MAKOSA MAKUBWA 10 YA VIONGOZI NA AINA MPYA YA UONGOZI MZURI UNAOTAKIWA | JIFUNZE UJASIRIAMALI

MAKOSA MAKUBWA 10 YA VIONGOZI NA AINA MPYA YA UONGOZI MZURI UNAOTAKIWA


Sababu kubwa 10 za kushindwa katika Uongozi. 
Tunakuja sasa kwenye makosa makubwa ya viongozi wanaoshindwa, kwasababu ni muhimu pia kufahamu ni nini cha kutokufanya kama ilivyokuwa muhimu pia kujua ni nini cha kufanya.

1.  KUSHINDWA KUPANGA MAMBO KWA KINA. Uongozi wenye ufanisi unahitaji uwezo wa kupanga na kufahamu kwa undani mambo. Kamwe hakuna kiongozi wa kweli anayekosa muda wa kufanya kitu chochote anachotakiwa kufanya kama kiongozi. Kiongozi ama mfuasi anapokosa muda wa kupanga au kuwa makini na dharura yeyote, ni ishara ya kutokuwa na ufanisi. Kiongozi mwenye mafanikio ni lazima afahamu majukumu yote yanayohusiana na nafasi hiyo. Bila shaka, ina maana kwamba tabia ya kugawa majukumu kwa wasaidizi waliokuwa na uwezo ni lazima iwepo.

2.  KUTOKUWA TAYARI KUTOA HUDUMA KWA UNYENYEKEVU. Ukweli viongozi wakubwa huwa tayari wanapohitajika kufanya jukumu lolote ambalo wangeweza kumwambia mwingine afanye. “ Aliye mkubwa zaidi miongoni mwenu, atakuwa mtumwa wa wote”  ni ukweli ambao viongozi wote wanaojiweza huzingatia na kuheshimu.

3.  MATAZAMIO YA MALIPO KWA KILE ‘WANACHOKIJUA’ BADALA YA KILE WAKIFANYACHO KWA KILE WANACHOKIJUA. Dunia hailipi kwa kile watu ‘wanachokijua’, Huwalipa kwa kile wanachofanya au kile wanachohimiza wengine kufanya.

4.  WOGA WA USHINDANI KUTOKA KWA WAFUASI. Kiongozi anayehofia kwamba mmoja wa wafuasi wake anaweza akachukua nafasi yake ana uhakika wa hofu hiyo kuwa kweli muda wowote. Viongozi wanaojiweza huwafunza wasaidizi wanaoweza kukaimu madaraka muda wowote. Ni kwa njia hii pekee viongozi hujiongeza wenyewe na kujitayarisha kuwa sehemu nyingi kwa wakati mmoja. Ni ukweli wa milele kwamba watu hupata malipo zaidi kutokana na uwezo wao wa kusababisha watu wengine kufanya kazi kuliko ambavyo wangeweza kupata kwa kutumia nguvu zao wenyewe. Viongozi wenye ufanisi wanaweza kupitia uelewa wa kazi zao na mvuto wa haiba zao, kuongeza kwa kiwango kikubwa ufanisi wa watu wengine na kuwahamasisha  kutoa huduma zaidi na bora kuliko vile wangeweza kufanya wenyewe.

5.  KUKOSA UBUNIFU. Bila ubunifu viongozi hawawezi kukabiliana na dharura, na kutengeneza mipango itakayowaongoza wafuasi kwa ufanisi.

6.  UBINAFSI. Viongozi wanaotaka heshima yote kwa kazi ya wafuasi wao wanajihakikishia kukutwa na maudhi. Ukweli viongozi wakubwa huwa hawatadai kutukuzwa. Wanaridhika kuona heshima inawaendea wafuasi wao kwasababu wanajua kwamba watu wengi watafanya kazi kwa bidii kwa ajili ya pongezi na kutambuliwa kuliko kufanya kwa ajili ya pesa peke yake.

7.  KUTOKURIDHIKA. Wafuasi hawamuheshimu kiongozi asiyetosheka(mlafi). Zaidi ya hayo kutokutosheka katika aina zake mbalimbali huharibu uvumilivu na nguvu ya wale wote wanaoiendekeza.

8.  KUKOSA UAMINIFU. Pengine hii ingepaswa kuja mwanzoni mwa hii orodha. Viongozi wasiokuwa waaminifu kwa kampuni na kwa washirika wao – waliokuwa  juu na chini yao - hawawezi kudumisha uongozi wao kwa muda mrefu. Ukosefu wa uaminifu huwatia watu alama ya kuwa wadogo kuliko vumbi la mchanga na kushusha chini juu ya vichwa vyao dharau wanayostahili. Ukosefu wa uaminifu ni moja kati ya sababu kubwa za kufeli katika kila nyanja ya maisha.

