SHAUKU: MWANZO WA MAFANIKIO YOTE(HATUA YA KWANZA KUELEKEA UTAJIRI) | JIFUNZE UJASIRIAMALI

SHAUKU: MWANZO WA MAFANIKIO YOTE(HATUA YA KWANZA KUELEKEA UTAJIRI)


Kitabu “Think & Grow Rich",(Fikiri Utajirike) au Msahafu wa Mafanikio, kilichoandikwa na Andrew Carnegie miaka 70 iliyopita, hakuna shaka yeyote kuwa ndiyo kitabu pekee duniani cha elimu ya pesa na mafanikio maarufu cha wakati wote.

Siku za nyuma tuliahidi kukitafsiri katika tovuti ya jifunzeujasiriamali.com, na tulifanya hivyo kwa Dibaji na sura ya kwanza tu na kuahidi sura zinazofuata tutaziweka katika blogu hii. Kuanzia leo tumeanza tena kuweka mfululizo wa  sehemu za kitabu hicho kidogo kidogo ila safari hii hatutasitisha tena, ni kila siku fuatana nasi usikose. Ikiwa hukusoma Dibaji na sura ya 1 basi fungua hapa kusoma.



Wakati Edwin C. Barnes aliposhuka kutoka kwenye treni ya mizigo katika mji wa Orange, NJ. Ungeweza ukamfananisha  na mzururaji, lakini mawazo yake yalikuwa ni sawa na ya mfalme!. 

Akiwa anaelekea ofisini kwa Thomas A. Edison akili yake ilikuwa kazini. Alijihisi mwenyewe kama vile tayari alikuwa mbele ya Edison. Alisikia sauti ndani mwake ikimuomba Bwana Edison fursa ya kutekeleza jukumu zito katika maisha yake, shauku kuu ya kuwa mbia kibiashara na mgunduzi mkubwa.

Shauku ya Barnes haikuwa matumaini wala matamanio. Ilikuwa ni shauku kali iliyokuwa ikimbubujika na iliyopitiliza kila kitu. Ilikuwa dhahiri.

Shauku hiyo haikuwa mpya alipomsogelea Edison. Ilikuwa shauku aliyokaa nayo Barnes kwa muda wa kipindi kirefu. Mwanzoni wakati shauku ilipojitokeza kwa mara ya kwanza akilini mwake, ingeweza kuwa, na pengine ilikuwa ni matamanio tu, lakini haikuwa tena matumaini matupu pindi alipofika mbele ya Edison.

Miaka michache baadae, Edwin C. Barnes akaja kusimama tena mbele ya Edison katika ofisi ileile alipokutana na huyu Mgunduzi. Safari hii hamu yake ikiwa imeshageuka kuwa kweli. Alikuwa katika biashara na Edison. Ndoto iliyokuwa imetawala katika maisha yake ilikuwa imegeuka kuwa kitu halisi.

Leo hii wanaomfahamu Barnes humuonea wivu kutokana na mafanikio aliyojaliwa maishani. Wanamuona katika siku zake za furaha, bila ya hata kujisumbua kuchunguza sababu za mafanikio yake.

Barnes alifanikiwa kwasababu alichagua lengo dhahiri, na akaelekezea kwalo nguvu zake zote, matumaini yake yote pamoja na jitihada zake zote katika kulitimiza lengo hilo. Alikuwa yuko radhi kuanza na kazi ya chini kabisa, ilimradi tu kazi hiyo ingempatia japo fursa ya kupiga hatua moja kuelekea lengo alilokuwa amelitunza.

Miaka mitano ilipita kabla hajafanikiwa kuipata nafasi aliyokuwa akiitafuta. Kwa kipindi chote hicho hakuwa na mwanga wowote wa matumaini, wala ahadi moja ya kufikiwa kwa shauku yake.

Kwa kila mtu, isipokuwa yeye mwenyewe, alionekana tu kama jino jingine la gurudumu(kitu kisichomuhimu) katika gurudumu la biashara ya Edison. Lakini ndani ya akili yake mwenyewe alijua alikuwa mbia wa Edison kila sekunde iliyokuwa ikipita, kuanzia siku ya kwanza kabisa alipokwenda kuanza kazi pale.

Huu ni uthibitisho mkubwa wa nguvu ya shauku iliyokuwa wazi. Barne’s alishinda lengo lake kwasababu alitaka kuwa mbia kibiashara na Bwana Edison zaidi kushinda alivyotaka kitu kingine chochote kile. Alitengeneza mpango ambao kwa kupitia huo aliweza kutimiza lengo hilo. Lakini “aliteketeza moto madaraja yote yaliyokuwa nyuma yake”  Alisimamia shauku yake mpaka ilipogeuka kuwa jambo lenye kutawala maisha yake na mwishowe kuwa kitu halisi.

Alipokwenda katika mji wa Orange, hakujisemea mwenyewe, “nitajaribu kumshawishi Edison anipe kazi ya aina fulani” Alisema “nitamuona Edison na kumpa ujumbe kuwa, nimekuja kuingia naye ubia wa biashara”

Hakusema, “Nitafanya kazi pale kwa miezi michache, na ikiwa kama sitapata motisha, nitaacha na kutafuta kazi mahali pengine” Alisema, “Nitaanza popote, nitafanya chochote Edison atakachoniambia nifanye lakini kabla sijakamilisha, nitakuwa nimeshakuwa mbia naye”

Hakusema, “Nitakuwa macho kwa fursa nyingine, ikitokea nikishindwa kupata ninachotaka kwenye kampuni ya Edison”, Alisema, kuna kitu kimoja tu katika Dunia hii ninachonuwia kuwa nacho, nacho ni ubia wa kibiashara na Thomas A. Edison. Nitayaunguza madaraja yote yaliyoko nyuma yangu, na kuweka rehani mustakabali wa maisha yangu yote yajayo kusudi niwe na uwezo wa kupata kile ninachokitaka”.

Mwenyewe binafsi hakujiachia kabisa uwezekanao wa kurudi nyuma. Ilikuwa ni lazima aidha ashinde au afe! Na hiyo ndiyo historia ya mafanikio ya Barnes.

Hapo zamani za kale, Mpiganaji mashuhuri alipaswa kufanya uamuzi ambao ulimhakikishia ushindi katika uwanja wa mapambano. Alikuwa akijiandaa kupeleka jeshi kupigana na adui aliyekuwa na nguvu, na ambaye idadi ya wanajeshi wake ilizidi ile yakwake.

Alijaza askari wake kwenye meli na kuelekea nchi ya adui, aliwashusha askari na vifaa kisha akatoa amri ya kuchoma moto ile meli iliyokuwa imewabeba. Akiwahutubia askari wake kabla ya pambano la kwanza alisema,  “Mnaiona meli ikiteketea kwenye moshi, hiyo ina maana kwamba hatuwezi tukaondoka ufukwe huu tukiwa hai ikiwa kama hatutashinda vita! Sasa hatuna chaguo- ni lazima tushinde, vinginevyo tuangamie!  Walishinda.

Kila mtu anayeshinda kwenye jambo lolote lile gumu, ni lazima kwanza akubali kuchoma meli yake na kukata vyanzo vyote vinavyoweza kumfanya arudi nyuma. Ni kwa kufanya hivyo tu ndipo mtu anapoweza kuwa na uhakika wa kudumisha ile hali ya akili inayojulikana kama shauku kuu(hamu kubwa) ya kushinda ambayo ni muhimu katika mafanikio.

1 Response to "SHAUKU: MWANZO WA MAFANIKIO YOTE(HATUA YA KWANZA KUELEKEA UTAJIRI)"