” lakini katika mchanganuo
wetu huu hatujaweka kipengele cha maono.
2.3 Malengo
Hapa tunataja
vile vitu tunavyokusudia kuvitimiza baada ya kutekeleza mpango wetu. Malengo
mazuri ni lazima yawe halisi, yanayopimika, yenye kutekelezeka na yaliyokuwa na
muda maalumu wa utekelezaji. Nayataja baadhi hapa chini;
· Kuongeza mauzo kwa asilimia 10% kila mwaka kwa kutoa
chakula na vinywaji bora.
·
Kuongeza
idadi ya wafanyakazi kutoka 10 mpaka 12 ifikapo mwaka wa 4
2.4
Siri za mafanikio.
Hapa
tutaorodhesha yale mambo tutakayoyapa kipaumbele katika biashara yetu kusudi tuweze
kufanikiwa, nayo ni;
· Kudumisha usafi na afya katika mazingira yote ya
mgahawa
· Ubora na uhalisia katika vyakula na vinywaji.
· Mazingira mwanana na rafiki.
“2.5 Umiliki na
historia ya biashara”
Hapa tunataja jina la
biashara ambalo ni “Mgahawa wa Jane”, majina ya wamiliki ambao ni Bibi Janeth
Mwalugaja na Bibi Grace Lyimo. Tutaelezea na historia ya biashara ilivyoanza. Katika kipengele hiki kidogo, tutataja pia
eneo biashara itakapokuwa ambalo ni Kijitonyama Sayansi jijini Dar es salaam
“2.6 Kianzio
Biashara hii japo siyo mpya
lakini imefanyiwa mabadiliko makubwa mno kiasi cha kuwa kama ni biashara
inayoanza hivyo tutaichukulia kama biashara mpya.
Hapa tutaorodhesha kwenye
jedwali mahitaji yote tukianza na gharama mbalimbali mpaka assets
zitakazohitajika. Namba tutakazozitumia hapa zitatokana na utafiti ule tulioufanya
pale mwanzoni mfano gharama za usajili, malighafi na vifaa. Chini yake tutaweka
Jedwali la mali na madeni.
Baada ya kumaliza sasa tutarudi
pale mwanzoni katika aya tuliyoiacha wazi kwenye namba “2.0 Maelezo ya Biashara.” Ilipoanzia sura yetu hii. Tutachagua
katika kila kipengele kidogo tulichokwisha andika mstari mmojammoja au maneno
muhimu na kuyapanga katika hii aya kutengeneza muhtasari mdogo wa kipengele au
sura nzima.
2.7 Maombi ya fedha (fund request)
Kama unafuatailia makala hizi
tokea mwanzo, kuna mahali nilisema kuwa unapoandika mchanganuo wa biashara kwa
ajili ya kuombea fedha mahali iwe ni mkopo au hata uwekezaji unatakiwa katika
mchanganuo wako uweke kipengele rasmi cha maombi hayo. Hamna mahali mahsusi
kinapokaa lakini ni vizuri kukiweka katika sura ya Kampuni/biashara kwenye
kianzio au katika kipengele cha fedha.
Fund Request / Maombi ya mkopo ni andiko linaloweza kusimama peke yake bila ya
kujumuishwa kwenye mchanganuo kamili wa biashara na ukalipeleka kama lilivyo
kwa mkopeshaji wako na unapoandika kipengele hiki ndani ya mchanganuo wa
biashara basi kinakuwa ni sehemu ya mpango huo na hakitakuwa na vitu vingi sana
kama vile umeamua kukiwakilisha kikiwa chenyewe kama kilivyo.
Kipengele hiki unatakiwa
kuweka mambo yafuatayo;
Maelezo ya buiashara yako kwa kifupi
Ikiwa maombi ya mkopo ni
sehemu ya mchanganuo wa biashara basi hapa hutaandika kwa kirefu kwani tayari
maelezo ya biashara unakuwa umeshayaandika kwa kirefu kwenye sura inayohusu
biashara kwenye mpango wako lakini ikiwa maombi ya mkopo unayapeleka yenyewe
kama yalivyo kwa mkopaji basi ni lazima uandike kwa kina zaidi.
Kiasi cha fedha unachoomba.
Hapa unataja ni kiasi gani
unahitaji kwa sasa na hata baadae unatarajia kuhitaji kiasi gani pia.
Matumizi ya fedha hizo ni nini?
Je ni kwa ajili ya mtaji wa
kuendeshea biashara? Kununulia vifaa, mashine au majengo? Kulipia pango,
Kununulia malighafi au Ni kwa ajili ya kutangaza biashara yako? Chochote kile
utakachoombea pesa eleza kitagharimu kiasi gani kila kimoja.
Dhamana za mkopo
Orodhesha vitu unavyotarajia
vitakuwa dhamana ya kulinda mkopo wako ikitokea umeshindwa kulipa.
