HUJAFA HUJAUMBIKA: NILIVYOONJA ULEMAVU WA MACHO KWA SIKU 14 | JIFUNZE UJASIRIAMALI

HUJAFA HUJAUMBIKA: NILIVYOONJA ULEMAVU WA MACHO KWA SIKU 14

Mlemavu wa macho akiwa na fimbo nyeupe
Kama ilivyokuwa kwa samaki unapomtoa kwenye maji, hawezi kufanya tena lolote, na mimi ilikuwa ni hivyohivyo tatizo lililonikuta najifananisha na samaki aliyetupwa nchi kavu kwani lilinifanya nishindwe kabisa kufanya majukumu yangu niliyozoea kuyafanya ikiwemo kuandika.

Ni stori binafsi mno na sidhani hata kama ilikuwa ni sahihi sana kuisimulia hapa lakini kuna vitu kadhaa nilivyoona kama uzoefu wangu binafsi ingefaa kuwashirikisha wasomaji wangu.

SOMA: Umekata tamaa ya maisha? hebu soma maajabu ya mwanasayansi huyu mkubwa duniani.

Mimi ni mwandishi nategemea kubadilisha maisha ya watu wengine kwa kile ninachokiandika hivyo si jambo baya kama nitaandika pia mambo ninayokutana nayo binafsi kama kuna la kujifunza kuliko tu kubakia kuandika mambo ninayosikia kutoka kwa watu wengine. Ndio maana nimeshawishika kuandika kisa hiki hapa, ikiwa hakitokupendeza tafadhali sana natanguliza samahani kwako.

Na pia ikiwa kama hutaweza kusoma blah..blah.. nyiingi nilizoweka hapa katikakati, basi nakusihi tu moja kwa moja uruke mpaka mwisho wa makala hii, utakuta hitimisho nililoweka pale lenye dondoo kama 6 hivi, zisome hizo dondoo inatosha. Utakuwa umepata ujumbe wote niliokusudia kuutoa kwako leo hii.  

Zimepita wiki mbili sasa tokea mkasa huu uanze, ilikuwa ni asubuhi ya tarehe 22 Septemba 2018  asubuhi baada tu ya kuamka, ghafla nilianza  kuhisi maumivu kwenye jicho langu la kulia yaliyokuwa yakiongezeka pindi nitazamapo mwanga mkali au chanzo chochote kile cha mwanga kama vile taa au upande inakochomoza miali ya jua. Maumivu hayo yaliambatana na jicho kubadilika rangi na kuwa rangi ya pinki inayoelekea kuwa nyekundu.

SOMA: Dengue ni kama tauni na ukoma zama za Yesu Kristo

Hali ile ilinifanya niwe nalazimika kufunga jicho la kushoto kusudi niweze kuona, lakini hata hivyo miale ya mwanga ilipopenye katika jicho la kushoto bado nilihisi kama vile inapenya pia kwenye jicho la kulia lililokuwa linauma hivyo kulifunga wala haikusaidia sana. Nilifikiria njia ya kuvaa miwani nyeusi ya jua na kweli nilipojaribu ikanisaidia kwa kiasi fulani kupunguza maumivu nikitazama mwanga japo siyo sana. Miwani pia ilinisaidia watu wengi wasitambue kama nilikuwa naumwa jicho kwani ilificha ule wekundu.

Siku iliyofuata iikuwa Jumapili na bila ya kujali kama ilikuwa ni siku ya mapumziko niliamua kwennda kumuona daktari wa macho hospitali ya serikali Magomeni kwa ajili ya tiba ya macho. Nilitoka zangu Mbezi ya Kimara kwa mwendokasi mpaka Magomeni Mapipa. Pale mapokezi waliniuliza kama natumia bima nikasema nitalipa mwenyewe. Kwakuwa haikuwa siku rasmi ya kazi hapakuwa na foleni kubwa kwenda kumuona daktari. Pale mapokezi pia waliniambia kuwa siku ya jumapili huwa hamna cliniki ya macho hivyo nikaonane tu na daktari wa kawaida(general)

SOMA: Ebola, tuachane na dawa za kizungu turudi kwenye muarobaini na kikombe cha babu?

