MADHEHEBU YA KIKRISTO WASIOSHEREKEA SIKUKUU YA KRISMASI NA SABABU KUBWA YA KUTOADHIMISHA | JIFUNZE UJASIRIAMALI

MADHEHEBU YA KIKRISTO WASIOSHEREKEA SIKUKUU YA KRISMASI NA SABABU KUBWA YA KUTOADHIMISHA

sikukuu ya Krismasi

*Kama mtafiti wa maswala mbalimbali ya kijamii, makala/Mjadala huu ulio na maudhui ya kidini nimeandika kwa lengo la kuhabarisha na wala siyo ushabiki, ikiwa kwa namna yeyote ile utakwazika na yaliyoandikwa humo basi natanguliza samahani halikuwa lengo langu kukwaza mtu yeyote.

Sikukuu ya kuadhimisha kuzaliwa kwa Yesu Kristo mtu anayeaminika na waumini  wa dini ya Kikristo kuwa ndiye mwokozi wao imekuwa ikiadhimishwa kwa karne nyingi lakini sikukuu hii historia yake inaaminika kuanzia karne ya 3 baada ya Yesu mwenyewe kuishi hapa duniani na hakuna kumbukumbu yeyote rasmi katika kitabu kitakatifu cha Biblia kwamba iliwahi kuadhimishwa na Wakristo wa mwanzo isipokuwa tu Biblia inachotamka ni tukio lenyewe la kuzaliwa, haitaji siku, mwezi wala tarehe ya tukio hilo.

SOMA: Nyimbo nzuri za Krismasi zinazopendwa zaidi na siri kubwa 2 zilizojificha ndani yake.

Historia ya vikundi na Madhehebu ya Kikristo duniani haiwezi kukamilika pasipo kutaja pande kuu tatu, Ukristo wa Magharibi(Wakatoliki), Ukristo wa Mashariki(Waorthodox) na Waprotestant(Wale wote waliopingana na matawi hayo makuu mawili). Baada ya Yesu kuondoka duniani pamoja na Wanafunzi wake(Mitume 12) wale waliobakia kuuendeleza Ukristo kwa nyakati tofauti walitofautiana kama ilivyokuwa kwa dini na imani nyinginezo zozote zile duniani anapokuwa ameondoka yule aliyeanzisha.

Upande wa wale wanaosherekea Krismasi.

Krismasi chimbuko lake ni katika Ukristo wa Magharibi na Mashariki huko Ulaya na ndio maana utakuta siku hizi wote Wakatoliki na Waorthodox wanaadhimisha Sikukuu ya Krismasi ingawa pia wanatofautiana kidogo tarehe na mwezi, wakati Wakatoliki na baadhi ya Wakristo wengine wa Magharibi wakiadhimisha Krismasi tarehe 25 Desemba Waorthodox wa Mashariki wao huiadhimisha Mwezi January tarehe 7. Tofauti hii hutokana na Magharibi kutumia kalenda ya Kigregori(Gregorian calendar) wakati Mashariki wao hutumia kalenda ya Kijuliani (Julian calendar)

SOMA: Heri ya siku ya kuzaliwa mr. Peter Augustino Tarimo

Sababu kubwa inayotolewa na makundi haya yanayoadhimisha Krismasi pamoja na kwamba Biblia imekaa kimya juu ya sikukuu hiyo ni kuwa, tukio hili wao hasa wanachozingatia zaidi ni maudhui au maana ya tukio lenyewe lililotokea kweli na wala siyo siku wala tarehe yenyewe. Wanadai hata kama biblia haitamki wazi Yesu Kristo alizaliwa siku gani lakini hiyo haiwezi kufuta ukweli kwamba Yesu Kristo alizaliwa kweli huko Bethlehemu ya Uyahudi. Suala la kukumbuka jambo mtu unaweza ukakumbu siku yeyote ile na wala si lazima iwe ni tarehe ileile tukio lilipotokea. Wangeweza hata kukumbuka katika tarehe nyingine yeyote ile au mwezi wala isingelikuwa tatizo.