Jinsi utakavyoulipa mkopo wako
Eleza unatarajia kulipa katika
muda gani, riba ni kiasi gani na marejesho ya mkopo kiasi gani kwa mwezi nk. Ikiwa
maombi ya mkopo ni andiko linalojitegemea siyo sehemu ya mpango wa biashara itakubidi
hapa uweke mahesabu kwa kirefu kidogo lakini ikiwa ni sehemu ya mpango wa biashara
tayari basi utaandika tu kwa kifupi kwani Mahesabu yatakuwa yameshaonyeshwa kwa
kirefu katika sura yenyewe ya fedha.
Na hapa ndio mwisho wa kipengele chetu
hiki cha Maelezo ya Biashara
3.0 MAELEZO YA BIDHAA / HUDUMA
Katika sura ama kipengele
hiki cha maelezo yanayohusu bidhaa au huduma, hapa ndipo unapotakiwa utoe
maelezo ya ndani kabisa yanayohusu kile kitu biashara yako inachouza. Kwa
biashara yetu hii ya Mgahawa wa Jane bidhaa zetu kubwa ni vyakula na vinyaji baridi.
Kama ilivyo kwa vipengele
vingine vikubwa vinavyounda mpango mzima wa biashara, hiki nacho kina vipengele
vyake vidogovidogo kadhaa ambavyo ndivyo tutakavyoelekeza nguvu zetu kwake.
Vipengele vidogo ni hivi;
3.1 Maelezo ya bidhaa/huduma
3.2 Utofauti/upekee wa
bidhaa/huduma na za
washindani
3.3 Vyanzo vya
malighafi/bidhaa
3.4 Kopi za matangazo
3.5 Teknolojia
3.6 Bidhaa au Huduma za
baadae
Kwahiyo maelezo yetu kwenye
kipengele hiki yatajikita katika mada hizi ndogondogo hapo juu. Hata hivyo siyo
sheria wala lazima kuweka vipengele vyote kwenye Sura yako, unaweka tu
kipengele unachoona kinafaa kulingana na mazingira ya biashara yako yalivyo
lakini angalao kuna vipengele kwa mfano “Maelezo
yenyewe ya bidhaa/huduma" ni lazima yawepo.
Kama tunavyoona kwenye
mchanganuo wetu huu wa mgahawa wa Jane siyo vipengele vyote vidogo vimeelezewa.
Kwa mfano hapa utaona ni maelezo ya bidhaa tu kwenye muhtasari halafu chini
yake kuna Bidhaa za baadae na Tathmini ya NUFUVI ambayo hata haipo
kwenye vipengele vyetu pale juu.
Unaweza kuandika maelezo
mafupi tu (Muhtasari) kuhusiana na
bidhaa zako kama aya mbili au tatu hivi pasipo kuorodhesha kila kipengele na
maelezo yake. Lakini katika maelezo hayo hakikisha yanagusa sifa muhimu za
huduma au bidhaa zako pamoja na upekee wake.
4.0
TATHMINI YA SOKO
Tathmini
ya soko nayo imegawanyika katika vipengele vidogovidogo kadhaa ambavyo vyote
ili uweze kuviandika unahitaji kupata takwimu na taarifa mbalimbali nje ya
biashara yako zinazohusiana na soko au wateja watarajiwa, sekta ya biashara
uliyopo pamoja na ushindani.
Taarifa
hizi na takwinu mbalimbali kama tulivyoona pale mwanzo niliposema ni lazima
kabla hujaanza kwanza ufanye utafiti wa soko, hapa ndio mahali penyewe hasa pa
kuzitumia taarifa tulizopata kwenye ule utafiti
Vipengele
vidogo kwenye sehemu hii ya Soko ni hivi vifuatavyo;
4.1
Mgawanyo wa soko
4.2 Mkakati wa soko lengwa
4.2.1 Mahitaji ya soko
4.2.2 Mwelekeo wa soko
4.2.3 Ukuaji wa soko
4.3 Tathmini ya sekta
4.3.1Washiriki katika sekta
4.3.2 Usambazaji ulivyo
4.3.3 Vigezo vya ushindani
4.3.4 Washindani wakuu
Hata
hivyo kama tulivyokwishaona huko nyuma wingi wa vipengele hivi utategemea
mpango wako wa biashara ni kwa ajili ya nini. Ikiwa katika mpango wako wa
biashara kitu fulani hakina umuhimu basi huna haja ya kukiweka. Kwahiyo unaweza
kukuta katika vipengele vyote vidogo vilivyotajwa hapo juu pengine unaweka
viwili, vitatu au hata vyote kulingana na aina ya mchanganuo unaoandika, urefu
au aina ya biashara unayoandikia.
Kwa upande wa biashara yetu
hii ya Jane Rstaurant, kwenye tathmini ya soko kama kawaida kuna muhtasari pale
mwanzoni kabisa ambao umeandikwa mwishoni baada ya kukamilisha vipengele
vingine vyote vidogovidogo.
