Bilionea DR. Reginald Mengi hakufa na siri yeyote moyoni, unajua siri zote alimwachia nani? | JIFUNZE UJASIRIAMALI

Bilionea DR. Reginald Mengi hakufa na siri yeyote moyoni, unajua siri zote alimwachia nani?

Ni takribani miaka saba 7 sasa imepita tangu niandike kitabu changu kijulikanacho kama MIFEREJI SABA YA PESA NA SIRI MATAJIRIWASIYOPENDA KUITOA. Kitabu hiki wakati huo kiliwasisimua watu wengi sana ukizingatia ukweli kwamba kabla ya hapo na hasa siku za nyuma kulikuwa na usiri mkubwa juu ya maisha na hata historia za utajiri wa watu mbalimbali.


Matajiri wengi nchini Tanzania hawakupenda kabisa mambo yao kujulikana hadharani na pengine waliogopa kufanya hivyo, si ajabu Tanzania kwa kipindi kirefu tumekuwa na Mabilionea wengi tu bila ya kujulikana mpaka pale jarida mashuhuri la FORBES walipoanza kuja kuwafuatilia na kuwaweka wazi mabilionea wa mwanzo mwazno wakiwamo kina Dr. Reginald Mengi, Said salim Bakhressa, Mohamed Dewji, Alli  Mafuruki na Rostam Azizi.
MAREHEMU MZEE REGINALD MENGI, SAID SALIM BAKHRESA NA MOHAMED DEWJI
KITABU: MIFEREJI 7 YA PESA NA SIRI MATAJIRI WASIYOPENDA KUITOA
Inawezekana kulikuwa na sababu kadhaa zilizowafanya matajiri wengi kutokupenda habari zao ziwe hadharani sana na kubwa ikiwa ni ile ya nchi yetu kuwa katika mfumo wa KIJAMAA wakati ule lakini kusema ule ukweli baadhi yao na hasa Mzee wetu Reginald Abraham Mengi yeye hakuogopa kabisa kuweka mambo yake hadharani tokea mwanzoni kabisa na hii ndio iliyonipa motisha mkubwa kabisa wa kukiandika kitabu hicho baada ya kuona kwamba Dr. Mengi na baadhi ya Matajiri hao walikuwa wameshaanza kuwa na moyo ule wa kujiweka wazi.

SOMA: Vijana wanaosubiri mifumo iliyowekwa iwasaidie kujikwamua kiuchumi wataendelea kubaki kuwa watumwa wa maamuzi ya watu wengine - Dr.Mengi 

Tokea miaka ya 90, 1992, 1993 na kuendelea Dr. Reginald Mengi alikuwa tayari amekwishaanzisha matamasha ya kuwahamasisha watu hasa vijana kujiunga katika vikundi na kuanzisha makampuni mbalimbali huku yeye binafsi akiwapa kianzio cha fedha taslimu pamoja na kuwatia moyo wa hali ya juu kabisa kama vile kuwahamasisha kwa kaulimbiu zake maarufu za, “ MSIOGOPE KUKOPA" “KAMWE USILOGWE UKALA PESA YA MTAJI” “USIKATE TAMAA” “MSIOGOPE CHANGAMOTO” “PENYE CHANGAMOTO NDIPO PALIPOKUWA NA FURSA” nk.

SOMA: Mengi, "Nilianza sina kitu niliona fursa nikakopa fedha, nikaanza kufanya biashara"

Hamasa hiyo kubwa ilinifanya hata katika Dibaji ya kitabu changu hicho cha MIFEREJI 7 YA PESA kuamua kuandika kama ifuatavyo;

SHUKRANI
Kwa Wazee wangu na washauri, Reginald Mengi na Said Salim Bakhresa pia na kwa kijana mwenzangu Mohamed Dewji, kwa mioyo yao iliyojaa ukarimu, watu hawa kusema ukweli walinifanya nipate hamasa na msukumo mkubwa katika kukiandika kitabu hiki. Kama wangelikataa taarifa zao zisisambazwe na vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo Forbes, sifikiri kama ningeliweza kukiandika kitabu hiki kwa jinsi nilivyokiandika. Mchango wao katika kuhamasisha kuukataa umasikini kwa vijana wa Kitanzania na hata makundi mengineyo katika jamii kwa hakika ni mkubwa kushinda hata kama ambavyo wangeliamua kuwagawia pesa mkononi. 