Sasa basi kwanini waadhimishe siku inayodaiwa kuwa ilikuwa ni sikukuu ya kipagani ya kuzaliwa kwa Mungu jua?

Huko Ulaya hasa Ulaya ya Magharibi enzi Ukristo unaingia huko watu walikuwa na dini zao za asili kama tu ilivyokuwa huku Afrika Wakoloni walipoingia na ilikuwa vigumu sana kuwabadilisha watu waamini Ukristo na moja ya mbinu zilizotumika ni pamoja na kubadilisha matukio ya kipagani kuwa ya Kikristo.

Kuna ubaya gani ikiwa siku watu waliyokuwa wakiamini Mungu wa uwongo badala yake ikafanywa kuwa siku ya kumuamini Mungu wa kweli?. Hivi ndivyo ilivyokuwa watu badala ya kuendelea kuamini siku ya kuzaliwa Mungu Jua wa uwongo wakafundishwa waamini kuzaliwa kwa Yesu Kristo aliyetumwa na Mungu Kuwaokoa. Hivyo pamoja na dhamira hiyo nzuri lakini bado watu hawakuweza kuacha moja kwa moja desturi walizokuwa nazo wakati wa hizo sherehe za kipagani mfano kupeana zawadi, miti ya krismasi nk. ndio maana mpaka sasa hivi desturi hizo zimeendelea kuwepo.

SOMA: Mji wa kale Ukristo ulipoanzia washambuliwa vikali. 

Kwa sababu hizo Wakristo wa madhehebu ya Kikatoliki, Waorthodox na hata wengi wa madhehebu ya Kiprotestant mfano Waanglikana, Walutheri, na makundi mbalimbali ya kilokole wameendelea kuona hakuna sababu ya msingi ya kuipinga Krismasi ilimradi tu dhamira yake kuu ni kukumbuka tukio kuu la Imani yao la kuzaliwa Yesu Kristo kama biblia inavyosema ingawa tarehe siyo muhimu.

Wanajitetea dhidi ya wale wanaopinga kuwa wako sahihi kwani hata kama Yesu mwenyewe angekuja leo asingeliweza kukasirika kwa watu kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa ilimradi tu wana nia safi. Wanaendelea kujitetea kwa kusema kuwa hata hao wanaopinga ni wanafiki kwani suala la mapokeo katika imani yeyote ile haliwezi kuepukika wakitolea mfano kwamba hata Biblia yenyewe Kitabu kitakatifu nyakati za kanisa la mwanzo hakikuwa kama kilivyokuwa sasa, maandishi yalikuwa yamechapwa katika magome ya miti na ngozi za wanyama.

SOMA: Vitabu chanzo cha maendeleo na mafanikio makubwa ya binadamu Duniani.  

Mbona sasa hao wanaojidai kupinga mapokeo ya aina yeyote ile mbali na yaliyoandikwa kwenye biblia wasikatae na kutumia biblia iliyochapishwa kwenye karatasi na kurudia kuendelea kutumia biblia zilezile zilizokuwa zimechapwa kwa ngozi, magome ya miti na katika miamba? Hawaoni kuwa ni mapokeo kutumia kitu tofauti na walichotumia wakristo wa mwazo?.

Si hivyo tu, Teknolojia nyingi ni mapokeo kutoka kwa watu mbalimbali na wengine walioziasizi hata hawako katika imani ya kikristo, ingetegemewa basi hata na vitu kama intaneti, kompyuta, simu na hata magari yanayotumia injini kuwa haramu kabisa kwa watu hao wapinzani kwani enzi zile za kanisa la mwanzo vitu hivyo havikuwepo na wala hamna mahali kwenye biblia palipoandikwa habari za intaneti na simu zije kutumiwa kueneza injili. Iweje sasa leo wajiongeze kuvitumia vitu hivyo katika kueneza imani yao, haya si mapokeo? Au ni kutaka tu kutafuta uhalali na sababu ya kujitofautisha na makundi wanayoyahama? Kwanini wasitumie ngamia, punda na miguu kuzunguka dunia nzima kama walivyofanya mitume 12 wa Yesu?