9.  MSISITIZO WA “MADARAKA” YA UONGOZI. Viongozi wenye ufanisi huongoza kwa kutia moyo na siyo kwa kujaribu kupandikiza hofu katika nyoyo za wafuasi wao. Viongozi wanaojaribu kuwavutia wafuasi kwa madaraka yao huja katika kundi la uongozi kupitia nguvu. Viongozi wa kweli hawana haja ya kutangaza ukweli huo isipokuwa kwa njia ya uendeshaji wao, huruma, ufahamu, usawa na kuonyesha kwa vitendo maarifa ya kazi.

10.              MKAZO WA CHEO. Viongozi wenye uwezo hawahitaji ‘cheo’ kupata heshima ya wafuasi wao. Viongozi wanaoendekeza sana vyeo vyao kwa ujumla hawana kitu cha zaidi wanachoweka msisitizo. Milango kuelekea ofisi ya viongozi wa kweli ipo wazi kwa wale wote wanaotamani kuingia na maeneo yao ya kazi hayana urasimu wala majivuno.

Hizi ni miongoni mwa sababu kubwa zaidi za kushindwa katika uongozi. Sababu yeyote kati ya hizi inatosha kusababisha kuanguka. Isome orodha hiyo kwa umakini kama unataka kuwa kiongozi, na hakikisha haufanyi makosa haya.

Baadhi ya Sekta zenye fursa ambazo ‘Uongozi mpya’ utahitajika.
Kabla ya kumaliza sura hii, umakini wako unahitajika katika sekta chache zilizo na rutuba ambazo kumekuwa na mapungufu ya uongozi na ambazo aina mpya ya uongozi inaweza ikapata fursa kubwa.

1.  Katika tasnia ya siasa kuna uhitaji mkubwa sana kwa uongozi mpya, uhitaji ambao hauashirii kitu kingine zaidi ya dharura. Wanasiasa wengi mno wameonekana kuwa walanguzi wa kiwango cha juu kabisa waliohalalishwa. Wameongeza kodi na kuharibu mfumo wa viwanda na biashara mpaka watu kushindwa tena kuhimili mzigo.
2.  Sekta ya fedha ipo katika mageuzi. Viongozi katika sekta hii karibu wanapoteza kabisa uaminifu wao kwa umma. Tayari watendaji katika sekta ya fedha wameshahisi uhitaji wa mabadiliko na wamekwishaanza.
3.  Viwanda vinahitaji viongozi wapya. Aina ya zamani ya viongozi walifikiria kwenda kwa mtindo wa kugawana faida badala ya kufikiri na kwenda katika mtindo wa kanuni za kibinadamu! Viongozi wa baadae wa kwenye viwanda ili wadumu ni lazima wajihesabu wenyewe kama maofisa wa umma ambao jukumu lao ni kuongoza kampuni zao kwa namna isiyosababisha ugumu kwa mtu mmojammoja au kikundi. Utumikishaji wa wafanyakazi ni kitu kilichopitwa na wakati. Waache wale wanaotamani kuingia kwenye uongozi katika sekta ya biashara, viwanda na ajira wakumbuke hili.
4.  Viongozi wa dini wa baadae watalazimishwa kuweka umakini mkubwa katika mahitaji ya muda mfupi ya wafuasi wao katika utatuzi wa matatizo yao binafsi na ya kiuchumi ya sasa, na kupunguza umakini katika wakati ‘mfu’ uliopita na wakati ujao ambao bado ‘haujazaliwa’
5.  Katika taaluma za sheria, dawa na elimu, aina mpya ya uongozi na kwa kiasi fulani viongozi wapya litakuwa ni hitaji muhimu. Hii sanasana ni kweli katika sekta ya elimu. Viongozi katika sekta hiyo wakati ujao ni lazima watafute njia na namna ya kufundisha watu jinsi ya kutumia ujuzi walioupata shuleni. Ni lazima washughulike zaidi na vitendo kuliko nadharia.
6.  Viongozi wapya watahitajika katika sekta ya uandishi wa habari. Vyombo vya habari vya wakati ujao ili viendeshwe kwa mafanikio ni lazima viondolewe ‘upendeleo maalumu’ na ruzuku inayotokana na matangazo.