Ngoja sasa tuangalie vipengele
vidogo jinsi vilivyoelezewa,
4.1 Mgawanyo wa Soko.
Katika mgawanyo wa soko tutataja ni makundi mangapi ya wateja watarajiwa
ambapo hapa yametajwa kuwa ni;
1. Wafanyakazi katika taasisi binafsi na za
serikali
2. Wamiliki wa Biashara.
3. Wakaazi wenye umri zaidi ya miaka 18
wanoishi peke yao.
Kila kundi tunaelezea sifa zake za ‘kidemografia’
mfano umri, jinsia, na hata tabia zao zinazowatofautisha kundi moja na jingine.
4.2 Mkakati wa Soko Lengwa.
Ni kipengele kingine kidogo
kilichopo katika Sura au kipengele kikubwa cha SOKO kwenye mchanganuo huu wa
Jane Restaurant, wamiliki wake waliamua kulenga makundi yote matatu,
Wangeliweza pia kulenge kundi moja tu au mawili lakini kulingana na utafiti wao
wameona makundi yote 3 ni muhimu kwao.
Unaweza pia kuelezea jinsi
utakavyohudumia kila kundi, kwa mfano Jane wameeleza ni kwa namna gani
watahudumia makundi hayo matatu.
4.3 Tathmini ya Sekta.
Kwenye tathmini ya sekta
tutaeleza ni sekta ipi biashara hii inaangukia ambapo ni sekta ya Hoteli na
Migahawa. Kwa kawaida hapa unaweza kueleza jambo lolote lile “linalotrend” kuhusiana na sekta husika
pamoja na kutaja wahusika mbalimbali kwenye hiyo sekta, kwa mfano kwenye hoteli
na migahawa tutasema, “Sekta hii
imegawanyika kwa kiasi kikubwa sana na inajumuisha wauzaji wadogowadogo wa
vyakula maarufu kama mama na baba lishe, vituo vya chipsi (fast foods),
cafeteria, mabaa, wapikaji kwenye shughuli mbalimbali hadi migahawa mikubwa na
hoteli”
4.3.1 Ushindani.
Katika kipengele hiki
tutaelezea hali ya ushindani ilivyo, tutataja washindani wakubwa ambapo kwa
upande wa Jane Restaurant wao wamewaweka washindani wao katika makundi 3
(1) Washindani wa Moja kwa moja.
(2) Washindani wasiokuwa wa moja kwa moja.
(3) Mama na Baba lishe.
Kwa
kila mshindani/kundi tutaelezea nguvu na udhaifu waliokuwa nao kwa kuzingatia, bidhaa, ubora, bei, usimamizi,
hali ya kifedha, kuaminika, mfumo wa usambazaji na teknolojia tukilinganisha na
biashara ya Jane Restaurant. Tunaweza pia kueleza na kipande cha soko
wanachokilenga na jinsi tutakavyoweza kukabiliana nao.
4.3.2 Mahitaji ya Soko.
Kwenye kipengele hiki
tunatakiwa kuonyesha ni kwanini soko linahitaji huduma za Jane Restaurant kwa
mfano tutasema Dar es salaam hususan maeneo ya Kijitonyama utakapokuwa mgahawa
huu, kuna ongezeko kubwa la watu (hapa
tungeliweza kuweka hata na takwimu za sensa ya watu na makazi kuthibitisha hilo)
Sababu nyingine ni kwamba kila mtu anahitaji kula mlo kamili na wenye afya
kigezo ambacho Jane Restaurant ndiyo kaulimbiu yao.
4.3.3 Mwelekeo wa soko.
Katika mwelekeo wa soko tutaeleza sababu inayoonekana kubadilisha hali ya soko au biashara. Kwa mfano
tutasema kwamba, “wateja wetu
watarajiwa wanaongezeka uelewa katika mitindo yao ya maisha wakitambua kati ya
vyakula vinavyoboresha afya na vile vinavyoharibu afya au kuchangia kuleta
magonjwa ya tabia”.
Tumemaliza
Kipengele (Sura) za BIDHAA na SOKO, kesho tutaendelea na sura za Mikakati &
Utekelezaji pamoja na Uongozi. Nitajitahidi kuziweka mchana ili jioni tumalizie
na Kipengele cha Fedha
Mwishoni
nitacompile sehemu zote toka juzi kuwa PDF moja halafu pia nitaweka hapa
Mchanganuo huo kamili kwa kiingereza na kwa kiswahili.
Unaweza kuona
kama ni vigumu kuelewa lakini unapojifunza sehemu ndogondogo kama ninavyoweka
hapa mwishowe utaona ni rahisi na utaelewa, huwezi kujifunza siku moja ukaelewa
ndio maana tukawa na hili group kusudi kwa kujifunza michanganuo mbalimbali yule
mwenye nia ya dhati ya kuelewa aweze kuelewa.
FUATILA
ZAIDI HAPA
0 Response to "SEMINA SIKU YA 1: KAMPUNI/BIASHARA, HUDUMA/BIDHAA NA SOKO(JANE RESTAURANT)"
Post a Comment