HEBU SOMA ALICHOKIFANYA MUIMBAJI HUYU WA INJILI OBADIA ALEX | JIFUNZE UJASIRIAMALI

HEBU SOMA ALICHOKIFANYA MUIMBAJI HUYU WA INJILI OBADIA ALEX

Siyo jambo la kawaida kwa blogu hii kuandika habari/makala zinazohusiana na maswala  ya imani, isipokuwa tu pale suala lenyewe linapokuwa linahusiana na ujasiriamali moja kwa moja, hivyo ndugu msomaji unayesoma hapa,ikiwa pengine wewe siyo wa imani ya Kikristo tafadhali usikwazike kwa kufikiri pengine labda tuna nia ya kujaribu kutaka kukubadilisha imani uliyokuwepo. 

Tunaandika jambo lolote lenye maudhui ya ujasiriamali hata likiwa lina uhusiano na dini gani, kifupi hatubagui watu kwa msingi wowote ule na tunaheshimu dini na imani zote hapa Duniani zinazomtaja Mwenyezimungu.

Tukirudi kwenye mada yetu ya leo, kuhusiana na Mchungaji huyu, Obadia Alex, ambaye pia ni muimbaji wa nyimbo za injili, kuna jambo moja ambalo niliona ni vizuri wajasiriamali wakajifunza kutoka kwake, jambo lenyewe halihusiani kabisa na imani yake bali na biashara yake ya kuuza DVD na CD za nyimbo anazoimba.

Bwana huyu nimewahi kumuona mara nyingi tu maeneo ya Buguruni sheli, sokoni na hata maeneo ya Rozana akiwa na kigari chake cha tairi mbili, mfano wa mkokoteni wa kubebea vitu, akiusukuma na huku ikisikika sauti kubwa ya nyimbo za injili ambazo zinapigwa na dvd player iliyokuwa ndani ya mkokoteni huo. Ndani ya mkokoteni huohuo  kuna jenereta ya umeme inayotumika kuendeshea mitambo yake hiyo ambayo pia kuna kipaza sauti anachotumia kutoa matangazo mbalimbali sambamba na muziki huo.

Muimbaji wa nyimbo za injili, Obadia Alex
Matangazo anayoyatoa yana ujumbe unaohamasisha watu wanunue CD yake iliyokuwa na nyimbo kumi, ukiwamo wimbo maarufu na ambao ndio huutumia zaidi kuuzia cd hiyo uitwao “MAMBO MAGUMU” pamoja na wimbo wa kwanza uliobeba albamu unaoenda kwa jina la “WEMA WA BWANA”.  Sina uhakika kama huwa anatembea maeneo yote ya jiji la Dar, na nilipanga nimuombe kufanya naye mahojiano lakini nilipokutana naye nikanunua CD hiyo ilikuwa usiku saa 1 pale sheli, na sikuweza kumsimamisha muda mrefu.

Nilichojifunza kutoka kwa Mjasiriamali huyu na ambacho kilinisukuma kuandika makala hii kusudi na wengine nao waweze kujifunza ni “UBUNIFU”. Kwa kweli kijana yule anastahili kuitwa mbunifu kwani staili ile ya kuuza kanda ama tuseme CD ni ya kipekee. Sijawahi kumuona mtu mwingine anauza kazi yake mwenyewe ya sanaa hasa katika upande huu wa muziki na video kwa mtindo ule, inawezekana wapo lakini  hawatakuwa wengi.

Nadhani changamoto nyingi wanazokumbana nazo wasanii wachanga ndizo zilizomsukua akaweza kubuni njia hiyo, wasanii wengi wachanga hulalamika mara nyingi kazi zao kuuzwa nakala nyingi na wale wanaozisimamia huku wakiwalipa kiasi kidogo kisicholingana na nakala zilizouzwa.


Ijapokuwa njia anayoitumia inaweza ikawa, ngumu, ndefu na itakayomchukua muda mwingi, lakini anao uhakika wa kurudisha gharama zake alizotumia wakati akiandaa kazi yake. Nimewahi kuona wasanii kadhaa walioamua kuuza kazi zao wenyewe lakini hawakutumia “approach” kama ya huyu bwana, Wengi huzunguka nazo mitaani wakiwa wamezishika tu mkononi, sasa wateja hawawezi kupata nafasi ya kusikiliza kile kilichokuwemo ndani ya CD hizo zaidi ya kuona picha iliyokuwepo juu ya kasha la CD au DVD.

Mbali na kuwa na uhakika na mapato yatokanayo na kazi yake, msanii huyu pia atakuwa na uwezo mkubwa wa “kucontrol”(kudhibiti) biashara yake, hawezi kupata ‘stress’ zisizokuwa na msingi na hali hii ya uthibiti, ni muhimu mno  hasa katika ngazi ya kuanza biashara kwani mjasiriamali anakuwa bado mtaji wake ni mdogo na hivyo changamoto ndogondogo tu zinakuwa na uwezo mkubwa wa kuidumaza biashara au hata kuiua kabisa ikiwa hana udhibiti wa kutosha na kila mazingira yanayohusiana na biashara yenyewe.

Ikiwa  kwa mfano(siyo idadi halisi anayouza)  anao uwezo wa kuuza hata nakala 5 tu kwa siku, anao uhakika wa kupata 5×5000  = 25,000/-, na fedha hizi anazipokea taslimu (cash) pasipo kupitia sijui kwa wakala wala nani.

Sikiliza na kuangalia nyimbo zake hapa chini;

MAMBO MAGUMU(VIDEO)

0 Response to "HEBU SOMA ALICHOKIFANYA MUIMBAJI HUYU WA INJILI OBADIA ALEX"

Post a Comment