Hizi ndizo baadhi ya sekta chache ambazo fursa kwa ajili ya viongozi wapya na aina mpya ya uongozi sasa zinapatikana. Dunia inapitia mabadiliko ya haraka. Hii inamaanisha kwamba njia ambayo mabadiliko katika tabia za binadamu zimekuwa zikitengenezwa ni lazima ziendane na mabadiliko hayo. Njia zilizoelezwa hapa ni zile zinazobainisha muelekeo wa ustaarabu zaidi ya nyingine zozote zile.

Lini, na ni jinsi gani ya kuomba nafasi.
Taarifa zilizoelezwa hapa ni jumla ya matokeo ya uzoefu wa miaka mingi ambayo maelfu ya wanaume na wanawake walisaidiwa kutafuta soko la huduma zao(kazi) kikamilifu. Kwa hiyo inaweza ikategemewa kama njia inayofaa na yenye kufanya kazi.

Njia ambazo huduma zinaweza zikatafutiwa soko.
Uzoefu umethibitisha kwamba vyombo vifuatavyo vinatoa njia bora na za moja kwa moja zaidi za kuwaleta pamoja mnunuzi na muuzaji wa huduma.

1.  MAWAKALA WA AJIRA. Uangalifu ni lazima uchukuliwe kuchagua mawakala wale  wenye sifa nzuri tu, uongozi unaoweza kuonyesha kumbukumbu za kutosha za utendaji wenye matokeo yanayoridhisha.
2.  KUTANGAZA kwenye magazeti, majarida ya kibiashara, majarida, na redio. Matangazo madogomadogo yanaweza kutegemewa kutoa matokeo ya kuridhisha kwa upande wa wale wanaotafuta nafasi za kiutendaji, nakala kuonekana katika sehemu ya gazeti iliyo na uwezekano mkubwa zaidi wa kusomwa na daraja la waajiri wanaohitajika. Wakati wa kuandaa tangazo ni jambo lenye faida kupata ushauri kutoka kwa mtaalamu anayefahamu jinsi ya kutoa sifa za kutosha za mauzo ili kuleta majibu.

3.  BARUA BINAFSI YA MAOMBI, huelekezwa kwa kampuni fulani au mtu binafsi aliye na uwezekano mkubwa zaidi wa kuhitaji huduma zinazotangazwa. Barua zinatakiwa kuchapwa kwa unadhifu KILA MARA, na kusainiwa kwa mkono. Pamoja na barua inatakiwa pia itumwe na CV kamili au maelezo kwa ufupi ya sifa za mwombaji. Vyote barua ya mwombaji na CV vinatakiwa viandaliwe kwa ushauri kutoka kwa mtaalamu(angalia maelekezo chini)

4.  MAOMBI KUPITIA KUFAHAMIANA NA MTU. Ikiwezekana muombaji anatakiwa ajitahidi kumfikia mwajiri mtarajiwa kwa kupitia kufahamiana pande zote mbili . Njia hii ya kukaribiana ina faida zaidi kwa wale wanaotafuta nafasi za kiutawala  na wasingependelea kuonekana kama wenyewe wanajipigia debe.

5.  MAOMBI YA MTU MWENYEWE
Katika hali fulani inaweza ikawa bora zaidi ikiwa waombaji watatoa huduma zao wenyewe kwa waajiri . Katika hali hiyo kauli kamili ya maandishi ya sifa kwa ajili ya nafasi hiyo inatakiwa kuwasilishwa kusudi waajiri watarajiwa waweze kujadili na washirika rekodi za mwombaji.

Taarifa zinazotakiwa kuwasilishwa katika CV iliyoandikwa.
 CV hii inapaswa kuandaliwa kwa uangalifu kama vile ambavyo mwanasheria angeandaa muhtasari wa kesi itakayosomwa mahakamani. Ikiwa kama mwombaji hana uzoefu na uandaaji wa CV, mtaalamu anatakiwa atafutwe . Wafanyabiashara wenye mafanikio huajiri wanaume na wanawake wanaofahamu sanaa na saikolojia ya kutangaza ili kuleta faida katika bidhaa zao. Aliye na biashara ya kuuza huduma naye anapaswa kufanya hivyo hivyo. Taarifa zifuatazo zinatakiwa zionekane kwenye CV,

1. Elimu: Eleza kwa kifupi, lakini kwa ukamilifu, elimu uliyokuwa nayo, na ni katika masomo gani umebobea, ukitoa sababu za kubobea huko.

2. Uzoefu: Kama umekuwa na uzoefu kuhusiana na nafasi inayofanana na ile unayoomba, elezea kikamilifu ukitaja majina na anuani za waajiri wa zamani. Hakikisha unaweka wazi uzoefu wowote ule maalumu ambao inawezekana ulikuwa nao na ambao unaweza kukufanya ujaze nafasi unayoiomba.