Daktari baada ya kunitizama kidogo kwenye jicho alinieleza kuwa nirudi siku iliyofuata yaani Jumatatu ili niweze kuwaona wataalamu wa macho katika kliniki ya macho huku akiniandikia nikanununue famasi dawa ya mafuta ya kuweka kwenye jicho  kama huduma ya kwanza. Kwa maumivu niliyokuwa nikiyasikia sikusubiri mpaka nifike nyumbani  ndipo niweke ile dawa, nilitafuta mahali palepale hospitalini na kuanza kuitumia.

Siku iliyofuata Jumatatu tarehe 24 nilijihimu asubuhi na mapema nikawa mtu wa pili kwenye foleni ya kliniki ya macho pale Magomeni hospitali. Daktari mmoja mwanaume alinichunguza ikiwa ni pamoja na kupima uwezo wa macho yote mawili wa kuona na yote bado yalikuwa yakiona vizuri kwani niliweza kusoma herufi zote nilizowekewa mbele nisome, isipokuwa tu zamu ya jicho la kulia nilisoma kwa taabu kidogo, kulikuwa na mchanganyiko wa mawingumawingu kidogo na maumivu makali.

SOMA: Uwezo wa akili ya binadamu ni wa ajabu na usiokadirika

Dokta yule aliniambia kuwa jicho langu lilikuwa jekundu sana na lilikuwa limeshambuliwa na aina ya ugonjwa wa macho utokanao na virusi ujulikanao kitaalamu kama (pink eyes au conjactivitis) hivyo alinipa dawa(antibiotic) nikaweke kuzuia maambukizi mengine zaidi ya bakteria na baada ya siku kadhaa lingeacha tu lenyewe  kwani virusi hawana tiba ni kama yalivyokuwa mafua, hutoweka vywenyewe kwa kinga ya mwili kuimarika.

Nilipoenda duka la dawa nikakuta kumbe dawa ya macho aliyoniandikia yule dokta wa macho ni sawasawa na ile niliyoandikiwa na daktari wa kawaida jana yake hivyo ilinibidi niache kununua nikatumie tu ileile ya jana.

Niliwahi kuugua macho siku za nyuma lakini kitu cha ajabu nilichoona safari hii ni kwamba jicho moja tu ndilo lililokuwa likiuma na kuwa jekundu, nilitegemea kama kweli ni maambukizi basi baada ya muda mchache  na jicho jingine nalo lingeanza kuathirika lakini haikuwa hivyo. Kadiri siu zilivyozidi kupita ndivyo jicho langu nalo lilivyokuwa “likiwiva”(likiwa jekundu) sambamba na maumivu makali yasiyotaka kabisa mwanga licha ya kuendelea  na matumizi ya ile dawa ya macho ya tube aliyoniandikia daktari wa Magomeni.

SOMA: Hivi unajua mswaki ni hatari unaweza kukuua?

Sasa ilikuwa ikipindukia siku ya nne tangu nianze matibabu hayo pasipo kuona nafuu yeyote ile. Ilifika mahali nikawa hata nakiuka masharti ya ile dawa na kuongeza kiasi cha dawa machoni kwa matumaini labda ingenisaidia lakini wapi!

Shughuli zangu zote ziliathirika, kazi za kuandika makala katika blogu ya jifunzeujasiriamali, kwenye email list na hata katika group la watsap la michanganuo-online zote niliona kama kituo cha polisi vile. Kila nilipojaribu kutizama kwenye kioo kiwe ni cha kompyuta au simu miali ilichoma kwenye jicho utadhani nimetazama mlipuko wa bomu la atomiki.

Ningelikuwa na imani haba nigeliweza kufikiria labda  kulikuwa na mtu ameniloga ili nishindwe kutimiza majukumu yangu, “Kwanini macho tu, ambayo ndiyo huniwezesha kufanya kazi zangu muhimu? si bure lazima kuna mkono wa mtu hapa” ningeliweza kuwaza hivyo lakini katu sikuruhusu kitu cha namna hiyo akilini mwangu.

