MZEE REGINALD MENGI HAJAFA, ATAENDELEA KUISHI KATIKA ROHO ZETU SIKU ZOTE


Ikiwa sababu na chanzo cha kifo cha Reginald Mengi, mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, tajiri na mfanyabiashara mashuhuri bado kujulikana rasmi kila mtu nchini Tanzania na nje ya nchi ana tashwishi ya kutaka kujua ugonjwa uliomuua mzee Mengi, ni nini hasa kilichomsibu Mzee huyu aliyekuwa mmiliki na mwenye mchango mkubwa katika tasnia nzima ya vyombo vya habari na viwanda kwa ujumla.

Ni takriban miezi miwili tu imepita tangu Mzee Mengi ahutubie katika shughuli ya kumuaga Ruge Mutahaba ‘kijana wake’, na mtu mwingine aliyekuwa na umuhimu mkubwa katika tasnia ya habari na biashara kwa ujumla nchini Tanzania. Katika hotuba yake Mzee Reginald Mengi alisema kuwa Ruge Mutahaba hakuwa amekufa bali anaendelea kuishi na sisi Kiroho.

Kwa hiyo kama ilivyokuwa kwa kauli yake hiyo, Watanzania hatuna budi kukubali ukweli huo kwamba Mzee Reginald Mengi hajafa, tunaishi naye kupitia maono yake mbalimbali aliyotuachia katika kazi zake zote kikiwemo kitabu chake cha I CAN I WILL IMUST.  Kilichokufa ni mwili wake tu au “Kasha” kama alivyosema yeye mwenyewe kwenye hotuba hiyo iliyonukuliwa yote hapa chini;

   
Bwana asifiwe, Assalaam Alaykum,
Ndugu zangu mimi sina mengi ya kuzungumza, nimekuja hapa kumuaga kijana wangu aliyeitwa na Bwana Mungu. Lakini nina habari njema kwenu, habari yenyewe ni kwamba Ruge hajafa kwasababu roho haifi, na mtu ni roho. Mwili ni kasha tu la roho. Tutazika mwili wake lakini hatutazika roho yake. Mkumbuke kwamba tuliumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na Mungu anatupenda sana.

Kwa hiyo nimesema kwamba kilichokufa ni kasha tu la Ruge siyo roho yake. Kwahiyo Ruge bado anaishi na siku moja atakuja kwenu kufahamu kwa kweli anaishi. Kwahiyo unakufa tu wakati  roho imekufa, lakini roho haifi. Na Ruge ataendelea kuishi mahali pawili(makao mawili) Ataendelea kuishi kwa Baba Mungu na katika roho zetu kwasababu alitupenda na tulimpenda. Kwa hiyo makao ya kwanza yatakuwa ni Mbinguni na ya pili katika roho zetu Wanadamu.
Mimi Ruge alikuwa kijana wangu, muungwana sana, He was a true Human Being ambaye alikuwa na upendo, na vijana wengi Tanzania wamefaidika sana kuishi kwa Ruge. Amewapa matumaini, na katika tasnia ya habari ameleta mabadiliko makubwa sana na mengine leo hamtafahamu lakini aliyaleta.


Naweza nikasema kwamba sisi badala ya kulia kama alivyosema Ruge, tusherekee, tufurahi naye. Badala ya kulia tumuombee ili roho yake ilale mahali pema Mbinguni. Ningependa kuwapa pole wote sana, wazazi, ee.. Kusaga na vijana wengine na Mungu naomba tu awape Moyo wa kuzidi kumuombea. Mkae kwa Amani ya Bwana. ASANTENI.

Chanzo cha habari hii ni Video kutoka AZAM TV, ukitaka kuangalia video hiyo bonyeza hapo.     

0 Response to "MZEE REGINALD MENGI HAJAFA, ATAENDELEA KUISHI KATIKA ROHO ZETU SIKU ZOTE"

Post a Comment