SOMA: Mbinu mpya za kufanya mambo Dunia, biashara ,ajira vinabadilika kwa kasi ya ajabu.

Wanaenda mbali zaidi kwa kusema hata wale Mitume walioandika Injili ya Yesu wenyewe hawakuweza kuandika neno kwa neno kila kitu kama Yesu alivyotenda sembuse ije kuwa mambo madogo kama kukumbuka kuzaliwa kwa Yesu, wanatolea mfano kwamba Injili za Luka Mathayo na Marko ingawa maudhui ni yaleyale lakini kuna tofauti kubwa katika lugha na maneno waliyotumia kuwasilisha ujumbe hivyo siyo kweli kwamba mapokeo hayawezi kabisa kukubalika katika kanisa lenye umri zaidi ya miaka 2000 linalopitia mabadiliko makubwa Kijamii, Kiteknolojia, kimuundo, kimtazamo na hata Kiuchumi.

Orodha kamili ya Madhehebu yanayosheherekea sikukuu ya Krismasi.

·       Wakatoliki
·       Waordhodox
·       Waanglikana
·       Waprotestant wengi wakiwemo wa makanisa ya Kiinjili ya Kilutheri, Wapentekoste, Moravian, Menonite nk.

Upande wa wale wanaopinga kusherekea sikukuu ya Krismasi.
Katika makundi 3 niliyoyataja ya Wakristo ni asilimia ndogo sana wanaopinga Krismasi. Na wengi wao wanatokea katika kundi la Kiprotestant wale wapinzani wakubwa wa Ukatoliki na Uorthodox. Taratibu na desturi nyingi za Wakatoliki na Waordhodox karibu ni sawa isipokuwa tu wanatofautiana kwenye Uongozi mkuu wa Kanisa kila mmoja akiwa na kiongozi wake mkuu(Papa). Waprotestant wanatofautiana na hao 2 kuanzia Uongozi mpaka mafundisho makuu ya kanisa hata na mafundisho mengine yaliyokuwa na msingi wake katika Kitabu Kitakatifu cha Biblia.

Vikundi vya Kiprotestanti ukiacha vile vikubwa kama Walutherani na Wapentekoste vipo vingi sana ingawa idadi ya kila kikundi ni ndogo, wingi huu unatokana na kila siku kuibuka tofauti ndogondogo za kimafundisho, mtu akitofautiana kidogo tu na kanisa alilopo huhama na kwenda kuanzisha kikundi chake. Sababu hizi ndizo zilizosababisha baadhi yao kutokusherekea Krismasi.

SOMA: Alichofanya mwimbaji huyu wa Injili  unakijua?

Unaweza kukuta vikundi vingine wao kujimega kutoka madhehebu yao ya mwanzo sababu kubwa ilikiwa ni Krismasi tu, wengine ni Kuabudu siku ya Jumapili tu nk. Tofauti ziko nyingi kulingana na jinsi kila mtu anavyoweza kuisoma na kuielewa Biblia kivyake, na wote wanaojimega hawawezi kukosa kifungu kwenye Biblia kinachotetea madai yao kama tu ilivyo kwa upande wa pili nao usivyoweza kukosa kifungu cha kutetea msimamo wao katika Biblia hiyohiyo. Vikundi vingi vinavyopinga Krismasi havikuanza siku nyingi, vingi ni kuanzia Karne ya 18

Madai yao makubwa.
Madai makubwa ya wanaopinga Krismasi ni kwamba, Kwanza Krismasi haipo mahali popote pale katika Biblia bali ni mapokeo tu ya imani za kipagani, tarehe kamili ya Krismasi siyo 25 Desemba kwani biblia iliandika kwamba Bikira Mariamu alipopewa habari za kumzaa Yesu ulikuwa ni mwezi wa 6 na hivyo isingewezekana mimba kukaa miezi 6 pekee mpaka kujifungua na hata majira yanayotajwa kwenye biblia kuwa ilikuwa ni kiangazi ni tofauti kabisa kwani mwezi Desemba Bethlehemu kuna baridi na theluji kali.

