VITABU: CHANZO CHA MAENDELEO NA MAFANIKIO MAKUBWA YA BINADAMU DUNIANI | JIFUNZE UJASIRIAMALI

VITABU: CHANZO CHA MAENDELEO NA MAFANIKIO MAKUBWA YA BINADAMU DUNIANI

Kitabu cha zamani kuliko vyote duniani
Kitabu cha zamani kuliko vyote duniani.

Hebu jaribu kuirudisha akili yako nyuma miaka kama 25 hivi iliyopita na linganishe na wakati huu tuliokuwa nao katika suala zima la kujipatia maarifa ya aina mbalimbali. Bila shaka utagundua kwamba miaka hiyo ya nyuma ilikuwa mtu ukihitaji maarifa ya namna yeyote yale basi ni sharti uyapate aidha kwa kusimuliwa kwa mdomo au kwa kuyasoma mahali hususani kutoka katika vitabu mbalimbali. Hizo ndiyo zilizokuwa njia kuu za kujipatia maarifa.Tunaporudi nyuma zaidi kihistoria, utaona kwamba miaka hata kabla ya kuzaliwa Yesu Kristo, njia kuu iliyokuwa ikitumika kuhifadhi maarifa ya aina yeyote ile iwe ni ya kidini, kisayansi, kitabibu, kifasihi na hata kijamii  ilikuwa si nyingine bali ni kwa njia ya maandishi na picha ambavyo vilihifadhiwa katika mfumo wa vitabu na vitabu vyenyewe haijalishi vilitengenezwa kwa aina gani ya karatasi, wakati mwingine yalitumika mawe, ngozi, vipande vya mifupa, vyuma, ardhi, kwenye miamba na hata katika vipande vya mbao.

Moja ya vitabu vya kale zaidi duniani.
Karatasi za kawaida zilipokuja kugunduliwa pamoja na mashine za kupiga chapa utengenezaji wa vitabu ukawa rahisi zaidi. Kitu cha kushangaza kabisa ni vitabu vya dini vya Quran Tukufu na Biblia Takatifu, kuna watu wanaofikiria labda vitabu hivi katika zama za mitume na manabii vilikuwa vile vile kama vilivyokuwa leo. Vitabu hivi vitakatifu viliandikwa kimaajabu katika karatasi zisizokuwa za kawaida hata kidogo, wakati mwingine katika ngozi za wanyama, mawe, miamba na hata katika magome ya miti.


Lakini kutokana na tekinolojia ya wakati huo kuwa ndiyo iliyokuwepo, basi watu wa nyakati hizo waliithamini mithili ya sisi tufanyavyo leo hii kwa vitu kama facebook, twitter, wassap na mtandao mzima wa Intaneti. Na hiyo ndiyo sababu iliyofanya vitabu hivyo pamoja na vitabu vya maarifa mengine ya kidunia viweze kuhifadhiwa kwa ustadi namna hiyo mpaka na sisi huku leo hii tukavikuta na vikatustaajabisha.

Kuhifadhi maarifa yeyote yale katika chombo chochote kile iwe ni kwenye vitabu vya kawaida, au katika kompyuta kunabakia kuwa na maana ileile iliyokuwepo enzi za manabii na mitume Biblia Takatifu na Quran Tukufu vilipohifadhiwa. Njia zote ni lazima alama zitumike, iwe ni maandishi ya kawaida au ya kielektroniki, ni vyombo tu ndivyo hubadilika kwa mfano ilikuwa ngozi, ikaja karatasi na sasa imeingia kompyuta lakini dhana ya kuhifadhi inabakia kuwa ni ileile.


Wazo la makala hii limenijia baada ya kufikiria dhana iliyoanza kuenea kwamba vitabu na hasa vya karatasi siku zake zinahesabika, maana yake ni kwamba itafika kipindi watu hawatasoma tena vitabu vya karatasi. Mimi hili silipingi na wala silikubali kama lilivyo. Mawazo yangu ni kuwa, vitabu vya karatasi vitaendelea kuwepo kwa karne nyingi zijazo sambamba na vile vya kielektroniki, hakuna atakayemmeza mwenzake. Zipo sababu nyingi zikiwemo za kihistoria lakini pia za kiuchumi na hata sababu za kitekinolojia.

Kwa mfano kihistoria watu ni vigumu sana kushawishika kwamba kitabu cha kielektroniki ni sawa sawa na cha karatasi, watu wameshajijengea mazoea ya muda mrefu karne kwa karne. Kiuchumi, maeneo mengi Duniani ni masikini na yataendelea kubakia kuwa masikini kwa kipindi kirefu bila ya watu wake kuweza kumudu teknolojia hizi za kisasa. Kuhifadhi maandishi ya karatasi ni rahisi na hudumu kwa muda mrefu bila ya kuharibika kutokana na sababu mbalimbali kama vile, hali ya hewa nk. hivyo maandishi ya karatasi yataendelea kuwepo.Tukiacha vitabu hivyo vitakatifu, maarifa mengine yote yaliyosababisha kutokea maendeleo makubwa zaidi duniani yakiwemo yale ya kompyuta na intaneti yote yalihifadhiwa kwa namna moja ama nyingine kwenye vitabu. Hivyo kusema kwamba mafanikio ya ustaarabu wote na maendeleo  ya mwanadamu yameletwa na vitabu ni sahihi kabisa.

0 Response to "VITABU: CHANZO CHA MAENDELEO NA MAFANIKIO MAKUBWA YA BINADAMU DUNIANI"

Post a Comment