KIONGOZI BORA MWENYE MAFANIKIO HUTENDA HAKI USAWA NA AMANI ILI KUENDELEA KUTAWALA | JIFUNZE UJASIRIAMALI

KIONGOZI BORA MWENYE MAFANIKIO HUTENDA HAKI USAWA NA AMANI ILI KUENDELEA KUTAWALA

SURA YA 7
MIPANGO MADHUBUTI
Kubadilisha Shauku kuwa Vitendo
(Hatua ya sita Kuelekea Utajiri)

Umeshajifunza kuwa kila kitu kinachoumbwa au kumilikiwa huanza katika mfumo wa shauku. Shauku hiyo huchukua safari yake ya mwanzo pasipo kuwa na kitu chochote mpaka kwenye kitu kinachoweza kushikika katika karakana ya Ubunifu mahali ambapo mipango kwa ajili ya mabadiliko yake hutengenezwa na kupangiliwa.

Katika sura ya 2 ulielekezwa kuchukua hatua kamili sita za kivitendo kama hatua ya kwanza katika kutafsiri shauku kuwa pesa. Moja ya hatua hizo ni kutengeneza mipango kamili ya kivitendo ambayo kupitia hiyo, mageuzi haya yanaweza kufanyika.

Sasa utaelekezwa juu ya namna ya kutengeneza mipango ya kivitendo.

(1)  Shirikiana wewe mwenyewe na kundi la watu wengi kwa kadiri utakavyohitaji kwa ajili ya kutengeneza na kutekeleza mpango wako au mipango yako  ya kujichumia fedha, ukitumia kanuni ya “Ushirika wa kushauriana maendeleo”(Mastermind Group)
iliyoelezwa katika Sura ya 9. (Kukubaliana na maelekezo haya ni muhimu kabisa. Usije ukayapuuza.)

(2)  Kabla hujaunda “Ushirika wako wa kushauriana” amua ni faida zipi na manufaa unayoweza kuyatoa kwa wanachama mmojammoja wa kundi lako kama malipo kwa ushirikiano wao. Hakuna mtu atakayefanya kazi milele pasipokuwa na aina fulani ya malipo. Wala hakuna mtu mwenye akili atakayemuomba ama kumtegemea mwingine afanye kazi pasipokuwa na malipo yanayofaa, ingawaje siyo kila mara malipo hayo yanaweza yakawa katika mfumo wa pesa.

(3)  Panga kukutana na wanachama wa Kundi lako la kushauriana angalao mara mbili kila juma, na mara nyingi zaidi kama itawezekana mpaka wote kwa pamoja mmekamilisha mpango au mipango kwa ajili ya kujichumia fedha.

(4)  Dumisha masikilizano kamili kati yako mwenyewe na kila mwanachama wa “Kundi lako la kushauriana”. Ikiwa utashindwa kutekeleza sharti hili kwa umakini unaweza ukakutana na kikwazo. Kanuni ya “Ushirika wa Kushauriana” haiwezi kufanya kazi mahali pasipokuwa na masikilizano kamili.
Zingatia ukweli ufuatao;

(a)        Unajiingiza katika jukumu lenye umuhimu mkubwa kwako. Kuwa na uhakika wa mafanikio, ni lazima uwe na mipango isiyokuwa na makosa.
(b)        Ni lazima uwe na faida ya uzoefu, elimu, uwezo wa asili na ubunifu wa akili za watu wengine. Hili linakubaliana na njia zilizofuatwa na kila mtu aliyewahi kujikusanyia utajiri mkubwa.

Hakuna mtu mwenye uzoefu wa kutosha, elimu, uwezo wa asili na ujuzi kuhakikisha anajikusanyia utajiri mkubwa pasipokuwa na ushirikiano wa watu wengine. Kila mpango unaotumia katika shughuli zako za kujipatia utajiri unatakiwa uwe wa pamoja, wewe mwenyewe na kila mwanachama mwingine wa Kundi Lako la Kushauriana. Unaweza ukaanzisha mipango yako mwenyewe, aidha mipango mizima au sehemu yake, lakini ona kwamba mipango hiyo inaangaliwa na kupitishwa na wanachama wa ‘Kundi lako La Kushauriana.’

Ikiwa mpango wa kwanza utakaotumia hautafanya kazi kwa mafanikio, ubadilishe na mpango mwingine mpya. Ikiwa mpango huo mpya utashindwa kufanya kazi, ubadilishe badala yake weka mwingine tena, hivyo hivyo mpaka unapata mpango utakaofanya kazi.  Mahali hapa hasa ndipo kituo ambapo watu wengi hukutana na maanguko kutokana na kukosa kwao msimamo katika kuunda mipango mipya kuchukua mahali pa ile ambayo imeshindwa.