3. Udhamini: Karibu kila kampuni ya  biashara hutamani kufahamu kila kitu kuhusiana na taarifa za nyuma za waajiriwa wake watarajiwa wanaoomba nafasi za kazi. Jiandae kuwasilisha kwa mwajiri, ilkiwa utaulizwa, majina ya watu watakaoweza kutoa taarifa kuhusiana na uzoefu na uwezo wako kama vile:

(a)Mwajiri wa zamani
(b)Walimu ambao ulisoma chini yao
(c)Watu mashuhuri ambao maamuzi yao yanaweza yakaaminiwa.

4. Picha yako binafsi, ambatanisha na CV yako picha yako mwenyewe ya karibuni.

5. Omba nafasi maalumu. Epuka maombi kwa nafasi pasipo kuelezea hasa ni nafasi gani unayotaka. Kamwe usiombe nafasi, “Ilimradi ni nafasi tu” Hiyo inaashiria huna sifa za kipekee.

6. Eleza sifa zako kwa nafasi hiyo unayoomba, toa undani wote kama sababu inayokufanya uamini unafaa katika nafasi hiyo unayoomba. Haya ndiyo MAEEZO MUHIMU ZAIDI YA MAOMBI YAKO. Ndiyo yatakayoamua, kuliko kitu kingine chochote kile, ni majibu gani utakayoyapata.

7. Jitoe kwenda kufanya kazi kwa majaribio. Katika hali nyingi, kama umeamua kwa dhati kuipata nafasi unayoomba , itakuwa vizuri zaidi kama utafanya kazi bure kwa juma moja, au mwezi au kwa muda mrefu unaotosha  kumwezesha mwajiri wako mtarajiwa kuamua thamani yako BILA MALIPO. Huu unaweza kuonekana kuwa ni uamuzi mgumu, lakini uzoefu umethibitisha kwamba ni mara chache  hushindwa kufanya vizuri angalao kwenye majaribio.

Kama una uhakika na sifa ulizokuwa nazo, majaribio ndiyo kitu pekee unachohitaji. Kwa bahati njema kujitolea huko kunaonyesha kwamba unajiamini katika uwezo wako wa kujaza nafasi unayoomba. Inashawishi zaidi ikiwa kujitolea kwako kutakubalika na ukafanya vizuri zaidi ya vile ambavyo ungelilipwa kipindi chako cha majaribio. Hakikisha ukweli kwamba kujitolea kwako kunazingatia yafuatayo,
 
(a)Imani yako katika uwezo wako kujaza nafasi hiyo
(b)Imani yako kwa maamuzi ya mwajiri wako mtarajiwa kukuajiri baada ya majaribio.
(c)Shauku yako ya kupata nafasi unayoomba. 

8. Ufahamu wa biashara ya mwajiri wako mtarajiwa. 
Kabla hujaomba nafasi, fanya utafiti wa kutosha kuhusiana na biashara ili kuijua vizuri biashara hiyo na kuonyesha katika maelezo yako mafupi ujuzi ulioupata katika sekta hiyo. Hili litakuwa jambo la kuvutia kwani itaonyesha kuwa unao ubunifu na mapenzi ya dhati katika nafasi unayoomba.

Kumbuka kwamba wakili anayeshinda kesi siyo yule anayeijua sana sheria, bali ni yule anayefanya matayarisho mazuri zaidi ya kesi. Ikiwa kesi yako itaandaliwa vyema na kuwasilishwa, ushindi wako pale mwanzoni utakuwa umepatikana zaidi ya nusu.

Usiogope kuifanya CV yako kuwa ndefu mno. Waajiri nao huvutiwa kununua huduma za waombaji waliofuzu vyema kama vile na wewe unavyovutiwa kupata ajira. Kwa kweli mafanikio ya waajiri wengi wenye mafanikio hutokana zaidi na uwezo wao wa kuchagua wasaidizi waliofuzu vizuri. Wanahitaji taarifa zote zilizopo.

Kumbuka kitu kingine; Unadhifu katika matayarisho ya CV yako yataonyesha kwamba wewe ni mtu mwenye bidii. Nimesaidia kutayarisha CV kwa wateja zilizokuwa bora na za kipekee kiasi kwamba zilisababisha waombaji kupata ajira pasipo kupewa udahili binafsi.