Shukrani pia ni kwa wafanyabiashara wengine waliotajwa katika kitabu hiki, Rostam Aziz na Ali Mufuruki, na wao pia kama walivyo hao watatu niliotangulia kuwataja, wangeliamua kufanya utajiri wao kuwa siri, watu tusingeliweza kuwajua na kupata hamasa kubwa kutoka kwao, wamekuwa pia mifano ya kuigwa(mentors) kwa Watanzania wengi. Mwisho lakini kwa umuhimu ndiyo wa kwanza, ni kwa familia yangu pendwa, kwa uvumilivu wao ambao muda wote wamekuwa wakiuonyesha kwangu ninapokuwa nikifanya kazi hii ya uandishi hata pale ninapokuwa nikiifanya pasipo kuwa na uhakika wa malipo mazuri.

Na kwa kweli tangia miaka hiyo sasa tumeshuhudia Matajiri wengi wakiweka wazi siri zao, siri hizo nilizokuwa nikimaanisha hapa si nyingine kama wengi walivyodhania bali ilikuwa ni mbinu mbalimbali za mfafanikio. Mtu aliyefanikiwa anapoamua kuwashika mikono watu wengine kwa hali na mali hasa kwa kuwapa njia za wao  pia kufika mbali hata kama siyo pesa taslimu mikononi, hiyo inatosha kabisa kusema kwamba mtu huyo amekubali kutoboa siri zake za mafanikio na kuwapa watu wengine nao wafanikiwe kama yeye au tu hata waweze kuishi maisha yaliyokuwa na unafuu badala ya kuishi maisha ya umasikini uliotopea.


MZEE MENGI SIRI ZA UTAJIRI WAKE ALIMWACHIA NANI? JE NI MKEWE JACQUELINE, WANAWE, ABDIEL NA REGINA, MAPACHA WAKE 2, AU WALINZI WAKE?

Siri za utajiri wa Dr. Reginald Mengi kusema ukweli hajaanza kuzitoa leo, jana wala juzi, kama nilivyotangulia kusema Dr. Reginald Mengi alikuwa ni mtu muwazi aliyeamini katika Sera za KILIBERALI, jambo lililosababisha hata kutokueleweka vizuri wakati huo na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

SOMA: Mzee Reginald Mengi hajafa, ataendelea kuishi katika mioyo yetu siku zote

Uliberali tofauti na ulivyokuwa Ujamaa, sera zake ni za soko huria, huna haja ya kujifichaficha ilimradi tu huvunji sheria za nchi na wala humdhulumu mtu tofauti na vile ilivyo kwa Ujamaa ambao, unahubiri vizuri usawa wa binadanu wote lakini nyuma ya Pazia kwa kuwa wanadamu tuna silika ya umimi, ubinafsi na uchoyo basi dhana hiyo inakuwa ngumu kweli kutekelezeka, na hatimaye kunaibuka wajanja wachache humohumo kwenye ujamaa wanaojinufaisha kwa migongo ya wavujajasho walio wengi.

Hili lilikuja kujidhihirisha pale Ujamaa aliouanzisha Mwalimu Nyerere kwa nia njema tu kuja kuanguka miaka ya 80 na Soko huria kushika kasi yake mwanzoni mwa miaka ya 90. Hivyo nilitaka tu kuweka wazi umuhimu wa Ukweli na Uwazi katika maswala ya kiuchumi jambo ambalo Mzee Reginald Mengi amekuwa akilihubiri tangia miaka ya 70 mpaka hivi leo tunapomuaga rasmi kwa safari yake ya mwisho.

SOMA: Dr. Mengi atoboa siri za biashara.

Ukitaka kufahamu kwa kina falsafa hii ninayojaribu kuizungumzia hapa leo, nakushauri tu kukisoma kitabu alichotuachia kama zawadi Marehemu Mzee Reginald Mengi, I CAN, I MUST, I WILL The spirit Of Success sehemu pekee ambamo Dr.Mengi ndimo alipoacha SIRI zake zote nzito za mafanikio. Siri hizo hajamwachia mtu mwingine yeyote yule, si mkewe kipenzi Jacqueline Ntuyabaliwe aliyempenda sana wala wanaye, Regina, Abdiel, mapacha wake 2, wala si walinzi wake, wapishi wala mfanyakazi mwingine yeyote yule ndani ya kampuni lake kubwa la Industrial Projects Promotion(IPP). Ni ndani ya I CAN, I MUST, I WILL The spirit Of Success, kitabu atakachokumbukwa nacho milele.

............................................................

Kupata vitabu vya Self Help Books Tanzania katika lugha ya kiswahili tembelea, SMART BOOKS TANZANIA

Kujiunga na MASTER MIND GROUP la MICHANGANUO-ONLINE, mahali ambapo watu makini hujifunza na kushirikishana mambo mazuri kila siku lipia kiingilio sh. elfu 10 kisha tuma ujumbe WASAP wa "NIUNGANISHE NA GROUP LA MASOMO"  kwa namba, 0765553030

0 Response to "Bilionea DR. Reginald Mengi hakufa na siri yeyote moyoni, unajua siri zote alimwachia nani?"

Post a Comment