Maumivu ya jicho yalinifanya nikumbuke vitu vingi  vilivyokuwa vimetokea siku chache jirani na ninapoishi.

Kwanza ulikuwa ni msiba wa kuhuzunisha mno wa kijana mmoja mtoto wa jirani yangu(mama mmoja) aliyekuwa ndio tu katoka kumaliza kidato cha sita(form six) mwaka huu na kufaulu mtihani wake vizuri.

SOMA:Unawezaje kuyakabili magumu, maanguko na mikasa ya kutisha maishani kama hii?

Akiwa anasubiri kupangiwa chuo kikuu alikwenda Mbagala kwa ndugu zake alipokaa wiki kadhaa kabla ya kurudi kwa mama yake Mbezi akiwa analalamika kichwa kumuuuma sana pamoja na taya na misuli ya shingo kukaza. Tangia utotoni alilelewa na mama yake pekee kwa shida ikiwa ni pamoja na kuhangaika naye kwa kila kitu zikiwemo gharama zote za masomo. Alikuwa ndio tegemeo pekee kwa mama yake.

Mama yake alimpeleka hospitali za kawaida pale mtaani ambapo walimpima na kugundua alikuwa na malaria wakampa dawa alizotumia bila nafuu yeyote ile. Alipelekwa hospitali ya Mwananyamala na walipompima hawakuona ugojwa wowote. Wakampa tu dawa za maumivu na kumfanyia kipimo cha kichwa walichomwambia arudi baada ya siku kadhaa kuchukua majibu.

Kwa karibu wiki mbili sasa tangu aanze kuugua, hali ilikuwa inazidi kuwa mbaya mpaka akawa sasa anaanza kupoteza fahamu na kupata kitu kama degedege ndipo watu wakamshauri mama yake amrudishe tena hospitali ya Mwananyamala labda watampa rufaa aende Muhimbili kwa vipimo zaidi.

Kutokana na hali ya kiuchumi ya mama yule hata nauli ya safari za hospitalini ilikuwa ni mtihani, pia ndugu wengine na jamaa walikuwa wakikazana kumshawishi kuwa mwanaye atakuwa alikuwa anasumbuliwa na maswala ya kienyeji(kulogwa au kutupiwa majini) hivyo nguvu zikawa zinagawanyika hospitalini na katika maswala ya kienyeji na maombezi. Mwishowe lakini mama alikubali kumrudisha mwanaye hospitali ya Mwananyamala baada ya hali kuzidi kuwa mbaya.

Moja kwa moja Mwananyamala walimuandikia rufaa apelekwe hospitali ya Mloganzila, iliyo chini ya Hospitali kubwa ya Muhimbili. Madaktari pale walijitahidi kuchukua kila aina ya vipimo siku hiyohiyo huku mama yake naye akienda kuhangaika kutafuta fedha kwani hakuwa na bima ya afya. Kwa bahati mbaya siku ya pili yake kabla hata ya kuanza matibabu kamili kijana yule alizidiwa na kuaga dunia kifo kilichoacha simanzi kubwa si kwa mama yake mzazi tu bali kwa kila mtu aliyemfahamu yule kijana.

SOMA: Ukweli mchungu kila mtu anaopaswa kuukubali maishani kabla hajaiaga dunia.

Ripoti ya madaktari wa Mloganzila ilikuja kuonyesha kwamba kjijana yule kilichomuua ni ugojwa wa Tetanus au Pepopunda. Ugojwa huu watu wengi huuhusisha na kukatwa au kutobolewa na kitu chenye kutu kama msumari au bati lakini ukweli ni kwamba unasababishwa na bacteria fulani ambao hupenda kuingia mwili wa binadamu kupitia vidonda au michubuko na huishi katika udongo, vinyesi vya binadamu na wanyama. Hauna tiba maalumu ila mgojwa akiwahi matibabu kuna uwezekano wa kupona. Huzuilika kwa kinga hasa watoto wachanga wanapozaliwa, mama zao wakiwa wajawazito na mtu yeyote yule anapohisi yupo hatarini kupata hao bacteria.