Mara CV yako itakapokamilika, mpe mgundisha vitabu mzoefu atie jalada kwa unadhifu na kuwekwa maandishi na mchoraji ama mchapaji kama ifuatavyo:

MAELEZO MAFUPI YA SIFA ZA
Robert K. Smith
AKIOMBA NAFASI YA
Katibu Muhtasi wa Rasi wa
KAMPUNI YA THE BLACK, Inc

Badilisha majina kila wakati CV inapoonyeshwa.
Mguso huu binafsi unao uhakika wa kuamsha usikivu, ichape CV yako vizuri, au idurufu katika karatsi nyeupe unayoweza kupata na ijaladie kwa karatasi ngumu ya aina ya jalada la kitabu, mchapishaji abadilishwe na jina halisi la kampuni liwekwe ikiwa itaonyeshwa kwa kampuni zaidi ya moja. Picha yako inatakiwa kubandikwa kwenye moja ya kurasa za CV. Fuata malekezo haya kwa umakini, ukiyaboresha popote pale ubunifu wako utakapoamua.

Wauzaji wenye mafanikioa hujitunza wenyewe kwa uangalifu. Wanafahamu kwamba muonekano wa kwanza hudumu muda mrefu. CV yako ndiyo mwakilishi wako wa mauzo, ivishe suti nzuri ya nguo kusudi iweze kusimama mshindi kinyume na kitu chochote mwajiri wako mtarajiwa alichowahi kuona katika mchakato mzima wa maombi ya nafasi hiyo. Ikiwa nafasi unayoomba inastahili, basi pia inastahili kuendewa kwa uangalifu.

Zaidi, kama unajinadi mwenyewe kwa mwajiri kwa namna ambayo itawavutia kwa sifa zako, bila shaka utapata pesa nyingi kwa huduma zako kutoka mwanzo kabisa kuliko ambavyo ungeliweza kupata kama ungeliomba kazi kwa njia ya kawaida iliyozoeleka.

Kama utaomba ajira kupitia chombo cha matangazo au wakala wa ajira, mpe wakala ruksa ya kutumia CV yako katika kutangaza sifa zako. Hii itasaidia kukupa kipaumbele , kwa wakala na pia kwa mwajiri mtarajiwa.

Jinsi ya kupata nafsi ile ile unayotamani.
Kila mtu hufurahia kufanya aina ya kazi anayoimudu zaidi. Msanii hupenda kufanya kazi na rangi, makanika na mikono yao, mwandishi hupenda kuandika. Wale wasiokuwa na vipaji maalumu mapenzi yao yapo katika tasnia fulani za biashara na viwanda.

Kuna aina nyingi za kazi za kuchagua, kuanzia uzalishaji, masoko na taaluma mbalimbali.

1.  Amua moja kwa moja ni aina gani ya kazi unayohitaji. Ikiwa kazi hiyo haipo tayari, pengine unaweza ukaitengeneza
2.  Chagua kampuni au mtu ambaye unatamani kufanya naye kazi.
3.  Jifunze kuhusiana na mwajiri wako mtarajiwa juu ya sera, wafanyakzi, na nafasi ya kujiendeleza.
4.  Kwa kujitathmini mwenyewe, vipaji vyako na uwezo wako, tafuta ni kitu gani unachoweza kutoa, na panga njia na namna ya kutoa faida, huduma, maendeleo na mawazo unayoamini unaweza kuyatoa kwa mafanikio.
5.  Sahau kuhusu ‘kazi’. Sahau ikiwa kama nafasi ipo au haipo. Sahau njia ya kawaida ya, “Naweza kupata kazi” Elekeza nguvu zako kwenye kile unachoweza kutoa.
6.  Mara utakapokuwa na mipango yako akilini, panga na mwandishi aliyekuwa na uzoefu kukusaidia kuiweka katika karatasi kwa unadhifu na kwa undani
7.  Iwasilishe kwa mtu sahihi mwenye mamlaka ya kufanya maamuzi. Kila kampuni inatafuta watu wanaoweza kutoa kitu chenye thamani, iwe ni mawazo, huduma au mawasiliano. Kila kampuni ina nafasi kwa mtu aliye na mipango dhabiti ya kivitendo kwa faida ya kampuni.

Mlolongo huu wa taratibu unaweza ukachukua siku kadhaa au majuma ya muda wa ziada, lakini tofauti katika kipato, katika maendeleo na katika kuongeza kutambulika itaokoa miaka mingi ya kazi ngumu kwa malipo ya chini. Ina faida nyingi, kubwa ikiwa kwamba mara nyingi itaweza kuokoa kuanzia mwaka mmoja mpaka miaka mitano ya muda utakaochukua kufikia lengo ulilochagua.



0 Response to "MAKOSA MAKUBWA 10 YA VIONGOZI NA AINA MPYA YA UONGOZI MZURI UNAOTAKIWA"

Post a Comment