WASOMI NA WATU WENYE MAFANIKIO HAWAACHI KUJIFUNZA MAARIFA MAPYA-HENRY FORD | JIFUNZE UJASIRIAMALI

WASOMI NA WATU WENYE MAFANIKIO HAWAACHI KUJIFUNZA MAARIFA MAPYA-HENRY FORD


SURA YA 5
UJUZI MAALUMU
Uzoefu Binafsi na Ushuhuda
(Hatua ya 4 kuelekea utajiri)

Kuna aina mbili za ujuzi(Maarifa), moja ni ujuzi wa jumla na mwingine ni ujuzi maalumu. Ujuzi wa jumla pasipo kujali ni mkubwa kiasi gani au ni mwingi kiasi gani, una matumizi kidogo sana katika kujipatia pesa.

Vitengo katika vyuo vikuu vikubwa vinamiliki kwa kiasi kikubwa karibu kila aina ya ujuzi wa jumla unaojulikana kwenye ustaarabu. Wanabobea katika kufundisha maarifa, lakini hawabobei katika kuyapanga au kuyatumia marifa(ujuzi)

Ujuzi hautavuta pesa ikiwa kama hautapangiliwa na kuongozwa kwa akili kupitia mipango inayotekelezeka ya kivitendo kuelekea kwenye lengo lililokuwa dhahiri la kujichumia pesa. Ukosefu wa ufahamu wa ukweli huu umekuwa chanzo cha mkanganyiko wa mamilioni ya watu ambao huamini uwongo kwamba, “Ujuzi ni nguvu” Hakuna kitu kama hicho. Ujuzi ni uwezekano tu wa nguvu ambayo bado haijadhihirika kuwa nguvu halisi. Huwa nguvu tu pale ambapo na ikiwa itaratibiwa kwa mipango halisi ya kivitendo kuelekea lengo lililokuwa dhahiri.

“Ukosefu wa kiungo” hiki katika mifumo yote ya elimu inayojulikana kwenye ustaarabu leo unaweza kuonekana katika kushindwa kwa taasisi za elimu kufundisha wanafunzi wao JINSI YA KUSIMAMIA NA KUTUMIA UJUZI BAADA YA KUUPATA.

Watu wengi hufanya kosa la kudhani kwamba, kwasababu Henry Ford alikuwa na “elimu ndogo” basi yeye siyo mtu wa “elimu” Wale wanaofanya kosa hili hawamjui Henry Ford, wala hawaelewi maana halisi ya neno ‘elimu’. Neno hilo limetoholewa kutoka Kilatini, ‘educo’ maana yake ni to “educe” “ kutoa kutoka ndani” au “kukua kutokea ndani”

Mtu aliyeelimika siyo lazima awe ni yule aliye na ujuzi mwingi wa jumla au maalumu. Watu walioelimika wamejenga vitivo vya akili zao kusudi ziweze kupokea kitu chochote wanachotaka, au ni sawa na kusema, pasipo kuingilia haki za watu wengine. Henry Ford ni mfano mzuri anafaa zaidi kwenye maana ya huu ufafanuzi.

Wakati wa vita kuu ya kwanza ya Dunia, gazeti moja la Chicago lilichapisha tahariri fulani ambazo miongoni mwa kauli nyingine, Henry Ford aliitwa, “Mpinga vita mjinga” Bwana Ford alipinga kauli hizo na kufungua kesi dhidi ya gazeti kwa kumkashifu. Wakati kesi ikizungumzwa mahakamani,wakili wa lile gazeti alitoa ushahidi na kumuweka Bwana Ford mwenyewe katika upande wa ushahidi kwa lengo la kuithibitishia mahakama kwamba alikuwa mjinga. Bwana Ford aliulizwa maswali kama ifuatavyo,

“Benedict Arnold  alikuwa nani?”
“Ni wanajeshi wangapi waliotumwa na Uingereza kwenda kuzima uasi wa mwaka 1776?”