Haijulikani kijana huyu alipatapata vipi hao bacteria na mama yake anadai inawezekana kipindi akiwa kwa ndugu zake huko Mbagala labda aliwahi kuumia mahali au kupata kidonda bila kujua kama kingeliweza kumletea madhara hayo. Hata hivyo hakuwa na jeraha lolote kubwa mwilini.

Maumivu makali ya jicho pia yalinifanya nikumbuke watu kadhaa waliowahi kupata ulemavu wa macho yote mawili au jicho moja na kutafakari ni maumivu na mateso  kiasi gani waliyopitia kipindi cha mpito walipokuwa wakitoka kwenye uoni wa kawaida kuelekea ulemavu kamili wa macho.

SOMA: Punde kabla hujakata tamaa ya maisha soma hapa.

Nilimkumbuka mwandishi na mhariri maarufu wa magazeti Absalon Kibanda aliyepoteza jicho lake moja baada ya kushambuliwa na majambazi wasiojulikana akitokea kazini usiku karibu na nyumbani kwake. Mungu mkubwa jicho moja lilipona halikudhurika. Sipati picha kama angewezaje kuendelea na majukumu yake ya uandishi  wa habari. Isingelikuwa tofauti tena na kumtoa samaki kwenye maji na kumweka nchi kavu.

Nilimkumbuka pia yule mtu aitwaye Saidi aliyetobolewa macho yake yote mawili na mtu hatari aliyejulikana kama Scorpion maeneo ya Buguruni Sheli, nikajaribu kuvaa viatu vyake lakini nikaona havinitoshi ni vikubwa mno! Hata kama ni ulemavu wa macho kwa upande wangu bado ingelikuwa ni jicho moja siyo mawili kama ilivyokuwa kwa bwana Said. Nilizidi kupiga picha na kujaribu kufikiria changamoto walemavu wa macho wanazokutana nazo wawapo barabarani nikathibitisha wana changamoto za kweli.

SOMA: Historia ya siku ya kutokomeza umasikini duniani ni ya kusisimua.

Siku ya Ijumaa, siku ya 6 baada ya matibabu pale Magomeni kutoonyesha nafuu yeyote, nilifikiria nirudi tena palepale nikawaeleze ili wanipe ushauri iwapo niende hospitali nyingine au la. Nilitoka nyumbani  asubuhi sana kusudi nisije kukutana na miale ya jua linapochomoza kabla sijafika hospitali kwani sasa jicho lilikuwa ndio limezidi kabisa kukataa mwanga hata uwe kidogo, hata miwani ya jua nayo ilikuwa haiwezi tena kunifanya nisisikie maumivu makali. Lilikuwa likitoa machozi mfululizo na nafuu pekee sasa ikawa ni kuweka kitambaa juu ya miwani tena kwa kufunika macho yote mawili huku nikigeukia upande usiokuwa na miale ya jua kwani hata mwanga kidogo tu kwenye jicho la kushoto nao ulionekana kama vile unapenya kwenye jicho la kulia. Chumbani taa ilizimwa muda wote usiku na mchana na mchana mapazia yalifungwa yote kusiingie mwanga wowote ule mkali.


Siku hiyo ya Alhamisi nikiwa kwenye daladala la Mbezi-Kimara ili nikapande mwendokasi, nilimpa kondakta nauli shilingi elfu moja akanirudishia chenchi sh. 600. Mara kondakta yule aliniita akiniuliza, “bro,bro, kwani una matatizo ya macho?”  nikamjibu ndiyo huku nikikazana  kufunika vizuri jicho la kulia kwa kile kitambaa. Alinitaka nimpe ile shilingi mia sita kisha na yeye akanirudishia ile elfu moja niliyompatia. Badala ya kufurahi kitendo kile kilinishtua kwani nilianza rasmi kuhisi namna ambavyo walemavu hutendewa na baadhi ya wasamaria wema. Ndio muda nilioanza rasmi kuonja hali ya kuwa mlemavu wa macho.

