SIRI KUBWA 2 ZA MAFANIKIO YA RUGE MUTAHABA CLOUDS FM: WENGI HATUKUZIJUA MPAKA ANAUMWA, KUFARIKI NA KUZIKWA LEO | JIFUNZE UJASIRIAMALI

SIRI KUBWA 2 ZA MAFANIKIO YA RUGE MUTAHABA CLOUDS FM: WENGI HATUKUZIJUA MPAKA ANAUMWA, KUFARIKI NA KUZIKWA LEO

Aliyekuwa Mkurugenzi wa vipindi na uzalishaji wa clouds fm Marehemu Ruge Mutahaba
Wakati redio ya Clouds fm inaanza mwishoni mwa miaka ya 90 kuelekea mwanzoni mwa miaka ya 2000 mtu angekuambia kwamba nyuma yake kulikuwa na kichwa cha “bwana mdogo” Ruge Mutahaba aliyekuwa katika miaka yake ya 20 usingeliweza kuamini kirahisi. Redio hii siri yake kubwa ya mafanikio ilikuwa ni mkakati kabambe waliokuja nao Ruge na mwenzake Joseph Kusaga wa kuliteka soko kubwa la vijana katika biashara ya burudani na habari kwa ujumla.

Joseph Kusaga akisimulia jinsi walivyokutana yeye na Ruge Mutahaba kabla hawajaanzisha Clouds aliwahi kusema hivi; “Ruge nimekutana nae miaka 22 or 23 iliyopita wakati huo ndiyo tulikuwa tunapiga disko na Ruge alikuwa wale watu wasiolala mpenda raha. Yeye alikuwa na mapenzi ya muziki na alikuwa mtoto wa kishua akija lazima umuweke pembeni umchunge ili wahuni wasimzingue….

SOMA: Utoke vipi kimaisha? Ruge anakupa fursa muhimu 10 hizi hapa.

Nakumbuka kipindi hicho hata kama ulikuwa mpenzi wa redio nyingine za wakati  huo, ilikuwa vigumu sana kujizuia kusikiliza Clouds fm kwa vionjo vyake vilivyokuwa na msisimko wa hali ya juu. Ujio wa redio hii ukawa ndio mwanzo pia wa mlipuko mkubwa wa muziki wa Bongo fleva, matamasha ya muziki na hata mashindano mbalimbali ya vipaji vya kuimba yaliyoratibiwa na clouds chini ya Ruge.

Binafsi kitu ambacho kamwe hakiwezi kunitoka akilini kirahisi ni baadhi ya Jingle za redio hii na matangazo mbalimbali ya biashara ambayo usingejua kama ni jingle au tangazo bali burudani ya aina yake. Jingle moja kwa mfano lililosisimua kiasi natamani hata leo wangelirudisha hewani ni lile lililosema hivi, “Sijalala mwanangu Utauwawa bure” Jingle hili lilimhusu jamaa mmoja dizaini kama vile alikuwa kibaka aliyemkuta mtu akisikiliza redio yake huku amelala akawa anainyatia ili amwibie ile redio kiulaini, lakini kumbe bwana yule hakuwa amelala usingizi aslani bali  alikuwa tu amepumzika akibembelezwa na mirindimo mwanana ya Clous fm. Ndipo  alipotaka kumuua na kumwambia yule kibaka, “SIJALALA MWANANGU UTAUWAWA BURE

SOMA: Una ndoto ya kufanikiwa? ungana na Ruge clouds TV saa 3 usiku kipindi kipya, ndoto za kitaa.