SOMA: Mungu hutenda kwa namna ya ajabu sana.

Sababu nyingine ni Watu kufanya ibada za kipagani na matendo yasiyompendeza Mungu wanaposherekea sikukuu ya Krismasi mfano kulewa, ulafi, starehe za kila aina, kupeana zawadi, kuabudu sanamu kwa kutengeneza vijumba mfano wa hori la mifugo alimozaliwa Yesu Kristo.

Madai yao makubwa ni kwamba ikiwa Yesu Kristo angelishuka leo hii angekasirika sana kukuta watu wakiabudu vitu ambavyo hakuamuru viandikwe kwenye kitabu chake Kitakatifu tena kwa namna inayomchukiza mno baba yake, ulevi na matendo mengi maovu. Tena wanaenda mbali zaidi kwa kutaja vifungu mbalimbali kwenye biblia vinavyokataza kuabudu Miungu na sanamu za kujichongea. Wanakataa kata kata mapokeo ya aina yeyote yale yanayoenda kinyume na yale yaliyoandikwa katika kitabu Kitakatifu cha Biblia. Wanadai Mkristo ni lazima aishi kulingana na muongozo wa Biblia Takatifu neno kwa neno na haitakiwi kabisa kutenda jambo hata moja lililokuwa nje ya kitabu hicho.

Vikundi hivi vingine hata vimefikia hatua ya kukataa kutambua sherehe au sikukuu za aina yeyote ile nyingine zaidi ya ile ya kufa kwa Yesu(Ijumaa Kuu), wanapinga kuanzia sikukuu za kuzaliwa(Birthdays), sikukuu za kiserikali na sherehe nyingine zote za kidini na kitaifa wakidai kufanya hivyo ni kuabudu Miungu na sanamu.  

Vikundi na Madhehebu ya Kikristo yanayopinga kusherekea sikukuu ya Christmas

·       Mashahidi wa Yehova
·       Waadventist Wasabato
·       Union Church of God (UCG)
·       Kanisa la Kibaptist la Magharibi(Westboro)
·       Baadhi ya Makanisa mengine mengi madogomadogo  yenye watu kuanzia 1 na kuendelea.

Mpendwa msomaji wangu kama ulivyoona katika mjadala huu mimi sina upande wowote, nimejitahidi kwa kadiri ya uwezo wangu kuwasilisha tu ukweli ulivyo kulingana na taarifa kutoka vyanzo mbalimbali, nisingelipenda unihusishe na upande wowote ule. Ikiwa wewe ni mshabiki wa upande fulani ni uamuzi wako mwenyewe. Kikubwa hapa kwa mujibu wa jukumu langu mimi ilikuwa ni kutoa tu taarifa(kuelimisha jinsi mambo yalivyo) kulingana na msimu wenyewe kuwa wa Krismasi.

................................................................

Karibu katika Group letu la masomo la Michanganuo-online kwa masomo kila siku ya fedha na michanganuo ya biashara kwa kiingilio cha shilingi elfu 10 tu unakuwa mwanachama wa kudumu. Mawasiliano ni, Wasap 0765553030 au simu 0712202244

Unaweza pia kujipatia vitabu vyetu hapa; Smartbookstz

0 Response to "MADHEHEBU YA KIKRISTO WASIOSHEREKEA SIKUKUU YA KRISMASI NA SABABU KUBWA YA KUTOADHIMISHA"

Post a Comment