Sikushuka Kimara mwisho shauri ya kukwepa kupanda daraja nikashuka Korogwe na kuingia moja kwa moja kwenye Mwendokasi lililokuwa limejaa sana abiria. Nikasimama kwa shida na miwani yangu ya jua huku kitambaa nacho hakibanduki machoni kuhakikisha mwanga wa jua ambalo tayari lilikuwa limekwishaanza kuchomoza hauingii moja kwa moja machoni.

SOMA: Pipi ya kijiti yaweza kuwa hatari sana kwa mwanao, chukua tahadhari.

Gari likiendelea na safari nilihisi mkono wa mtu ukinigusa begani, “Kaka, kaka, njoo ukae hapa inaonekana unaumwa ” Dada mmoja aliyekuwa ameketi kwenye siti alivyoona hali niliyokuwa nayo akashindwa kujizuia na kuniita nikakae kwenye kiti alichokuwa amekalia. Hili nalo pia lilinishitua sawasawa tu na lile la kurudishiwa nauli na konda, nikazidi kuona dhahiri sasa naelekea kuwa na ulemavu kamili wa macho.

Nilipofika kwa daktari wa Magomeni, alishtuka kuniona tena huku hali ikiwa mbaya zaidi. Nikamsikia akimuita daktari mwingine wa macho mwanamke wanayefanya pamoja, “Mama hebu mcheki huyu” Nilimpa lile kadi akalisoma kisha akanichunguza jicho, hawana vifaa vingi sana vya kupimia macho, akachukua smartphone yake na kuwasha tochi kisha akanimulika kwenye jicho kama anapiga picha vile. Mama alionyesha kama kushtuka hivi halafu akaniambia niketi kwenye kiti kingine maalumu kwa ajili ya kupima uwezo wa macho kuona.

Nilitakiwa kusoma maandishi kama ile siku ya kwanza lakini jicho lililokuwa na ugonjwa safari hii lilipoteza kabisa uwezo wake wa kuona kwa karibu asilimia 50. Ina maana nilipofunga jicho la kushoto, jicho la kulia halikuwa na uwezo wa kutambua  nusu ya herufi za maandishi yaliyokuwa yamewekwa mbele yangu.

Yule mama Daktari aliniambia kuwa tatizo langu pale wasingeweza kuendelea tena kulitibu kutokana na jicho kuanza kupoteza uwezo wa kuona hivyo angeniandikia rufaa niende hospitali  kubwa, mwananyamala au  Muhimbli lakini alifikiria kidogo kisha akaniambia, “ Sijui lakini ninavyokuona sidhani kama utashindwa kwenda pale Mikocheni CCBRT, kama utaweza ni bora uende pale moja kwa moja kwani ukisema uendelee kuhangaika hospitali za kawaida huku jicho likiendelea kupoteza uwezo wa kuona namna hii ni hatari, unaweza ukalipoteza jicho lako kabisa”.

 SOMA: Ua zuri lakini hatari linaloweza kuua dakika kumi na tano tu

Aliandika andika pale kwenye kadi, nikatoka zangu kuelekea CCBRT Iili pamoja a vipimo vingine wakanipime na ugojwa wa presha ya macho(glakoma) ambao daktari huyu alihisi naweza kuwa nao kwani dalili za presha ya macho nazo ni pamoja na maumivu na macho kuwa mekundu. CCBRT  hutoa matibabu ya matatizo ya macho kwa walemavu na watu wengine  wa kawaida, hutibu aina zote za magojwa ya macho ikiwemo glakoma, upasuaji, miwani, uoni hafifu, mtoto wa jicho na dalili za matatizo ya macho za aina zote.

Niliingiwa na hofu kubwa sana baada ya kusikia naenda kupima presha ya macho, nikaanza kufikiria kama nitakuwa nayo itakuwaje kwani ugojwa huo ni serious sana hasa ukishaanza kusikia dalili kama nilizokwishaanza kuziona. Mara nyingi unaweza kutibu athari zake tu usipofuke iwapo utawahi kuzigundua mapema. Isitoshe inasemekana huanza na jicho moja kisha muda mfupi baadae la pili nalo hufuatia.

