SIRI ILIYOFICHIKA KIPINDI CHA UTAWALA WA MKAPA

Hayati Rais Benjamin William Mkapa
Baada ya kutokea kwa kifo cha Mheshimiwa Benjamini William Mkapa Rais wa awamu ya tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kama raia mwingine yeyote yule wa Tanzania, binafsi nilishtushwa na kujawa na huzuni kubwa ya kuondokewa na mzee huyu aliyekuwa mpenda maendeleo kwa wananchi wake akiwa madarakani lakini hata wakati akiwa hayupo madarakani. 


Kama mwandishi wa blogu kuhusiana na masuala ya maendeleo na mafanikio ya watu nilihisi kuwa na wajibu wa kuandika japo kidogo kuhusiana na mchango wa Hayati Mzee Mkapa kama nilivyowahi kuandika juu ya michango ya watu wengine mashuhuri hapa nchini waliopata kunivutia na kunifanya nipende kufuatilia maisha yao mfano Wafanyabiashara, Hayati Mzee Reginald Abrahamu Mengi, Ali Mufuruki, Ruge Mutahaba na wengineo.

SOMA: Siri kubwa 2 za mafanikio ya Ruge Mutahaba Clouds FM: Wengi hatukuzijua mpaka anaumwa, kufariki na kuzikwa leo

Hata hivyo katika siku zile za maombolezo nilipanga nipost kitu lakini roho yangu ikawa nzito, si kwa sababu sikuwa na cha kuandika hapana, bali niliishiwa tu nguvu ya kuandika kutokana na kukata tamaa. Nilijiuliza moyoni, “Kwanini wale watu ninaowahusudu sana kutokana na michango yao katika maendeleo ya Watanzania na binadamu kwa ujumla Mwenyezi Mungu huwa  anawachukua wakati ninaohisi siyo sahihi kuwachukua?”  

“Ni juzijuzi tu kamchukua Ruge Mutahaba, hatujakaa vizuri akamchukua Mzee wetu Reginald Mengi, hata hatujapoa akamchukua tena Mzee Ally Mufuruki. Basi Moyo wangu ulinyongonyea nikaona hata sina sababu ya kuandika, ni bora nikae tu kimya lipite hivihivi, nikiomboleza ndani kwa ndani”.

Jana wakati nikipekuapekua makabrasha yangu ya zamani, nikakutana na nakala za magazeti yangu ya zamani miaka ya 2000 wakati nilipokuwa nafanya uandishi wa habari katika vyombo vya habari hususani katika magazeti(Print Media). Nilikutana na gazeti(Jarida) nililokuwa nikilimiliki mimi mwenyewe binafsi lililoitwa SAYARI MPYA, mbele katika stori zilizoongoza niliona picha ndogo ya Hayati mzee Mkapa kipindi hicho akiwa Raisi wa nchi na kichwa cha habari kilichosema;  SIRI ILIYOJIFICHA KIPINDI CHA UTAWALA WA MKAPA”
Makala hii niliyoiandika miaka 15 iiliyopita nilikuwa wakati huo nataka kufichua mambo mbalimbali aliyokuwa ameyafanya Rais Mkapa wakati akimalizia muhula wake wa pili na wa mwisho madarakani, mambo ambayo inawezekana kuna watu wengi walikuwa hawayajui au pengine walikuwa hawayachukulii kwa uzito unaostahili.

SOMA: Mzee Reginald Mengi hajafa, ataendelea kuishi katika roho zetu siku zote

Kukutana na majarida hayo kuliamsha upya moyoni mwangu moto na ari kubwa ya kuandika chochote kile kumhusu Hayati Mzee Benjamini William Mkapa. Nilihisi upya kuwiwa na kuona sitakuwa nimemtendea haki Mentor wangu huyu niliyempenda na kuzihusudu mno kazi zake. Mara moja niliketi kitini na kuanza kuandika makala unayoisoma sasa hivi.

Nilijifariji kwa kuikumbuka Zaburi 90:10,


“Miaka ya kuishi ni sabini, au tukiwa wenye afya, themanini; lakini yote ni shida na taabu! Siku zapita mbio, nasi twatoweka mara!”