Mtu mwenye akili  zaidi anayeishi hawezi akafanikiwa kupata utajiri wala katika shughuli nyingine yeyote – pasipo mipango inayotekelezeka na inayofanya kazi. Weka ukweli huu akilini  na kumbuka wakati mipango yako inapoanguka, kuanguka huko kwa muda siyo anguko la kudumu. Inaweza tu ikamaanisha kwamba mipango yako haikuwa mizuri. Tengeneza mipango mingine. Anza tena upya.

Thomas A. Edison “alifeli”  mara 10,000 kabla hajakamilisha kikamilifu  kuunda balbu ya umeme. Ina maana kwamba alikutana na vikwazo vya muda mfupi mara 10,000 kabla juhudi zake hazijazaa matunda.

Anguko la muda linatakiwa limaanishe kitu kimoja tu, - ujuzi fulani kwamba kuna kitu fulani kisichokuwa sahihi kuhusiana na mipango yako. Mamilioni ya watu hupitia maisha ya mateso na umasikini kwasababu ya kukosa mipango imara ya kuwawezesha kujipatia utajiri.

Henry Ford alipata utajiri, siyo kwa sababu ya kuwa na akili ya kipekee, lakini ni kwa sababu alikubali na kufuata Mpango  uliothibitika kuwa timamu. Maelfu ya watu waliweza kupewa elimu bora kuliko ile ya Ford lakini bado wameishia katika umasikini kwa sababu hawana mpango sahihi kwa ajili ya kujipatia utajiri.

James J. Hill alikutana na kikwazo cha muda mwanzoni wakati alipoanzisha shughuli ya kukusanya mtaji uliohitajika kujenga barabara ya treni kutoka Mashariki kwenda Magharibi, lakini aligeuza kikwazo kuwa ushindi kupitia mipango mipya.

Henry Ford alikutana na anguko la muda siyo tu mwanzoni mwa biashara zake, lakini hata baada ya kuwa alikuwa amekwenda mbali kufika kileleni. Alitengeneza mipango mipya na kusonga mbele kwenye ushindi kifedha.

Tumewaona watu waliojikusanyia utajiri mkubwa, lakini tunatambua tu ushindi wao, hatutazami vikwazo vya muda walivyopaswa kuvishinda kabla “hawajafika.”

HAKUNA MFUASI WA FILOSOFIA HII ANAYEWEZA KWA MAKUSUDI KUTEGEMEA KUPATA UTAJIRI PASIPO KUKUTANA NA ANGUKO LA MUDA MFUPI.
Anguko linapokuja, likubali kama ishara kwamba mipango yako siyo mizuri, tengeneza tena upya mipango hiyo na anza safari kwa mara nyingine tena kuelekea lengo lako ulilotamani. Kama utakata tamaa kabla lengo lako halijafikiwa, wewe ni “muachaji”

MUACHAJI KAMWE HAWEZI KUSHINDA - NA MSHINDI KAMWE HAACHI

Ichukue sentensi hii, iandike juu ya kipande cha karatasi kwa herufi zenye urefu wa nchi moja kwenda juu, na uiweke mahali ambapo utaiona kila usiku kabla hujakwenda kulala,na kila asubuhi kabla hujakwenda kazini.

Wakati unapoanza kuchagua wanachama wa Kundi lako la Ushirika wa  Kushauriana,(Master Mind group) jitahidi kuchagua wale wasiojali sana kuanguka. Baadhi ya watu huamini kwa ujinga kwamba pesa pekee inaweza kutengeneza pesa. Hii siyo kweli! Shauku iliyobadilishwa kuwa katika kipimo chake cha fedha kupitia kanuni zilizotajwa hapa ndiyo wakala ambaye kupitia yeye fedha ‘hutengenezwa’. Fedha, yenyewe siyo kitu bali nguvu iliyolala. Haiwezi kusogea, kufikiri, au kuongea, lakini inaweza “ikasikia” wakati mtu anayeihitaji anapoiita ije!

Kupanga Mauzo ya Huduma
Sehemu iliyobakia ya Sura hii imepewa maelezo ya njia na namna ya kutafuta soko la huduma. Taarifa iliyotolewa hapa itakuwa ni ya msaada wa kivitendo kwa mtu yeyote aliye na aina yeyote ya huduma za kutafutia soko, lakini litakuwa jambo la faida isiyopimika kwa wale wanaotamani kuwa viongozi katika shughuli zao walizochagua.