Nilipanda basi la Msasani nikashuka ilipo hospitali ya macho CCBRT, nilikata kadi na moja kwa moja nikaelekezwa kuketi kwenye viti kusubiri namba yangu ya faili iitwe nikaonane na dokta. Kabla ya kuwaona madaktari kwanza unafanyiwa vipimo na manesi kikiwemo hicho kipimo cha presha ya macho. Foleni ilikuwa ndefu na mpaka kufikia saa 9 nilikuwa bado sijaitwa. Ila uzuri wa pale ni kwamba hawaruki namba ya mtu, aliyewahi amewahi na ukichelewa umechelewa.

SOMA: Kwanini chanjo ya malaria imekuwa ngumu hivyo kupatikana?

Zamu yangu ilipofika, mtaalamu alinipima presha ya macho kwa kidude mfano wa bunduki ya ‘toy’ kisha akajaza katika kadi langu nambanamba fulani, sikuelewa namba aliyoandika ilimaanisha kitu gani hivyo nikawa bado na wasiwasi  ambao hatima yake ingeenda kujulikana kwa daktari mwenyewe. Nilielekezwa na yule mtaalamu(nesi) nielekee chumba namba 12 wanakopatikana madaktari. Huko nako nilikuta foleni ni ndefu lakini ilikuwa ikitembea harakaharaka. Kuna kama hall hivi ambalo wapo madaktari wengi kila mmoja na kizimba chake. Mbele ya Daktari ipo mashine kubwa ya kisasa ya kioo kwa ajili ya kuchunguzia macho inayofanana na darubini kubwa.

hospitali ya macho ccbrt
Mfano wa mashine hiyo wanayotumia madaktari kupimia macho, mwanaume aliyeko kulia ndio daktari, kushoto ni mgonjwa wa macho akichunguzwa.
Daktari aliyenitibu alikuwa mwanaume wa makamo, alianza kulichunguza jicho langu kwa kuniambia niingize kichwa kwenye mashine ambapo macho hulenga katika chombo kinachomwezesha kuyachunguza. Alinitaka niangalie juu, chini kisha kila upande  na baada ya hapo akaandika kwenye kadi. Aliniambia kuwa jicho langu lilikuwa na maambukizi (infection), hivyo ataniandikia dawa za matone(aina mbili) nitakazokwenda kutumia kwenye jicho lililokuwa na tatizo tu mpaka tarehe ya kurudi tena kwa uchunguzi.

SOMA: Vitu vitano (5) vitakavyokupa utulivu wa nafsi na amani ya moyo katika maisha yako

Mpaka naondoka pale hospitalini ilikuwa yapata kama saa 11 jioni hivi, muda ulikuwa umekwenda sana lakini sikujali kwani nilikuwa angalao nina matumaini kwamba nimepata matibabu. Muda ule nadhani hata madaktari na wahudumu katika ile hospitali wengi wao walikuwa wakiondoka makwao. Hili ungeweza kuliona dhahiri hata kwa madaktari mle chumbani kwani walionekana wamechoka kwa kazi nyingi na foleni ndefu ya wagojwa. Hata hivyo niliwasifu kwa uvumilivu wanaouonyesha kwa wagojwa kwani mgojwa faraja yake ni kuona anapata huduma bila kujali muda atakaosubiri.

Nilikwenda kuzitumia zile dawa za macho kama nilivyoelekezwa na daktari na baada ya siku tatu (3) nikaanza kupata nafuu. Wiki moja baadae sasa jicho langu limeanza kurudia tena katika hali yake ya kawaida.