Kulikuwa na jingle pamoja na vionjo vingi vilivyogusa nyoyo za watu ile mbaya si hivi tu, nadhani clouds wangefanya kuwe na kipindi maalumu cha kukumbuka vitu hivyo kwa kuvipiga tena. Kulikuwa pia na Jingle moja hivi, jina la clouds lilikuwa likitajwa kwa sauti ya muungurumo mkubwa uliokuwa na msisimko wa aina yake wa kuvuta, “CLOOOOOOUDS FM
  Ruge Mutahaba enzi za Uhai wake.
Vitu vingine vya kusisimua ninavyokumbuka ni pamoja na kile kilichokuwa kipindi maarufu cha burudani nyakati za jioni kila siku cha AFRICAN BAMBATAA kilichokuwa kikirushwa hewani wakati fulani na mtangazaji Marehemu Amina Chifupa. Yalikuwa ni mapinduzi makubwa ya burudani yaliyokonga nyoyo za wasikilizaji kiasi kwamba kila mtu wazee kwa vijana waliupenda muziki wa Kiafrika. Ilikuwa ikifika jioni tu hakuna mtu aliyebadilisha stesheni zaidi ya Clouds fm.

SOMA: Seth Katende mwanaume utajiitaje Bikira?

Mapinduzi haya yote kumbe nyuma yake alikuwepo Marehemu Ruge Mutahaba kitu ambacho nimekuja kukijua siku hizi mbili tatu tangu ameondoka Duniani mpaka kuzikwa kwake leo na nadhani si mimi tu mwenyewe bali ni watu wengi walikuwa hawajui. Hata kama kuna watu walioandaa burudani na shughuli zote hizo kama vile wasanii na waigizaji mfano kina Mzee Onyango na Mwita, lakini imebainika kuwa kumbe Ruge mutahaba ndiye aliyekuwa MASTERMIND wa kila kitu.

(Siri kubwa 2) Ubunifu huu wa aina yake Ruge aliutoa wapi?
Watu wengi wanashindwa kujua kwamba Mafanikio huchangiwa na vitu vingi lakini kuna baadhi ya vitu ambavyo mtu ukiwa navyo na ukavifanyia kazi barabara mafanikio kwako litakuwa ni jambo la lazima. Lakini pia inawezekana mtu akawa na vitu vyote nitakavyovitaja lakini ikiwa kama hatachukua hatua yeyote hamna mafanikio yatakayotokea. Kwa hiyo hapa nitataja baadhi ya vitu muhimu Ruge alivyokuwa navyo kisha akajitambua mapema na kuvitendea kazi na bila shaka yeyote ile vikamfanya afike pale alipofikia kimafanikio katika taaluma yake na tasnia nzima ya habari na Burudani.

1. FURSA:
(Kipaji cha kutambua fursa haraka na kuitumia)
Kama watu walivyomuita mwenyewe kuwa ni mzee wa Fursa, Ruge Mutahaba tokea utoto wake hakuwa mtu anayechezea fursa hata sekunde moja. Kwanza fursa ya kwanza kuiona ilikuwa ni mazingira mazuri ya kupata elimu. Mtu kukuta baba na mama yako ni watu walio na mwamko wa elimu na pengine baba ni profesa kama ilivyokuwa kwa Mzee Gelasi Mutahaba baba yake na Ruge si kitu kidogo. Kwa mtu unayejitambua huwezi kufanya ajizi hata kidogo.

SOMA: Fursa zipo, chagua utakacho, tengeneza mpango, tekeleza na kufuatilia kwa uvumilivu utafanikiwa.

Ni vijana wangapi hukuta wazazi wao hata ni waalimu au wana nafasi kubwa tu lakini hujibweteka na kupuuzia kujiendeleza wao binafsi wakitegemea kuja kurithi mali za wazazi wao? Kwa Ruge hili lilikuwa ni tofauti kabisa na fursa yake ya kwanza kukamata ikawa ni elimu. Alisoma mpaka kupata shahada zake za Masoko na Fedha tena ughaibuni, Marekani. Hili lilimpa ujasiri mkubwa uliokuja kumsaidia sana baadae. Ukishakuwa na elimu kuna mambo mengi yatawezekana ambayo yasingeliwezekana kama hukuwa nayo.