Kupanga kwa weledi ni muhimu kwa mafanikio katika shughuli yeyote iliyobuniwa kuleta utajiri. Hapa yatapatikana maelezo ya kina kwa wale ambao ni lazima waanze kutafuta utajiri kwa kuuza huduma zao.

Inatia moyo kufahamu kwamba karibu utajiri wote mkubwa ulianza katika hali ya kubadilishana na huduma, au kutokana na mauzo ya mawazo. Ni kipi kingine isipokuwa mawazo na huduma ambacho mtu angepaswa kutoa kubadilishana na utajiri?

Kusema ukweli, kuna aina mbili za watu duniani, Viongozi na Wafuasi. Amua mwanzoni kabisa ikiwa unapanga kuwa kiongozi katika taaluma yako uliyochagua au kubakia kuwa mfuasi. Tofauti katika malipo ni kubwa. Mfuasi hawezi kwa makusudi kutegemea malipo ambayo kiongozi anastahili, ingawa wafuasi wengi hufanya kosa la kutegemea malipo ya namna hiyo.

Siyo aibu kuwa mfuasi. Kwa upande mwingine, siyo sifa kubakia kuwa mfuasi. Viongozi wengi wakubwa walianzia katika kiwango cha wafuasi. Walikuwa viongozi wakubwa kwa sababu walikuwa wafuasi werevu. Isipokuwa mifano michache, watu wasioweza kumfuata kiogozi kwa werevu hawawezi kuwa viongozi wenye ufanisi. Watu wanaoweza kumfuata kiongozi kwa ufanisi zaidi mara nyingi ni wale wanaoibuka kuwa katika uongozi haraka zaidi. Mfuasi mwerevu anazo faida nyingi, miongoni mwazo ni fursa ya kupata maarifa kutoka kwa kiongozi.

Sifa Kubwa Za Uongozi
Zifuatazo ni sifa muhimu za uongozi:

1.  UJASIRI USIOYUMBA uliojengeka juu ya msingi wa maarifa binafsi na kujitambua binafsi  na shughuli aifanyayo. Hakuna mfuasi anayependa kutawaliwa na kiongozi asiyejiamini wala kuwa na ujasiri. Hakuna mfuasi mwerevu atakayetawaliwa na kiongozi wa namna hiyo kwa muda mrefu.

2.  KUJIZUIA BINAFSI: Watu wasioweza kujidhibiti binafsi kamwe hawawezi kuwaongoza wenzao. Kujizuia binafsi hutoa mfano wenye nguvu kwa wafuasi wa kiongozi ambao kwa wale waliokuwa werevu hujifunza.

3.  MTAZAMO THABITI WA HAKI: Bila hali ya usawa na haki hakuna kiongozi anayeweza kuamrisha na kuendelea kutunza heshima ya wafuasi wake.

4.  UKAMILIFU WA MAAMUZI: Watu wanaoyumba kwenye maamuzi huonyesha kwamba hawajiamini wenyewe.

5.  UKAMILIFU WA MIPANGO: Kiongozi mwenye mafanikio ni lazima apange kazi, na kufanyia kazi mpango. Kiongozi anayejiendesha kwa kubahatisha bila mpango kamili unaotekelezeka ni sawa na meli isiyokuwa na usukani. Muda wowote ule itagonga juu ya miamba.

6.  TABIA YA KUFANYA KAZI ZAIDI KULIKO MALIPO: Moja kati ya penati za uongozi ni umakini na utayari juu ya sehemu ya uongozi kufanya mengi zaidi ya yale wanayowataka wafuasi wao kufanya.

7.  HAIBA INAYORIDHISHA: Hakuna mtu mchafu, asiyekuwa makini anayeweza kuwa kiongozi mwenye mafanikio. Uongozi unataka heshima. Wafuasi hawatawaheshimu viongozi ambao hawatapata alama za juu katika vigezo vyote vya haiba inayovutia.

8.  HURUMA NA UELEWA: Viongozi wenye mafanikio ni lazima wawe na huruma kwa wafuasi wao. Zaidi ya hayo, ni lazima wawaelewe pamoja na matatizo yao.

9.  UFAHAMU WA KINA: Uongozi wenye mafanikio unahitaji ufahamu wa kina juu ya nafasi ya uongozi.

10.              UTAYARI WA KUBEBA WAJIBU WOTE: Viongozi wenye mafanikio ni lazima wakubali kuwajibika kwa makosa na kasoro za wafuasi wao. Ikiwa watajaribu kubadilisha wajibu huu, hawataendelea kubakia kuwa viongozi. Kama wafuasi watafanya makosa na kushindwa, ni viongozi walioshindwa.