HITIMISHO:

VITU NILIVYOTAKA MSOMAJI UJIFUNZE KWA KIFUPI KUTOKANA NA MKASA HUU ULIONIKUTA

1.  KABLA HUJAFA HUJAUMBIKA.
Ukiwa ungali bado unaishi hapa duniani tegemea lolote kukukuta na wala haijalishi kama ulizaliwa na viungo vyako vyote kamili, hivyo wajali wale waliokuwa na mapungufu mbalimbali katika viungo vyao au akili kwani hawakupenda kuwa kama vile walivyo, wengi walikuwa tu kama ulivyokuwa wewe sasa. Wenye macho mekundu hawajapenda kuwa vile hata wewe unayemuua kikongwe mwenye macho mekundu leo ukisema ni mchawi unaweza kuja kuuwawa pia na wewe hivyohivyo hali hiyo itakapokuja kukukuta

Walemavu wasioona, wasiosikia, walewmavu wa ngozi, wenye ulemavu wa miguu au kiungo kingine chochote kile, changamoto wanazozipata ni za kweli wala si kama wanadeka kama watu wengi wanavyowachukulia. Taabu wanazozipata wakiwa kwenye vyombo vya usafiri, majengo ya umma, tasisi na hata maeneo mengine mbalimbali wanastahili kupewa msaada na upendeleo wa kipekee kuwapunguzia makali ya taabu hizo.

2.  UMASIKINI NI CHANZO KIKUBWA CHA MATATIZO MENGI KWA WATU.
Uchunguzi wa afya wa mapema unaweza kuepusha madhara mengi na hata wakati mwingine vifo. Yule kijana mama yake kutokana na kutokuwa na uwezo alihangaika na matibabu madogomadogo mtaani mpaka pale hali ilipokuwa mbaya zaidi akiwa ameshachelewa  akampoteza mwanaye. Ukiwa mzima huna tatizo lolote la kiafya, pigana kufa na kupona katika shughuli zako za kiuchumi ili wakati wa majanga kama ya homa uweze kujisaidia mwenyewe kwa matibabu ya maana.

3.  MAGONJWA MENGINE HUWEZI HATA KUDHANIA KAMA YAPO.
Ni vigumu sana kwa mtu wa kawaida kuamini kama magonjwa hatari kama vile tetanus, homa ya inni, glakoma na mengineyo bado ni hatari na yanaendelea kuua watu. Kwa kuwa hayatokei mara kwa mara, mtu anapougua magojwa hayo wale wanaomzunguka  huwa hawaamini,  wanabakia tu kuhangaika na kulaumu nguvu za giza ambazo ni vigumu mtu kuzithibitisha.

4.  CHELEWACHELEWA NAYO SIYO NZURI, KUNA MAMBO MENGINE SI YA KUSUBIRI HATA MASAA.
Nilichelewa sana kuchukua hatua za haraka jambo ambalo lingeweza kunifanya nipoteze jicho langu au yote mawili. Nimegundua kuna magojwa mengine ambayo mtu hutakiwi kabisa kuyachelewesha. Nilitakiwa kuchukua hatua za maana tangu siku ile ya kwanza tu nilipoanza kuhisi maumivu ya jicho, gharama haikuwa kikwazo sana kwangu bali ile kusema tu, ‘ngoja kwanza nianzie hospitali ndogo’ hata hivyo ndani ya zile siku saba bado nilizembea sana.

5.  BIMA NI  MUHIMU MNO DUNIA YA SASA!
Gharama za bima ya afya kwa mwaka huwezi ukalinganisha na gharama utakazokuja kulipa pindi ukiugua ugojwa mkubwa na huna bima. Ifike mahali sasa watu tuone bima kama ni kitu cha lazima katika maisha yetu.

6.  KAMA VIUNGO VYA MWILI VINAVYOTEGEMEANA, MAISHA NAYO ILI YAENDE VIZURI NI LAZIMA KITU ZAIDI YA KIMOJA VIBALANSI, AFYA, UCHUMI, MAHUSIANO NA ROHO.

Pamoja na kuhangaika kutafuta maisha mazuri kiuchumi, lakini unatakiwa pia kuichunga sana afya yako ya kimwili, mahusiano yako na watu wengine yakiwemo ya kifamilia & ndoa, lakini pia mahusiano yako na Mungu(kiroho). Kila kimoja kipe nafasi yake kwani kimoja kati ya hivyo kikitetereka huwezi kufikia maisha mazuri unayoyatamani.

2 Responses to "HUJAFA HUJAUMBIKA: NILIVYOONJA ULEMAVU WA MACHO KWA SIKU 14"