Wanadamu sote tutalala mavumbini na siku zetu za kuishi ni miaka 70 au 80, na Kwa Mzee Mkapa alishapita miaka 70 hivyo sina sababu kubwa ya kuendelea kuomboleza bali kukumbuka hima yote mazuri aliyotufanyia wakati tukiwa nae hapa Duniani huku tukienzi yale aliyotuachia kupitia kitabu chake cha MY LIFE MY PURPOSE sawa sawa na kile cha Mzee  Mengi, I Can, I Must, I Will: The Spirit ofSuccess

Kiukweli naweza kusema Mzee Mkapa alikuwa ni “Role Model” wangu na mtu aliyenifanya niipende  kazi ya uandishi wa habari. Ni katika kipindi chake ndipo nilipopata msukumo wa kwenda kujiunga na chuo cha uandishi wa habari, nilihusudu sana na kuzipenda hotuba zake kila nilipozisikia nikawa nazirekodi kwa taperecorder yangu ndogo na kisha kuja kuzisikiliza baadae.

Kilichonifanya nimpende Mkapa kiasi hicho ni kauli zake za kuuchukia sana umasikini, kama ile, “Mtaji wa masikini ni nguvu zake mwenyewe”, maswala ya utandawazi pamoja na Sayansi na teknolojia. Rais Mkapa aliamini katika ukweli kwamba, UKITAKA KUMSAIDIA BINADAMU MWENZAKO, BASI MPATIE MSAADA UTAKAOMWEZESHA KUJISAIDIA YEYE MWENYEWE (Usimpe samaki bali mpe nyavu na mafunzo ya kuzitumia nyavu zenyewe) 

SOMA: Bilionea Dr. Reginald Mengi hakufa na siri yeyote moyoni, unajua siri zote alimwachia nani?  

Mkapa aliamini maendeleo yanaweza tu yakaletwa kwa njia za kisayansi na kiteknolojia jambo ambalo litabakia kuendelea kuwa kweli mpaka kesho. Namimi kama kuitikia na kuunga mkono juhudi zile za Mheshimiwa Mkapa sawasawa na vile watu wafanyavyo siku hizi kwa Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli, niliamua kwa udi na uvumba kuanzisha gazeti japo sikuwa hata na mtaji wa kuliendesha zaidi ya nguvu zangu mwenyewe kama mwenyewe Mkapa alivyokuwa akituasa Watanzania,kuwa “Mtaji wa masikinini nguvu zake mwenyewe”.

Katika kila toleo la gazeti langu hilo nilihakikisha natenga nafasi ya kutosha kwa ajili ya kuandika mambo mbalimbali ya kimaendeleo aliyokuwa akiyapa kipaumbele Mheshimiwa Rais Mkapa. Nakumbuka hata katika Toleo nililochapisha Makala hii ya Siri iliyojificha kipindi cha utawala wa Mkapa niliandika pia na Tahariri iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho, “MKAPA ALITUDANGANYA?”

Mkapa alitudanganya?


Niliweka pia safu maalumu ya UTANDAWAZI ambayo ilikuwa ni kwa ajili ya kuandika mikakati mbalimbali tu ya Kitaifa dhidi ya Umasikini na fursa za utandawazi. Safu hii niliweka zaidi nukuu mbalimbali muhimu za Rais Mkapa wakati huo kama utakavyoziona hapo chini.


Isitoshe kulikuwa na safu moja ukurasa wa mwisho wa 31 iliyoitwa, UKWELI KUHUSU UKIMWI, katika safu hii nilipenda sana kuweka nukuu za Rais Mkapa juu ya ugonjwa hatari wa Ukimwi kama hii hapa chini,

Kwa kifupi gazeti la SAYARI MPYA Sera yake kubwa ilikuwa ni kuandika masuala mbali mbali yahusuyo maendeleo katika mlengo wa Kisayansi na Kiteknolojia. Kazi yake kubwa ilikuwa ni kuamsha ari na moto wa maendeleo kwa vijana na Watanzania wote ili kujiletea maendeleo yao wenyewe bila ya kumtegemea ‘mjomba’ wala ‘shangazi’ kutoka nje, na maono haya sikuyatoa kwingine bali kwa Hayati Rais Mtaafu Benjamini William Mkapa.