Fursa nyingine aliyoitendea haki vilivyo ni ile ya soko lililokuwepo katika sekta ya habari na burudani wakati huo, aliweza kutambua haraka soko linataka kitu gani kwa wakati ule na akafanya vilevile soko lilivyokuwa linataka. Watu na hasa vijana walikuwa na kiu kubwa ya burudani, si kama hapo kabla burudani hazikuwepo hapana, ila watu hususani vijana walitaka mabadiliko, ubunifu zaidi siyo kitu kilekile miaka nenda rudi.

SOMA: Professa J: Historia ya muziki wa bongo Fleva, sisi ni wachonga barabara.

Na kwa kuwa mwenyewe alikuwa tayari ameshasomea maswala hayo ya Masoko(Marketing) tena katika ngazi ya digirii ndio maana tulishuhudia jingle na matangazo yaliyoenda shule kiasi kile, hivihivi tu yangelikuwa ni ya kawaida tu. Aliamini pia katika vipaji ndio maana utaona hata wafanyakazi wengi wa kampuni yake ni watu wenye vipaji vikubwa.


2. UTHUBUTU NA UJASIRI
Ruge alikuwa shupavu na mwenye tabia ya ujasiri mkubwa, ni wangapi hata leo hii wenye uthubutu wa kuunganisha nguvu na mtu/watu wengine kuanzisha kitu, kampuni au taasisi kwa maslahi yao wote wakavumiliana mpaka kufikia hatua ya juu kabisa? Wengi ushirikiano huvunjika kabla hata ya kwenda BRELA kusajili kampuni au biashara yenyewe. Ruge Mutahaba na Joseph Kusaga hili waliliweza na sasa miaka zaidi ya 20 ushirikiano wao umekuwa wa kuigwa na vijana wengi.
Ruge akiwa na Kusaga
Ijapokuwa binadamu huwezi kuwa mkamilifu kwa asilimia 100% Ruge katika harakati za kutimiza ndoto yake kuna baadhi ya watu wamemuona kama vile hakuwatendea sawa lakini kwa kweli kasoro hizo utakubaliana nami kuwa mema mengi aliyoyafanya yanafunika hayo yote. Hakuwa mbinafsi na alipenda kuona watu wengi zaidi wakifanikiwa kupitia vipaji vyao walivyokuwa navyo.

Tofauti na binadamu wengi, Ujasiri wa Ruge wa kuwasaidia na kuwapa watu wengine nafasi si kitu cha kawaida. Watu wengi husita kuwasaidia wengine au kuwaonyesha njia kwa hofu kwamba wakija nao kufanikiwa watawafunika au hawatakuja kuwajali na kuwaheshimu. Ruge hakujali hilo yeye aliwasaidia vijana wengi pengine kuliko kijana mwingine yeyote hapa Tanzania aliyepata mafanikio kama yeye. Alianini katika falsafa kwamba, dunia ilivyotapakaa fursa nyingi ni sawa na lilivyokuwa anga, anga ni kubwa mno hivyo kila nyota huweza kung'ara kwa kadiri itakavyo pasipo kuzuiliwa na nyingine.

SOMA: The sky is very wide, every star can shine (Mbingu ni kubwa mno kila nyota inaweza kung'ara)

Mtu yupo radhi amsaidie mtu mwingine akiwa kesha kufa kwa kumchangia pesa za jeneza lakini si akiwa hai, Ruge yeye badala yake aliwasaidia watu wakiwa hai, hakusubiri wafe ndipo aje atoe rambirambi mamilioni ya michango, na huu ni ujasiri mwingine mkubwa aliokuwa nao Ruge.

Mwisho, Ruge ana mengi vijana na hata makundi mengine ya watu wanaweza kujifunza kutoka kwake. Ijapokuwa amekufa kimwili lakini ataendelea kuishi nasi kwani alama aliyoiacha haiwezi kufutika kamwe. Mungu ailaze roho ya Marehemu Ruge Mutahaba mahali pema peponi Amina.      

0 Response to "SIRI KUBWA 2 ZA MAFANIKIO YA RUGE MUTAHABA CLOUDS FM: WENGI HATUKUZIJUA MPAKA ANAUMWA, KUFARIKI NA KUZIKWA LEO"

Post a Comment