11.              USHIRIKIANO: Viongozi wenye mafanikio ni lazima waelewe na kutumia kanuni ya nguvu za ushirikiano na kuwa na uwezo wa kuwahamasisha wafuasi kufanya hivyo. Uongozi unahitaji nguvu, na nguvu huhitaji ushirikiano.

Kuna aina mbili za uongozi. Ya kwanza na ambayo ndiyo inayofanya kazi vizuri zaidi, ni uongozi kwa hiyari ya, na kwa ridhaa ya wafuasi. Ya pili ni uongozi kwa nguvu bila ya hiyari na ridhaa ya wafuasi.

Historia imejaa mifano kwamba uongozi kwa nguvu hauwezi ukadumu. Kuanguka na kutoweka kwa “Madikteta” na Wafalme ni jambo lililokuwa wazi. Ina maana kwamba watu hawatafuata utawala wa nguvu milele.

Dunia imeingia zama mpya za mahusiano kati ya viongozi na wafuasi, ambazo kwa uwazi kabisa zinawataka viongozi wapya na aina mpya ya uongozi katika biashara na viwanda. Wale walio katika mtindo wa zamani wa uongozi wa nguvu ni lazima wapate uelewa wa aina mpya ya uongozi(Ushirikiano) au kushushwa vyeo na kuwa wafuasi. Hakuna njia nyingine kwao.

Mahusianao ya mwajiri na mwajiriwa au ya kiongozi na mfuasi kwa nyakati zijazo yatakuwa ni ya ushirikiano, unaozingatia mgawanyo uliokuwa sawa wa faida ya biashara. Wakati ujao, uhusiano wa mwajiri na mwajiriwa utakuwa zaidi kama ubia kuliko kama ilivyokuwa hapo zamani. Hitler na Stalin ni mifano ya viongozi waliotawala kwa nguvu. Utawala wao ulipita. Watu wanaweza wakafuata utawala wa nguvu kwa muda mfupi, lakini hawatafanya hivyo kwa hiyari. Uongozi kwa hiyari ya wafuasi ndiyo aina pekee inayoweza kudumu.

Aina mpya ya uongozi itakumbatia zile sifa 11 tulizoelezwa kabla katika sura hii, pia na sifa nyinginezo. Watu wanaozifanya sifa hizi kuwa msingi wa uongozi wao watapata fursa nyingi ya kuongoza katika nyanja yeyote ile ya kimaisha.

…………………………………………………………………………

Tukutane tena wakati ujao katika sehemu ya (ii) ya Sura hii ya 7 ya kitabu chako, FIKIRI UTAJIRIKE(Think & Grow Rich). Kumbuka kuanzia sasa tafsiri hii itakuwa ikichapishwa mara kwa mara kusudi kuendana na dhamira yetu kuu ya kuhakikisha kitabu hiki kinakamilika mwaka huu wa 2017 na wasomaji wetu mnapata fursa ya kukisoma chote hapa, bure kabisa katika blogu hii.

Nakusihi msomaji na mfuatiliaji wa ile kampeni yetu ya mwaka huu ya #jirudishieukuuwakotena au #makeyourselfgreatagain kwamba hakuna lisilowezekana chini ya jua, na unaweza kutimiza malengo yako uliyojiwekea mwanzoni mwa mwaka huu hata ikiwa imebakia miezi 2 tu.

Sisi tunaamini hivyo na ndiyo maana hata unaona tumeahidi kukamilisha shughuli hii ya kuhakikisha kitabu hiki unakisoma chote katika lugha ya kiswahili hapa mwaka huu huu. Haikuwa kazi rahisi, mwaka karibu wote huu lengo letu kuu lilikuwa ni kutimiza kazi hii ya kutafsiri na tunamshukuru Mwenyezi Mungu tumeshaimaliza kazi hiyo, kilichobakia ni wewe tu kusoma Sura zote kwa Kiswahili hapa ili uyafanyie kazi yote uliyojifunza.

Tunatambua kitabu hiki siyo kigeni, wapo watu wengi waliokwisha kisoma, lakini pia wapo wengine wengi hawajakisoma kwa ukamilifu wake kutokana na changamoto mbalimbali zikiwemo lugha nk. Sasa ni wakati muafaka wa kufaidi kila kitu kilichoandikwa humo bila kujali tena changamoto hizo.

Usikose pia kujipatia vitabu vingine kutoka Self Help Books Tanzania, na unaweza kuviona au kupata maelezo yake zaidi kupitia ukurasa huu wa, SMART BOOKS TANZANIA








0 Response to "KIONGOZI BORA MWENYE MAFANIKIO HUTENDA HAKI USAWA NA AMANI ILI KUENDELEA KUTAWALA"

Post a Comment