Akijibu swali la mwisho Bwana Ford alisema,
“Siijui idadi kamili ya wanajeshi Uingereza iliyotuma, lakini nimesikia kwamba ilikuwa ni idadi kubwa kushinda idadi ya wale waliorudi”

Mwishowe, Bwana Ford alichoka na huu msururu wa maswali. Katika kujibu swali hilo la uchokozi, aliegama akamnyooshea kidole wakili ambaye alikuwa amemuuliza lile swali na kusema,

“Ikiwa kama kweli ningetaka kujibu swali la kijinga ambalo umetoka kuuliza, au maswali mengine yeyote ambayo umekuwa ukiniuliza, ngoja nikukumbushe kwamba nina mstari wa vitufe vya umeme vya kubonyeza juu ya dawati langu, na kwa kubofya kitufe sahihi, naweza nikaita msaada wa watu wanaoweza wakajibu swali lolote ninalotamani kuuliza kuhusiana na biashara ambayo naelekeza nguvu zangu nyingi. Sasa tafadhali unaweza kutuambia kwanini nihangaike kuichanganya akili yangu kwa maarifa ya jumla, kwa lengo la kuweza kujibu maswali, wakati ninao watu wanaonizunguka wanaoweza kunipa ujuzi wowote ninaouhitaji?

Hapo bila shaka kulikuwa na mantiki kwa jibu hilo.

Jibu lile lilimshinda wakili, kila mtu kwenye chumba cha mahakama alitambua lilikuwa ni jibu siyo la mtu mjinga, bali la mtu mwenye elimu(msomi). Mtu yeyote aliyeelimika ni yule anayefahamu pa kupata maarifa anapoyahitaji, na jinsi ya kuyapangilia hayo maarifa katika mipango dhahiri ya kivitendo kupitia msaada wa Kundi lake la kushauriana”(Mastermind Group). Henry Ford alikuwa ana mamlaka na ujuzi maalumu wote aliouhitaji kumfanya kuweza kuwa mmoja kati ya watu matajiri zaidi Marekani. Haikuwa muhimu kwamba alikuwa na maarifa hayo katika akili yake mwenyewe. Ukweli hamna mtu mwenye mwelekeo wa kutosha na akili kusoma kitabu cha aina hii anaweza kutoona umuhimu wa mfano huu.

Kabla hujaweza kuwa na uhakika wa uwezo wako wa kubadilisha shauku kuwa katika kiwango chake cha fedha kinacholingana nayo, utahitaji ujuzi maalumu wa huduma, bidhaa au utaalamu unaokusudia kuutoa kwa ajili ya kupata utajiri. Pengine unaweza ukahitaji ujuzi maalumu zaidi kuliko vile  ulivyokuwa na uwezo au mwelekeo wa kuupata, na kama hili litakuwa kweli, unaweza ukauziba udhaifu wako kupitia msaada wa kundi lako la kushauriana(Mastermind group)

Andrew Carnegie alisema kwamba, yeye mwenyewe hakuwa anajua kitu kuhusiana na maswala ya kiufundi ya biashara ya chuma cha pua, zaidi ya hapo hakujisumbua kabisa kujua kitu chochote kuhusiana nayo. Ujuzi maalumu aliouhitaji kwa ajili ya kuzalisha na kuuza chuma cha pua aliupata kutoka kwa mtu mmoja mmoja katika kundi lake la kushauriana(Master mind group)

Ulimbikizaji wa utajiri mkubwa huhitaji nguvu na nguvu hupatikana kupitia ujuzi maalumu uliopangiliwa vizuri na kuongozwa kwa akili, lakini ujuzi huo siyo lazima uwe ni mali ya yule mwenye kulimbikiza huo utajiri.

Aya iliyotangulia inapaswa kutoa matumaini na ari kwa mtu mwenye nia ya kupata utajiri ambaye hakuweza kupata “elimu” ya kutosha ya kutoa huo ujuzi maalumu kama unavyohitajika. Watu wakati mwingine huumia maishani kutokana na “hali ya kutokujiamini” kwasababu hawakupata elimu rasmi.

Mtu mwenye uwezo wa kuunganisha na kuongoza “kundi la watu wenye kushauriana”(Mastermind group) wenye ujuzi unaoweza ukatumika katika kulimbikiza utajiri(pesa), mtu huyo anahesabika kuwa na elimu sawa tu na mtu mwingine yeyote yule katika kundi hilo. Kumbuka hili kama unakabiliwa na hisia za kutokujiamini kutokana na kutokupata elimu ya kutosha.