SOMA: Hatimaye ile nyama ya kutengenezwa maabara yaanza kuliwa.

Nilikuwa kwa mfano naweza kuandika Makala inayohusiana na Safari za Warusi na Wamarekani anga za juu, lakini lengo langu kubwa hapo hasa likiwa ni kuonyesha jinsi Sayansi inavyoweza kufannya maajabu endapo tu itatumika vizuri na kwa malengo yaliyokusudiwa.
Makala nyingi kwa kweli zilikuwa ni za kusisimua sana mfano zile za Viumbe wa ajabu (UFO) kutoka sayari nyingie, Samaki Mtu(Nguva), Safina ya nuhu iliyosadikiwa kugunduliwa mlimani huko uturuki, Lugha ya ajabu na siri ilyopo ndani yake, Siri ya mtu aliyeishi miaka 122, na habari za Wagunduzi mbalimbali wa Kitanzania waliokuwa wamegundua vitu mbalimbali vya kiteknolojia  mfano mkazi mmoja wa Manzese aliyebuni jiko la kutumia mionzi ya jua kwa kutumia makaratasi ya sigara yanayotupwa ovyo mitaani na ‘Ford wa Tanzania’, mzee mmoja aliyebuni jiko linalotumia Oil chafu huko Arusha. Vyote hivi na mengineyo mengi vilichapishwa katika jarida hili kila mwezi.
SAMAKI MTU


Nakumbuka sana kipindi kile Rais Mkapa yeye kama mwandishi nguli wa habari na makini alikuwa akipenda sana kutuasa waandishi tusiwe wavivu, alichukia sana waandishi wanaoandika mambo pasipo kufanya utafiti wa kina na kubalance stori zao kiasi kwamba baadhi ya waandishi walimchukulia kama mtu asiyewapenda Waandishi wa habari wakati yeye mwenyewe ni zao la tasnia hiyo. Hata hivyo baadae tulimwelewa vizuri kwamba aliwapenda waandishi pale walipoonyesha kujituma na kuwajibika kitaaluma sawa na yeye mwenyewe alivyokuwa akiwajibika enzi zake akiwa mwandishi wa magazeti ya chama na serikali.

Kwa kweli hivi ndivyo na mimi ninavyoweza kuukumbuka mchango wa Hayati Rais Mtaafu Mheshimiwa Benjamin William Mkapa ambaye jina lake halitafutika kamwe katika vitabu vya historia ya nchi hii ya Tanzania, alifanya makubwa mengi ya maana ambayo pengine kwa bahati mbaya hatukuweza kuyaona kipindi kile akiwa madarakani na hata muda baada ya kuondoka madarakani lakini kidogokidogo tumekuja kutambua kumbe aliyoyafanya yalikuwa ni mambo makubwa ambayo pengine kama asingeliyafanya tusingelikuwa hapa tulipo leo hii.

SOMA: Seth Katende, Mwanaume utajiitaje bikira?

Ni kweli hakuna binadamu aliyekamilika duniani na Mkapa kama binadamu wengine naye hakosi kuwa na mapungufu yake japo ni vema tukayachukua tu yale mazuri na kuacha mapungufu kwani hata yeye mwenyewe aliwahi kukiri hivyo.

Naipenda kauli yake moja ambayo pia aliinukuu kutoka katika hotuba ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere siku za nyuma isemayo;

Kupanga ni kuchagua, kwenye kila hatua ya maendeleo yetu yapo mambo tunayoweza kwa wakati huo na yapo mengine ambayo hatuyawezi kwa wakati huo, na kwa kadiri nchi ilivyo masikini ndivyo ambavyo ilivyo vigumu kuchagua baina ya mahitaji ambayo yote yanaonekana ni muhimu- Benjamin William Mkapa.


0 Response to "SIRI ILIYOFICHIKA KIPINDI CHA UTAWALA WA MKAPA"

Post a Comment