Inalipa Kufahamu Jinsi ya Kununua Ujuzi
Kwanza kabisa, amua juu ya aina ya ujuzi maalumu unaouhitaji na lengo la kuhitaji ujuzi huo. Kwa kiasi kikubwa lengo lako kuu maishani, lengo unalofanya kazi kulifikia, itasaidia kutambua ni ujuzi gani unaohitaji. Swali hili likiwa limeshapata majibu, kazi yako nyingine inahitaji kwamba una taarifa sahihi kulingana na vyanzo vya kuaminika vya maarifa. Vyanzo muhimu zaidi kati ya hivyo ni;

a)  Uzoefu na elimu ya mtu mwenyewe
b)  Uzoefu na elimu vinavyopatikana kupitia ushirikiano na wengine
c)  Vyuo na vyuo vikuu
d)  Maktaba za umma(kupitia vitabu na majarida ambamo unaweza ukapatikana ujuzi wote uliokusanywa na ustaarabu
e)  Kozi maalumu za mafunzo(kupitia madarasa ya jioni na zaidi mafunzo kwa njia ya posta.

Kadiri ujuzi unavyopatikana, ni lazima upangiliwe na kutumiwa kwa ajili ya lengo lililokuwa wazi kupitia mipango inayotekelezeka. Ujuzi hauna thamani isipokuwa ule unaoweza kupatikana kutokana na matumizi yake katika jambo lenye manufaa. Hii ni sababu moja kwanini shahada za vyuo vikuu haziwezi kuwa hakikisho la ajira zenye mafanikio.

Kama utafikiria kuchukua masomo ya ziada, kwanza tambua lengo linalokufanya utake ujuzi unaoutafuta, halafu jifunze ni wapi aina hiyo ya ujuzi(maarifa) inapoweza kupatikana kutoka vyanzo vinavyoaminika. Watu wenye mafanikio, katika nyanja zote kamwe hawaachi kujifunza ujuzi maalumu unaohusiana na lengo lao kuu, biashara au taaluma. Wale wasiokuwa na mafanikio, kwa kawaida hufanya kosa la kuamini kwamba kipindi cha kujiongezea maarifa huishia wanapomaliza shule. Ukweli ni kwamba shule haifanyi chochote zaidi ya kumuelekeza mtu jinsi ya kupata maarifa ya kivitendo.

Nidhamu binafsi mtu anayopata kutokana na programu dhahiri ya mafunzo maalumu huwa kiasi hicho kutokana na fursa iliyopotezwa wakati ujuzi ulipokuwa ukipatikana bila gharama. Njia ya mafunzo ya nyumbani ya kufundisha sanasana hufaa kwa mahitaji ya watu walioajiriwa ambao hukuta baada ya kumaliza shule ni lazima wapate ujuzi maalumu wa ziada, lakini hawawezi wakapata muda wa kurudi tena shuleni. Mabadiliko endelevu ya hali ya kiuchumi katika jamii yetu yamesababisha maelfu ya watu kutafuta kipato cha ziada au vyanzo vipya vya kipato. Kwa waliokuwa wengi suluhisho la matatizo yao huweza kupatikana kwa njia ya kujipatia ujuzi maalumu.

Wengi watalazimika kubadilisha shughuli zao kabisa. Mfanyabiashara atakapokuta kwamba aina fulani ya bidhaa haiuziki, kwa kawaida ataibadilisha na bidhaa nyingine inayohitajika zaidi.Watu ambao biashara zao ni zile za kutafuta soko la huduma zao ni lazima pia wawe wafanyabiashara hodari. Kama huduma zao hazileti mapato ya kutosha katika shughuli moja, ni lazima wahamie kwa nyingine ambapo fursa pana zaidi zinapatikana.

Watu wanaoacha kujifunza kwasababu tu wamemaliza shule, daima wataangamia kwenye umasikini bila ya matumaini pasipokujali wanafanya kazi gani. Nija ya mafanikio ni njia ya kutafuta maarifa bila kukoma. Hebu tuangalie tukio la kipekee…

.................................................................................................

Ndugu msomaji mfululizo wa sehemu za kitabu hiki sasa tutakuwa tukikuletea kila siku ya Jumatatu na Alhamisi, tafadhali usikose mpaka mwisho wa kitabu.










0 Response to "WASOMI NA WATU WENYE MAFANIKIO HAWAACHI KUJIFUNZA MAARIFA MAPYA-HENRY FORD"

Post a Comment